Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Prof. Norman Adamson Sigalla King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. PROF. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wenzangu walivyochangia, nimpongeze Profesa Maghembe na wenzake kwa kazi nzito waliyonayo. Mmoja alisema mzigo mzito mpe Mnyamwezi nadhani kwa mzigo huu hata Mnyamwezi anaweza akashindwa kuubeba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nimemsikiliza sana Waziri mwenye dhamana, Mheshimiwa Profesa Maghembe nikafikiri sikumsikia vizuri. Nikaisoma hotuba yake nikaridhika kwamba nilichosikia jana ndicho kilichoandikwa. Nimesikitika sana kuona katika kitabu chake chote ameacha hifadhi pekee ya maua kwenye Bara letu la Afrika lakini ukisoma kitabu chake, utalii Tanzania unapungua. Yeye hasemi chochote kabisa kuhusu habari ya kuendeleza Hifadhi ya Kitulo iliyoko Makete, hasemi chochote kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Makete wa Kata za Mfumbi, Mlondwe, Matamba, Kinyika, Ikuwo, Kigala, Ipelele pamoja na Kitulo yenyewe, wamehamishwa ili kupisha hifadhi hii muhimu. Sasa miaka inakwenda Wizara haifanyi chochote na bahati mbaya sana kwenye hotuba ya Waziri hasemi chochote kabisa juu ya mkakati wake wa kuendeleza Hifadhi ya Kitulo. Nimesikitika sana na nasikitika sana, kwa vyovyote vile sitaunga mkono hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi utalii katika nchi yetu unachangia kiasi kikubwa sana cha Pato la Taifa lakini mkakati wa Wizara ni nini kuongeza watalii? Hasemi chochote juu ya kuboresha Hifadhi ya Kitulo, hasemi chochote juu ya kuboresha miundombinu ili angalau sasa watalii waone Makete kwenye Hifadhi ya Kitulo ni sehemu ya kukimbilia. Sikutaka kushawishika kwamba Mheshimiwa Profesa Maghembe yeye anaziona hifadhi zilizoko Kaskazini tu, sikutaka kufika huko, lakini naanza kushawishika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana, ni lazima Waziri aje na majibu ni jinsi gani anafanya kwenye bajeti hii kuwafanya wananchi wa Makete ambao wanaitunza hifadhi hii, wamehama kuacha maeneo yao wasilime ili kuheshimu Pato la Taifa, basi wagawane Watanzania wote, maana wangelima wao mapato yale ni ya kwao. Wamepisha ili sasa hifadhi hii iwe mali ya Watanzania wote. Waziri atoe majibu hapa anaifanyia nini hifadhi hii ili kuongeza pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kwamba Ngorongoro na Serengeti zimetajwa lakini Waziri anafahamu moja ya sifa zilizopelekea Hifadhi zetu za Ngorongoro, Serengeti na Manyara kuongeza watalii ni baada ya kuboresha miundombinu hasa barabara ya kutoka Arusha kuelekea Manyara na Monduli pia kuelekea kwenye lango la Ngorongoro, Kitulo mnafanyaje? Ni wazi ni lazima barabara ya kutoka Chimala – Matamba – Kitulo - Makete ijengwe kwa kiwango cha lami ili kuimarisha utalii kwenye hifadhi hii, ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tufikiri heuristically kwa sababu ni kweli utalii ni leisure, utalii ni burudani, siyo mateso. Hakuna mtalii atakayekwenda Kitulo kama miundombinu mingine haionyeshi kuwasaidia wao. Sambamba na hilo, ndiyo maana nilimfuata Mheshimiwa Profesa Maghembe nikasisitiza umuhimu wa TANAPA kuweka hoteli au kutengeneza mazingira ya kuweka hoteli za kitalii eneo la Matamba ili kuboresha au kuongeza Pato la Taifa, kwenye hotuba yake, kimya!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kidogo kuhusu mwingiliano wa mipaka kati ya mifugo pamoja na hifadhi zetu. Kwa suala hili ni lazima Serikali ijipange, bahati nzuri mimi natoka wilaya ambayo ina wachungaji wa ng‟ombe, ina wafugaji wa ng‟ombe, ina wakulima na pia ina hifadhi. Narudia, ina wachungaji, ina wafugaji na ina wakulima lakini hifadhi pia inayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani dhana hapa, pia weledi kidogo unatofautiana kwenye kufasili kwa usahihi juu ya wachungaji wa ng‟ombe. Duniani kote inajulikana, ukisema unafanya kuchunga, wachungaji wote wanafuata malisho, nchi zetu hizi ni za ki-tropic, kwa hiyo mvua ina kiangazi na masika. Wakati wa kiangazi lazima mchungaji, siyo mfugaji, mchungaji atahama na mifugo yake kufuata malisho, lazima ugomvi na wakulima utakuwepo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana naunga mkono hoja iliyotolewa na Mbunge wa Mbinga Mjini, Mheshimiwa Sixtus kwamba Wizara lazima wakae, and on this you must be strict. Hamuweze ku-compromise na Wabunge kwa sababu its impossible, kama anatoka eneo ambalo watu wanachunga nitatetea wananchi wangu na ndiyo sifa kwangu. Ninyi lazima mje na ukweli kwamba pamoja na kwamba unatetea wachungaji wako lakini dunia ya sasa ni ya kufuga siyo ya kuchunga, lazima tuelewane hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Wizara husika ishirikiane na Wizara nyingine kutengeneza mkakati ambao ni endelevu. Ni lazima tutafika mahali tutachagua, tunataka hifadhi au tunataka ng‟ombe wa kuchungwa. Kama tunataka wa kufuga, yes you can set aside a piece of land kwa ajili ya kuchunga lakini huwezi kutengeneza eneo kwa ajili ya kuswaga ng‟ombe, haiwezekani, kiangazi kitaingia lazima watatafuta malisho. Sisi ambao tumetumika sehemu mbalimbali kwenye eneo ambalo ni la wafugaji zikiwemo Wilaya za Hai, Siha, Mbeya, Songea na Makete kwenyewe tunajua, uko mtihani mkubwa wa ku-harness kati ya ufahamu wa kuchunga na kufuga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize hoja yangu kwa kusema, ndiyo maana nilisema Mwalimu Nyerere na Mzee Karume wamezikwa kaburini lakini wana hekima kuliko sisi, wao waliweka shamba la mifugo Kitulo ili wachungaji wakajifunze kufuga Kitulo. Bahati mbaya Serikali haisemi chochote kuhusu hili. Ni muhimu sana shamba lile lifufuliwe ili wachungaji, waswagaji wa ng‟ombe wajue kwamba zama za sasa ni kufuga siyo kuchunga siyo kuswaga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ifufue shamba la mifugo la Kitulo lililopo Makete pamoja na hifadhi ile ili liwe shamba darasa kwa mikoa yote Tanzania. Tutapona na tutaondoa migongano kati ya wafugaji na wakulima, vinginevyo haiwezekani, narudia, vinginevyo haiwezekani. Ukitaka kutibu hili ni lazima ukumbuke shamba darasa ni shamba la mifugo kule Makete, lakini Hifadhi ya Kitulo ipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisisitize, nakusudia kushika shilingi kama Waziri, Mheshimiwa Profesa Maghembe hatakuja na majibu ya kwa nini katika mpango wake Hifadhi ya Kitulo ameiacha kirahisirahisi tu, ameiacha tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.