Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. RITA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara kwa kuwasilisha bajeti yao ili tuweze kuijadili. Yapo mambo ambayo napenda kutoa ushauri na pia kupatiwa ufafanuzi wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini mkakati wa Serikali katika kukuza na kutangaza utalii Kimkoa au Kikanda? Mkoa wetu wa Iringa ni kati ya mikoa ambayo ina vivutio vingi ambavyo kama Serikali ingekuwa na mkakati wa kutosha naamini mkoa wetu ungeweza kuiingizia Serikali pato kubwa sana na pia tungeweza kutengeneza ajira kwa vijana wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Iringa una mbuga ya Ruaha National Park, katika Afrika ni mbuga ya pili kwa ukubwa lakini miundombinu ya barabara ni mibovu sana na bado Serikali haijaweza kuona umuhimu wa kuweka barabara ya lami ili kuvutia watalii wengi kwenda katika mbuga hiyo. Bado Serikali haiwezi kuona umuhimu wa kujenga au kukarabati kiwanja cha ndege cha Nduli, ni vema sasa Serikali ingeweza kuzifanyia upembuzi yakinifu baadhi ya miradi kama ya barabra na viwanja vya ndege ambavyo ni changamoto katika kukuza utalii wa nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wetu eneo la Isimila Olduvai Gorge lingeweza kuongeza pato kubwa sana la utalii lakini halitangazwi na halina maboresho kabisa. Mkoa wetu una kaburi na fuvu la kichwa cha Mtwa Mkwawa, bado hakuna matangazo ya kutosha ili tupate utalii wa ndani na nje ya nchi ili tuongeze utalii na vijana wetu kupitia watalii watengeneze ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu TANAPA, shirika hili ni kati ya baadhi ya mashirika na taasisi za umma zinazofanya vizuri sana katika sekta hii ya utalii lakini ni tatizo gani linasababisha Serikali kutokuweka bodi? Mambo mengi na changamoto nyingi zinakosa maamuzi kutokana na shirika kukosa bodi. Ninaomba Mheshimiwa Waziri atakapojibu atoe ufafanuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fidia kwa wananchi wanaoliwa na mamba, kwa kuwa kumekuwa na vifo mara kwa mara kwa wananchi na hasa wanawake wamekuwa wakipata ajali wanapokwenda kufuata maji katika Mto Lukosi katika Wilaya ya Kilolo, Kata ya Ruaha Mbuyuni. Je, ni utaratibu gani unatakiwa kutumika ili wananchi waweze kupatiwa haki zao na je, ni kwa nini wasisaidiwe na Halmashauri kuvuta maji ya bomba katika Mto huo Lukosi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zinazojitokeza katika kutoa vibali vya uvunaji miti msitu wa Taifa wa Sao Hill, kumekuwa na malalamiko makubwa sana ya wananchi katika utoaji wa vibali vya kuvuna miti katika msitu wa Taifa wa Sao Hill. Ninaomba kujua utaratibu unaotumika na Serikali inatambua hilo? Je, ili kuondoa tatizo hilo nini mkakati wa Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wabunge tumekuwa tukiombwa kuchangia katika taasisi za elimu, afya na hata jamii, je, Serikali ina utaratibu gani wa kuwapatia vibali hivyo vya uvunaji ili kuweza kusaidia jamii na Serikali katika kupunguza changamoto ambazo huwa zinajitokeza wakati tukiwa kwenye ziara za kikazi katika Majimbo na Mikoa kwa ujumla? Ninaomba kupatiwa jibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.