Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye mjadala huu unaoendelea wa hali ya uchumi lakini pia na bajeti yetu kuu ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu subhanahu wataala, kwa kunijalia siku hii ya leo kuwa ni siku ya kipekee kwangu mimi Abdallah Hamisi Ulega na familia yangu ikiwa ni pamoja na mke wangu kipenzi Bi. Mariam Abdallah kwa kutujalia kupata mtoto, tena mtoto wa kike. Kwa kweli, nazidi kuthibitisha kwamba akinamama ni wastahamilivu, wavumilivu, ni watu wenye uwezo mkubwa sana kila mahali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mke wangu huyu mwaka wa jana alipoteza mtoto wa umri wa miezi tisa. Mwaka juzi pia alipoteza mtoto wa umri wa miezi tisa. Hakukata tamaa, hatimaye mwaka huu wakati wake umefika na mambo yamependeza. Huyu mtoto katika moja ya jina zuri nitakalompa nitampa jina la Tulia. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni katika ile kuthibitisha kwamba ninyi akinamama mnaweza. Wallah nataka nikuhakikishie kwa mikasa hii aliyoipitia mke wangu kipenzi, ningekuwa mimi ningekata tamaa, lakini yeye hakukata tamaa kama vile ambavyo wewe hukati tamaa na hawa manyang‟au wanaotaka kutusumbuasumbua humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, naendelea kumpa pongezi sana mke wangu kipenzi kwa kazi kubwa sana anayoifanya kwa ajili yangu na kwa ajili ya nchi hii ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze katika kuchangia bajeti. Kwanza kabisa hali ya uchumi na nashukuru sana baadhi ya wasemaji wamesema juu ya hali ya uchumi na mimi nitasema kwa muhtasari sana. Ombi langu kubwa kwa Mheshimiwa Waziri wetu wa Fedha atakapokuja kufanya winding up hapa atueleze, maana sitaki kusema kwamba sisi watu wa Mkoa wa Pwani tumewekwa katika bahati mbaya ya kuwa matajiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuwa tajiri ni jambo jema sana lakini nataka atuambie ni criteria gani alizotumia za kutufanya sisi kuwa ni miongoni mwa mikoa matajiri. Maana nilikuwa napitia kwamba ni vigezo gani vinaweza vikamfanya mtu akaambiwa wao ni matajiri, per capita income au huduma za kijamii? Sisi kule kwetu huduma za kijamii hali ni mbaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, mmoja katika wasemaji waliowahi kusema siku ya jana nilipokuwa nikifanya mijadala yangu, anasema kwa kuwa ninyi mpo karibu na Dar es Salaam, hospitali za rufaa ziko karibu, nikamwambia hospitali ya rufaa si ya watu wa Mkoa wa Pwani, Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili ni ya watu wa Taifa zima la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni nini hasa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwingine akaniambia ninyi mna lami inapita kila mahali katika mkoa wenu. Nikamwambia si kweli, sisi kutoka Nyamwage - Utete tuna shida kubwa, kutoka Mkuranga Mjini - Kisiju tuna shida kubwa, kutoka Bungu - Nyamisati kuna shida kubwa, kutoka Mlandizi - Makofia Bagamoyo kuna shida kubwa, kutoka Mlandizi - Mwaneromango - Mzenga – Vikumbulu - Mloka pana shida kubwa, sasa kwa nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuna haja ya kuwa na wasiwasi isipokuwa tunataka tujue ugunduzi gani uliofanyika katika Mkoa wa Pwani ukawafanya watu wa Mkoa wa Pwani leo wakawa na maisha makubwa ya kuwashinda wengine katika Taifa letu? Maana sisi tuna korosho na korosho yenyewe watu wa Mtwara wanatuzidi kwa mbali, watu wa Lindi wanatuzidi kwa mbali, ni nini hasa, ni vigezo gani, atuambie waziwazi ili na sisi tuongeze jitihada zetu. Pale ambapo atapataja kwamba ninyi watu wa Mkoa wa Pwani mahali hapa mko vizuri, basi inshallah sisi tuongeze nguvu zetu na tufanye vizuri zaidi ili tuweze kuwa na maisha bora ambayo Taifa letu linataka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hilo, naomba sasa niende kwenye maji. Kama walivyosema wenzangu, naomba sana Mfuko wetu wa Maji uendelee kuongezewa nguvu. Tazama mimi katika Jimbo langu la Mkuranga uko mradi wa muda mrefu wa pale Mpera na Kimbiji, unahitaji shilingi bilioni 12 tu. Tutazipataje pesa hizi bila ya kuongeza nguvu katika Mfuko wetu wa Maji?
Mheshimiwa Naibu Spika, nina shida kubwa ya maji katika Mji wa Mkuranga, hatuwezi kupata pesa ya kuweza kuusababisha mradi ule wa Mkuranga unaohitaji takriban shilingi bilioni 2.2 uanze. Tunasema tunaendelea kufanya mazungumzo na kampuni ya Strabag ya Australia kwamba hii ndiyo itakayotusaidia, wasipokubali hawa kutusaidia maana yake watu wa Mkuranga Mjini waendelee kuwa na shida ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana kwa heshima kubwa na taadhima, nguvu zetu tuzielekeze katika kuongeza Mfuko wa Maji ili tutatue kabisa tatizo la maji ambalo linawakabili hasa hawa niliowasifu pale nilipokuwa naanza kutoa hotuba yangu, akinamama. Unaposaidia tatizo la maji unawasaidia akinamama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ningeomba sana tuongeze nguvu zetu katika utalii. Naomba niseme kwamba suala la utalii kuongezewa kodi zote hizi ni tatizo kubwa. Katika takwimu inaonesha kwamba bajeti yetu ya 2015/2016 sekta ya utalii iliongoza kwa asilimia 25. Katika mwaka wa 2014/2015, inaonesha kwamba pesa za kigeni takriban shilingi trilioni 8.3 zimetoka katika utalii. Inaonekana kwamba mwaka 2015 takriban ajira milioni moja, laki mbili na tisini na nne elfu zimetokana na utalii. Leo hii utalii huu umeongezewa kodi nyingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi zetu za Afrika Mashariki Wakenya wameondoa kodi mbalimbali katika utalii na nia yao ni kuongeza utalii katika nchi yao, nia yao ni kuongeza idadi ya watalii, ajira na kipato chao. Tusipofanya jitihada ya kuondoa kodi hizi utalii utashuka. Tazama katika utalii kazi ambazo zimepangwa kufanywa na Watanzania peke yake ni pamoja na kukodisha magari, wakala wa safari (travel agents), kupanda milima na waongozaji watalii na zote zimewekewa kodi. Kwa hiyo, hii itasababisha kupunguza idadi ya watalii, projection yetu ya kupata idadi kubwa ya watalii itapungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapiga kelele hapa ya kupata pesa za kutosha kwa ajili ya miradi yetu ya maji, afya, ambapo afya imeachwa mbali katika bajeti hii. Tutazipataje hizo pesa kama tunaongeza kodi ambazo zitawakimbiza watalii wetu? Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa positive measure aliyoifanya ya kuongeza kodi ya utalii katika vyombo vya usafiri wa anga lakini apunguze kule kwingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena kumpongeza sana mke wangu na kuwapongeza akinamama wote. Naunga mkono hoja hii na ahsanteni sana.