Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia katika Bunge lako Tukufu, naomba nianze kwanza kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa fursa aliyonipa ya afya njema na kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kusema yale nitakayoyasema ikiwa ni katika hali ya kujibu baadhi ya hoja za Wabunge ambazo wamezitoa na nyingi tutazijibu kwa maandishi na watapata nakala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nichukue fursa hii pia kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo ameniamini na kunipa fursa ya kuweza kuniteua kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na niseme sitamuangusha. Kwa kupitia kwake pia niwashukuru sana wananchi wa Ilemela ambao wamenipa dhamana hii ya kuwawakilisha Bungeni na hatimaye Mheshimiwa Rais akanipa wadhifa mwingine wa kuweza kumsaidia katika Wizara niliyoitaja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais. Ni wazi atatuwakilisha vizuri na ameonyesha njia kwa namna alivyoanza. Nimpongeze pia Waziri Mkuu kwa kuteuliwa kwake na hasa wananchi wa Jimbo lake la Ruangwa kwa kumchagua kuwa Mbunge na hatimaye akateuliwa kuwa Waziri Mkuu na Bunge hili likamthibitisha. Niwapongeze Mawaziri na Naibu Mawaziri wote ambao wamechaguliwa. Nimpongeze Spika pamoja na Naibu Spika na Wabunge wote kwa nyadhifa zenu ambao mnategemewa sana na wananchi kwa sababu ya kuwapa ridhaa kwa hiyo wana matumaini makubwa kutoka kwenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shukurani zangu pia zimwendee sana Waziri na mtani wangu Mheshimiwa William Lukuvi kwa ushirikiano anaonipa katika kufanya kazi. Ni muda mfupi tu ambao tumekuwa pamoja naye lakini najisikia kuwa na faraja kubwa kwa sababu ni mentor mzuri ambaye anaweza kukuelekeza, akakushirikisha na ukaweza kufanya kazi vizuri. Na mimi nasema nitatoa ushirikiano kwake wakati wote kwa namna ambavyo anaelekeza nadhani imenifanya pia nitambue na nielewe Wizara kwa muda mfupi, nasema tutafanya kazi vizuri.
Pia niwashukuru watendaji wote wa Wizara pamoja na taasisi na mashirika yaliyoko chini ya Wizara wamekuwa na ushirikiano mzuri katika kufanya kazi hizi na hatimaye kwa muda mfupi sana huduma katika Wizara zimeboreka na watu wanahudumiwa vizuri na mrejesho tunaupata. Kwa hiyo, namshukuru sana Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi na watendaji wote walioko katika idara nilizozitaja.
Aidha, pia nishukuru sana Ofisi ya TAMISEMI ambayo nayo tumekuwa tukishirikiana sana katika kutatua kero mbalimbali. Ardhi ni suala mtambuka na mambo mengi yanaletwa ardhi lakini yanagusa Wizara nyingi, kwa hiyo, nishukuru kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shukrani zangu nisisahau familia yangu, namshukuru sana mume wangu Julius Mabula, watoto wangu David, Javine, Diana na Dorothy, baba na mama wazazi Silvester Lubala ambao wameweza kunilea na kunifanya niwe kama nilivyo. Nashukuru ndugu, jamaa na marafiki ambao wote wamekuwa karibu sana katika kunitia moyo na kuweza kufanya kazi kwa umoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru Wabunge wote wa Mkoa wa Mwanza ambao tunashirikiana sana katika kazi zetu kuhakikisha kwamba Mkoa unakwenda vizuri. Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru viongozi wa dini madhehebu yote Mapadri, Mashehe, Maaskofu katika madhehebu mbalimbali ambao kwa muda wote wamekuwa wakiniombea na kunipa ushauri wa kimwili na kiroho na wamenifanya kwa kweli nisimame imara katika kazi zangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie shukurani zangu si kwa umuhimu kwa kukishukuru sana Chama changu ambacho kimeniamini kikaniteua na kunifanya nigombee katika Jimbo ambalo kwa miaka mitano tulikuwa tumepangisha lakini mpangaji akashindwa masharti ya upangaji tumemwambia apumzike ili tuweze kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani zangu naomba sasa nianze kujibu baadhi ya hoja ambazo zimetolewa na Wabunge katika michango yao ya maandishi na wengine kwa kuzungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuzungumzia ile taarifa ya Kambi ya Upinzani ambayo Waziri Kivuli aliiwasilisha hapa na nimshukuru tu kwamba taarifa yake ilikuwa ni nzuri kwa jinsi alivyoileta ina changamoto na mambo ambayo ameyasema hapa tutakwenda kuyatolea taarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa ya Upinzani imezungumzia suala la uporaji holela wa ardhi katika maeneo mbalimbali, wamezungumzia ufisadi wa ardhi unaofanywa na viongozi na hakuna hatua zinazochukuliwa na wamezungumza kuhusu watu wa chache kuhodhi ardhi. Katika haya yote niseme utoaji wa ardhi kwa wawekezaji unazingatia zaidi sheria za nchi. Wizara inaelekeza mamlaka ya ugawaji kuzingatia sheria hiyo na Wizara imekuwa ikilisimamia hilo na imetoa mwongozo kwa Wakuu wote wa Wilaya ili kupitia katika vikao vyao ili ardhi isitolewe kiholela kama ambavyo imekuwa ikileta migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia hatua zinachukuliwa kwa ardhi ambayo inapatikana kinyume na utaratibu. Wizara imeagiza Halmashauri zote nchini kufanya ukaguzi na uhakiki wa mashamba pamoja na viwanja ili kuweza kuratibu na kuona yapi ambayo yanamilikiwa isivyo kihalali ili hatua ziweze kuchukuliwa. Katika kutekeleza hilo pia ni wazi wote ni mashahidi tumeandaa kitabu ambacho kila mmoja anacho kimeainisha migogoro yote ambayo ipo. Mingine kweli inatokana na watu kukiuka taratibu, lakini mingine pia ni kwa utendaji pengine ambao umekiuka maadili ya kazi kwa watendaji wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la fidia ambalo amelizungumzia. Sheria ya Ardhi na kanuni zake zimeweka utaratibu wa kukadiria na kulipa fidia ya ardhi na fidia yake inatofautiana kutegemeana na eneo ambapo ardhi ipo. Kwa hiyo, kuna ardhi nyingine unakuta bei yake iko juu na nyingine iko chini. Pia hapa tutambue kuna wengine ambao wanalalamika lakini ardhi zao zilitwaliwa kabla ya ile sheria ya mwaka 2002 ambayo imeingiza ardhi pia kuweza kuthamanishwa. Kwa hiyo, wengi wanarudi kudai kuongezewa fidia lakini wakati huo huo walishathaminishwa kwa sheria ya kabla ya sheria mpya ambayo imeingiza na ardhi kuwemo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la ukaguzi wa ardhi ambalo limetolewa na Mheshimiwa Mdee, lakini na hapa mmeliongelea. Niseme Wizara ilishaanzisha kitengo kinachoshughulikia ardhi kwa ajili ya uwekezaji na pia imeziagiza Halmashauri zote nchini kufanya ukaguzi wa mashamba. Hii tunayofanya katika kunyang‟anya baadhi ya mashamba ambayo yametelekezwa sehemu kubwa pia tutachukua ili kuweza kuwa na akiba ya ardhi katika mtazamo huo kwa sababu siyo yote itakayogawiwa kwa wananchi na siyo yote ambayo watapewa tena wawekezaji lazima tutakuwa na sehemu ambayo itakuwa ni kwa ajili ya akiba kwa matumizi ya baadaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kutolipwa fidia ambalo limezungumziwa na hasa wamezungumzia pia maeneo ya jeshi, walizungumzia maeneo ya Kaboya na maeneo mengine yako Mwanza, Ilemela na mengine yametajwa eneo la Kusini. Niseme Waziri wa Ulinzi wakati anazungumzia aliainisha vizuri kabisa namna ambavyo wanakwenda kulipa fidia katika ile migogoro ambayo wanatofautiana sana kati ya jeshi na watu. Kwa hiyo, niseme jeshi limeweka utaratibu wa kutambua mipaka yao na kujipanga katika kulipa fidia. Wameliweka wazi hili na nisingependa kulirudia kwa sababu tayari iko kwenye hotuba ya Waziri wa Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumziwa suala la wananchi wa Kata ya Kahororo kutolipwa fidia. Tukumbuke kwamba maeneo mengi ambayo yanachukuliwa na wawekezaji au taasisi mbalimbali suala la kulipa fidia linakuwa siyo suala la Wizara ya Ardhi ni la mwekezaji au taasisi inayochukua. Hili suala la Kahororo ni suala la Mamlaka ya Maji ya Bukoba ambapo thamani yake ni shilingi 1,961,609,000. Kwa hiyo, hizi zinatakiwa kulipwa kwa wale wananchi kwa kadri walivyothaminishwa katika uthamini uliofanyika mwaka 2014 kwa wananchi 186 na kiasi hiki kinatakiwa kulipwa.
Kwa hiyo, suala la ulipaji wa fidia lazima pia tuangalie ni nani anayehusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara ilishatoa Waraka kwamba hatutapokea jedwali lolote linalotaka watu waliofanyiwa uthamini kwa ajili ya kulipwa fidia kama hatutaridhishwa au kuhakikishiwa kwamba kuna pesa iliyotengwa. Kwa hiyo, nitoe rai kwa Halmashauri zote wakileta madai yoyote ya fidia na wakitaka wathamini waende ni lazima tuwe tumejiridhisha kwamba kuna pesa imetengwa na watu watalipwa ili tuweze kufanya kazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna maeneo ya EPZ ambayo nayo yanadaiwa fidia. Kuna baadhi ambayo yalichukuliwa na yalikuwa yanalipwa fidia kulingana namna fedha zinavyopatikana. Maeneo ambayo yamecheleweshewa fidia kwa muda mrefu Serikali itaangalia uwezekano wa kuyarejesha mikononi mwa wananchi ili yaweze kutumika kwa kazi nyingine kwa sababu imekuwa ni kero kubwa na wananchi wamekuwa wakilalamika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu makampuni makubwa ya nje kuhodhi maeneo sehemu mbalimbali. Niseme tu Serikali inafanyia kazi orodha ya mashamba kama tulivyosema tayari tumeshaliweka katika utaratibu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumzia pia suala la Mabaraza ya Ardhi na hili limezungumzwa na Wabunge wengi kwa uchungu sana. Naomba niseme tu kwamba ni wazi kama ilivyozungumziwa Mabaraza ya Ardhi hayako ya kutosha lakini hayana watendaji wa kutosha na kesi zake zinakaa kwa muda mrefu. Niseme tu kwa mwaka huu tumepeleka maombi maalum kwenye Wizara inayohusika kuomba tupatiwe Wenyeviti kwa ajili ya Mabaraza hayo yatakayofunguliwa. Tutafungua Mabaraza 47 na tutaanza na matano. Katika kuyafungua Mabaraza hayo kuna maeneo mengine ambayo yanahitaji ushirikiano wa Wilaya husika kwa sababu shughuli ya kuwa na maeneo na ofisi kila mahali inakuwa na ugumu wake kulingana na rasilimali zilizopo. Hata hivyo, tumebaini mahitaji halisi ya Mabaraza haya kwa lengo la kuboresha na tayari vifaa mbalimbali vimeanza kupelekwa katika maeneo kusudiwa. Aidha, kuhusu watumishi kama nilivyosema tumewakilisha ombi maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme katika suala la Mabaraza ya Ardhi naomba tu tuwe na imani kwamba tunakwenda kulitatua tatizo hilo muda ambao si mrefu kuanzia sasa ili wananchi waweze kupata haki kwa wakati. Pia tutaangalia katika zile Wilaya kama watakuwa hawajapangiwa kuwekewa Baraza ambapo unakuta Wilaya moja inahudumia Wilaya zaidi ya tatu au nne, tutaangalia ni Wilaya gani ambayo ina kesi nyingi na inahitaji huduma hiyo kwa haraka. Kwa hiyo, tutaangalia badala ya Mwenyekiti kuwa katika eneo ambalo halina kesi nyingi basi itabidi tumhamishie katika eneo ambalo lina kesi nyingi ili aweze kuhudumia na atakuwa anakwenda kama visiting chairperson kwenye lile eneo kwa maana ya Mwenyekiti wa Baraza. Kwa hiyo, tuseme tu kwamba hili tutalifanyia kazi kulingana na namna ambavyo tutakuwa tumeyapata. Kwa hiyo, tunaanza na hayo ambayo tayari yapo matano, lakini yale mengine 47 yote yako katika mchakato mzuri wa kuweza kuyaanzisha, kote tutakwenda kuanzisha kama ambavyo tumesema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la National Housing. Kambi ya Upinzani kwenye hotuba yao nao wamelizungumza, lakini wachangiaji wengi sana pia wamezungumzia suala hili na wamezungumza kwa uchungu sana. Niseme walikuwa na haki ya kuyasema hayo yote kwa sababu National Housing ni kioo cha jamii na ni shirika pekee baada ya uhuru linafanya vizuri zaidi kuliko mengine yaliyoanzishwa kipindi hicho na mtakumbuka lilianzishwa mwaka 1962 baada tu ya uhuru. Kazi wanayoifanya sasa na wote ni mashahidi, mmeweza kusifia msimamizi wa shirika hilo lakini tuseme pongezi hizo zinaenda kwa watumishi wote katika idara husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wamezungumza sana kwamba nyumba zinazosemwa ni za gharama nafuu si za gharama nafuu. Naweza kukubaliana na wanachozungumza kwa sababu ya hali halisi ya namna ambavyo National Housing wanavyopata maeneo yale na namna wanavyohangaika na miundombinu. Kama Wizara tumetoa maelekezo, tumesema kama National Housing sasa wanataka kujenga nyumba za gharama nafuu ni lazima waendelee kuwa wabunifu, waendelee kufanya utafiti kuweza kujua ni kwa namna gani watajenga nyumba za gharama nafuu kwa kuangalia vifaa. Achilia mbali lile suala la VAT ambalo tumelizungumzia, hili bado tunalizungumza Kiserikali kuweza kuona ni jinsi gani VAT itakuwa waved ili waweze kupata nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa sasa hivi tunaloangalia ni namna ya kushirikisha taasisi zingine kama TANESCO, Idara ya Maji, Idara ya Ujenzi (barabara) ambao ni Halmashauri zenyewe, waweze kufanya maandalizi ya ile miundombinu mapema ili National Housing wanapokwenda kule basi waweze kufanya kazi kwa pamoja. Lingine pia Halmashauri zetu pamoja na kwamba tunalalamikia National Housing kutowafikia, lakini bado hatujawapa fursa ya kuweza kuja kupata maeneo ambayo yatapunguza gharama. Kwa sababu wakija pale NHC wanatakiwa walipe fidia, watengeneze miundombinu hiyo, tumewaambia wajipange vizuri na wafanye networking na mashirika mengine ambayo yanashughulika na huduma nilizozisema ili waweze kuona ni jinsi gani hizo nyumba zitapungua gharama kulingana na namna ambavyo wamejipanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa NHC wameshafikia Halmashauri 25 na wameshajenga nyumba ziipatazo 1,076 kwa maana ya zile za gharama nafuu. Kwa hiyo, niseme kwamba wapo katika utaratibu ambao unakwenda sambamba na mahitaji jinsi yalivyo ili kuweza kuona wanafikia wananchi kutegemeana na hitaji la Halmashauri. Niwaombe Halmashauri ambazo ziko tayari katika hilo basi waweze kuwapa nafasi ya kuweza kufika katika maeneo haya na kuwapa maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumzia hati za kimila kutotambulika. Naomba niwataarifu tu Waheshimiwa Wabunge kwamba hati za kimila kuna Benki ambazo tayari zinazitambua na zinapokea. Ttunayo benki ya CRDB, TIB, Exim Bank, NMB, Meru Community Bank ambazo tayari zimeshazitambua hizi hati za kimilila na zinatoa mikopo. Niseme haya yote yanafanyika na bado Serikali inaendelea kuongea na taasisi za fedha ili waweze kuthamini na kutambua kwamba zile hati ni hati ambazo zinahitaji kutambulika kama ambavyo benki zingine zimeanza kuzitambua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumzia masuala ya upangaji miji na huduma za jamii katika maeneo mbalimbali. Uvamizi wa maeneo bila kuwa na mipango mizuri ya matumizi bora ya ardhi hatutafika. Kama tulivyosema ni asilimia 15 tu ya ardhi ambayo imepangwa lakini ni jukumu pia la Halmashauri zetu kupima ardhi. Halmashuri zetu zinapaswa kutenga bajeti kidogo kidogo angalau wakapima kwenye maeneo yao. Tukikaa tukisubiri Wizara tutafanya kazi hiyo lakini itatuchukua muda mrefu.
Kwa hiyo, niombe Halmashauri zetu ziweze pia kuchukua wasaa wa kuweza kuyapima yale maeneo na kuweka matumizi bora ya ardhi ili kupunguza migogoro hii ambayo ipo. Kwa sababu kama tutaachia Wizara, kazi itafanyika kama tulivyoanza katika Wilaya ya Kilombero, Ulanga na Malinyi lakini tumeona kwamba huu ni mradi wa miaka mitatu ambayo ni mingi sana tutafikia vipi maeneo yote kama mlivyosema. Niseme hilo ni la kwetu sote tushirikiane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kutokuwa na Maafisa Ardhi Wateule, Halmashauri pendekezeni majina ya wale ambao wamefikia sifa hizo, mlete kwa Kamishina. Kwa sababu tayari tunao Makamishna Wasaidizi kwenye Kanda nane, watafanya kazi ya kuwateua watumishi hao ili waweze kufanya kazi hiyo.
Suala la upungufu wa watumishi bado tunalifanyia kazi kama nilivyosema pia tumeomba watumishi wengine waweze kuongezwa katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba mambo yaliyozungumzwa ni mengi ambayo yanahitaji pia kuwa na utulivu katika kuweza kuyapitia moja baada ya lingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ambalo nataka kusema ni kwamba masuala haya na hasa ya upimaji na mipango miji, tuna master plan ambazo zimeandaliwa katika miji yetu ya Mwanza, Arusha, Dar es Salaam ambao ulikuwa umeharibika sana unaandaliwa upya kwa kuzingatia mpango kabambe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana tuwaelimishe wananchi wetu wasiwekeze katika maeneo ambayo watakuja kupata shida baadaye kwa sababu master plan zinakuwa zimeandaliwa lazima waangalie waweze kujua katika eneo lake katika mpango uliopo panatakiwa kujengwa nini? Kwa hiyo, kama ni suala la umilikishaji na uendelezaji aweze kuendeleza katika hali halisi ambayo ndiyo mpango uliopangwa ili asijepata hasara baadaye anaambiwa abomolewe kwa sababu amejenga kinyume na taratibu au hakuzingatia mpango mji kwa kule ambako tayari mipango miji imeandaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge wa Misenyi amezungumzia habari ya kupanga mji mzuri kule kwao. Eneo lolote ambalo wamejiandaa katika kuweka kamji kadogo kazuri katakakofuata sheria na taratibu walete, Wizara ipo tayari tutasaidiana pia na wenzetu wa National Housing kuhakikisha kwamba huo mji unapangika vizuri na unajengwa majengo mazuri. Hata kama siyo National Housing tutaangalia pia nani anaweza akafanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Wabunge walilalamikia kuhusu ubovu wa majengo yanayojengwa na kulazimu kubomolewa. Naomba niwaambie, katika jengo lililobomolewa pale Dar es Salaam National Housing hakuwa amejenga yeye lilijengwa na mtu mwingine, majengo yote ya Nationa Housing yanakwenda vizuri. Kwa hiyo, wale wanaotaka kuwa na miji mizuri bado msisite kutumia Shirika la Taifa ambalo linaweza likafanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi yamejadiliwa lakini niseme haya ambayo nimeyadodosa tu kwa kuyapitia moja moja, kidogo kidogo bado niseme kwamba tutayajibu yote na Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa na yeye atajibu baadhi ya hoja. Niseme kwa wale wanaojenga maeneo yasiyofaa na kupatiwa huduma za maji, umeme na kadhalika, utoaji wa huduma kwa wakazi waliojenga maeneo hatarishi unafanywa na mamlaka na taasisi kwa kutoa huduma kwa msingi wa kibiashara na hata wale waliobomolewa ambao pengine walikuwa wana hati, Wizara ilishawaambia walete ili tuweze kutambua. Kama alikuwa na hati halali ya Wizara, tunajaribu kupitia na kuweza kuona tutawapa alternative ipi ya kuweza kuwapatia viwanja vingine. Habari ya kuwekewa maji, umeme isiwe ni sababu ya kujenga kwenye maeneo ambayo ni hatarishi. Wale wanafanya kazi zao kibiashara ukimwambia alete maji analeta kwa sababu anajua tu kwamba ni eneo ambalo anapeleka huduma. Kwa hiyo, niseme tupo pamoja katika kuhakikisha tunapanga miji yetu ili tuweze kuona kwamba ni jinsi gani tutakwenda pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala zima ambalo tumesema ni la utatuzi wa migogoro ambalo Waziri wangu atalizungumzia kwa kirefu. Hili suala ni mtambuka na kama ambavyo tumelieleza tutakwenda kukaa pamoja na Wizara zinazohusika ambazo ni Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Maliasili na Utalii, Kilimo, Uvuvi na Mifugo na Maji tuweze kuona kwa sababu migogoro mingi imekuja kwenye Wizara lakini ukiangalia kitabu chetu tulikuwa tunaainisha pia kuona kwamba mgogoro huu utatatuliwa na Wizara ngapi, kama ni ya kwetu tumeonesha na Wizara nyingine anayofuatia tumeionesha. Haya yatafanyika katika utaratibu ambao utakuwa umewekwa vizuri ambao utatusaidia sisi sote kuepuka hiyo migogoro ambayo inajitokeza mara kwa mara na si lengo la Serikali kuweza kusema kwamba tuweze kuhatarisha maisha ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba haya yote tunayokwenda kuyafanya tunategemea zaidi ushirikiano wa Wabunge. Tayari kama Wizara tumeshawezesha kwa maana ya kupata zile nyaraka muhimu. Kwa hiyo, tunategemea pia mtakuwa ni sehemu ya utoaji wa elimu. Kwa sababu siku zote tunasema ardhi ni mtaji bila kufahamu sheria na kanuni zinazotawala ardhi bado itakuwa ni shida. Kwa hiyo, nyaraka hizo ni nyenzo mojawapo ambayo tumeitoa itakayotusaidia sisi sote, Wabunge pamoja na Waziri mwenye dhamana katika maeneo hayo ili kuweza kuona kwamba kazi hii tunaifanya katika muda muda mfupi kwa kusaidiana na hatuzalishi migogoro mingine kwa sababu taratibu tutakuwa tumezizingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nimalizie kwa kuwashukuru sana Wabunge kwa ushirikiano wao na Wizara. Baada ya kuwa tumepokea hoja na migogoro, Wizara itaishughulikia yote na baadaye tutaona namna bora ya kuweza kuona kwamba Taifa ambalo halina mgogoro linapatikana. Kwa sababu kazi tuliyopewa na Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha migogoro iliyopo inakwisha na tusizalishe mingine lakini ni mimi na wewe ambao tutakwenda kuhakikisha migogoro inakwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nimuachie Mheshimiwa Waziri aweze kuendelea kwa sababu najua kila ambalo limeandikwa litafanyiwa kazi na litakwenda kutolewa ufafanuzi kama ambavyo tumepanga. Nashukuru kwa kunisikiliza.