Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii kubwa, kunipa zawadi ya uhai ili nami nisimame leo kuchangia katika Bajeti ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamekupongeza kwa umahiri wako wa ufanyaji kazi, lakini nataka nifafanue kidogo. Kuna kipindi watu wanachanganya sana hizi mada. Wapinzani walipotaka kuelezea kutoridhishwa kwao na Naibu Spika, kwanza walianza kuzungumzia habari ya uteuzi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo Mbunge wa kwanza kuteuliwa na Rais wa nchi yetu. Katika Bunge lililopita Mheshimiwa James Mbatia alikuwa Mbunge wa kuteuliwa na Rais na hapo ndipo alipopatia na mtaji wa kugombea Ubunge; lakini siku zote tulikuwa tunamwita Mheshimiwa Mbunge na Wapinzani walikuwa wanamwita Mheshimiwa Mbunge Mbatia. Hakuna mtu aliyemwita ndugu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo wamekuja na hoja nyingine tena; imekuwaje umetoka kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ghafla, umeingia na kuchaguliwa kuwa Naibu Spika? Nikawaambia tu, ndugu zangu, mbona Mheshimiwa Tulia alishaoneshwa njia na Mzee Lowassa? Mheshimiwa Lowassa Jumatano katoka CCM, kahama; Alhamisi ni Mgombea Urais CHADEMA. Mheshimiwa Tulia naye alitumia ile ile! Amechomoka kwenye Unaibu Mwanasheria Mkuu, amezama Bungeni – Naibu Spika wa Bunge.
Tena kwa kupigiwa kura, wala siyo kwa kuteuliwa. Wewe tumekuchagua sisi. Mheshimiwa Rais alikuteua kuwa Mbunge, lakini nafasi hiyo tumekupa sisi Wabunge. Siyo kwamba Rais amesema Mheshimiwa Dkt. Tulia awe Naibu Spika, aah, tumesema sisi kwa kukuamini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme jambo lingine ambalo watu wengi wamelisahau. Tanzania imezalisha viongozi wanawake wengi mahiri. Akina mama Mongella tunakumbuka, walikuwepo akina Bibi Titi Mohamed, wapo sasa hivi akina Samia Suluhu Hassan, akina mama Magreth Sitta; wamefanya kazi kubwa kwenye nchi hii. Leo nataka niwaambie msifikiri Wapinzani wanakimbia tu, kushindana na kiongozi shupavu mwanamke siyo kazi rahisi. Ni kazi ngumu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliwaambia wakajifanya mahiri wa kujenga hoja za kisheria, sijui wana uwezo mkubwa; huyu ni Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, yaani amebobea kwenye nafasi hiyo. Kwa hiyo, walipoona yameshindikana, ndiyo unaona wanachomoka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, duniani wanaume ndio tumeshika nafasi kubwa ya kuwa viongozi mahali pengi, lakini ikitokea mwanamke akapata nafasi, ogopa! Angalia akina Magraret Thatcher, amekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza pale. Mwangalie Indira Gandhi, amekuwa Waziri Mkuu wa India pale; mwangalie Golda Meir, amekuwa Waziri Mkuu wa Israel. Hawa ni akinamama wachache waliofanya mambo makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka nikuhakikishie kwamba unakoelekea ni kuzuri. Komaa, endelea kufanya kazi nasi tunakuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie Bajeti ya Serikali. Waheshimiwa Wabunge wamesema kwa uchungu sana, tunakuomba Mheshimiwa Waziri; tumefikia kipindi ambacho makusanyo sasa ni makubwa. Impact ya makusanyo yenu yatakuwa na maana sana kama yatashuka kwa wananchi wa chini maskini. Vinginevyo, hata mkijisifu kukusanya itakuwa haina maana. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais anabana matumizi, Serikali nzima inabana matumizi, lakini mategemeo yetu ni kuona bajeti hiyo ni kwa namna gani itashuka kumaliza matatizo ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wamesema habari ya kujichanganya kwenu hapa. Amesimama Mheshimiwa Waziri hapa anasema amefuta ushuru. Hao vijana mnaotaka tuwainue kiuchumi, mwaka huu ndio wamelima ufuta na alizeti. Leo bado kuna mageti ya vijana kuchangishwa kutoka kwenye kilimo chao duni walicholima, siyo sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ufuta umeshuka bei, alizeti haina bei, halafu mageti ya kuwachangisha ushuru mkubwa. Hili mlitazame, linatupaka madoa Waheshimiwa Wabunge tuliotoka kwenye Majimbo ya vijana wakulima. Watu wanataka kuinuka kiuchumi. Kwa hiyo, naomba Serikali wakati wa kutoa majibu ilisemee hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumezungumzia habari za Zahanati hasa za Vijijini, zinahitaji pesa. Akinamama wengi wanaojifungua wanapoteza maisha yao kwa kukosa vyumba vya kufanyia upasuaji kwenye hospitali zetu za Kata. Tumesema tuwe na Vituo vya Afya kwenye kila Kata. Vituo vile havina theatre maalum ya kuwafanyia upasuaji akinamama wajawazito.
Mheshimiwa Naibu Soika, kwa hiyo, inatupa shida na Kata nyingine zina kilometa ndefu sana kutoka Kata moja kwenda Kata nyingine. Kwa hiyo, tunamwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, asukume fedha kwenye Wizara muhimu; Wizara ya Afya na Wizara ya Maji ili kuweza kuwapunguzia usumbufu wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchezo wa kuigiza unaofanyika kwenye nchi yetu ni wa ajabu sana. Mwaka 2015 tulikuwa na mashindano ya kisiasa ya nchi nzima. Kila mwanasiasa maneno aliyokuwa nayo aliyasema. Wananchi wamepiga kura, siasa zimehamia Bungeni. Haiwezekani tena ukakimbia Bungeni ukaenda kuwaambia wananchi yanayoendelea Bungeni, wamekutuma kazi hiyo? Hili lazima niweke sawa! Serikali haiwezi kuleta maendeleo kama nchi haina utulivu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nchi lazima iwe na utulivu, iwe na amani yake ili hayo makusanyo ya Serikali yanayotafutwa yaweze kuwafikia wananchi. Kwa hiyo, hiki kiini macho kinachotumiwa na Wapinzani kwamba tunaenda kuwaambia wananchi yanayotokea Bungeni, tuko Wabunge wa Majimbo, hiyo tutaenda kuwaambia wananchi wetu waliotutuma! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kila Mbunge akafanye kazi kwenye Jimbo lake. Hivi, Mbowe anavyosema anaenda Kahama, Kahama kuna Mbunge wa CHADEMA? Kwa nini asiende kuwaambia wananchi wa Hai? Aende akawaambie wananchi wa Jimbo lake; lakini kwenda Kahama ambako hakuna Mbunge wa CHADEMA, ni uchokozi na ni kuwapotezea muda wananchi wa Kahama wasifanye kazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme kuhusu udikteta. Hili sitaki kuficha, moja ya viongozi madikteta kwenye nchi hii ni pamoja na Mheshimiwa Mbowe. Anawatoa Wabunge kwa nguvu. Waheshimiwa Wabunge wako hapo kwenye chai, wamenituma nije niwasemee humu ndani. Wameniomba, wamesema, Lusinde, kuna mambo sisi hatuwezi kumwambia Mbowe, nenda kamwambie.
Mheshimiwa Naibu Spika, natumia fursa hii kumwambia Mheshimiwa Mbowe warudishe Wabunge ndani ya Bunge! Usiwanyanyase! Anawapigia simu wakae kwenye chai badala ya kuingia Bungeni. Tabia gani hiyo? Hiyo ni kutumia Uenyekiti vibaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya siyo maamuzi ya Chama ndugu zangu, tusiwalaumu. Hawa wamepigiwa simu, wamekatazwa; atakayeingia atapewa adhabu. Kwa hiyo, wako kwenye chai, wameniomba; nenda katusemee Bungeni, sisi hatuwezi kusema. Najua huko waliko wananipigia makofi kwa sababu natekeleza agizo walilonituma. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiendeleza siasa uchwara za kufanya fujo wakati Serikali imeshapatikana, tutamnyima fursa Mheshimiwa Dkt. Magufuli ya kuwahudumia Watanzania. Tumpe nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu, wengi hapa mnajua mpira; mpira una sheria zake. Hivi mchezaji wa Simba au wa Yanga anapewa kadi nyekundu kwenye mchezo wa mpira, Wanayanga wanaweza kuandamana nchi nzima kupinga? Haiwezekani! Mbunge akipewa kadi nyekundu ndani ya Bunge, ni kwa kufuata kanuni za ndani ya Bunge, siyo nje ya Bunge. Haiwahusu wananchi hiyo. Hiyo inatuhusu wenyewe; tumewekeana sheria, tumewekeana kanuni; Mbunge akifanya kosa hili, red card, anatoka nje. Hiyo huwezi ukaandamana nchi nzima kwenda kuwaambia ooh, demokrasia inaminywa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna demokrasia isiyo na mipaka. Demokrasia isiyo na mipaka ni fujo. Tunaitaka Serikali isimamie amani, Serikali idumishe utulivu ili pesa zinazokusanywa ziende ziwahudumie wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia habari ya usambazaji wa umeme. Mkisambaza umeme kwenye vijiji, mnainua uchumi na mnapunguza msongamano mijini. Leo kama kila kijiji kitakuwa na umeme; kila kijiji wananchi watakuwa wamejiwekea pale miundombinu ya kujiletea maendeleo, wana sababu gani ya kwenda Dar es Salaam? Hawana sababu. Kwa hiyo, hata ile foleni ya Dar es Salaam itapungua na hayo yote yatafanyika kama nchi ina utulivu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mjumbe wa Kamati ya PAC, hapa nataka ku-declare interest. Naiomba Serikali badala ya kupeleka bajeti ya shilingi bilioni 72 kwa TAKUKURU, waitazame Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali. Leo unawapa shilingi bilioni 34 na point ngapi sijui, siyo sawa. Huyu ndio Mkaguzi. Huyu ndiye anayekwenda kuwaonesha TAKUKURU hapa kuna wezi. Huyu ndiye anayekwenda kuonesha ubadhirifu, ndio jicho la Bunge. Kwa hiyo, naomba, sisi Wabunge kwa kulithamini jicho letu, tunaomba jicho lisafishwe, liwekewe dawa, liwekewe miwani ili likawaone wabadhirifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Serikali iwe makini kwenye ushauri wa Waheshimiwa Wabunge. Waheshimiwa Wabunge tunapoomba, Serikali itusikilize; Ofisi ya CAG ni Ofisi kubwa. Ndiyo Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali; akikosa pesa hawezi kufanya kazi hiyo.
Kwa hiyo, tunawaomba waongezewe pesa ili wakafanye ukaguzi ili hata hiyo Mahakama ya Mafisadi iende na ushahidi. Hawa wasipofanya kazi yao vizuri, wote mtakaowashtaki watashinda kesi kwa sababu kutakuwa hakuna ushahidi wa kuaminika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme, kwenye Bunge, tunapokutana Waheshimiwa Wabunge, yanakutana Majimbo yote kuzungumzia maendeleo ya nchi nzima. Wabunge wa CCM tunao wajibu; sisi ndio tumepewa dhamana na wananchi wa Tanzania kuongoza nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata Wabunge wao wanapokosa hoja za msingi, tusimame kutetea Majimbo yale kwa sababu yana wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tutakapofika, wananchi watagundua, wananchi sio wajinga, watagundua kwamba amekuja Mheshimiwa Rais, anafanya mabadiliko ya vitendo; Mheshimiwa Rais anapozungumza, unamwona mpaka macho yanalenga lenga machozi kwa uchungu alionao. Watu wanamwona, wamemwamini, leo hawa wamekosa hoja wanapokimbia nje kutekeleza kauli ya Mheshimiwa Mbowe, inawauma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi Waheshimiwa Wabunge wa CCM tuzibe lile pengo kuhakikisha kwamba tunayasemea Majimbo yao, wananchi watusikilize kwamba Iringa ipelekewe maji, kwamba Kigoma ipelekewe maji na miundombinu ijengwe na Moshi Mjini pale patekelezewe miradi yao. Hiyo ndiyo kazi tuliyonyo Wabunge wa CCM maana sisi ndio mama, sisi ndio baba, sisi ndiyo tumeaminiwa na wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kweye miradi ya maendeleo. Kwa mara ya kwanza, Serikali imetenga asilimia 40 kwenye bajeti ya maendeleo. Miaka yote Wapinzani wamekuwa wakilalamika, bajeti ya maendeleo ndogo, hakuna pesa zilizotengwa; lakini mwaka huu Mheshimiwa Dkt. Magufuli na Serikali yake amekuja na asilimia 40 ya maendeleo…
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na namshukuru sana Mheshimiwa Kanyasu kwa kuniongezea dakika zake tano kwa niaba ya nchi hii, nami naendelea sasa kupiga dawa taratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tujifunze. Kama nchi inataka kufanya siasa za ustaarabu, tufanye siasa za ustaarabu. Tusiige kila kinachofanywa na watu wengine na sisi tukakileta hapa Tanzania, haiwezekani. Hata mashindano ya ma-miss tu, yakiisha, hakuna ugomvi tena. Hakuna mtu anapita kujitangaza kwamba yeye mzuri kuliko aliyechaguliwa, hakuna! Wanakuwa wamemaliza. Siasa za Tanzania ni siasa gani ambazo hazina muda? Lazima tuwe na muda wa kampeni, ukiisha tumwachie Rais atekeleze kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nalisema hili kwa sababu tukiendeleza tabia hii, nataka niwaambie, itakuwa ndiyo Taifa peke yake ambalo watu hawafanyi kazi, wanafanya siasa muda wote. Haiwezekani! Lazima tuwe tunajitenga. Tukimaliza kampeni, viongozi wamechaguliwa, tunawapa fursa ya kutekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais aliyeko wa Awamu ya Tano, slogan yake na msimamo wake ni Hapa Kazi Tu! Anachotaka ni watu wafanye kazi. Watu tufanye kazi, siyo turudi kwenye majukwaa tena sijui ooh, Dkt. Tulia kafanyaje! Haiwezekani. Mheshimiwa Dkt. Tulia hawezi kuwa msingi wa Wapinzani kutoka; wamekimbia kwa sababu hoja haipo. Mheshimiwa Mbowe ametumia nafasi hiyo vibaya kuwaambia sasa tokeni, kaeni kwenye chai mpaka mtakaponisikiliza. Huo ndiyo uongozi bora? Siyo uongozi bora! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia uongozi bora, tunazungumza kwa wote sisi, ndiyo kodi yetu inatumika kulipa Upinzani, kulipa Chama kinachotawala na kuleta maendeleo ya nchi. Kwa hiyo, mchango unapokosekana, lazima CCM tuzibe lile pengo, kama ambavyo imetokea Kambi Mbadala. Huo ndiyo wajibu wetu na tuwaambie wananchi kwamba kinachofanywa na Wapinzani siyo kweli, siyo sahihi. Hata viongozi wa dini wanajua, akishachaguliwa Mufti, hakuna uchaguzi mwingine tena. Anaachiwa Mufti aongoze. Akichaguliwa Askofu, hakuna uchaguzi mwingine wa Askofu. Anaachiwa aliyechaguliwa afanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kinachotaka kufanyika kupitia upinzani, ile ni fujo; kuiweka nchi katika fujo za maandamano yasiyo na msingi. Haiwezekani! Serikali isimamie amani, isimamie haki, isimamie maendeleo kwa nchi nzima. Mbunge anayejisikia kwenda kuwaambia wananchi wake kaonewa Bungeni, akafanye kwenye Jimbo lake, siyo kwenye Jimbo la Mbunge mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge yeyote akitoka hapa Bungeni naye ataenda kueleza nini tumepata, nini Serikali itafanya katika miaka mitano. Hatuhitaji msaada toka kwa Mheshimiwa Mbowe wala kwa mtu mwingine yeyote. Pale Kahama yuko Kishimba wamemchagua, atakwenda kuwaeleza yanayotokea hapa. Hatuhitaji msaada wa mtu mwingine. Hatuwezi kufanya siasa muda wote, haiwezekani. Tunafanya siasa, tukishamaliza, siasa zinahamia Bungeni, wananchi wanachapa kazi kuleta maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumza kidogo kuhusu kiinua mgongo. Waheshimiwa Wabunge, naomba mnisikilize. Naamua nijitoe muhanga kwenye jambo hili. Kujitoa kwangu muhanga ni hivi, hili jambo Serikali imesema kama yatakuwepo hayo makato, yatakatwa 2020. Sisi tunahoji kwamba kwa nini hoja hiyo muilete saa hizi? Sisi hatuitaki saa hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, jambo hili tukae wote. Serikali hii ni ya kwetu na sisi ni Wabunge tunaoongoza nchi hii. Wananchi wasije wakatuelewa vibaya wakafikiri sisi hatutaki kuchangia maendeleo, hapana. Moyo wa kuchangia maendeleo na sisi tunao. Tunachosema, jambo hili linahitaji mazungumzo, twende tukae, tukubaliane, utaratibu gani utumike ili kuweza kusonga mbele, wala siyo la kubishania hapa. Wala hatuwezi kusema hatutaki, haiwezekani. Huu ni ushauri wa Serikali na sisi hatuwezi tukailazaimisha Serikali kwa nguvu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawashaurini kwamba jambo hili linahitaji mjadala wa pande zote mbili. Waheshimiwa Wabunge, tunalipa kodi, tunakatwa kwenye mishahara yetu. Kama mnataka kuendelea mbele kukata tena gratuity, tuzungumze, tuone impact yake, maendeleo yatakavyosukumwa, wala siyo jambo la kubishania hapa. Jambo hili ni zuri. Isije ikachukuliwa kwamba Waheshimiwa Wabunge wote wanapinga kukatwa hela zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaambie, kuna waandishi wanasema, Waheshimiwa Wabunge wa CCM, imewauma kusikia wanakatwa hela. Mimi haijaniuma, niko tayari hela yangu ikatwe, lakini kwa mazungumzo. Tuone hiyo hela inakatwa kuelekea wapi na utaratibu gani utatumika ku-balance jambo hili ili liweze kuleta afya badala ya malumbano hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii ni yetu wote. Siyo kazi yetu kuwashtaki wengine kwamba viongozi wote wa kisiasa lazima wakatwe. Hiyo siyo kazi yetu. Kazi yetu sisi ni kuangalia kitakachopatikana. Kama hakitoshi, ndiyo tutashauri Serikali sasa iangalie na viongozi wengine ili kuongeza mfuko, maendeleo yaweze kupatikana. Tusikae tunabishania hapa, tunabishania kitu gani? Kwa sababu juzi hapa tumeondoa matangazo live ili pesa itakayopatikana iende kuwahudumia wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na hoja za msingi hapa, tukasema anayetaka kurusha live, hata harusi siku hizi watu wanarusha live; kalipie mwenyewe. Nenda lipia pale TBC, mtakapopewa dakika 15, rusheni live wananchi wako wakuone. Mbona tulipitisha na tukakubaliana? Hili lisilete ugomvi. Hili ni jambo dogo sana. Tunahitaji muda wa kuzungumza na Serikali kukubaliana juu ya jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna Mbunge anayepinga Bungeni, sijui kumekucha, sijui Waheshimiwa Wabunge wameamua kumkatalia Mheshimiwa Dkt. Magufuli. Mheshimiwa Dkt. Magufuli tumemchagua sisi, ni Rais wetu, tutamuunga mkono kwa hoja yoyote atakayoileta humu ndani, tukiwa na imani kwamba Rais hakosei. Rais hawezi kukosea. Nia yake ni njema katika kuitumikia nchi hii. Anataka Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi wote turudi katika mstari sawa. Kama Mheshimiwa Mbunge ulikuwa unakunywa bia kumi, kunywa moja ili tuweze kusonga mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kuna mwezi Mtukufu huu, Waislamu wamefunga, wanaweza kuombea nchi hii watu wakaachana kabisa na ulevi. Nawahakikishieni kabisa, tutapata maendeleo makubwa ya kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka kuwatia moyo sana Waheshimiwa Mawaziri, Dkt. Mpango na dada yangu pale, fanyeni kazi. Tuna imani na nyie. Mheshimiwa Rais anawaamini na sisi Waheshimiwa Wabunge tunawaamini. Tutafanya kazi kwa mshikamano kuhakikisha nchi hii inasonga mbele bila mikwaruzano, bila nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.