Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Andrew John Chenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii niweze kuchangia kidogo tu katika hoja hizi mbili zilizo mbele ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa taarifa zake nzuri alizoziwasilisha siku ya Jumatano, tarehe 8 Juni humu Bungeni, kwa maana ya kwamba ile taarifa ya uchumi (the state of the economy) pamoja na taarifa kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2015/2016 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha. Aliziwasilisha kwa ufasaha, na nimshukuru sana na timu yake, sio kazi rahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, hii ni bajeti ya kwanza kwa uongozi wa awamu ya tano ya nchi yetu. Lakini kama ilivyo bajeti yoyote, lazima uangalie kwa mwaka uliopita, kwa maana hiyo ni mwendelezo wa hayo mazuri ambayo yamefanyika huko nyuma, na tunaendelea kuyaboresha zaidi. Na unaiona sura ya bajeti hii, imebeba mambo mengi mazuri, ukianzia kwenye mpango, na bahati nzuri mwaka huu tunaanza kutekeleza mpango huu wa pili wa maendeleo, na mwaka wa kwanza katika Mpango huo wa Pili wa Maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 30, ameeleza maeneo ya vipaumbele katika mwaka ujao wa fedha; yapo katika makundi manne, kwa sababu ya muda sitaweza kuyasema, lakini ndiyo naona mwelekeo mzuri wa kule ambako Serikali inataka kuipeleka nchi yetu, lakini hasa katika kukuza uchumi na hivyo kuleta ustawi mzuri wa wananchi wetu, mimi naipongeza sana Serikali kwa hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, niwapongeze sana, unafahamu ukiangalia mapato, ongezeko la makusanyo ya mapato, Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tuipongeze Serikali, tuipongeze TRA na wote hao walioifanikisha kwa sababu kwa mara ya kwanza tumeweza kwenda zaidi ya shilingi trilioni moja kwa mwezi, sio kitu kidogo, ukilinganisha na mwaka jana ambapo tuliweza kwenda mpaka shilingi bilioni 900 na kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tuna changamoto kubwa ambayo Waziri wa Fedha ameielezea kwenye hotuba hii, kwamba tukiweza kuyasimamia maeneo ambayo tunajua ni oevu kwa mapato ya Serikali, tutaweza kufanya vizuri zaidi. Ameelezea matumizi ya mfumo wa zile mashine elektroniki. Tupende tusipende Waheshimiwa, najua bado utamaduni wetu wa kutodai risiti na kutotaka kufanya nini, bado, lakini huu ni mwanzo mzuri. Tukiweza kuyasimamia hayo sasa hii dhana nzima mimi naiona ya kuingiza mapato yasiyo ya kodi kwamba TRA iyakusanye, mimi naamini tutafanya vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili la misitu na mazao yanayotokana na misitu, mimi naelewa there is a lot to be collected na ninarudia msemo wa Kiingereza; taxes are never paid, taxes are collected. Na tukiangalia maeneo ambayo tunajua yapo mapato halali ya Serikali tutayakusanya, na hilo nimpongeze sana Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kuanza na kasi hiyo ya kuziba mianya ambayo ilikuwa inapoteza mapato ya Serikali. Kwa hiyo natoa pongezi hizo kwa nia njema kabisa na kuwataka wote tukaze buti, twende mbele kwa faida ya Taifa hili. (Makofi)
Kwa Watanzania, na sisi kama viongozi, mimi nasema kama tunataka Tanzania uchumi ukue, lazima tukubali wote sasa leo tutoe jasho kidogo kwa faida ya kesho. Unaumia leo, lakini unajua unajenga msingi imara wa uchumi wa nchi yako kwa faida ya watoto wako, kwa faida ya wajukuu zako, kwa faida ya Tanzania hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo moja, wataalam wa uchumi watasema, lakini mimi niliyefundishwa, unaiona kabisa bajeti ya Serikali, nia ni nzuri kabisa lakini nakisi ya bajeti tuliyonayo ni shilingi trilioni 7.48. Sasa imepanda kidogo ukilinganisha na huu mwaka tunaomaliza na ukiipima dhidi ya Pato la Taifa unaona imepanda kutoka asilimia 4.2 kwenda asilimia 4.5, sasa hii ina implications nyingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nasema wataalam wetu waliangalie hili, kwa sababu standard norm ni asilimia tatu, sasa tukiruhusu iende kwa speed hiyo, hii nakisi ya bajeti itatusumbua. Ukiangalia kwa sasa Waziri anapendekeza shilingi trilioni 5.37 zipatikane kutoka ndani, maana yake ni nini kwa benki zetu? Kwa benki zetu hizi, shilingi trilioni 5.37 ni pesa nyingi, na maana yake uwezo wa sekta binafsi kwenda kufika tena kwenye benki hizi tunaanza kuiminya; tulione hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mimi nasema lazima tukope na nilisema juzi, tunakopa pesa hizi kwa masharti yapi na tunazielekeza wapi? Naona haziendi kwenye matumizi ya kawaida, hongereni sana Serikali kwa hilo, zinakwenda kwenye maendeleo, zinakwenda kulipa hati fungani na dhamana za Serikali ambazo zimeiva, huo ni utaratibu wa kawaida. Lakini sehemu kubwa inakwenda kwenye maendeleo na ndiko tunakotaka tuone. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema juzi wakati tunajadili Fungu 50 (Vote 50), basi Serikali itueleze zoezi la nchi yetu kupata sovereign rating limeishia wapi? Kwa sababu tukiweza kupata sovereign rating na inakuwa inahuishwa kila wakati tutaweza ku-access mikopo hii kwa gharama nafuu lakini pia na Private Sector itaweza na yenyewe hivyohivyo ikapata access kwenye masoko ya Kimataifa kupata fedha ambazo tunazihitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niunganishe hapo hapo miradi ya maendeleo kwa upande wa PPP. Kweli twende mbali zaidi, maana sasa hivi kila siku unaambiwa ni mradi wa Dar es Salaam, mabasi ya kasi yale; sawa ni PPP ile au kutengeneza dawa inasemwa inakuja, sawa, barabara ya Chalinze - Dar es Salaam, sawa, Kinyerezi umeme sawa. Lakini yapo maeneo mengi, kwa nini Serikali inakuwa nzito sana katika eneo hilo la ubia kati ya sekta binafsi? Kwa sababu hiyo ndiyo itaiwezesha Serikali kuachana, maeneo fulani yaende kwa sekta binafsi kwa ubia na Serikali, tufanye hivyo kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho, unaona ukurasa wa sita wa taarifa ya uchumi, kilimo...
Ohoooo! Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, naunga mkono hoja hizi mbili.