Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia Wizara hii juu ya mambo muhimu matatu yanayohitajika ndani ya Wilaya ya Tarime na hasa Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Tarime kwa kiasi kikubwa haijapimwa. Mfano, Halmashauri ya Mji wa Tarime kwenye kata nane, ni kata mbili tu ndiyo zimepimwa. Hilo eneo lingine halijapimwa licha kuwa sasa hivi vijiji na vitongoji vyote vimekuwa mitaa na tuna idadi ya mitaa 81. Hivyo upangaji wa mitaa ni muhimu na uhitaji wa kupanga mitaa ni lazima ili tuweze kupima viwanja na kupandisha thamani ya ardhi yetu. Tunaweza kutumia ardhi ile ili kukopa katika taasisi za kifedha; vilevile mji ukipangwa vyema utavutia wawekezaji mbalimbali kuja katika Halmashauri yetu na kuwekeza kwenye sekta mbalimbali kama vile viwanda, ufugaji, uwekezaji kwenye majengo ambapo tunahitaji strategic master planning ya mji wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa ni Kata ya Bomani kwa sababu tu ndiyo zimepimwa. Tunahitaji upimaji wa haraka kwenye Kata za Turwa, Nyamisangura, Nkende, Kenyemangori, Ketare na Nyandoto ziweze kupimwa ili kuweza kuruhusu utoaji mwingine wa huduma za kijamii kama umeme, barabara, shule, vituo vya afya, vituo vya biashara, maeneo ya viwanda na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za upimaji wa ardhi ni ghali sana kwa Mtanzania wa kawaida kuweza kumudu, maana ni kuanzia shilingi milioni moja na kuendelea. Vilevile taratibu hizo zinachukua muda mrefu sana na zina mlolongo na urasimu. Hivyo tunaomba sana upimaji wa viwanja kwenye Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa kipindi cha mwaka huu. Hii itaweza kupunguza kasi ya migogoro kama ule uliopo kwa wananchi wa Mtaa wa Mafarasini, Kata ya Bomani ambapo walipimiwa ardhi kwa ada (gharama) ya shilingi 20,000, shilingi 40,000, shilingi 70,000. Cha kushangaza baada ya muda Serikali inawaambia walipie tena upya gharama za kumiliki ardhi kuwa ni kuanzia shilingi 2,000,000 na kuwaambia kuwa wanaoshindwa kulipia gharama hizo watanyang‟anywa ardhi hizo na kupewa wenye uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili halikubaliki kwa maskini wale waliomilikishwa ardhi kwa kufuata sheria na walilipia. Iweje leo tena mnawapoka? Hadi sasa wananchi hawa wa Mafarasini wanashindwa/huogopa kuendeleza makazi yao kwa kuhofia kupokwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ni juu ya waraka ambao umetoka Serikali Kuu (Wizarani) kwenda kwenye Halmashauri ya Mji ikitaka kutokutumia matumizi ya ardhi pale inapoona inafaa. Hili kiukweli limekuwa kikwazo kikubwa sana na ukizingatia Halmashauri yangu ni changa na hivi katika upangaji wa mji kuna maeneo yanaweza kubadilishwa matumizi ili yaweze kutumika katika shughuli za kijamii kama vile mashamba na hata viwanja vya michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inarudisha nyuma maendeleo ya Tarime Mjini. Mfano Ofisi ya Mbunge iliandika barua kwenda Halmashauri ya Mji kuomba eneo ambalo litatumika kujenga maktaba ya umma ambayo itasaidia kuongeza ufaulu wa wanafunzi wetu. Vilevile kuongeza idadi ya Watanzania wanaosoma vitabu ili kupanua uelewa. Cha kushangaza na kwa masikitiko, Mkurugenzi wa Halmashauri wa Mji kasema kwamba Serikali imezuia ubadilishwaji wa matumizi ya ardhi. Hii inarudisha nyuma maendeleo ya Tarime Mjini. Naomba Wizara ione umuhimu wa kupatiwa eneo la kujenga maktaba ambayo ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ni tatizo sugu ni juu ya kucheleweshwa kwa malipo ya fidia kwa wananchi ambao ardhi yao imepokwa na JWTZ. Wananchi hawa walifanyiwa tathmini tangu mwaka 2012 hadi leo hawajalipwa na walizuiliwa kufanya shughuli za maendeleo tangu mwaka 2007 na wakapora hadi mkataba wa mnara wa Airtel, kinyume kabisa na sheria za nchi hii. Je, katika tathimini itakayofanywa tena itafidia mkataba wa mnara pamoja na uhalisia wa mali tangu mwaka 2007? Kutakuwa na riba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nawataka Serikali imalize malipo ya Ranchi wa Ronsoti, Msati (Nyamisangura) Kenyambi (Nkende) na nyinginezo. Ni aibu kuwapoka wananchi ardhi kinyume na Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 lakini mkashindwa kulipa fidia. Vilevile Serikali ione umuhimu sasa ya kuhakikisha Bodi ya Mifuko ya Fidia inaundwa mwaka huu ili tuepushe ucheleweshaji wa malipo ya fidia. Tunaomba NHC waje kuwekeza Tarime, maeneo tutawapatia ili kuweza kupunguza adha ya malazi na kukuza mandhari ya mji wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile fidia za wananchi wa Nyamoyo ambao walifanyia tathmini tangu mwaka 2011/2012 waweze kulipwa fidia zao maana waliondolewa na kwenda kutafuta makazi mengine ambapo ilibidi wakope fedha benki waweze kuanzisha makazi mengine. Hivyo wameshindwa kulipia mkopo na kubaki na adha kubwa sana. Hawa sasa ni wakazi wa mji wa Tarime, hivyo tufuate Sheria za Ardhi bila kunyanyasa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inachukua muda mrefu kweli kurejesha retentions katika Halmashauri husika, mfano Halmashauri yangu ya Mji wa Tarime ambayo haina mapato ya kutosha. Hivyo hizo fedha za upimaji ardhi ni vyema ziwe zinapelekwa mapema kuliko kucheleweshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kuwasilisha.