Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Jamal Kassim Ali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magomeni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi asubuhi ya leo kuchangia katika bajeti hii ya Serikali. Kwanza, nikupongeze kwa umahiri ambao umeuonesha ndani ya Bunge hili na kwa Watanzania wote katika kuendesha vikao vya Bunge kwa uimara na ujasiri mkubwa kwa kufuata kanuni na taratibu ambazo tumejiwekea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kwenda, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mipango na timu yake kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya kuhakikisha kwamba Serikali inakusanya pesa za kutosha kwenda kugharamia gharama mbalimbali za maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwenye suala la VAT. Mheshimiwa Dkt. Mpango katika mawasilisho yake ya mapendekezo ya bajeti, katika marekebisho ya Sheria ya VAT amesema kwamba sasa VAT baina ya pande hizi mbili za Muungano yaani Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara zitatozwa at a point of destination.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie Mheshimiwa Waziri, biashara baina ya pande hizi mbili za Muungano zimekuwa zikikabiliwa na changamoto kubwa ya kodi mpaka sasa bado hatujaweza kuzitatua. Kuruhusu utaratibu huu ni sawasawa na kwenda na kijinga cha moto kwenye petrol, tunakwenda kuongeza matatizo ya kodi ambazo wafanyabiashara wetu wamekuwa wakizilalamikia, wale ambao wanafanya biashara zao baina ya pande mbili za Muungano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Afrika Mashariki tumeona wameingia makubaliano ya redemption, kodi zikusanywe at a point of entry, na kule mzigo unapofika basi atakuwa remitted ile kodi yake iliokusanywa. Na mfumo huu ndio uliokuwa unatumika hapo kabla ya mabadiliko ya Sheria mpya VAT ya mwaka 2015. Nimwambie Dkt. Mpango, katika utaratibu huu mpya, kwanza tunaenda kutengeneza mgogoro wa kikodi kwa wafanyabiashara wetu, lakini pia tunaenda kusababisha au kutengeneza loophole ya watu kukwepa kodi. Kwa mfano leo hii, mtu akinunua mabati yake hapa Dar es Salaam akasema anayapeleka Zanzibar hatotozwa VAT. Lakini yale mabati yanaweza yasifike Zanzibar yakaishia hapa hapa Dar es Salaam, kwa hiyo, tutakuwa tunapoteza kodi yetu. Kwa hiyo, nikuombe kabisa katika hili tunaomba utaratibu ule ambao ulikuwa unatumika hapo awali uzidi au uendelee kutumika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye mabadiliko ya Sheria ya Kodi ya Mapato, niungane na baadhi ya Wabunge wenzangu ambao hawakuunga mkono hoja ya kutozwa kodi Wabunge katika gratuity, niunge mkono hilo. Nilivyopitia Sheria Namba 11 ya mwaka 2004 ya Kodi ya Mapato katika jedwali la pili nilikuta kwamba watu na taasisi ambazo zinasamehewa kodi si Wabunge peke yake. Wapo watu wengine, zipo taasisi zingine ambazo zinasamehewa kodi. Kwa hiyo, Dkt. Mpango katika hiyo hoja yako ya kusema unataka ujenge mazingira ya usawa naona kwa hapo itakuwa haina mashiko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe kabisa, kama ambavyo umeona kuna hoja na haja ya wale wote wengine waendelee kusamahewa kodi za mapato kwa mujibu wa sheria yetu ile kama ilivyo katika jedwali lake la pili basi, hoja na haja hizo bado ipo kwa Wabunge; Wabunge waendelee kusamehewa kodi katika gratuity zao ambazo wanalipwa baada ya kumaliza kipindi chao cha Ubunge. Hoja na haja hiyo ipo, wenzangu wengi wamezungumza na mimi nikuombe kabisa, niombe Serikali yangu sikivu katika hili itufikirie sana. Kwa vile muda ni mdogo sitaki kuzungumza mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini eneo lingine kwanza nikupongeze na niwapongeze wafanyabiashara wa Tanzania kwa kuutikia wito wako wa kuanza kutumia mashine za kielekitroniki yaani hizi za EFDs katika kutoa risiti pale ambapo wanauza bidhaa zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ningependa kujua kwa sasa ukuaji wa sayansi na teknolojia umepelekea mabadiliko makubwa kabisa hata katika transaction zetu hizi za mauzo. Kumekuwa na ukuaji mkubwa katika e-commerce na naamini Wabunge wenzangu mnashuhudia hilo. Leo hii kuna miamala inayofanywa kupitia moja kwa moja baina ya benki zetu kwenda kwa wauzaji. Kuna miamala ambayo inafanywa kupitia simu zetu, mfano mdogo tu asilimia kubwa leo ambao wanatumia ving‟amuzi, hawalipi cash dirishani wanatumia simu zao kulipia gharama mbalimbali za ving‟amuzi hivyo vya televisheni. Katika eneo hili Mheshimiwa Dkt. Mpango tunaomba uje utuambie basi Serikali kupitia TRA imejipangaje, ku-track records zote za mauzo hayo kuhakikisha kwamba na wao basi, wanachangia au wanakuwa sehemu ya kuchangia katika kodi ya Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwa upande wa CAG. Ofisi yetu ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Serikali imefanya kazi kubwa na nzuri sana kwa Taifa letu. Imefanya kazi kubwa na nzuri kwa Taifa letu na sote mashahidi, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali imekuwa ikitoa mapendekezo ya maboresho mbalimbali ambayo yameisaidia Serikali yetu hii kutokuingia katika hasara au upotevu mbalimbali wa fedha za umma. Lakini ofisi hii hii imesaidia Serikali kurudisha pesa mbalimbali ambazo aidha, watu walikwepa kulipa au watu walifanya ubadhirifu na kuwa sababu ya watu kuchukuliwa hatua kisheria kwa makosa hayo. Nimuombe Mheshimiwa Waziri katika Bajeti ya mwaka jana, ofisi hii tuliitengea shilingi bilioni 74; katika bajeti ya mwaka huu tumeitengea shilingi bilioni 44.
Mheshimiwa Naibu Spika, nini maana yake? Maana yake tunaenda kumfunga miguu CAG asiende kukagua tunaenda ku-reduce ile scope yake ya ukaguzi na hii athari yake ni nini kwa Taifa letu? Kwanza kwa vile mwaka huu tumeona asilimia 40 ya pesa za bajeti ya Serikali zinaenda kwenye miradi ya maendeleo tutatengeneza mianya ya watu ambao hawana nia nzuri na Serikali yetu kwenda kuzitumia hizi pesa kutokidhi yale malengo ambayo yamewekewa kwa sababu ambayo watajihakikishia kwamba, hakutokuwa na ukaguzi wa kutosha ambao unaweza ukabaini huenda ubadhirifu au wizi katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika nimepitia ripoti ya CAG ya Taarifa za Ukaguzi kwa Mwaka wa Fedha 2015, ukisoma tu katika preamble ripoti ile inabainisha kwamba CAG amefanya kazi kubwa na nzuri. CAG katika ripoti yake ile ile ameweza kutubainishia kwamba Serikali imepoteza takribani shilingi bilioni 100 katika eneo la ukwepa wa kodi.
Baada ya kusema hayo, naamini Mheshimiwa Waziri atakuja na hoja ya haya niliyoyaibua. Ahsante sana.