Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Salum Mwinyi Rehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami kupata fursa ya kuchangia katika hoja iliyokuwepo sasa hivi Mezani ya Bajeti ya Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishukuru Serikali, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuwasilisha hapa taarifa yake nzuri. Vile vile naishukuru sana taarifa ya Kamati ya Bajeti, imeshauri mambo mengi ya msingi, Namwomba Mheshimiwa Waziri aiangalie kwa jicho la aina yake. Nina mambo kadhaa ambayo napenda niishauri Serikali kuweza kuyaangalia na ikiwezekana kuyafanyia marekebisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza nataka kuzungumza juu ya suala zima la tozo ya bidhaa za mbogamboga za kilimo na hasa kwa wafanyabiashara wale ambao wanatoka Bara kwenda Zanzibar na wale ambao wanatoka Zanzibar kuja Tanzania Bara. Mheshimiwa Waziri hili linarudisha tena kidonda cha kero za Muungano; isitoshe, suala hili halijaangaliwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Zanzibar hivi sasa ina zaidi ya mahoteli 450 ya utalii. Asilimia 70 ya vyakula ambavyo ni mboga mboga na matunda vinatoka Tanzania Bara. Mazao haya ni very perishable, yaani hayana uwezo wa kustahimili kwa muda mrefu. Leo ukichukua nyanya Ilula, ukifika Dar es Salaam, umemaliza siku moja au siku moja na nusu; robo ya ile bidhaa tayari imeshaharibika. Unangoja meli uyasafirishe kufika Zanzibar, nusu yake nyingine tayari imeshaharibika; lakini bado unatoa pale uyapeleke Kiwengwa au Nungwi ambako ndiko kwenye ulaji wa yale matunda. Mfanyabiashara yule atakwenda mara mbili mara tatu, biashara ile imemshinda. Hapa hatujengi. Tunawavuruga hawa wafanyabiashara na mwisho wake badala ya kwenda mara tatu, mara nne, biashara hii imemalizika. Hakuna biashara itakayokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utafiti tulioufanya mwaka 2014 kwa mwezi mmoja, biashara ya mboga mboga na matunda ni zaidi ya tani 160,000 kwa mwezi mmoja zinasafirishwa kutoka Bara kwenda Zanzibar. Biashara hizo zinaingiza zaidi ya shilingi bilioni 2.6, fedha zinazunguka kila siku kutoka Bara kuja Unguja; yaani eneo hili tunalivuruga. Lazima tuwe makini na tupate maelezo yaliyo sahihi kuhusiana na mazao haya kutozwa tozo hizo ambazo zimependekezwa na Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nataka kuzungumza suala zima la makato au tozo za Waheshimiwa Wabunge. Ni eneo ambalo kwa kweli limemgusa kila Mbunge aliyekuwemo ndani ya Bunge hili. Siyo hivyo tu, hasa wale Wabunge ambao wanatoka katika Majimbo waliyogombea; hali ni ngumu Mheshimiwa. Sms zaidi ya 300 kwa siku, kati ya hizo sms 200 zote zinaomba hela. Leo Mbunge huyu unakwenda kusema unamkata kile kiinua mgongo chake unategemea nini? Atarudi vipi hapa? Ni wazi kabisa huo ni mkakati wa kuwadhibiti kwamba hapa wasirudi mwaka 2020 au 2021. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo tu athari yake haitokani na hapo, athari hiyo itatokana vilevile na ile miradi ambayo ilionekana kwamba Mbunge huyu angeweza kusaidia kuleta maendeleo katika maeneo yake. Kwa mtazamo ninaouona, katika watu wenye hali ngumu hivi sasa ni Waheshimiwa Wabunge. Waonewe huruma! Waangaliwe kwa jicho ambalo litaweza kuwafanya Wabunge hawa, hasa wengi wa CCM, warudi katika miaka mitano ijayo. Vinginevyo, wanakwenda na maji kama eneo hili halikufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumza vile vile suala zima la zile shilingi milioni 50. Naomba nishauri kwamba fedha hizi tusiangalie kuzipeleka kwenye SACCOS, ziangaliwe kuboresha mazingira ya vijiji ambavyo vinapelekewa hii fedha, kwa sababu, kuna mahitaji mengi ya msingi; hospitali hazijamalizika, zahanati, shule zimekaa magofu na zilizomalizika hazina vitendea kazi, hazina madawati, hazina vitu mbalimbali; maji hamna na barabara ni mbovu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi fedha ni muhimu sana, lakini ziangalie kujenga maendeleo ya vile vijiji, viwe bora zaidi na watu wanahitaji kuishi maisha bora zaidi kuliko hali ilivyo sasa hivi. Kila mmoja anatamani fedha ile iende katika eneo lake kwa ajili ya kuboresha vijiji vilivyokuwa na hali mbaya katika maeneo husika. Naomba kasma ikatwe kwa ajili ya kuangalia vikundi vya akinamama na hizo SACCOS, lakini zaidi fedha hizi zielekezwe kuangalia miradi ya maendeleo katika kila kijiji ili kuboresha mazingira yaliyokuweko kule na kuwafanya watu wawe na maisha bora zaidi kwa kila Mtanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania bado tuna fursa nyingi ambazo Serikali kama itaweza kusimamia vizuri, tunaweza kutengeneza maeneo mengine ya mapato kuliko vyanzo ambavyo sasa hivi vimeainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Fursa iliyokuweko katika corridor ya Mtwara na hasa kwenye yale maeneo ya uchimbaji wa makaa ya mawe na chuma…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja.