Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nilishakupongeza sana, nilishasema sana kuhusu sifa zako, leo sirudii, lakini pia kabla ya kuendelea niwasaidie Waheshimiwa Wabunge wanaom-judge Mheshimiwa Mlinga haraka haraka. Wakati wa kipindi cha vitendawili, Mwalimu aliwauliza wanafunzi, haya vitendawili; mmoja akasema mimi. Akamwambia, Mariam, sema. Akasema, nivue nguo nikupe utamu. Mwalimu akaja juu sana, kaa chini wewe, tabia yako mbaya, lakini basi haya toa jibu, akasema ndizi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napata tabu watu ambao hawamwelewi Mheshimiwa Mlinga. Naomba wamwelewe Mheshimiwa Mlinga, dogo yule kama alivyo Mheshimiwa Mlinga ana mambo mengi ya kusema, lakini tumwelewe. Mwalimu yule alijielekeza kubaya, aliposema mwanafunzi nivue nguo nikupe utamu, akamtukana, lakini baadaye akasema toa jibu akasema ndizi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo sasa nije kwenye mjadala huu wa hoja ambayo iko mezani kwetu. Kwanza nifafanue mambo mawili, matatu ambayo wananchi na pia Wabunge hawa wanataka kujua, nayo ni mimi kwenda Geneva mwaka huu nikipeleka kijiti cha Uongozi wa Bara la Afrika, Urais; na kama mnavyojua, Tanzania ilikuwa Rais wa Waajiri Afrika kwa muda wa miaka miwili na mwaka huu tulikuwa tumemaliza, lakini tulipofika kule Geneva, wenzetu ambao walitakiwa kupokea kijiti hicho DRC Congo wakasema hawakuwa tayari kwa hiyo, Mkutano Mkuu wa Waajiri Afrika ulimteua tena Mtanzania wa nchi ya Tanzania. Mtanzania huyo ni Mbunge mwenzenu, aendelee kuwa Rais wa Waajiri Bara la Afrika. Nawashukuru sana na Mtanzania huyo ni Almasi Maige, Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye bajeti ambayo tunaiongelea leo. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, wamesema mambo mengi katika bajeti yao hii waliyoipendekeza katika mwaka huu wa 2016/2017. Nami nawapongeza kwenye maeneo ambayo yananihusu sana; maeneo ya Pay As You Earn, kupunguzwa kutoka ile 11% mpaka single digit ya 9%. Pia, niwashukuru kwa kupunguza SDL kutoka 5% mpaka 4.5%. Nafikiri Serikali ingeenda mbele zaidi, ingetupa 1% na mwelekeo wa kuteremka uendelee kwa kupanua wigo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliwaambia yako makampuni mengi hayalipi kodi na biashara ambazo siyo rasmi zingelipa kodi, mngepunguza asilimia hizi za kutuwezesha sisi waajiri na hasa wawekezaji waweze kuwa na mazingira safi, mazingira bora ya kuanzisha biashara hapa nchini kwa kupunguza SDL. Bado SDL hii ya 4.5% ni kubwa kuliko zote duniani, inayofuatia ni 1.2%. Sasa katika ushindani wa kibiashara Payroll ni moja ya cost za mwajiri anapopiga hesabu zake na anapolipa kodi. Kwa hiyo, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa 0.5 waliyotupa, lakini tulitegemea wangetupa at least 1% na wakusanye kodi kutoka katika maeneo mengine kufidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, niongelee sasa mambo ambayo ni mtambuka. Bajeti hii inaongelea kununua ndege tatu za ATCL; Shirika la Ndege Tanzania. Mimi nasafiri sana, nimesafiri na ATC kabla haijafa mpaka nikaacha kwa sababu mimi ni mzalendo na baadaye nikapanda ndege hizi za mashirika mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania haiko tayari kuendesha Shirika la Ndege yenyewe. Ningefurahi sana kama wangesema sisi tununue ndege tatu tutafute na mbia mwingine naye anunue ndege tatu au hata ndege tano, tufanye ubia, lakini anayekuja awe na taaluma na uwezo wa kuendesha biashara ya abiria wa ndege au mashirika ya ndege. Sisi wenyewe hizi ndege, wanasena Wanyamwezi “zitahomba,” zitalala pia! Hatuwezi kuendesha shirika la ndege sisi wenyewe. Tiketi nyingi watu walikuwa wame-book wakati ule shirika la ndege, wameandika majina yao, watu wamejua ndege imejaa, inaenda na watu nusu. Wameyafuta wapi hayo?
Mheshimiwa Naibu Spika, ndege yetu imekwenda ikapasuka matairi kule Zimbabwe haikuridi tena, matairi ya spare hakuna. Mafuta tumekopa, madeni mpaka leo hatujalipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, iko haja ya ku-call spade a spade! Koleo, koleo! Ninavyoamini, Shirika la Ndege la Tanzania haiwezekani tukaendesha Watanzania peke yetu. Kwa hiyo, bajeti hii ingekuja na sisi tukanunua ndege tatu, lakini vilevile tuwe na mpango wa kupata wenzetu wa kutuunga mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nimekuwa naliongelea sana ni Sheria ya Manunuzi. Namwamini sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango kwamba kabla ya kufunga Mkutano huu wa Tatu wa Bunge la 11, Sheria ya Manunuzi marekebisho yake yataletwa humu Bungeni, sina matatizo na hayo. Ni muhimu sana; asilimia kubwa ya bajeti hii ni manunuzi. Kama Sheria hii ya Manunuzi haikurekebishwa, tutapoteza hela nyingi hizi, badala ya kufanikisha, tutafeli kama ilivyokuwa miaka iliyopita. Nina imani Wabunge wengi humu ndani wanajua kwamba hii Sheria ya Manunuzi ni tatizo kubwa sana. Sijui kwa nini hailetwi humu ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia namwamini sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, atakuja sasa na utekelezaji wake wa yale mambo niliyoyalalamikia kuhusu Benki Kuu kwa sababu ushahidi nimeshampelekea.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni suala la maji. Kule kwangu Jimbo la Tabora Kaskazini, Uyui, hakuna maji chini. Sijui Mungu aliumba hivyo kuwa maji yapite tu mvua zikinyesha yanaenda kujaza Wembele na maeneo mengine ambayo yako chini; lakini Jimbo langu lote halina maji chini. Kwa hiyo, mpango wa kuchimba visima kuwapatia maji wananchi wa Tabora Kaskazini imeshindikana. Kwa hiyo, kipekee mradi ambao unawezekana ni wa kuchimba malambo ili yajae maji na wananchi watumie. Naomba katika bajeti hii, Mheshimiwa Waziri wa Fedha aangalie kutekeleza mawazo aliyoyatoa humu Bungeni kwamba Serikali itachimba malambo kama mradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia liko suala la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (Workers Compensation Fund). Mfuko huu malengo yake ni mazuri sana, lakini Mfuko huu malengo yake hayo yanagongana na mafao ya mifuko mingine. Kwa mfano, Mfuko ule wa NSSF unao pia fao la bima; lakini pia wako waajiri ambao wamewawekea bima wafanyakazi wao, nzuri sana ya Kimataifa. Hawa wafanyakazi watapoteza mafao mazuri haya ambayo waajiri wao wa makampuni ya kigeni na kadhalika wamewawekea. Kwa hiyo, tungependa Mfuko huu ujaribu kuongea na waajiri hawa ambao wana bima zao au ulinganishe mafao ya Mifuko mingine yasigongane ili kuleta harmonization ya Mifuko yote hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri Mfuko huu una mafao mazuri sana, lakini hauzidi baadhi ya mafao ambayo waajiri tumewawekea wafanyakazi wetu. Kwa kutekeleza mafao ya Mfuko huu, wafanyakazi watapoteza zaidi kuliko kupata. Hatuombi mtu apate ajali, lakini tumeweka mambo mazuri sana kwa wafanyakazi wetu, hasa makampuni haya ambayo yamewawekea bima.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.