Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Rose Cyprian Tweve

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia siku ya leo. Kwa kuwa hoja iliyoletwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2016/2017 inagusa maslahi mapana ya wananchi wa Mkoa wa Iringa hususani wanawake ambao wameniwezesha kufika hapa leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni miongoni mwa Wabunge wanaowakilisha wananchi wa Mkoa wa Iringa. Sasa ndani ya huu Mkoa wa Iringa tunahifadhi kubwa ya Msitu wa Taifa wa Sao hill. Kwa muda huu niliopewa nina jambo moja kubwa ambalo nitalizungumzia, ni suala zima la TFS na utaratibu mzima wa utoaji wa hivi vibali vya kuvuna msitu wa Sao hill. Hili limekuwa ni tatizo kubwa sana. System nzima ya utoaji wa hivi vibali haieleweki. Vibali hivi vimekuwa vinawanufaisha wachache. Watanzania ambao ni wazawa, wavunaji wadogo wadogo, kundi la akinamama, vijana na walemavu hawapewi kipaumbele. Hawa wazawa ndiyo waliolima msitu huu, hawa ndiyo wameweza kuutunza huu msitu mpaka umefikia hapo ulipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka Serikali inatoa cubic meter 600,000 kwa Watanzania waweze kuvuna msitu huu. Hapa ndipo nina tatizo napo na ndipo panaposikitisha. Watanzania hawa ambao ni wazawa hawanufaiki na huu mgao, ni wawekezaji ambao wanapewa kipaumbele kuweza kunufaika na huu msitu. Nitatoa mfano mmoja, tuna hawa Wawekezaji ambao wamepewa kuendesha Kiwanda cha Mgololo, wanajiita RAI-Group. Hawa ndio wamekuwa beneficiary wakubwa wa huu mgao wa vibali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hii 600,000 inayotolewa na Serikali RAI-Group wanapewa cubic meter 250,000 na kinachosikitisha zaidi, hawa RAI-Group wanalipa nusu ya bei ambayo wanatakiwa kulipia vibali hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kibali kimoja, Mtanzania, Mwanairinga, Mwanamufindi analipa sh. 28,000/=, RAI-Group wanalipa sh. 14,000/= tu. Sasa ukipiga mahesabu kutoka kwenye hizo cubic meter 250,000 wanazopewa, ukizidisha mara hiyo Sh. 14,000/= maana yake wanalipa bilioni 3.5 kwa mwaka. Sasa wangeweza kulipa hiyo Sh. 28,000/= ambayo Mtanzania wa kawaida analipa, Serikali ingeingiza bilioni saba kwa mwaka. Sasa namwomba Mheshimiwa Waziri anipe maelezo, ni vigezo gani wanatumia kuwapunguzia bei hawa RAI-Group na ni vigezo gani wanafanya hawa Watanzania waendelee kulipa hii Sh. 28,000/=? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa nipewe maelezo ni kwa sababu gani hawa RAI-Group wanapewa kipaumbele? Wanapewa hizi cubic meter 250,000 wakati hawa Watanzania wa kawaida Wanairinga hawawezi kunufaika na msitu huu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa nipewe ufafanuzi wa ukusanyaji wa kodi kutoka kwa hawa wawekezaji wa hiki Kiwanda cha Mgololo. Cha kusikitisha zaidi hawa RAI-Group wanapasua haya magogo, wanatengeneza hizi raw materials wanapeleka Kenya, wanaenda ku-process makaratasi ndipo waturudishie sisi hapa kununua wakati haya makaratasi yangekuwa processed hapa Tanzania, tungetengeneza ajira kwa vijana wetu. Kwa hiyo, naomba majibu yanayonitosheleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa RAI-Group walishakuwa na Kiwanda Malawi, wamefukuzwa wamekuja hapa, sasa sisi tunawa-protect, moja tuwape vibali vingi, mbili bei ya chini, hii kweli inahuzunisha, inatukatisha tamaa sisi Wanairinga, inatukatisha tamaa sisi Wanamufindi, naomba tulifanyie kazi hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, hawa RAI-Group wapande misitu yao na kama bado wataendelea kupanda msitu huu wa sao hill basi walipe bei moja sawa na Watanzania. Hata kama wakilipa bei hiyo moja lazima hivi vibali vipunguzwe, viende kwenye makundi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua asilimia kubwa ya wanawake na vijana sasa hivi wako kwenye hivi vikundi vya ujasiriamali. Tatizo la hivi vikundi ni maskini, havina pesa, hakuna miradi endelevu ambayo ingeweza kuwasaidia wao kuendelea kupambana na hizi changamoto zao za kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri angewawezesha hawa vijana, angewawezesha hawa akinamama katika Wilaya zote, Iringa Mjini, Iringa Vijijini, Kilolo na Mufindi waweze kutumia hivi vibali angekuwa; moja, amewainua kiuchumi; pili, hivi ndivyo vitakavyokuwa vikundi darasa vya kuwashawishi watu wengine waendelee kupanda miti kwa sababu watakuwa wameona matunda na benefits ambazo zinatokana na upandaji na upasuaji wa miti hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa RAI-Group tunawapa vibali vikubwa. Hawajihusishi na mambo yoyote ya kijamii, barabara mbovu, madawati watoto wanakaa chini, kuna manufaa gani ya kuendelea kuwashikilia watu hawa wakati pale Mufindi tuna wavunaji wazuri wana viwanda, wamekuwa msaada mkubwa kuchangia madawati, kuchangia hospitali, hebu tuwape kipaumbele watu hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri please, doesn’t get me wrong. Najua ndiyo umepata kuongoza Wizara hii, so prove to me kuwa unakasirishwa na jambo hili, tuwapiganie Watanzania wetu waweze ku-enjoy matunda ya nchi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, after all Mheshimiwa Waziri tunasema tunataka Tanzania iende katika uchumi wa kati, Wizara hii ina nafasi kubwa ya kuwainua hawa wananchi, tuwawezeshe, tuwape kipaumbele hii ita-trickle down sasa tukiendelea kuwashikilia hawa RAI-Group tunawapa vibali cubic meter 250,000, hawa wengine hawanufaiki tutafikaje huko, lazima tuwaonjeshe matunda ya nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti sasa kwa kumalizia namwomba Mheshimiwa Waziri, najua yeye ni msikivu, he is competent. Naomba tufike Mufindi, hawa wavunaji wanajua matatizo ya hivi vibali, wanajua solution ya kuweza kutatua hili tatizo…
MWENYEKITI: Ahsante.