Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Mawaziri na watendaji wa Wizara kwa maandalizi na kuwasilisha bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa ya Katavi katika Mkoa wa Katavi upande wa Kaskazini inapakana na Kijiji cha Sitalike lakini kwa mujibu wa mipaka sehemu ya kijiji ipo eneo la hifadhi. Hivyo, tunaomba mpaka urudishwe nyuma mpaka ng‟ambo ya Mto Katuma kwa kuwa wananchi hapo wanaishi tangu miaka ya 1990.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TANAPA inahitaji kuwa na ujirani mwema yaani tunaomba sehemu ya Mto Katuma iruhusiwe wananchi kuvuna samaki angalau eneo lenye urefu wa kilometa tano ili kuwezesha wananchi kupata vitoweo na pia kuondoa ugomvi. Hivi karibuni vijana watatu walikamatwa eneo la mto na walipigwa sana na kuumizwa ambapo hali zao siyo nzuri. Jambo hili lilipelekea wananchi kutaka kuchukua hatua zinazopelekea kuvunja amani kati ya watumishi na wafugaji. Kwa mantiki hiyo, tunaitaka Serikali itoe tamko la watumishi wa TANAPA kufuata taratibu, kanuni na sheria katika utendaji wao ili kuondoa hali ya kuvunja amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu promosheni ya hifadhi, kwa muda mrefu sana Serikali imekuwa ikitangaza sana baadhi ya hifadhi maarufu na kubwa hapa nchini bila kuhusisha pia hifadhi ambazo zinahitaji kutangazwa sana. Mfano mzuri ndege zetu zinabeba majina ya hifadhi kubwa. Tunahitaji Mbuga ya Katavi kuboreshwa na kutangazwa ili kupata watalii kwa kuwa uwanja wa ndege upo. Vilevile miundombinu na huduma nyingine ziboreshewe zaidi kama zilivyo sehemu nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujangili, Serikali imekuwa na juhudi kubwa zaidi kupambana na ujangili lakini uhalifu huo bado unaendelea. Tunahitaji Serikali iboreshe mbinu za kukabiliana na wahalifu. Watumishi wa TANAPA wameonekana kuhusika, hivyo utaratibu wa kuwahamisha utumike na kuwafuatilia mienendo yao. Pia Serikali lazima ifuatilie taarifa zinazotolewa na vyombo vingine vya usalama. Vilevile maeneo yanayozunguka Hifadhi za Taifa yawe yanachunguzwa mara kwa mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi ya misitu na pori la akiba. Nchi yetu imekuwa na ongezeko la watu kila mwaka, vilevile nchi yetu ilipokea wakimbizi kutoka jirani za Burundi, Rwanda na Congo DRC hivyo kuhitaji maeneo. Vilevile baadhi ya maeneo ya nchi yamekuwa na ufinyu wa maeneo yenye rutuba na nyasi za kulisha mifugo na wafugaji na wakulima kuhamia maeneo mengine. Athari zilizotokea ni uvamizi wa maeneo ya hifadhi za misitu na mapori ya akiba. Vilevile migogoro imekuwa mingi. Pia tatizo la zana za kilimo imepelekea watu kutafuta maeneo mapya ya kulima. Athari imekuwa wananchi kuchomeana nyumba na kufyeka mazao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na athari hizo tunaishauri Serikali iongeze kusimamia sheria husika kuanzia ngazi ya kijiji mpaka Taifa kwa kuwa rushwa imekuwa tatizo. Pili, ufugaji bora kwa kulima nyasi zinazokaa muda mrefu. Serikali ipange matumizi bora ya ardhi kwa kutoa fedha za kupima maeneo. Serikali ipunguze maeneo ya hifadhi ambayo tayari yamevamiwa muda mrefu, zaidi ya miaka 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la vitalu vya uwindaji, kwa kupitia utaratibu wa sheria, wahitaji au kampuni zinaomba na kupata leseni za uwindaji kwa mfumo wa vitalu lakini tatizo lililopo ni taarifa kamili za mapato na uvunaji unaofanywa na kampuni zenye leseni. Hivyo, kuna umuhimu wa Serikali kuangalia upya mfumo wa vitalu kwa takwimu za kifedha na idadi ya wanyama. Vilevile vitalu vifanyiwe uchunguzi katika kudhibiti ujangili wa nyara za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tozo za misitu; Wizara imekuwa na tozo mbalimbali za mazao ya misitu lakini tozo kwenye mbao ni kubwa. Vilevile wachimbaji wadogo wa madini wanatozwa ada kubwa kwa hekta moja shilingi 1,400,000 ambayo haiendani na ukubwa na uharibifu. Hivyo tunaomba Serikali tozo ziendane na miti inayokatwa katika eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Memorandum of Understanding, Serikali ya Tanzania mwaka 2015 ilisaini mkataba kudhibiti biashara ya magendo kati ya Tanzania na Kenya na kuokoa fedha nyingi. Hivyo tunaomba Serikali iangalie upya MoU na nchi nyingine pia hata za mbali ili kuokoa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.