Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kidogo kwenye hii bajeti ya mapato na matumizi. Nianze kuanza kwa kukushukuru wewe binafsi na kukupongeza kwa kuendelea kukalia hicho Kiti, usiwe na wasiwasi wewe tulia kama jina lako linavyosema, sisi tuko pamoja na wewe kuhakikisha kwamba mambo yanaenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee nimpongeze Waziri wa Fedha na Naibu Waziri wake kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Bajeti yao iliyoletwa inaonyesha weledi na umahiri mkubwa wa kazi ambayo wamepewa na Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, inaonyesha kazi hii wanaweza wakaimudu vizuri na watatusaidia kuhakikisha kwamba uchumi wetu unakua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia kidogo kwenye upande wa huduma ya maji. Tumesikia Wabunge wengi wamesema sana hapa kuhusu suala la maji na wametoa mapendekezo mengi sana, tunaomba jambo hili tulitilie mkazo sana na tulifanyie kazi. Wabunge wapendekeza kwamba tuwe na tozo ya Sh.50 ili kwenye shilingi bilioni 125 basi ziongezeke zifikie shilingi bilioni 250 ili wananchi wetu wengi ambao wanaishi huko vijijini waweze kupata maji, tatizo liko wapi? Kama sisi ndiyo tunaopanga na tunawashauri kwa nini tusiongeze hizi Sh.50 kwa lita ya mafuta ili wananchi wengi wanaoishi vijijini waweze kupata maji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vijijini kule sasa hivi tunawahamasisha wajenge vyoo vya kisasa lakini vijiji vingi havina maji. Hata ukiangalia kwenye bajeti ya maji, miradi mingi ya maji mikubwa mikubwa imeelekezwa mijini na hata fedha iliyotengwa kwa maana ya maji vijijini bado zinaelekezwa mijini. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kutoa majumuisho tunataka kujua ni nini amefanya hasa kuhakikisha tozo ya Sh.50 kwa kila lita moja ya mafuta inaongezeka na kuwa Sh.100 na hatimaye tuweze kuongeza usambazaji wa maji vijijini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kidogo kwenye kilimo, niipongeze Serikali kwa kuondoa kodi hasa kwenye mazao ya matunda na mboga mboga kwa maana ya mazao yale ambayo hayajafanyiwa processing, niwapongeze sana. Pia niipongeze Serikali kwa kupunguza kodi kwa baadhi ya mazao ya biashara kama vile chai, kahawa, korosho na mazao mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba pamoja na kupunguza kodi kidogo bado tusipokuwa makini tutafanya Watanzania wabaki kwa kutokuwa na uwezo wa kulima kwa kiasi kikubwa na kuweza kuzalisha kiasi ambacho kitatutosha kulisha hivi viwanda vyetu ambavyo tunaanza. Ni lazima tuhakikishe kwamba hawa wananchi wanawezeshwa ili kuzalisha kwa kiasi cha kutosha, kingi zaidi na kuzalisha matunda ambayo yanakuwa ni bora ili yaweze kupata soko, waweze kupata kuuza kwenye hivi viwanda ambavyo tunatarajia vitakuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutawezaje kufanya hivyo? Ni lazima tuwawezeshe kwa kuwapelekea Maafisa Ugani. Vijiji vingi sasa hivi havina Maafisa Ugani, wananchi wanalima kilimo kile kile cha utamaduni bila kuzingatia kanuni bora za kilimo. Kwa hiyo, tuombe Wizara husika kwa pamoja tupeleke Maafisa Ugani wa kutosha ili waboreshe kilimo vijijini na hatimaye waweze kupata faida kwenye mazao yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nijaribu kuchangia kwenye upande wa elimu. Ni kweli Serikali imepeleka fedha nyingi, tumeona ina mpango wa kupeleka trilioni 4.77 ambayo ni sawasawa na asilimia 22.1. Fedha hizi ili ziweze kufanya kazi ambayo imekusudiwa. Ni muhimu sana hizi fedha zipelekwe kwenye maeneo haya ya shule kwa wakati. La sivyo fedha hizi hazitafanya yale malengo ambayo yamekusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumejifunza miaka ya nyuma, fedha zimekuwa zikitengwa kwa ajili ya kuendeshea mashule, lakini zinakwenda kwa kuchelewa, zinaenda miezi ya Tano na Sita; na inapofika tarehe 30 wale Wakurugenzi na Wakuu wa Shule wanatakiwa kurejesha hizi fedha tena Hazina, zinarudi tena bila kufanya kazi. Kwa hiyo, niombe mamlaka husika zipeleke hizi fedha kwa wakati ili zifanye kazi ambazo zimekusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongee kidogo pia kwenye suala la afya. Ni kweli, nitoe pongezi kwa Serikali, tumetenga trilioni 1.99 ambayo ni sawasawa na asilimia 9.2 ya bajeti nzima na hizo fedha tumesema zinaenda kwa ajili ya vifaa tiba, vitendanishi (reagents) na miundombinu, kwa hiyo, tuombe hizi fedha ziende kwenye vituo vya afya vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wengi wanategemea sana hivi vituo vya afya, kwa hiyo ni muhimu sana kuviboresha ili kuhakikisha kwamba angalau vituo vyote vya afya vinatoa huduma ya upasuaji pamoja na huduma kwa akinamama. Tunasema wanawake na watoto wengi wanafariki, ni kwa sababu huduma za afya hasa vijijini hazijaboreshwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia statistics wanaokufa wengi ni wale watu wa vijijini, ni kwa sababu wanakwenda hospitalini kwanza kwa kuchelewa kutokana na kutembea umbali mrefu, wakifika hakuna huduma nzuri, wanatakiwa wasafiri au wasafirishwe kwenda kwenye Hospitali za Wilaya ambazo zipo mbali. Wanafika huko wakiwa wamechelewa, hatimaye watoto wao wanafariki au wanapata operation na mwisho wa siku wanapata matatizo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nisemee kidogo kuhusu hii sheria ya magari, kwa maana ya kodi ya usafiri na uhamisho wa umiliki, ambayo ipo Sura namba 124, hasa kwenye upande wa pikipiki. Katika Ilani yetu tulisema tunataka hawa bodaboda sasa kwa hizi kazi wanazozifanya za kusafirisha, ziwe ni kazi rasmi. Nilitegemea kwamba leo hii tungekuwa tunaongelea kupunguza kodi za pikipiki, kwa kuwa hizi pikipiki nyingi wanazozitumia ni zile ambazo wamekodishwa na matajiri. Sasa tunataka hawa waendesha bodaboda waendelee kubaki maskini? Waendelee kuwasaidia watu wengine wenye fedha?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba hili ongezeko la kodi kutoka sh. 45/= mpaka 95/= liondolewe ibaki ile ile na ikiwezekana ipunguzwe zaidi ili vijana wetu ambao huko nyuma walikuwa wanafanya kazi za wizi, utapeli na kupiga watu nondo wajiajiri kwenye uendeshaji wa boda boda. Kwa kuwa boda boda zimesaidia kutafuta ajira kwa hawa vijana wetu, basi tupunguze kodi za pikipiki ili nao waweze kununua pikipiki na hatimaye wakapata fedha kwa ajili ya kuendeshea familia zao na maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wamesema pia juu ya kodi ya mitumba. Hakuna mtu ambaye hatambui, wote hapa ni Watanzania na wengi wetu tunatoka vijijini, wananchi wengi wanaoishi vijijini ndizo nguo wanazozitegemea. Mwananchi wa kijijini hutegemei akaenda kununua nguo dukani, anategemea mwisho wa mwezi aende kwenye mitumba apate nguo za kuweza kujisitiri, sasa sisi tunaongeza kodi. Ni vizuri tufanye kwanza utafiti, au wakati huu ambao tunataka kupeleka viwanda vya uzalishaji wa nguo basi kodi ziwe za chini, ili wananchi wengi waishio vijijini waweze kumudu kununua nguo. La sivyo wananchi wetu vijijini watashindwa kununua hata nguo tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. Ahsante sana.