Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia katika Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje. Kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Waziri Kivuli kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, mimi naomba nizamie katika diplomasia ya kiuchumi. Naona nchi yetu tumeongelea hili tangu 2001 mpaka leo na inaelekea hata Mabalozi wetu hawajui katika diplomasia kiuchumi wanatakiwa wafanye nini. Tunaongea juu juu tu hatuzamii kusema diplomasia ya kiuchumi maana yake ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Waziri ni mwanadiplomasia sana lakini nasikitika kusema hotuba yake yote au sehemu kubwa imeenda katika mambo ya kisiasa kwa maana na diplomasia ya kiisiasa. Kwanza tuanzie karibu hapa nyumbani katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, inasikitisha sana kuona Wabunge wetu wa Afrika Mashariki hawajui wanaripoti kwa nani au wako chini ya nani? Je wako chini ya Bunge hili au wako chini ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi hawana hata ofisi. Sasa unampaje mtu jukumu kubwa kuitwa Mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini hana hata Ofisi nyumbani kwake. Nchi ndogo kama Burundi wana ofisi za Wabunge wao wa Afrika Mashariki hata Rwanda na Kenya lakini Tanzania hatuna. Hii inaonesha jinsi Tanzania ambavyo tunachukulia mambo yetu kwa urahisi rahisi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hebu tuangalie, angalia shilingi yetu ya Tanzania na shilingi ya Kenya. Mpaka jana shilingi yetu ishirini na mbili ya Tanzania ndiyo unapata shilingi moja ya Kenya. Hivi wenzetu wametuzidi nini na tunazungumzia diplomasia ya kiuchumi. Mabalozi wetu wa East Africa wanajifunza nini au wanatuambia kwa nini wenzetu Kenya wanapiga hatua? Wakenya wako mbali sana angalia supermarket tu hata iliyoko Dar es Salaam, Mkenya ndiyo anaiendesha hata Kenya Commercial Bank, Tanzania Kenya tuna nini, Uganda tuna nini na Rwanda tuna nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ninachoshangaa kama tunazungumzia mambo ya diplomasia kiuchumi, nakumbuka Awamu ya Pili kule Saudia walieleza kwamba wanataka mbuzi wengi kwa vile watu wakienda Hija wanatumia sana nyama ya mbuzi. Watu wakaja hapa (Waarabu), Ubalozi wetu sijui ulifanya kazi yoyote kufuatilia suala lile lakini foreign officers wakapigapiga ikaishia hapo. Sasa hivi wenzetu wa Comoro ndiyo wanapeleka Uarabuni ng‟ombe na mbuzi kutoka Tanzania. Tunaongelea diplomasia ya kiuchumi, uko wapi uchumi wetu tunaouzungumzia hapa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie wawekezaji, wanakuja wawekezaji sijui Foreign Ministry yetu inasaidiaje kuonyesha hawa wawekezaji kule kwao wana uwezo kiasi gani ili waweze kutushauri kwamba hao muwakubali kama wawekezaji au msiwakubali? Unakuta wawekezaji wengine wanakuja kukopa kwenye benki zetu hizi hizi, halafu unaambiwa ni mwekezaji huyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi angalieni migodi yetu wageni kutoka nje wametawala migodi yetu Watanzania tunabakia kufanya kazi za vibarua. Wizara yetu ingeshauri kwamba hawa wawekezaji labda tuwape position moja, mbili hizi nyingine zote zibanwe na Watanzania. Watanzania mali yetu (contribution) yetu iwe ardhi yetu na wale wawekezaji waje na hela ili tuwe equal partners. Leo tunaongelea uchumi wa kidiplomasia lakini migodi yetu watu wetu ni kupigwa risasi kila siku na wageni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, angalieni hoteli zetu mfano Hoteli ya Serena na iliyokuwa inaitwa Kilimanjaro sijui sasa hivi imeshabadilishwa jina au bado.
Haya Hyatt. Hawa wenzetu wanapewa grace period kwamba msilipe kodi muangalie kwanza biashara, miaka mitano wakimaliza wanabadilisha jina leo Sheraton, kesho Serena sijui keshokutwa wataitwa nani? Tumekaa kimya, hiyo diplomasia kweli ya uchumi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie wawekezaji wanapewa umiliki wa mashamba kwa muda wa miaka 99, mwananchi sisi mpaka na watoto wetu hamna atakayekaa kushuhudia mkataba umeisha, tunawapa wawekezaji. Huko nchi za nje, je, kuna Mtanzania anakwenda apewe ardhi miaka 99? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshangaa kwamba tumejivunia tunaletewa msaada wa pikipiki na Wachina, jamani juzi sijui miaka kumi iliyopita tuliletewa baiskeli wanakuja ku-assemble pikipiki kiwanda chetu cha jeshi pale Nyumbu ambacho kilikuwa kinatengeneza magari pale Kibaha, kingeombewa hela wangekuwa mbali siye tunarudi kwenye pikipiki. Pikipiki zitabeba mizigo gani, ndiyo diplomasia ya uwekezaji huo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu vyuo vya ufundi, tumeenda kuomba hela, wakati nafanya Danish Embassy tulitengeneza Chuo cha Chang‟ombe na Dodoma kwa grant leo tunaenda kuomba mikopo kurudi tena kutafuta technical assistance kutoka nje. Tunajivunia Italia wanatusaidia, hivi Engineers wetu wote kutoka chuo kikuu kutoka iliyokuwa technical college wameshindwa kusaidia kutengeneza VETA kweli mpaka twende tukaombe huko Italia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba USD milioni 55 kujenga maghala, maghala mangapi tunayo yamewekwa uchafu hayawekwi hata mazao? Leo tunaomba USD milioni 55 msaada wa kujenga maghala, hivi kweli hata kujenga maghala jamani tushindwe nchi hii? Wenzetu wanatengeneza ndege wako mbali sisi bado tunatafuta msaada wa kujenga maghala? Hii diplomasia ya kwamba tuna marafiki siyo urafiki siye ni ombaomba, hakuna urafiki na ombaomba. Ukiwa na rafiki kila siku yuko mlangoni kwako anaomba utasema huyo ni rafiki yangu siyo rafiki. Tumekuwa nchi ya ombaomba hata vile vitu tunavyoweza kutengeneza wenyewe, inatuaibisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante