Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Kemirembe Rose Julius Lwota

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. KEMIREMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii ya kwanza ya Serikali hii ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kuipongeza Serikali kwa jitihada na uthubutu iliyoweza kufanya na kutenga asilimia 40 ya fedha za bajeti yote kwenda kwenye mfuko wa maendeleo. Fedha hizi zilizotengwa za kwenda kwenye mfuko wa maendeleo ni nyingi na ni mara ya kwanza, haijawahi kutengwa fedha nyingi kiasi hicho kwenda kwenye mfuko huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni jukumu na rai yangu kwa Watanzania wote kum-support Mheshimwa Rais kwa kukusanya mapato, kuyatunza na kuyatumikia vyema haya mapato yetu ambayo tutakuwa tumeyapata ili tuweze kufikia dhamira yetu ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, maendeleo ni ya Watanzania wote kwa ujumla, hayachagui Chama wala itikadi. Kwa hiyo, ni rai yangu kwamba wote tuwe kitu kimoja ili haya mambo tuweze kuyafanikisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie kwenye suala la utalii, wenzangu wengi wamelizungumzia hili suala nami naomba nilichangie. Suala la kuongeza kodi kwenye utalii ni janga la kitaifa na Waheshimiwa Wabunge tukiliunga mkono hili tunavunja kabisa utalii wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kodi inayowekwa kwenye utalii ukilinganisha na nchi nyingine za jirani kwa mfano Kenya ambao ndio competitives wetu wakubwa kwenye masuala ya utalii, bajeti yao ya mwaka huu peke yake wametenga fedha za Kenya zaidi ya bilioni 4.5 ambayo ni sawa na shilingi bilioni 90 za Kitanzania, kwenye utalii pekee. Sisi bajeti yetu ni takribani bilioni 135, kwenye Utalii na Maliasili. Kwa hiyo, bado changamoto ni kubwa sana kwenye suala hili la utalii kwa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la utalii tumeweka kwenye mpango wetu wa mwaka huu kwamba tunaweka target ya kufikisha watalii 2,000,000 kwa mwaka. Watalii hawa kwa vigezo hivi vinavyowekwa vya kuongeza kodi, dhamira hii ya kufikisha watalii 2,000,000 itakuwa ni ndoto, haitawezekana. Watalii hawa hawatakuja kwa sababu ya ongezeko la kodi kwenye utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiachilia hapo, Tanzania, ni moja ya one of the expensive destination in East Africa kwa utalii. Kwa hiyo, kwa kuongeza hili, tunafanya gharama ziwe maradufu kwa sababu ya kodi hizi. Vile vile katika suala la utalii siyo kitu cha kujaribisha; tumetumia muda mwingi na gharama kubwa kuweza kufikisha watalii ambao tuko nao sasa hivi. Mwaka 2016 tumekuwa na watalii zaidi ya milioni 1.1 na target yetu kama nilivyosema ya 2,000,000 tukishaanza kuweka haya mambo ya kodi tutafanya watalii wetu wakimbie na wasije tena Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nataka kuongelea suala la kilimo. Kuna changamoto nyingi sana kwenye kilimo na napenda kuipongeza Serikali kwa kuweza kutoa kodi kwenye mazao ya kilimo, kwa mfano, maharage ya soya na mbogamboga. Ili kukamilisha sera ya viwanda ambapo tunataka uchumi wetu uwe wa viwanda, asilimia 65 ya kilimo inategemewa kwenye kuendeleza viwanda vyetu nchini. Kwa sababu hizo, kwenye bajeti nzima hakuna sehemu yoyote ambayo inaongelea investment kwenye kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kitabu cha Mpango wa Bajeti 2016, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, amezungumzia suala la kilimo cha umwagiliaji, lakini kwenye bajeti halisi ya mwaka huu hakuna fedha yoyote ambayo imetengwa kwenye kilimo cha umwagiliaji. Tukitaka kuendeleza kilimo chetu, hatuwezi kutegemea kwenye kilimo cha msimu wa mvua peke yake, inabidi ifike mahali tuwekeze kwenye kilimo cha umwagiliaji kama tunataka kufanikisha Serikali ya viwanda na kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tatizo kubwa sana la kilimo cha umwagiliaji. Asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima na asilimia 23 ya pato la Serikali linatokana na kilimo, lakini hakuna investment yoyote ambayo imefanyika hapa pamoja na kwamba kuna maelezo tu ya kusema umwagiliaji utafanyika, lakini hamna suala lolote ambalo linazungumzia umwagiliaji. Umwagiliaji ni asilimia 10 tu ya hawa wakulima wote zaidi ya asilimia 70. Kwa hiyo, inabidi tujikite zaidi kwenye miundombinu na kuwawezesha wakulima waweze kulima kwa kilimo cha kisasa cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la kuondoa kodi kwenye mazao ya maharage na mbogomboga; misamaha hii inalenga usalama wa chakula na siyo zaidi ya hapo. Misamaha hii ingeweza kusaidia na kuwa na tija kwenye uchumi wetu kama tungewekeza kwenye viwanda vidogo vidogo vya usindikaji. Tungewapa wasindikaji wa mbogamboga hizi na maharage waweze kufungua viwanda vidogo vidogo ambavyo vingeweza kusaidia kwenye ajira na vile vile kuongeza thamani ya mazao yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza uamuzi wa kuinua viwanda vidogo vidogo na usindikaji wa mazao ya mbogamboga kwa kutangaza misamaha ya kodi na ongezeko la thamani kwenye bidhaa zitokanazo na usindikwaji na ukuaji wa viwanda vidogo vidogo.
Vile vile, napenda kuipongeza Serikali kwa juhudi zake na kuweza kutenga fedha za kutengeneza reli ya kati ambayo imekuwa ni mazungumzo ya muda mrefu; wananchi wa Mkoa wa Mwanza wamekaa na wamesafiri na mabehewa haya ambayo yamekuwa mabovu kwa muda mrefu. Natoa pongezi sana kwa Serikali kwa kuamua kulifanya hilo na kununua meli ya Ziwa Victoria ambayo pia itaweza kusaidia wananchi wa Tanzania hasa ukanda wa Ziwa, Mwanza pamoja na Kagera. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna hili suala la CAG kuongezewa fedha. Suala hili limezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wengi na naomba kutia msisitizo, suala la CAG kukatiwa fedha na fedha nyingi kupelekwa TAKUKURU, sidhani kama ni sawa, kwa sababu bila kuwepo huyu CAG, TAKUKURU hawatakuwa na kazi ya kufanya. Mambo mengi yanaibuliwa huko kwa CAG na baada ya hapo ndipo TAKUKURU wanaweza kupata mashiko na meno ya kufanya kazi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba hili suala liangaliwe na fedha kama inawezekana iongezwe kwa CAG ili aweze kufanya mahesabu yake na ukaguzi wake na kutuletea ripoti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.