Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii, lakini kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuweza kusimama mahali hapa kwa siku ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ndiyo mara yangu ya kwanza kusimama kwenye Bunge hili la Kumi na Moja, napenda kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Nyang’hwale kwa kunipa kura nyingi sana za kishindo mimi pamoja na Waheshimiwa Madiwani. Kwa kipindi cha pili Halmashauri yetu iko ndani ya mikono ya CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, pia napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa Mpango wake mzuri ambao ameuweka hapa mezani. Pia napenda niseme jambo moja ambalo lilizungumzwa jana, upande wa upinzani walisema Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwenye kampeni zake alipiga push-up.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema kwamba zile zilikuwa ni mbinu, lakini hata ninyi kuna mizunguko mlikuwa mkiifanya, ile zungusha pamoja na helicopter nyingi kwenye Jimbo langu mara nne, lakini hamkufua dafu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kujielekeza kwa kuipongeza hotuba hii nzuri. Na mimi pia naungana na wenzangu kuhusu ujenzi wa reli. Ujenzi wa reli utaongeza mapato makubwa sana katika nchi yetu, lakini pia sisi wananchi tunaoishi pembezoni mwa nchi ni kwamba vifaa mbalimbali vitashuka bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa mfano, cement kwa Kanda ya Ziwa ni shilingi 18,000/=, shilingi 20,000/= mpaka shilingi 22,000/=; wakati Iringa Mheshimiwa aliyekuja kuwekeza nchini kwetu, Mheshimiwa Dangote, amesema kwamba cement itashuka bei mpaka shilingi 8,000/=. Kwa kupitisha kwa njia ya barabara, tutaendelea kuipata ile cement wananchi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla kwa bei kubwa. Lakini pindi reli ile itaanza kufanya kazi, naamini kabisa kwamba cement na mazao mbalimbali kwa kuja Dar es Salaam na mali mbalimbali kutoka na kwenda Kanda ya Ziwa, zitashuka bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu ni mzuri, lakini kuna jambo moja naomba nishauri, kuna bwana mmoja na jeshi kubwa sana, hakuingizwa kwenye Mpango huu, naye anaitwa mzee watoto wa mitaani. Mpango huu haukuwekwa. Kwa nini? Kwa sababu jeshi hilo kila mwaka linaongezeka. Serikali ina mpango gani kupunguza watoto wa mitaani? Mtaa hauzai! Serikali ina mpango gani kuhusiana na suala hilo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Nyang’hwale, mimi nimekuwa Mbunge wao takriban huu ni mwaka wa sita, nimekuwa nikipigania tatizo kubwa la maji. Mkondo wa Ziwa Victoria unaanzia kwenye Jimbo la Nyang’hwale, lakini cha ajabu wananchi wa Nyanghwale hawana maji.
Mwaka 2013, Waziri Maghembe nilikataa kupitisha bajeti yake; bahati nzuri Serikali kupitia Benki ya Dunia tuliweza kupewa mradi huo wenye thamani ya fedha shilingi bilioni 15.7. Cha ajabu, mpaka leo hii pesa ambayo imetoka ni shilingi bilioni 1.8. Bajeti ya mwaka 2015/2016 tuliongezewa shilingi milioni 752 lakini fedha hiyo haijatoka. Sasa hivi Wakandarasi wamesimama, hawaendelei na kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, kwa mwaka wangu wa sita waje wamejipanga vizuri Wizara ya Maji. Sitakubaliana! Sisi wananchi wa Nyang’hwale tuna mkosi gani? Naiomba Serikali ya Chama cha Mapinduzi, ni Serikali sikivu.
Ndugu zangu, naomba nizungumzie suala la elimu bure. Naishukuru Serikali, imeanza kutekeleza; lakini kuna jambo moja sikuliona ndani ya Mpango kuhusu elimu. Kuna familia nyingine, kaya moja unaikuta inajaza darasa; lakini kuna kaya moja ina watoto wawili. Je, ndani ya Mpango huu, kaya moja ina watoto inajaza darasa moja, kaya mbili zinajaza madarasa mawili.
Ndugu zangu, tujaribuni kuliangalia; ndani ya Mpango tuwekeeni utaratibu mzuri. Yule ambaye ana watoto kuanzia 10, 20, au 30, awekewe naye Mpango mzuri. Nusu ichangie Serikali na nusu achangie. Hili suala ni la msingi sana. Kuna wengine wana wanawake kumi, wengine watano na wengine wamejaliwa kuzaa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alifanya ziara kwenye jimbo langu. Alikuja akaahidi Kituo cha Afya Kalumwa, kukipandisha kuwa Hospitali ya Wilayana tayari imeshapandishwa, lakini ukifika pale, hali ni mbaya! Kuna wodi ya akina baba ina vitanda nane. Wagonjwa wa aina zote wanalazwa mle. Naiomba bajeti hii inayokuja, Wizara ya Afya mje mmejipanga vizuri kwa ajili ya kuboresha hospitali yetu ya Wilaya ya Nyang’hwale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miundombinu, kwa kweli miundombinu ya Wilaya ya Nyang’hwale, kuna barabara moja ambayo imeahidiwa kuanzia mwaka 2010 alipokuja Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, alituahidi kutujengea barabara kutoka Busisi kupita Busorwa, kupita Karumwa, Nyang’hwale kupita Msala kwenda Kahama. Leo miaka mitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alikuja tena mwaka 2011 wakiwa katika msafara huo, Mheshimiwa Waziri Maghembe alikuwa yumo, Mheshimiwa Majaliwa alikuwa yumo, Mheshimiwa Rais wetu huyu wa sasa hivi wa Awamu ya Tano alikuwa Waziri wa Ujenzi na Mheshimiwa Jakaya Kikwete, walisimama na wakalizungumzia suala la barabara tutajengewa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwenye Mpango huu, barabara hii haimo. Naomba sasa hii awamu ya hapa kazi tu, atutekelezee. Anaielewa vizuri hiyo barabara, alituahidi akiwa Waziri na leo ni Rais wa nchi. Ninaomba ahadi ya Rais, iwekeni humo barabara hiyo kwenye Mpango huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo. Wananchi wa Nyang’hwale tuna mabonde mazuri sana, tuna mito mingi, maji yale yanaporomoka yanakwenda Ziwani. Naomba tuweke mpango mzuri wa kuyatega yale maji yaweze kuwasaidia wakulima wetu. Tuweze kupata maji kwa mifugo na matumizi ya binadamu, pia tuweke mpango mzuri wa kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema tunataka tunyanyue viwanda vidogo vidogo, vya kati na vikubwa: Je, material hayo yatapatikana vipi? Sisi wananchi wa Nyang’hwale ni wakulima wa mpunga, tunategemea mvua za masika, lakini kama tutatengenezewa mabwawa mazuri, kwa umwagiliaji tutalima mara mbili au tatu na tutakuwa watu wazuri sana wa kuweza kuongeza kipato chetu kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.