Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Ahmed Mabukhut Shabiby

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gairo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami kuwa mmoja wa wachangiaji kwenye hotuba ya Wizara ya Fedha. Kwanza nitaanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, maana kwenye ukweli lazima tuseme ukweli. Mimi huwa sipongezaji sehemu ambazo naona zina matatizo, lakini kama sehemu ni ya ukweli, tutapongeza sehemu ya ukweli na tutasema ukweli. Nitampongeza kwenye kufuta misamaha ya maduka ya majeshi. Hapa nampongeza. Kwa nini nasema nampongeza?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wale ambao hawajatembelea haya maduka au hawajawahi kupitia haya maduka, wanaweza wakaona wamefanya kosa kubwa sana, lakini kama ulishawahi kwenda kwenye haya maduka ukajionea kinachofanyika pale, utagundua alichokifanya ni sahihi kabisa. Niwapeni mfano mmoja tu, hapa Dodoma kuna duka la Magereza, liko hapa Magereza na hata sasa hivi ukienda liko wazi muda wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia wanunuzi wa vile vitu, mtu yeyote pale ananunua kwa msamaha wa kodi na kibaya zaidi viwango vya vile vitu ni vibovu vilivyopindukia. Unaweza ukaenda ukapata kitu cha Sumsung, labda TV ya Sumsung lakini ukiingalia ile inafanya kazi miezi sita, imekufa. Kwa hiyo, siyo kuwasaidia wanajeshi au siyo kuwasaidia watu askari wetu, hapo ni kuwaumiza na kuzidi kuwalia fedha zao kwa kutumia exemption. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hilo, niko tofauti kidogo na baadhi ya wenzangu kwa sababu naona kwamba hilo ni tatizo, liwekewe utaratibu mzuri ambao utawanufaisha hawa askari wetu, nao wataridhika, ndiyo cha msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 64 anazungumzia kodi za magari na pikipiki. Mimi ni mfanyabiashara wa magari lakini leo sizungumzii habari yangu, nitazungumzia habari ya Watanzania. Amezungumzia usajili, sasa hapa hatujaelewa ni ule usajili wa mara moja, ukishasajili gari hulipii tena au ndiyo road licence?
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ni road licence, ukiangalia hapa kwenye pikipiki sh. 95,000/= kwa mwaka, hii ni pesa nyingi mno kwa mtu wa bodaboda. Kwa gari ni sh. 250,000/=, hiyo siyo shida. Kwa nini usiweke utaratibu mwingine? Ubadilishe utaratibu! Utaratibu huu ndiyo ule ambao ulileta matatizo miaka ya nyuma; na Bunge la nyuma watu walilalamika sana. Mabunge ya miaka iliyopita, TRA haiwezi ikaanza kufukuzana na watu wa bodaboda, hawana askari wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa Polisi wetu hawatoshi kufukuzana na watu wa bodaboda kisa hawajalipa hiyo sh. 95,000/=. Ibadilisheni system yake, iwekeni angalau katozo kadogo kwenye mafuta ili msiwe mnapata usumbufu wa kufukuzana na hawa watu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, pikipiki moja ikitumia lita saba tu kwa siku, kwa mwezi ina lita 210 kwa mwaka ina lita 2,520; kwa hiyo, ukimwekea shilingi kumi, atalipa 25,200/=. Ukienda kwenye magari kwa mfano, malori yanayokwenda nje na yanayotembea mikoani, kwa safari moja tu au tuseme kwa mwezi, weka kima cha chini, litatumia lita 4,800 pamoja hata na mabasi, kwa kima cha chini kabisa kwa mwezi. Ukiangalia kwa mwaka litatumia lita 57,600/=; ukiweka kwa shilingi kumi tu utakusanya sh. 576,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pamoja na kuwa bodaboda atakuwa amelipa kiasi kidogo cha pesa, lakini hawa wengine huku watakuwa wamefidia ile gharama na kufikia lengo la Serikali, kuliko kwenda kusukumana na hawa wafanyabiashara wadogo wadogo kufukuzana nao.
Nakumbuka mwaka juzi 2014 kilichotokea Morogoro, kutaka kuuana watu wa TRA na hawa watu wa bodaboda kwa ajili ya hayo mambo ya kufukuzana na watu wa bodaboda. Kamua ng‟ombe wako huku unamlisha majani, unamkamua polepole kuliko kwenda kufukuzana fukuzana huko. Wekeni tozo hii ya sh. 10/= tu kwenye mafuta imalize haya matatizo yote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, sasa hivi hakuna asiyejua nchi hii ukame wa pesa ulioko mitaani. Kuna ukame mbaya sana wa pesa huko mitaani, nani asiyefahamu? Kama mfanyabiashara mkubwa leo hii ataweza kwenda kukopa Standard Bank, City Bank, Stanbic, lakini je, hao walipa kodi mnaowatarajia kuwaongeza, watakopa wapi? Watakopa NMB, watakopa CRDB, watakopa NBC, watakopa TIB na ukiangalia hizi Benki zina asilimia ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii wanachukua pesa zote; pesa za bandari, Mashirika ya Umma, wanazipeleka zote BOT; mzunguko wa pesa utatoka wapi ili hao watu wadogo wakope? Ni sawasawa na binadamu unaitoa damu yote unaipeleka kwenye kichwa ikae huko huko isizunguke, haiwezekani hiyo! Huo ndiyo ukweli wenyewe. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mnaona mabenki yanafaidika, basi wapeni hizo pesa at least kwa interest, nao muwapangie interest kiasi cha kuwakopesha wafanyabiashara wadogo wadogo, lakini ukichukua pesa ukizipeleka BOT ambapo haina mzunguko wa aina yoyote kifedha, BOT Gairo haipo, BOT haipo Ngara, BOT haipo Sengerema, haipo Kaliua wala Kasulu, wanaenda kukusanya pesa zote wanaziweka. Wafanyabiashara nao wakiamua kukusanya pesa zao waweke kwenye madebe, kutakuwa na pesa nchi hii? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lazima tuangalie, wakizizuia pesa sehemu moja kama BOT, wanazuia mzunguko wa pesa kwenye hili Taifa, maana yake itafikia sasa wafanyabiashara nao watachukua pesa nao wataweka kwenye debe lake hapeleki Benki. Wa bajaji naye ataweka kwake, sasa mzunguko utatoka wapi? Hao watu wanaokopa shilingi milioni mbili, shilingi milioni 10, watakopa wapi? Maana mfanyabiashara mkubwa ataenda kwenye mabenki ya nje, atapata pesa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tujiangalie, kama tunaona mabenki yanafaidika, basi hizi pesa tuziwekee mpango mwingine angalau hata tuwape hawa mabenki kwa interest lakini siyo kuzizuia sehemu moja hizi pesa. Tukizuia huo mzunguko, pesa itakuwa shida nchi hii, nakwambieni ukweli kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hili suala la mafuta, nashukuru kwamba kuongeza mafuta kwenye mafuta ya nje ni jambo jema kwa asilimia 10, lakini aangalie na viwanda vya ndani toeni kodi ya VAT kwenye viwanda vya alizeti vya ndani ya nchi na viwanda vingine vya mafuta. Kwa sababu mpaka sasa hivi ukiona mafuta ya nje yako sh. 50,000/=, ujue ya alizeti itatofautiana sh. 2,000/= tu bei yake, kwa sababu bado kuna kodi. Kwa hiyo, bado hujamsaidia mkulima hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wakulima wadogo wadogo wote wana viwanda vyao vidogo vidogo; lakini katika vile viwanda vimetofautiana; yuko yule ambaye hajafikisha kodi ya shilingi milioni 100 ambaye haingii moja kwa moja kwenye VAT, anasaga alizeti na yuko yule wa kwenye shilingi milioni 20, 30 anasaga alizeti hiyo hiyo lakini hana VAT.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sasa usawa uko wapi? Usawa haupo. Ili upate usawa, viwanda vya ndani vyote vitolewe hiyo kadi ya VAT. Mimi sina kiwanda, lakini ukweli ndiyo huo; ili pale tuweze kupata hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu kwenye ngano pale, mmezungumzia ngano kutoka asilimia 35 kuja asilimia 10. Ahsante.