Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Ester Alexander Mahawe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kwanza niwapongeze tu walioandaa bajeti hii, lakini pia nielekeze zaidi mchango wangu kwenye suala zima la afya. Afya ni jambo la msingi sana kuzingatiwa katika uwekezaji wowote ule unaotakikana kama tulivyosema kwamba tunataka kutengeneza Tanzania ya viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii Tanzania ya viwanda ambayo tunataka kuitengeneza bila kujali ama kuweka kipaumbele kwenye afya za watu wake ambao wengi ndio wazalishaji, wengi ndio wanaofanya kilimo cha mkono, ama ni wakulima wadogo wadogo ambao wako vijijini; hawa watu tusipowapelekea zahanati za kutosha, tusipopeleka Vituo vya Afya vya kutosha, tusipowapelekea watumishi wa kutosha wa kada za afya, hawa watu wanawezaje kusaidia uzalishaji na hatimaye viwanda vyetu vikafanya kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona upungufu kidogo katika bajeti yetu hii kwamba ingawa Serikali imeweka kipaumbele kwenye Sekta ya Kilimo na kuainisha kwamba mazao ya kilimo yatakuwa moja ya malighafi kwenye viwanda hivyo, bado vipaumbele vinaenda kwenye kujenga reli, barabara, Viwanja vya Ndege na kadhalika; lakini kwenye vyanzo vya kilimo ambavyo ndivyo vitakuwa malighafi, kusababisha uzalishaji ukue hakujawekewa mkazo huku; na asilimia 80 ya wanawake walioko kijijini ndio wakulima, lakini bajeti hii haioneshi ni jinsi gani afya ya mwanamke huyu imezingatiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikirudi upande wa Mkoa wa Manyara na Wilaya zake zote, hatuna watumishi wa kutosha katika kada ya afya na hatuna vituo vya kutosha. Kwa mfano, katika Kata ya Eshikesh, mama mjamzito anatembea kilometa 40 kwenda kwenye Zahanati ya Yaeda Chini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya hii ya Mbulu Vijijini haina Hospitali ya Wilaya wala gari la wagonjwa. Akinamama hawa wanapata shida kusema ule ukweli; siyo Mbulu tu, tuna maeneo kama Simanjiro, mahali ambapo gari la wagonjwa ni moja, hawana Hospitali ya Wilaya, wanatumia Hospitali ya KKKT. Mama akishindwa kujifungua, anatakiwa apatiwe operation lakini anatakiwa alipe shilingi 400,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi yule mama wa Kimasai anayetembea na punda, anayepoteza muda wote kwenye maji, ni saa ngapi ametafuta shilingi 400,000 za kuweza kumsaidia yeye kwenda kujifungua? Nafikiri tungehakikisha kwamba kipaumbele kinawekwa kwanza kwenye afya, watu wetu wakiwa na afya njema watazalisha kwa tija. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, nizungumzie hili suala la asilimia tano ya akinamama na vijana. Tulijinadi sana kwenye kampeni zetu kupitia asilimia tano kwa akinamama na vijana. Sasa inaonekana sehemu kubwa ya own source inakusanywa na Serikali Kuu. Changamoto ipo kubwa; mara nyingi, hata leo Mheshimiwa Umbulla ameuliza hapa, akinamama ama Wabunge wa Viti Maalum hawaingii kwenye Kamati ya Mipango na Fedha ya Halmashauri zetu, ndiyo maana hizi fedha zimekuwa misused wakati mwingi. Hakuna mtu wa kuzisimamia; tunaziona tu kwenye makaratasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliwahakikishia akinamama ambao ndio wamekipa Chama chetu kura nyingi ya kwamba tunakwenda kudai asilimia hizi. Je, tunarudije kwao? Tunaomba hizi fedha ambazo zinatengwa kwa ajili ya akinamama, kwa mwaka huu haidhuru, basi kwa mara ya kwanza zifike katika ukamilifu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna shilingi milioni 50 kila Mtaa na kila Shehia na kila Kijiji. Nako tulijinadi kwa sababu ni ahadi ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri tu kwamba pamoja na Mikoa 10 inayotaka kutengwa hapa ya pilot run, nashauri ili wananchi wetu mioyo yao isikunje ngumi, kwa nini isitumike mikoa yote, halafu haidhuru vichukuliwe vijiji hata kama ni vitano kwa kila mkoa? Maana changamoto na mazingira hayafanani. Haidhuru na sisi tupate cha kusema tukirudi kwa wananchi wetu. Hawa kumi tu, tuseme Mkoa wa Manyara, haufanani na Dar es Salaam; Mkoa wa Manyara haufanani na Kilimanjaro; changamoto zinatofautiana. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sijajua kwamba labda hawa walioweka hivyo kwamba wanachukua mikoa kumi wamezingatia nini. Ila nashauri tu, kama inawezekana, mikoa yote ichukuliwe na vijiji haidhuru vitano vitano kila Mkoa ili tuone kwamba tunawezaje kuokoa maisha ya wananchi wetu kupitia mikopo hii ya shilingi milioni 50 kupitia SACCOS.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna mgongano wa maslahi. Pale mwongozo unapoelekeza kuwa mapato yote ya mamlaka ya Serikali za Mitaa yawasilishwe Serikali kuu, changamoto kwenye mamlaka ya Serikali za Mitaa ni kwamba fedha hizi huwa zinachelewa sana kuteremka chini huko kwenye Halmashauri zetu. Sasa itakuwaje ikiwa fedha hizi zinakusanywa na Serikali Kuu?
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nasoma kiambatanisho cha masuala ya afya; elimu ya watoto wetu wa kike ni tatizo. Imeelezwa sana, kwamba tunaomba kodi ziondolewe kwenye vifaa vyote vinavyosaidia akinamama pamoja na mabinti mashuleni. Kwenye towel zao kodi iondolewe. Binti anakosa shule siku saba katika mwezi. Mwisho wa siku inaonekana watoto wa kike ni vilaza; kumbe ni kwa sababu hawa-attend shule inavyotakiwa kama wanavya-attend watoto wa kiume.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hili litazamwe upya, tuwasaidie watoto wetu wa kike. Utakuta miundombinu kwenye shule, watoto 400 vyoo viwili au watoto 600 vyoo vitatu, watoto wa kike wanapataje kujisitiri? Je, bajeti hii inamwangaliaje mtoto wa kike? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kushea hii keki sawasawa, naomba tuwekeze zaidi kwa akinamama ambao ni waaminifu hata wanavyochukua mikopo kwenye mabenki, wamekuwa wakirejesha kwa uaminifu mkubwa. Kwa hiyo, naomba sana akinamama watazamwe kwa jicho la pekee ili waweze kusaidia pato hili la Taifa hasa kupitia kilimo na ujasiriamali. Hakuna asiyejua kwamba akinamama ndiyo wanaokimbia kimbia asubuhi mpaka jioni kutafuta riziki za familia zao, kupitia biashara ndogo ndogo. Akinamama hao watazamwe kwa jicho la pili ili waweze kusaidia katika kukua kwa uchumi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna upungufu mkubwa wa urari baina ya matumizi ya kawaida na yale ya maendeleo. Matumizi ya kawaida ni karibu mara tatu ya yale ya maendeleo. Kwa hiyo, nashauri tu kwamba, bajeti hii iangalie ni jinsi gani inaweza ikawekeza zaidi kwenye bajeti ya maendeleo, japo imepandishwa mpaka asilimia 40, lakini kama inawezekana, iendelee kusogea hata ifike mahali iwe asilimia 50 kwa 50.
Mheshimiwa Naibu Spika, basi naomba nisisuburi kengele inayofuata, niseme tu kwamba yangu ni hayo. Zaidi sana, nawalilia akinamama waweze kusaidiwa na bajeti hii pamoja na watoto wa kike ili waweze kupata elimu sawasawa pamoja na watoto wa kiume.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naunga hoja mkono.