Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Martha Moses Mlata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii lakini naomba tu kwanza nikupongeze kwa kazi kubwa unayoifanya na nataka nikuhakikishie kwamba Mungu yupo upande wako, upo hapo kwa makusudi ya Mungu na ataendelea kukulinda, sisi tupo pamoja na wewe. Kupitia Mwezi huu Mtukufu naamini wengi wanakuombea kwa hiyo tunaomba Mungu aendelee kukubariki, songa mbele mwanamke mwenzetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nimpongeze na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu amerejesha imani kubwa sana kwa Watanzania. Ninasema haya kwa sababu nidhamu makazini imerejea, watu wanatulia maofisini, watu wanawahi maofisini na wanafanya kazi wanayostahili kulipwa mshahara huo, kwa hiyo nampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri na watendaji wote tunawaamini, tunaomba muendelee kuchapa kazi lakini naomba sana mtembee kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais wakati anaomba kura na wakati analihutubia Bunge, nataka nimpongeze kwa sababu anatembea kwenye yale maneno yake aliyokuwa anayasema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri sijaona kipengele kimojawapo ambacho Mheshimiwa Rais alikuwa anazungumza wakati akiomba kura na wakati anahutubia Bunge. Alizungumza sana kuhusu watu wa kima cha chini, wafanyabiashara ndogo ndogo, kina mama lishe, wauza nyanya, viazi, vitunguu, boda boda na wengine wote, nashangaa ametoka kwenye mstari hata hao boda boda sasa naona amewapandishia tozo badala ya kutembea kwenye maneno ambayo Mheshimiwa Rais aliongea.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alisema mgambo watatafuta kazi nyingine ya kufanya lakini hotuba ya Waziri haionyeshi kama mgambo watatafuta kazi nyingine ya kufanya kwa sababu wale mama lishe au wafanyabiashara ndogo ndogo kwenye ushuru mdogo mdogo ambao Mheshimiwa Rais alisema usio na maana utaondolewa hatujasikia, nilidhani TAMISEMI wangeleta lakini halikuonekana hili na bajeti hii iko kimya. Naomba Waziri atamke jambo kwa ajili ya wafanyabiashara hawa wadogo wadogo hasa akina mama lishe, wauza nyanya, vitumbua, wanaofukuzwafukuzwa na mgambo. Ukienda Singida pale utakuta kuna miwa, nyanya, vitunguu, karanga, tunaomba utulivu wa hawa watu ambao walisubiri sana kauli ya Mheshimiwa Rais itekelezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli wafanyabiashara hawa wanategemewa na watu wengi sana. Kuna watu ambao ni wafanyabiashara wanategemewa na watoto wao, wazazi wao lakini wale wanaofanya kazi kwenye viwanda wenye vipato vya chini wanategemea kupata huduma kutoka kwa hawa mama lishe ambao wanatoa huduma kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nizungumzie suala la Mkoa wangu wa Singida. Waziri amesema kwamba Mkoa wa Singida ni miongoni mwa mikoa ambayo uchumi wake bado upo chini sana lakini nashangaa sana kwamba mtoto ambaye amekonda ndiye ambaye bado unaminywa. Sasa sielewi Mkoa wa Singida tumekosa nini? Ametaja reli ya kati ambayo inaenda kujengwa, akataja michepuo ya reli zote lakini akaacha kuitaja reli inayotoka Dodoma - Manyoni - Singida na reli ile ndiyo iliyokuwa inawasaidia sana wananchi wa Mkoa wa Singida. Mkoa huo unategemea uchumi wake kupitia reli ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi ni wakulima wazuri sana wa zao la alizeti, tunategemea uchumi wa viwanda, lakini tuna mifugo, tuna kuku, tunalima viazi vitamu ambavyo hakuna mkoa mwingine unaolima viazi vitamu kama Mkoa ule wa Singida. Tuna vitu vingi ambavyo tunategemea kuvisafirisha kwa kutumia reli ile. Kwa hiyo, naomba sana aiingize kwenye hiyo michepuo ya reli nyingine alizozitaja, vinginevyo anawavunja moyo wananchi wa Mkoa wa Singida ambao wao wameinuka kwa kasi kubwa sana katika kujiletea maendeleo na wamejitahidi sana mpaka sasa hivi na nawapongeza. Kwa hiyo, naomba asiwavunje moyo, vitunguu vilivyo bora Afrika Mashariki vinatoka Singida. Kwa hiyo, namuomba sana reli hii aiweke katika list yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nizungumzie pia miradi ya zamani. Kuna miradi ambayo imekuwa ikitengewa fedha, inaanzishwa lakini matokeo yake inaachwa, fedha zile zinakuwa zimepotea. Tunafika hapa tunatenga tena fedha tunapeleka kwenye miradi mingine, hivi hatuwezi tukaanza na kitu kimoja tukakimaliza ili twende kwenye kitu kingine? Kwa mfano, ukienda Mkalama utakuta kuna mabwawa ambayo yalishaanza kuchimbwa, miradi ile haikukamilika imeachwa takribani miaka kumi sasa ipo tu na fedha zilitumika. Kuna bwawa la Mwanga, Mwangeza, Msingi, ukienda Iramba kule Urugu na maeneo mengine miradi mingine imekuwa kama magofu. Naomba fedha hizi ziende kukamilisha miradi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la wakulima kuna ruzuku lakini wavuvi mbona wametengwa hakuna ruzuku yoyote? Hebu ondoeni kodi kwenye vifaa vya uvuvi. Mheshimiwa Rais alisema anatamani kuona meli ya uvuvi ambayo ni kiwanda kuanzia mwambao Tanga, Dar es Salaam, Lindi mpaka Mtwara. Hebu ondoeni ushuru kwenye mafuta yanayoendeshea vyombo vya uvuvi ili muwasaidie na wenyewe maana hawana ruzuku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kuzungumzia tozo kwenye utalii, wengi wamezungumza. Hivi mnataka Kenya waendelee kutupiga bao kwamba ukifika Kenya utauona Mlima Kilimajaro! Mkishaongeza na hiyo tozo ambayo mnaiweka watafika Kenya wataona Mlima Kilimanjaro wataondoka zao. Halafu tunasema tunaongeza ajira kwa vijana, hapa tunawaminya wale ambao wapo kwenye sekta ya utalii. Kwa hiyo, naomba sana kwenye eneo hili na lenyewe Mheshimiwa Waziri mliangalie.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie tu na suala la mikopo upande wa wajasiriamali wanawake. Amezungumza mwenzangu, akina mama wanazalilishwa sana, wengine wamevunja ndoa zao kwa sababu asubuhi anakuja kunyang‟anywa TV na mume wake anashuhudia, anaambiwa TV ikiondoka, friji ikiondoka ongozana navyo, hakuna kurejea hapa nyumbani. Kwa hiyo, naomba sana suala hili liangaliwe na hizi benki zinazohudumia akina mama ni lazima ziende kwenye mikoa mingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana.