Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa namna ya pekee naomba niwape hongera nyingi sana Waziri na Naibu Waziri na timu nzima ya wenzetu wa Wizara ya Maliasili. Naomba pia niwape hongera za dhati kabisa Mhifadhi Mkuu na Wahifadhi wa Gombe na Mahale National Parks kule Kigoma, wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijasema ninachotaka kusema, mimi hii Kampuni ya Green Miles naifahamu, nilikuwa kwenye Tume ya Wanyamapori. Kama haya yanayosemwa na Kambi ya Upinzani ni ya kweli, basi lipo tatizo kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo kampuni ya Green Miles tulii-disqualify nikiwa kwenye Tume kwa sababu ilikosa sifa. Nafikiri ni mambo ambayo Wizara mnaweza mkakaa na wenzenu mkayafanyia kazi vizuri kuhakikisha kwamba mambo yanakwenda vizuri. Moja ya disqualification yao waliidanganya Tume kipindi kile na kwa kweli tukawa-disqualify. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara na wataalam wenu mkae chini ikibidi mwende kule kwenye eneo lenyewe muweze kujiridhisha na hali halisi iliyopo pale. Maana yake nakumbuka Waziri wa Maliasili aliyepita hiyo kampuni aliinyang‟anya leseni kwa kukosa sifa. Sasa nasema haya mambo yako ndani ya Wizara, mnaweza mkaangalia namna ya kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie juu ya ikolojia ya Kigosi Moyowosi. Hii ikolojia Kigosi Moyowosi inaanzia Mkoa wa Shinyanga eneo la Bukombe inakuja Kibondo inakwenda Kasulu mpaka Uvinza. Naomba niseme eneo hili limevamiwa na mifugo wengi sana na kusema ukweli linatishia uhai wa Mto Malagarasi na siyo Mto Malagarasi tu inatishia hata chepechepe (wet land area) ya Mto Malagarasi na hakika inatishia uwepo wa Ziwa Tanganyika. Nadhani ni jambo muhimu sana Serikali ikae na kuangalia namna njema na nzuri ya kuwaondoa hawa wafugaji na kuwatafutia maeneo mengine ya kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme siyo jambo jema sana Mheshimiwa Waziri mkaanza kuwa na utamaduni wa kuua ng‟ombe kwa risasi, hilo jambo linatufedhehesha sana kwa kweli. Kama nchi kunakuwa na makosa yamefanyika basi nchi hii ni ya kiistaarabu yatatuliwe kistaarabu. Wafugaji hawa waelekezwe, waondoshwe kwenye hifadhi, wasiharibu mazingira yetu, lakini kitendo cha kuua ng‟ombe, kupiga risasi ng‟ombe kinaturudisha kwenye ujima kwa kweli siyo ustaarabu wa leo. Naomba hilo jambo lizingatiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ikolojia hiyo hiyo ya Moyowosi kuna msitu mashuhuri sana unaitwa Msitu wa Makere Kusini maarufu kama Pori la Kagera Nkanda. Hilo pori lilikuwa gazetted mwaka 1954, Septemba, nina hakika Wabunge wengi mlikuwa hamjazaliwa kwa sababu hata mimi mwenyewe nilikuwa sijazaliwa. Eneo hilo lilikuwa halina watu kipindi hicho lakini sasa hivi limejaa watu na kuna misuguano mikubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naangalia hotuba ya Waziri inazungumzia juu ya usimamizi wa misitu na Wakala kufanya mapitio, ukurasa wa 59 wa hotuba yake. Katika hilo eneo la Kagera Nkanda lenye wanavijiji wengi kuna migongano ya wakulima na hawa wenzetu wa TFS. Naomba mipaka ile ya mwaka 1954 iweze kuhuishwa hawa wakulima wapate maeneo yao ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda nimuarifu Profesa kwamba ikolojia ile haitishiwi na kilimo cha wananchi wale wa vijiji vya Wilaya ya Kasulu bali ikolojia ile inatishiwa na mifugo mingi toka nchi jirani na mifugo mingi inayoingia katika eneo lile bila utaratibu. Tafadhali sana, kama alivyobainisha ukurasa wa 59 wa hotuba yake, naomba mipaka ile ihuishwe vizuri, tena wametumia neno zuri soroveya. Tunaomba usoroveya huo mkaurudie upya ili yale maeneo ambayo wananchi wameyalima kwa muda mrefu waendelee kuyatumia bila kuwasumbua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wenzetu wa TFS wamekuwa ni walaji rushwa, wanasumbua watu wetu na kusema kweli hakuna tija hata kidogo. Mheshimiwa Waziri naomba hilo alizingatie na nimeshazungumza naye. Wananchi wetu wa vijiji vinavyozunguka pori lile wamekuwa wakilima pale kwa miaka 20 iliyopita na tumewazuia sisi kama Halmashauri wasikate miti wanalima kilimo rafiki. Kwa hiyo, ni muhimu sana Profesa akatoa maelekezo hawa watu wa TFS wasiwasumbue waendelee kujikimu kupata maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo Mheshimiwa Waziri ningeomba Sheria ya Misitu Na.14 itazamwe upya kwani imepitwa na wakati.
Nchi hii ina watu wengi sasa, kabla watu hawakuwa wengi kiasi hiki. Ni vyema sheria hii ingeangaliwa na kusema kweli yale maeneo ambayo yamekosa sifa, yako maeneo Profesa yamekosa sifa kwa mfano mapori ya akiba na open area wapewe wananchi wakiwemo wafugaji tupunguze migogoro hii ambayo kama Taifa inatufedhehesha kwa kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mmoja mdogo, kwa mfano eneo la wazi la Wembere lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 10,000 limepoteza sifa, hakuna mnyama tena, wananchi wanakatakata mikaa mle lakini hawa watu wa maliasili wanazuia watu kufanya shughuli zao. Maeneo kama hayo mngeyahuisha tukapunguza migogoro hii ya wakulima na wafugaji ili watu wafanye shughuli zao kwa sababu yale maeneo hayana sifa tena ya uhifadhi na yako mengi tu mkifanya tathmini mtagundua hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda nilizungumzie ni kuhusu Sekta ya Utalii. Ukisoma hotuba ya Waziri ukurasa wa 81 unazungumza Wizara na World Bank kuandaa mpango mkakati wa kuendeleza utalii, ni jambo jema, lakini hawajaeleza time frame ya huo mpango mkakati wao. Ukurasa wa 89 umezungumzia kuainisha vivutio vya utalii nchini na wametaja Mikoa ya Mwanza, Mara, Kigoma, Geita na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Wizara, nilidhani kuanza kubainisha vivutio vya utalii pamoja na vivutio vya utamaduni ingekuwa ni input kwenye mpango mkakati wa Wizara. Kipi kinaanza, bila shaka unaanza mpango mkakati kabla ya kuzungumzia habari ya vivutio na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 81 na 89 wa hotuba ya Wizara, naomba wautazame upya ili kuleta maana zaidi kwamba lazima uanze na mpango mkakati halafu vivutio vya utalii katika Mikoa ya Kigoma, Mwanza, Mara na kadhalika pamoja na culture tourism ziwe ni input kwenye mpango mkakati wenu. Bila shaka kama mnafanya kazi hiyo na World Bank ingekuwa jambo la busara sana basi mpango mkakati huo uwe na time frame na mtueleze katika mpango mkakati huo mmeandaa kufanya mambo gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri baada ya mpango mkakati kukamilika, basi tu kwa mahusiano mema na Wabunge wenzake, Waziri atuletee mpango mkakati huo tuuone ili tuweze kuwasadia baadhi ya mambo ambayo tunafikiri yanafaa kuwemo katika mkakati huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ambalo napenda niliseme kwa ujumla wake kwa Mheshimiwa Waziri, ni kutangaza utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo hasa Kagera Nkanda, naunga mkono hoja hii. Ahsante sana.