Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Philipo Augustino Mulugo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia Wizara hii ya Maliasili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya msingi ni moja tu katika Wizara hii. Najaribu kukumbuka kwamba katika Maziwa madogo madogo katika Afrika, Ziwa Rukwa ndiyo Ziwa pakee kwa nchi ya Tanzania ambalo limetengwa kwa ajili ya kufuga mamba. Mamba ni wengi kweli na hata sasa hivi ninavyoongea samaki hakuna Ziwa Rukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wangu wa vijiji vya Some, Manda, Udinde, Rukwa, Maleza, Mbangala wanategemea samaki, lakini wanapoenda kuvua samaki hakuna samaki na wamedumaa. Nilikuwa nawasiliana na Mheshimiwa Mwigulu alipokuwa kwenye Wizara yake hapa nikamwambia jamani hebu tengeni fedha kwa ajili ya kufanya utafiti wa kuona kwa nini samaki hakuna Ziwa Rukwa. Katika hali ya kawaida samaki hawapo kwa sababu ya mamba ni wengi sana. Serikali inavuna mamba kidogo kwa mwaka vibali vya mamba 60 kwa mwaka wakati mamba wanazaliana sana kwa kila mwaka. Mheshimiwa Waziri, hebu jaribu kuliangalia hilo jamani wenzenu tunakufa kwa mamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani mimi kule Jimboni kwangu, Jimbo la Songwe malaria au magonjwa mengine haya hatuyajui sana, lakini mamba ndiyo kilio kikubwa kwa wananchi wa Jimbo la Songwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwa Mheshimiwa Malocha kule Jimbo la Kwela ni vilio vya mamba, vijiji ambavyo vimezunguka Ziwa Rukwa hata kwenye Jimbo la Mheshimiwa Silinde vilio ni mamba. Sasa wenzenu tunakufa kwa mamba Serikali inakuja hapa inasema eti huwa inawafidia watu wanaoliwa na mamba! Hebu niambieni mlishawahli kumfidia nani ambaye ameliwa na mamba?
Naomba kesho Mheshimiwa Waziri uniambie ulishawahi kumfidia mwananchi gani katika Ziwa Rukwa ambaye ameliwa na mamba ama labda mamba amemkamata hata mkono, sijawahi kuona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayesema hapa ndiyo muhanga wa mamba namba moja, baba yangu Mzee Augustino amekamatwa na mamba ni marehemu na mimi ndiyo nimemrithi, sijawahi kuona kwamba kuna pole ya Serikali, sasa siyo kuja kudanganya hapa kwamba huwa mnawafidia watu. Kesho nitashika shilingi uniambie fedha za baba yangu zipo wapi, hakuna! Huyo ni baba yangu, lakini mdogo wangu amekamatwa na mamba hakuna fidia, mama yangu aliyenizaa mimi amekamatwa na mamba hakuna fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni muhanga namba moja ndiyo maana nasema nachangia kwa uchungu au labda nitoe machozi hapa. Mimi ni yatima kwa sababu ya mamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena mimi ni yatima kwa sababu ya mamba! Mamba ni adui yangu namba moja. Sasa kama mamba ni adui kwa sababu yupo kwenye maji siwezi kumkamata, adui yangu mwingine ni Mheshimiwa Maghembe, Waziri wa Maliasili na Utalii kwa sababu ya mamba.
Naomba kesho uniambie fedha za baba yangu na mama yangu kwa ajili ya kunifidia mimi, kunipa pole ya mamba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nimefanya research toka mwaka 1990 mpaka leo wananchi wangu 128 wameuliwa na mamba. Wengine wananchi hawaendi kuvua samaki wanakwenda kuoga, wanakwenda kufua nguo na kadhalika wanajeruhiwa miguu, mikono, ni mamba. Nenda hospitali ya Mwambani pale Mkwajuni majeruhi ni kwa ajili ya mamba, sasa Serikali ipo wapi? Jamani tuoneeni huruma. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi lete watu wafanye utafiti, samaki wapo wapi Ziwa Rukwa mbona mmelitelekeza Ziwa Rukwa, hakuna namna nyingine yoyote ukisikia bajeti hapa zinakwenda Lake Tanganyika, zinakwenda Lake Victoria, zinakwenda Lake Nyasa, utafiti wa bahari, jamani Ziwa Rukwa kwetu ndiyo uchumi wetu ukiacha kilimo! Hebu njooni muangalie wenzenu tunakufa jamani, kama nilivyosema mimi nimeathirika sana naomba niache tu, naweza nikaanza kulia hapa.