Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Conchesta Leonce Rwamlaza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. CONCHESTA L. LWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia machache kuhusu hoja iliyo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongea kuhusu halmashauri kuweza kupima viwanja na kupanga miji. Ni kweli halmashauri zimepewa jukumu la kupanga miji, kupima mashamba, kupima viwanja, kuweka makazi kwa ustawi wa watu wao, lakini kwa muda mrefu halmashauri hizi nchini zimeshindwa kufanya kazi hii kwa sababu ya ukosefu wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huku nyuma halmashauri zilikuwa zina retain pesa yake ile asilimia 30 inayotokana na kodi za ardhi na hivyo wanapata uwezo wa kufanya kazi ya kupima viwanja. Baada ya kuwaondolea mapato hayo kwenda katika Wizara ya Ardhi, fedha hizi hazirudi na kama zinarudi zimechelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nafuatilia katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukurasa wa tisa umeweza kutuonyesha mapato ambayo yametokana na kodi za ardhi. Ametuambia kwamba wameweza kukusanya bilioni 54.35, lakini tukienda ukurasa wa 83 unaotuonyesha mgao uliorudi katika halmashauri wa asilimia 30 yaani utaona maajabu, asilimia 54 bilioni zimekusanywa, lakini halmashauri 138 zimepata bilioni nne nukta nne. Kwa hiyo, naweza kuangalia uwiano na nimekwenda mbali nikaangalia Mkoa wa Kagera ambao ni mkoa wangu mimi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mgao wa mwaka huo tumeweza kupata milioni 113 na point, lakini unaweza kuona katika trend hii ni namna gani halmashauri zinaweza kupata fedha ya kuweza kupima viwanja. Siyo hivyo, nashauri Serikali itazame upya hata hii asilimia 30 ni sawa hata kwenye barabara halmashauri zinapewa hela ndogo, lakini kama ni sheria ibadilishwe ili hawa watu waweze kupata angalau hata asilimia 40 hata kama ni nusu kwa nusu kwa sababu kazi nyingi ziko ndani ya Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupima viwanja ndani ya halmashauri kuendana na ubia hata kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri amesema kwamba Wizara inafikiria au tayari imeanza kufanya ubia. Halmashauri nyingi zinakopa pesa kwa ubia tuseme na UTT, lakini fedha hizo ambazo mara nyingi halmashauri wanakopa nani anazisimia. Kumekuwa na malalamiko katika hali hii ya Wizara ya Ardhi, haieleweki maana yake inasimamiwa na TAMISEMI, Wizara ya Ardhi inasimamia vyake, kwa hiyo, matokeo tunakuwa na mkanganyika mkubwa. Halmashauri ziko TAMISEMI zinakwenda kukopa pesa, pesa hiyo inatumika vibaya, nani anasimamia mikopo hiyo? Wizara ya Ardhi inawekaje mikono yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, naweza kukupa mfano katika halmashauri yetu ya Manispaa ya Bukoba, kulizuka mgogoro mkubwa nafikiri mlihusika wanakopa pesa za kulipa fidia, lakini fidia zinazolipwa wanalipwa wale watu ambao wana ardhi na hata CAG alienda kukagua akaona kitu kama hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa kwenye Kamati ya TAMISEMI tulienda kuona hivyo hata Lindi imefanyika hivyo, kwa hiyo fedha zinakopwa. Je, nani kati ya TAMISEMI na Wizara ya Ardhi ambao wanaweza kusimamia mikopo hii ili fedha zitumike kadri inavyotakiwa. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie hili maana yake TAMISEMI wanasema wao mikopo ipitie kwao, Wizara ya Ardhi ni vipi, kwa hiyo, naona kuna mkanganyiko hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niende moja kwa moja kwenye kodi ya majengo. Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani upande wa ardhi amejaribu kusema, yeye anafikiria na sisi kambi kwamba inawezekana mnapenda kutuchonganisha na hizi halmashauri zetu ambazo tunasimamia kama upinzani lakini siyo hivyo. Kwa mfano, tuchukue Dodoma hapa hii halmashauri ni ya Chama cha Mapinduzi, mnafikiri mnaondoa majengo hii manispaa itajiendesha namna gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri msipeleke ushuru au kodi ya majengo kwa Serikali Kuu. Miaka miwili ya mwisho kwenye Bunge nilikuwa kwenye Kamati ya TAMISEMI tumekwenda pale Dar es Salaam tuliona jinsi TRA walivyoshindwa kukusanya kodi ya majengo walikuwa wanafanya uthamini wa upendeleo yaani yule mwenye kajumba kadogo ndiyo anawekewa fedha nyingi nani atafanya uthamini ili kwa kweli kupata hali halisi ya mapato ya majengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TRA walishindwa na kama walishindwa kipindi hiki mimi sioni sababu, mnakwenda kuua halmashauri hizi hata za kwenu ambazo sio za upinzani peke yake zote mtakwenda kuziua. Kwa hiyo, mwangalie kwa makini kwamba kodi za majengo zirudishwe, halmashauri ziweze kujiendesha kama kweli mnakwenda kufanya D by D na kwamba kweli hapa Halmashauri zifanye nini ziweze kujitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye wawekezaji, Wabunge wengi sana wamelalamika kuhusu wawekezaji lakini wawekezaji hawa wako hata wanasiasa ambao nao wanakwenda kwa ulaghai wao, wanakwenda kuhodhi ardhi kubwa katika maeneo ya halmashauri zao. Mfano katika Mkoa wa Kagera tuna mgogoro mkubwa katika Wilaya ya Muleba, mgogoro huo nina uhakika uko mezani kwa Mheshimiwa Waziri, kama haupo nina documents hapa akihijtaji kama hana nitampa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kijiji cha Kitene, Kata ya Kasharunga uko mgogoro kati ya kijiji na aliyekuwa Waziri wa zamani marehemu Edward Barongo. Mwaka 1990 aliomba kijiji kimpe ardhi eka 2000 sasa hivi ana eka zaidi ya 11,000. Tuje kwa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi sijui nimtaje jina, aliyemfuata huko nyuma, Mheshimiwa Waziri anamjua. Yeye kwenye kata hiyo hiyo katika Kijiji cha Kamyora aliomba ardhi eka 1098 sasa hivi anahodhi ardhi zaidi ya eka 4000, kwa hiyo, uko mgogoro mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namtaja si Profesa Tibaijuka ni dada yangu si kwamba namsema ndani ya Bunge, lakini nakataa hii tabia ya kila kitu changu, kila kitu changu, hapana. Ukiwa kiongozi wakati mwingine na wewe uwaachie wengine. Kama ni kiongozi huwezi kuhodhi ardhi, watu wanakuja kukodi kwako au watu hawawezi kufanya nini, ni tabia mbaya ambayo lazima tuikemee. Hatujasema kwamba kiongozi wa siasa hawezi kumiliki lakini, naomba tumiliki kwa ustaarabu, tumiliki ili tuwaachie na wenzetu wale ambao tunawaongoza, ndiyo hoja yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunachomwomba Mheshimiwa Waziri, mgogoro huu tunaomba waende wapime upya hiyo ardhi ili kusudi kama mtu aliomba eka 1098 abaki na hizo, ili zile zinazobaki wananchi wapate maeneo ya kutumia. Hivyo hivyo katika kile Kijiji cha Kitene, japokuwa marehemu Edward Barongo, alishafariki, Mungu amweke mahali pema, lakini ana watoto wake. Kwa hiyo, kama aliweza kuomba eka 2000, kwa nini ahodhi eka 11,000? Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri aende kwa kutumia vyombo vyake wakapime upya hiyo ardhi ili haki iweze kutendeka na migogoro hii iweze kwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba nimalizie kuhusu wataalam wa ardhi ni kweli mna vyuo lakini vyuo hivi wataalam hawatoshi. Nimegundua kwamba inawezekana watu hawaoni maana ya kwenda shule kujifunza haya mambo ya ardhi. Mwendeshe kampeni maalum, vijana wetu waweze kuona kwamba wanastahili kwenda kusoma mafunzo haya na muwahakikishie ajira ili kusudi vijana wetu wa Kitanzania waende kwenye vyuo hivi, wasome wapate utaalam ili muweze kuajiri wataalam wengi katika halmashauri zetu. Kusema ukweli halmashauri hazina wapimana hazina wachora ramani. Kwa hiyo, tunaomba kwa hayo machache muweze kutangaza watu waende wasome na waweze kupata ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, nakushukuru sana.