Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa mara ya kwanza kuongea katika Bunge hili la Kumi na Moja, nilikuwa Mbunge wa Viti Maalum kwa miaka mitano. Kwa kutambua kwamba wanawake tunaweza bila kuwezeshwa, nikaenda kugombea Jimbo la Mlimba, na wananchi wa Mlimba bila kujali itikadi zao walinipa kura za kutosha na sasa ni Mbunge wa Jimbo jipya la Mlimba ndani ya Wilaya Kilombero Mkoa wa Morogoro. Kwa hiyo, nawashukuru sana wananchi wote wa Jimbo la Mlimba Mabibi na Mabwana na Wachungaji na Mashekhe waliokuwa wananiombea bila kujali itikadi yangu, bila kujali dini yangu, na jinsia yangu, nasema ahsanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa mara ya kwanza nachangia nikiwa Mbunge wa Jimbo kwenye haya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa. Naomba nijikite kwenye mambo kadhaa, ambayo nikijikita nayo, nikizungumza hapa nitakuwa nawasemea na wananchi wa Jimbo la Mlimba na Watanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu Mpango kwa sasa umekuja kama mapendekezo na natarajia haya ninayoongea hapa na Wabunge wengine wanayoyaongea, basi katika mpango kamili unaokuja basi kutakuwa na vionjo ambavyo sisi kama Wabunge tumetoa mapendekezo yetu na mpango wakauchukua ili kwenda kupatikana kwenye hiyo bajeti inayokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la Utawala Bora; Hivi ninavyokuambia Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero haijaapisha Madiwani wake, hivi ninavyokuambia Halmashauri zingine zote zimeshaanza kukaa na kuangalia bajeti ili waingize kwenye Bajeti Kuu, Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero haijawahi kufanya kikao chochote, Madiwani hawajaapishwa, uchaguzi haujafanyika, eti kwa sababu tu kwa kazi tuliyofanya ndani ya Wilaya Kilombero CHADEMA, UKAWA tumepata Madiwani wengi na Wabunge wote tumebeba, sasa ni kigugumizi Serikali ya Chama cha Mapinduzi, inashindwa kupitia Waziri wa TAMISEMI anashindwa kuruhusu wananchi wa Kilombero wapate Wawakilishi wao. Ni kilio, ni kizungumkuti, hapa hamna utawala bora bali kuna wizi, utapeli, uliokithiri kipimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo maendeleo ya Wilaya ya Kilombero yatarudi chini, Wilaya ya Kilombero yenye Majimbo mawili, Jimbo la Mlimba na Jimbo la Kilombero, leo Mbunge Peter Lijualikali, Mbunge wa Kilombero, Waziri wa TAMISEMI ameandika barua, eti asiwe mpigakura ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, shame! Hiyo haikubaliki. Sasa, katika utawala bora nataka mtuambie, Wilaya ya Kilombero mnatuweka wapi, tuko Tanzania au tuko nje ya Tanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii bajeti inayokuja ya Wilaya ya Kilombero itaidhinishwa na nani ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero? Naomba majibu ya Serikali maana hapa hamna utawala bora. Hili ni jambo kubwa sana kama ulikuwa hulijui ni aibu kwa Taifa hili, ni aibu Serikali kujisifu kwamba ina utawala bora lakini kuna ukandamizaji uliopitiliza, wanatutolea Wabunge wa Viti Maalum kutoka Dodoma eti waende wakaape Kilombero, wanaijua wao Kilombero? Matatizo ya Kilombero tunayajua sisi hawezi kujua mtu mwingine. Kilombero hatuna barabara, Kilombero kuna migogoro ya ardhi, Kilombero hakuna maji, Kilombero pamoja tunazalisha umeme kwenye vituo viwili, Kihansi na Kidatu, lakini vijiji vingi havina umeme. Mnatutaka nini wananchi wa Kilombero. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo halikubaliki, katika utawala bora naishia hapa ingawaje kuna mambo mengi, kwa sababu katika utawala bora na haki za binadamu, tulitakiwa tuwe na kituo cha Polisi Kilombero, lakini hakuna Kituo cha Polisi Wilaya ya Kilombero tangu uhuru. Wilaya ya Kilombero Askari wamejibana kwenye kituo cha Maliasili, hivi wakati wa mafuriko Askari wanaogelea kama bata pale, kwenye mpango nataka tujue ni namna gani Wilaya ya Kilombero, tutapata kituo cha Polisi, cha uhakika kilichojengwa na Serikali hii ili wananchi wapate huduma zao na haki zao. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mlimba ni kubwa lenye Kata 16, hakuna kituo cha Polisi, Askari wamejibana kwenye kituo kidogo kwenye ofisi za TAZARA. Mnatutaka nini wananachi sisi, mnatutaka ubaya kwa sababu gani, tumewakosea nini, lakini ukiachilia hiyo, pale pale hakuna Mahakama ya Mwanzo. Leo mahabusu wakipatikana ndani ya Jimbo la Mlimba wanawekwa Idete, haki za binadamu zinavunjwa hata miaka miwili, kwa sababu hawana usafiri wa kuwapeleka Mahakamani, hawana Mahakama ya Mwanzo, huu utawala bora na haki za binadamu ziko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango u-reflect ni namna gani mtatuboreshea katika utawala bora ndani ya Wilaya ya Kilombero na Jimbo la Mlimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi oevu, utawala bora uko wapi? Leo ninavyoongea kuna kesi Namba 161 ya mwaka 2012, wananchi, wakulima na wafugaji wameipeleka Serikali Mahakamani, hasa Wizara ya Maliasili na Mahakama Kuu ikatoa order kwamba wale wananchi wasibughudhiwe kwenye lile eneo la oevu kwa sababu, walivyoweka mipaka kule hawakuwashirikisha wadau na Wizara ilikubali inakwenda kurekebisha mipaka, tangu mwaka 2012 mpaka leo! Leo wananchi wanashindwa kulima kule! Hii njaa itaingia mwaka huu! Watu wanapigwa, wafugaji wanachukuliwa pesa zao! Hawapewi risiti, nimelalamika, nimekwenda kwa Waziri Mkuu, nimekwenda kwa Waziri wa Maliasili, Mkurugenzi wa Wanyamapori, hivi ninyi mnatutaka nini sisi? Kwa nini mnatuonea namna hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Wasukuma wako kule wafugaji na makabila yote ukienda ndani ya Wilaya ya Kilombero Jimbo la Mlimba wapo kule, kuna uchakataji, utafutaji wa gesi, wananchi hawajui! Wanakuja tu na magari yao wanaondoka kwa nini msitoe taarifa kwa wananchi kwamba mnakwenda kuchakata kule kutafuta gesi na mafuta?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka Mpango utuambie ni namna gani tunaboresha masuala mbalimbali ndani ya Wilaya ya Kilombero, hususan Jimbo la Mlimba. Najua kuna mradi mkubwa wa upimaji ardhi, kama nilivyoongea na Mheshimiwa Lukuvi, lakini mradi huo pamoja unavyokuja sawa, Wilaya ya Kilombero na Ulanga, lakini hivi sasa wakulima wameshindwa kulima! Mnataka mwaka huu tukale wapi? Mnataka mtuletee chakula cha msaada sisi Mlimba, hatukubali! Aisee muda hautoshi! Mambo mengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara, balaa! Mnasema eti katika Mpango, Mheshimiwa Mpango naomba unisikie, mnasema tu reli ya kati, mmeisahau TAZARA? TAZARA mnaiboreshaje? TAZARA mnaifanyaje? Wafanyakazi hawalipwi! Reli shida! TAZARA mliijenga kwa gharama kubwa wakati wa Nyerere, leo mnaiua kwa sababu gani? Nataka Mpango u-reflect ni namna gani mtaboresha barabara, reli ya TAZARA, Mpango uzungumzie barabara ya kutoka Ifakara mpaka Mlimba, Mlimba mpaka Madeke-Njombe mtaiboreshaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ghala la chakula liko Jimbo la Mlimba. SAGCOT, kuna kilimo kikubwa cha mpunga pale KPL (Kilombero Planting Limited), malori yanapita pale yanye tani 30 kila siku yamebeba mchele, barabara hamna! Leo kwenye Mpango hakuna hata ile barabara hamuizungumzii! Naomba mzungumzie hiyo barabara.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa!....
MWENYEKITI: Mheshimiwa Susan Kiwanga, Taarifa hiyo unaikubali au vipi?
MHE. SUSAN L. A. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa siikubali.
MWENYEKITI: Haya, malizia dakika yako moja!
MHE. SUSAN L. A. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nimpe tafsiri kwamba, shame, maana yake aibuuu! Kwa Taifaaa! Hiyo ndiyo habari ya sasa. Halafu wewe tuna wasiwasi na uraia wako!
Mheshimiwa Mwenyekiti, linda dakika zangu. (Makofi/Kicheko)
MWENYEKITI: Ulikuwa na dakika moja tu.
MHE. SUSAN L. A. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mpango uzungumzie kuhusu barabara ya kutoka Ifakara – Mlimba, Mlimba mpaka Madege, Njombe, hili ni eneo ambalo lina uzalishaji mkubwa ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mpango uzungumzie masuala ya elimu; leo ninavyozungumza kuna shule moja ya Tanganyika mwaka uliopita hakufaulu hata mwanafunzi mmoja wa darasa la nne! Elimu kule siyo nzuri sana, nitawapa takwimu baadaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maji; pamoja na kuwa Wilaya ya Kilombero na Jimbo la Mlimba lina mito 38, ilikuwa mpaka 49 lakini maji hakuna! Naomba Wizara ya Maji ifanye mkakati, sisi hatuhitaji visima, mkaboreshe ile mito, ili tupate maji. Kama inatoa umeme kwa nini maji ya kunywa safi na salama tusipate?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba niwape vyanzo vya mapato, kimoja tu! Naomba mfanye pilot area Dar-es-Salaam kuna umeme, hebu hamasisheni mtu ukienda dukani leo mtu anakuhamasisha, nikupe risiti ya TRA au nikupe ya mkono? Hii hapa ina kodi, hii hapa haina kodi! Hivi ni nani Mtanzania leo atakubali yenye kodi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wekeni mfano mzuri kwa pilot area ambayo ina umeme kwamba, wale wote Watanzania na mtu yeyote atakayenunua kwa risiti ya umeme ile ya TRA, baada ya muda fulani, mwaka mmoja, mnampigia hesabu amelipa kodi kiasi gani halafu mnamrudishia kitu kidogo! Mtaona kama watu hawatadai hizo risiti madukani; hicho kitakuwa chanzo kikubwa cha kukusanya kodi ndani ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba kuwasilisha. (Makofi)