Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuzungumza juu ya hali halisi ya bajeti yetu ambayo tunaitegemea na Watanzania wengi sana wanaitegemea.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja kwenye mada kutokana na muda. Cha kwanza naomba niwashukuru sana watu wa Wizara ya Maji. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuangalia umuhimu wa kutoa kodi kwenye dawa zinazotibu maji kwa sababu kuondoa kodi hii kunazisaidia sana Mamlaka za Maji kuweza kutekeleza miradi yao midogo midogo kwenye kila eneo ambapo wapo. Hata hivyo, kutoa kodi kwenye dawa peke yake haitoshi, tungetamani sana na vifaa vinavyohusika katika shughuli za utengenezaji wa maji kama mabomba, pipes na nuts na vitu vingine ambavyo vinafanana na hivyo viondolewe kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha pili tumezungumza juu ya kujenga vituo vya afya na zahanati na huu ndio msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano. Hata hivyo, ingependeza sana tuseme tutajenga vituo vingapi na kila Halmashauri ijue tutaipa vituo vingapi ambapo mwisho wa siku tutafahamu tunao wajibu kwenye kila Halmashauri kujenga vituo vitano, kujenga zahanati tatu na kadha wa kadha, kama ambavyo tunaona Wizara ya Maji na Wizara ya Miundombinu wameelekeza vyanzo vyao kwa namba.
Mheshimiwa Naibu Spika, tungetegemea sana namba hizi kwani zingetusaidia kwa sababu tunatambua tunayo sera ambayo inasema kila zahanati inapojengwa kuwe na wakazi wasiopungua 10,000, tunafahamu iwe na umbali wa kilometa zisizozidi 10 lakini leo tunataka kujenga vituo vya afya kwenye kila Kata. Vituo vya afya hivi tunafahamu ni sawa na hospitali kwa sera ya sasa inavyotaka, ni lazima kuwe na OPD, ni lazima kuwe na maternity ward, ni lazima kuwe na ward ya wanaume na wanawake. Tutavijenga kwa mpango upi, kila Halmashauri itawezeshwa kwa kiasi gani, kuhakikisha vituo hivi vinajengwa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine ni juu ya kodi ya usajili wa bodaboda. Tunafahamu kwamba kodi hii inamhusu mtu anayeingiza pikipiki hii nchini, lakini huyu anapokwenda kuinunua bado hamjatoa maelekezo vizuri kule kwenye Halmashauri. Mngeelekeza vizuri kule kwenye Halmashauri, ziko kodi za leseni wanazotakiwa kulipa watu wa bodaboda hawajawahi kulipa hata shilingi moja. Sababu ni nini? Hakuna maeneo sahihi ya kuwapanga na kuwaelekeza kwamba hivi ndivyo vituo vyenu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu wa bodaboda yenye magurudumu mawili anapaswa kulipia leseni Sh. 22,000, mwenye gurudumu tatu analipa Sh. 23,000. Uliza Halmashauri yoyote haijawahi kulipwa fedha hii kwa sababu Wakurugenzi wamekuwa wagumu kutenga maeneo ambayo yatasaidia sana kuhakikisha kodi hii inalipwa. Ukichukulia Mkoa wa Mwanza peke yake, kuna bodaboda zisizopungua 18,000 mpaka sasa hivi, kwa Sh.22,000 unapoteza zaidi ya shilingi milioni 396. Sasa tukiangalia haya tunaweza tukaona namna gani tunaweza kuwasaidia vijana hawa pamoja na gharama zingine ambazo zinaongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunazungumza juu ya shilingi milioni 50 kwenye kila kijiji, wengine tunakotoka sisi kuna mitaa, tumeizungumzia vipi hii mitaa? Nimshukuru kwa kugundua Mikoa mingi ya Kanda ya Ziwa maana katika mikoa mitano, mikoa minne yote inatoka Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa najiuliza ikabidi nifanye utafiti kwa nini Mwanza tunaitwa maskini, kwa nini Kigoma wanaitwa maskini lakini nikagundua kulingana na idadi ya watu wengi tulionao Kanda ya Ziwa, umaskini wa watu wetu, watu wenye kipato kikubwa ni wachache na watu wenye kipato cha kati ni wachache na maskini ndiyo wengi zaidi kuliko maeneo mengine. Kwa sababu mmelijua hilo tungetamani sana tuone tunasaidiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwanza uwezo wetu wa umaskini ni asilimia 35, Mheshimiwa Waziri ameongelea Geita umaskini uko kwa asilimia 48 na Kagera ni asilimia 43 na mikoa mingine. Sasa hizi shilingi milioni 50 tunazozizungumza tungetamani sana zianzie mikoa hii maskini, kwenye mitaa ili watu wake walioonekana kuwa na umaskini mkubwa waweze kusaidiwa na waweze kujikwamua na wao angalau wasogee kwenye kipato cha kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumza suala la kuhamisha kodi ya majengo kutoka kwenye Halmashauri kwenda kwenye TRA, iko mifano mingi. Mwaka 2007 walijaribu Dar es Salaam ikashindikana na leo tunarudi upya. Pamoja na sheria nyingi ambazo amezitaja humu ndani lakini Mheshimiwa Waziri hajatuambia kama anakumbuka Halmashauri hizi kupitia TAMISEMI Tanzania Bara na Ofisi ya Rais Zanzibar (TAMISEMI) ziliingia mkataba mwaka 2006 na World Bank (GIZ) na kupata fedha nyingi na malengo ya fedha zile ilikuwa ni kuboresha Miji, Makao Makuu ya Miji, Manispaa na Majiji na zimefanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ukipitia mradi wa TSCP, ukienda Mwanza, Mbeya, Arusha, Kigoma utaona haya ninayoyazungumza. Pia wameenda mbali zaidi wakaziwezesha Halmashauri hizi kupata fedha na kutengeneza mfumo wa GIS ambao umesaidia watu wamepewa mafunzo, wameelimisha watu, kwa ajili ya kuhakikisha wanapata data za majengo yote kwenye kila mji, leo tunakwenda kuondoa hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na sheria hizi alizozitaja, tunasahau iko Sheria Na. 2 ya mwaka 1983 inazozitambua mamlaka hizi za mitaa kwamba ndiyo mamlaka pekee zenye haki ya kukusanya kodi ya majengo. Hatukatai, inawezekana ninyi mmekuja na mfumo mzuri zaidi ambao sisi hatujui lakini kama Halmashauri na sisi kama wadau tunafahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo Halmashauri hizi zimeingia kwenye mikataba mikubwa hii tunayoizungumza, zimepewa vifaa kwa ajili ya kuboresha ukusanyaji wa taka, zimepewa vifaa kwa ajili ya kutambua majengo yaliyopo na thamani yake, kuondoa kodi hizi hawaoni kama ni athari kwa Halmashauri hizi? Ni lazima watuambie vizuri lengo na makusudi ni nini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, limezungumzwa hapa suala la kumpunguzia uwezo, mimi naita kumpunguzia uwezo CAG. Nilipokuwa nasikia michango ikabidi nitafiti zaidi, lakini Mheshimiwa Waziri atagundua mwaka huu wa fedha unaokwisha tulikuwa tumempangia CAG shilingi bilioni 74 ukijumlisha na fedha za wadau wengine alipaswa kuwa na shilingi bilioni 84. Mpaka tunavyozungumza CAG kapata shilingi bilioni 32 peke yake na maeneo aliyoyakagua ni ya matumizi peke yake, maeneo ya mapato ameshindwa kukagua.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kashindwa kufika kwenye mikataba mingi ya mgawanyo wa rasilimali za Taifa kama gesi kwenye madini na kadha wa kadha. Katika maeneo 27 ameenda maeneo sita peke yake. Leo tunamtengea shilingi bilioni 44 out of 74 ya mwaka huu unaokwisha, je, hawezi kupata shilingi bilioni 22 chini hata ya zile alizozipata mwaka huu? Hili ni lazima tuliangalie. Inawezekana wao wameliangalia vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tusitafakari vibaya, ni lazima tuhakikishe maeneo tunayotaka yakaguliwe vizuri na sawasawa tujiridhishe. Huyu CAG ndiyo tunamtegemea sisi, ili TAKUKURU afanye kazi yake vizuri anamtegemea CAG na ndiyo maana ata-Audit ripoti ya TRA mwaka huu imechelewa kwa sababu wamekosa fedha hizi, ni lazima tukubaliane tunachokiamua kiwe na maslahi kwa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho kabisa tunafahamu kwamba tunayo matatizo mengi. Tunazungumza viwanda lakini karibu miji yote nchini ardhi iliyotengwa kwa ajili ya viwanda siyo zaidi ya asilimia 2.5 na wakati matarajio na matakwa ni kuwa na asilimia 10 kwenye kila Halmashauri, ni wapi tumeweka?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naomba niunge mkono hoja, lakini lazima tuangalie kinaga ubaga ni nini tunataka kuwatengenezea wananchi wa Taifa hili ili wafikie malengo ya Mheshimiwa Rais yaliyokusudiwa. Nakushukuru sana.