Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Lucia Ursula Michael Mlowe

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Mpango uliopo mezani. Nianze kwanza kwa kumshukuru Mungu kwa kunijaalia afya njema. Vile vile nichukue nafasi hii kwa namna ya pekee kukishukuru chama changu kwa kuniteua kuwa Mbunge wa Viti Maalum ili niweze kuwatetea Watanzania. Niende moja kwa moja kwenye mchango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na suala la Utawala Bora, tunaimba amani, amani, amani na utulivu, lakini niseme ukweli ni miaka 54, hakuna amani na utulivu Tanzania. Wanawake hatuna amani wala utulivu kwa sababu tunadhalilishwa, mfano kwenye Mkoa wangu wa Njombe... (Makofi)
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mkoa wangu wa Njombe wanawake wengi wanabakwa, vilevile wafanyakazi wa kike wanaokwenda maofisini wanatakiwa kutoa rushwa za ngono. Hii ni wazi na ni dhahiri lakini sisi tumefumba macho tunasema amani. Hii ni amani kwa watu wachache, lakini kwa watu wengine hatuna amani au hawana amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, kuna mambo mengi ambayo yanaendelea ya wanawake wajasiriamali. Wanawake wajasiriamali sasa hivi wanahangaishwa, wanakimbizwa huku na huku. Mfano, Mkoa wangu wa Njombe, wanawake wanatolewa barabarani kama vifurushi. Wanatolewa mizigo yao au bidhaa zao zinawekwa kwenye magari ya kutolea takataka, kwa kweli huu ni udhalilishwaji na huu ndiyo tunasema utawala bora, huu siyo utawala bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bomoa bomoa, wanaodhalilishwa sasa hivi, wanaopata matatizo ni wanawake na watoto kwa sababu mali zao ziko nje na baridi, wanahangaika na baridi na watoto. Ni kweli! Kwa hivi kwa kweli tunasema bado Serikali ya sasa ijipange, ndiyo mmetuletea Mpango lakini je, utatekelezwa? Utatekelezeka?
MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge utulivu tafadhali, tumsikilize.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi naiomba Wizara, Wizara husika inayohusika na wanawake na kwanza niiombe Serikali, nasikitika sana kwa sababu imefuta Wizara moja inayohusika na Wanawake Jinsia na Watoto. Nasikitika kwa sababu ni chombo ambacho kingeendelea kuwatetea wanawake, Wameunganisha na Wizara kubwa, kwa nini wanatuonea wanawake? Kweli naiomba Serikali mtufikirie wanawake inatuumiza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema tena juu ya utawala bora tunaona kabisa malalamiko na kutoridhishwa baadhi ya watu kwa mfano watu wa Zanzibar, tunaona kuna kilio kikubwa sana lakini bado tunaimba utawala bora. Naomba hilo tulifikirie Serikali. Tuifikirie na tuone ni namna gani tunawasikiliza hao watu. Jamani Rais aliyetakiwa kutangazwa atangazwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo; asilimia kubwa ya wakulima ni wanawake na wanawake ndiyo wanaoshinda mashambani wanabebeshwa mizigo wakiwa na watoto wao, lakini ni wanawake hao hao wanaonyanyasika na Serikali haiwaangalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pembejeo wanazopatiwa ni feki, mfano Mkoa wa Njombe, safari hii wamepata ridom, dawa ile ya kupuliza ya ukungu ili viazi visipate ukungu, wamepata ridom feki ambayo imesababishia watu hawa kukosa mazao yanayotakiwa kama kipindi kingine wanavyovuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii ni hasara kwa hawa akinamama ningesema, maana akina mama ndiyo Taifa kubwa, ndiyo wanaolima sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile pembejeo; Pembejeo zingine ni gharama sana kwa mfano, mbolea ya kupandia, watu wengi wanashindwa kupandia mbolea, wanapanda bila mbolea matokeo yake wanakuwa na mashamba makubwa, wanalima bila utaalam mwisho wa siku wanavunia kwenye kiganja. Halafu bado tunasema kwamba tunataka mapinduzi ya viwanda, tunataka kuwa na viwanda ambavyo vinategemea tena kilimo, sasa kilimo cha aina hii ni kweli tutaweza kutoka hapa tulipo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi; tunaomba wanawake kwenye huu Mpango, ioneshe wazi kwamba wanawake na wenyewe wanaweza kuwa wasemaji au waingie kwenye mpango na vilevile washirikishwe katika maamuzi ya ardhi. Pia wawe wamiliki wa ardhi. Kwa nini ardhi wamiliki akinababa peke yao na sisi akinamama tuna haki. Haki sawa kwa binadamu wote. Kwa hiyo, naomba huu Mpango tujaribu kuangalia namna gani tunawaingiza akinamama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara; tena akinamama ndiyo waathirika wa miundombinu mibovu, kwa sababu akinamama ndiyo wanaobeba ujauzito kwa miezi tisa, wanatakiwa kwenda hospitalini kupimwa, lakini mwisho wa siku kwa sababu barabara ni mbovu wanajifungulia njiani. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mlowe, muda wako umekwisha.