Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo kuchangia bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri. Kwanza nampongeza Waziri kwa kazi nzuri kwa bajeti aliyoiwashilisha na tumeona asilimia 40 imetengwa kwa ajili ya kutatua kero za wananchi, fedha za maendeleo asilimia 40. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchango wangu nijielekeze kwenye ofisi ya CAG. Wabunge wengi wamezungumza juu ya kumpa uwezo CAG ili aweze kufanya kazi mimi binafsi na-declare interest, ni Mjumbe wa Kamati ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jicho letu ni CAG, lakini pia hata Bunge hili CAG ndiye jicho letu. Pamoja na wote kuwa jicho letu ni CAG hata Rais mwenyewe jicho lake ni CAG. Haiwezekani tuseme hapa kazi tu, tutenge fedha nyingi tupeleke kwenye maendeleo na sehemu mbalimbali halafu tusimtengee fedha mtu ambaye anaweza kuzikagua ili kurudisha feedback kwa Mheshimiwa Rais kwamba, fedha ulizopeleka zimetumiwa kwa kiwango gani kwa utaratibu mzuri au mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili Mheshimiwa Rais aweze kutamba ni lazima apate report kutoka kwa CAG na ndipo ataweza kumsaidia yeye sasa kujua wapi wanaharibu na wapi wanafanya vizuri. Hivyo Ofisi ya CAG hiyo bajeti iliyotengwa ya bilioni 42 ambapo maombi yake yalikuwa ni zaidi ya bilioni 65, tuombe Wizara itenge fedha, siyo aje aombe, itengwe fedha kwa ajili ya utendaji kazi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ameona kila Mbunge akisimama akizungumza anazungumzia uwezeshwaji wa Ofisi ya CAG, nafikiri ame-take note hapo, kwamba CAG inatakiwa sasa katika ku-finalize akapeleke fedha ili tumwezeshe huyu. Hata PCCB hawezi kufanya kazi bila CAG, haiwezekani PCCB afanye kazi, kwa report kutoka kwa nani?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapopunguza fedha za bajeti ya Ofisi ya CAG maana yake LAAC na PAC zinakuwa hazina kazi ya kufanya, lakini hata Rais report yake ya kutambua wapi kuna udhaifu atashindwa kutambua. Tunaomba sasa Wizara iangalie jinsi ya kuwasaidia hiyo Ofisi ya CAG kwa kuwapa fedha ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine nichangie kwenye hili suala; Serikali ina nia nzuri ya kuweka tozo katika crude oil katika alizeti, ina nia nzuri katika kukusanya mapato lakini tuangalie outcome yake isije kutokea kama ile ya sukari. Muda mfupi uliopita ukatokea uhaba wa sukari na mwisho wake tukaanza kufanya kutafuta njia za haraka kutatua tatizo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwashauri tunapoweka tozo hizi ambayo ilikuwa haipo mwanzo tutasababisha upungufu wa mafuta haya ambayo uhitaji wake ni zaidi ya lita laki sita na uzalishaji wetu ndani ya nchi ni karibu laki moja na nusu, hivyo, kuna asilimia 75 ya mafuta haya tunaagiza nje ya nchi. Kwa hiyo, tuangalie athari yake isije kutokea sasa kwa wauza chipsi hawa maana mafuta yanapanda bei kutokana na tozo hii au ulipaji wa kodi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mafuta haya yakipanda bei hata muuza chipsi atazipandisha bei chipsi zake, hata mama ntilie anayeuza chakula pale naye atapandisha bei chakula chake. Hiyo itapelekea yule mbeba zege kununua chakula kwa mama ntilie kwa bei ya juu. Kwa hiyo tunapandisha maisha ya mtu wa chini yaende kuwa ghali zaidi hali itakayopelekea ugumu wa maisha kujitokeza kwa kasi ya ziada. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe Serikali iangalie hii tozo isije ikaja kuumiza watu wa chini. Nia ya Serikali ni nzuri; tuangalie, Mheshimiwa Rais ana uchungu sana na watu wa chini, lakini kutowekeza katika sehemu kama hizi ambazo zinawagusa moja kwa moja watu wa chini tutawaongezea ugumu badala ya kuwarahisishia maisha. Niombe Wizara ya Fedha iangalie tozo kwenye hii crude oil hasa kwenye mafuta ya sun flower na mengineyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze lingine la maji. Tumeona jitihada za Serikali katika kutatua kero mbalimbali za nchi yetu, mfano tumeona jitihada kubwa za ujenzi wa barabara Tanzania, tumeona jitihada kubwa inayofanyika katika kutatua tatizo la umeme vijijini lakini hatujaona Serikali ikiwekeza kwa njia ya dhahiri ya dhati kabisa kutatua tatizo la maji nchini kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila Mbunge akisimama hapa anazungumza tatizo la maji, kila Mbunge akisimama maji, maji, maji, sasa kumbe ipo haja, hebu tuongeze fedha, tutenge fedha za kwetu kwa ajili ya kutatua tatizo la maji, kwa maana tuongeze. Wameshauri hapa wengine wamesema tuongeze Sh. 50/= kwenye mafuta na Mfuko wa Maji uwepo, kwa sababu miradi mingi ya maji inayotekelezwa ni fedha za wahisani, fedha zetu wenyewe hatujawekeza vya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna uhaba wa maji, uhaba wa maji kwa mama zetu, uhaba wa maji kwa mama lishe, uhaba wa maji kwa wafugaji, uhaba wa maji kwa kada mbalimbali ndani ya nchi yetu. Tuangalie sasa namna gani huu Mfuko wa Maji tunauweka.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo Sh. 50/= tubariki sasa ipitishwe, ili fedha itakayopatikana ipelekwe kwenye kutatua shida ya maji. Tukisimama hapa tunamwangalia Waziri wa Maji. Mbunge yeyote atakayesimama anazungumzia maji. Kwa hiyo, hii inaonesha suala la maji hatujalipa uzito wa hali ya juu. Sasa ni wakati wa kuhakikisha kwamba, tatizo la maji tunaliondoa ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wamezungumza wengine hapa tuna mabwawa, tuna maziwa, tuna bahari, tuna vitu vingi, lakini bado tumebaki kuwa na tatizo la maji ndani ya nchi yetu. Ukienda nchi zingine za wenzetu ambazo zina uhaba wa vyanzo vya maji wanatatua tatizo hili la maji wenyewe wakati sisi tunavyo lakini tuna tatizo la maji ndani ya nchi. Niombe Wizara iangalie namna ya kulitatua hili jambo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo naweza nikachangia ni juu ya suala la bajeti. Tunatenga bajeti hapa, tunaiomba Wizara, fedha hizi ziende kwa wakati, kwa sababu fedha tunavyozipitisha hapa halafu mwisho wa siku tunakwenda kwenye mwezi Machi au Mei mwakani tunakuta asilimia tano, kuna sehemu zimepelekwa asilimia 10, asilimia saba; mwisho wa siku maana yake ile kazi kubwa tuliyoifanya na kutumia muda mrefu kuijadili ile miradi inashindwa kutekelezeka kwa wakati. Niiombe Wizara ipeleke hizi fedha kwa wakati ili miradi na yale malengo ya Serikali yaweze kutimizwa kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo nichangie pia kwenye suala zima la lugha yetu ya Kiswahili. Lugha yetu ya Kiswahili tunatambua mchango wake ndani ya nchi yetu na juzi kati nimesoma katika vyombo vya habari Zimbabwe wameanzisha somo la lugha ya Kiswahili katika mitaala yao. Je, fursa hizi Tanzania tunazitumiaje? Mabalozi wetu watumie fursa hii kwa kuwaangalia vijana wetu, vijana wetu ndiyo hivyo wana-graduate, wamesomea mambo haya ya kufundisha Kiswahili, lakini hatujapeleka Walimu wa kutosha nje ya nchi kwenda kufundisha lugha hii ya Kiswahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona Taifa la Kenya linapeleka watu wetu sana wanafundisha mpaka vyuo vikuu, lugha ya Kiswahili. Nilipata bahati ya kuhudhuria kongamano moja nchini Ekuador mwaka 2013. Nilikutana na mwanafunzi ametoka kusoma chuo kimojawapo nchini Marekani, akaniuliza umetokea nchi gani nikamwambia Tanzania…
Mheshimiwa Naibu Spika, naona muda wangu umekwisha. Ahsante sna na naunga mkono hoja.