Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Stephen Hillary Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukushukuru wewe binafsi kwa kuniona na vilevile nianze kumshukuru Mheshimiwa Rais wangu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Pombe Magufuli kwa safari hii kutuchagulia Mawaziri majembe. Mheshimiwa Lukuvi wewe ni jembe na Mawaziri wote waliochaguliwa safari hii na Mheshimiwa Dkt. Pombe Magufuli wote ni majembe, mnafanya kazi kwa kujitolea sana, Mungu awabariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Shirika la Nyumba. Shirika la Nyumba linaendeshwa na Mkurugenzi mzuri asiyekuwa na majivuno, mchapakazi mzuri asiyekuwa na makundi. Mungu ambariki sana pale alipo. Nataka kutoa maoni yangu, kwamba katika Shirika la Nyumba kuna matatizo makubwa ambayo inatakiwa Serikali hii ya sasa yashughulikiwe sana. Kuna nyumba ambazo zimejengwa kwa gharama nafuu na kuna nyumba ambazo zimejengwa kwa gharama nafuu ambazo haziwasaidii Watanzania maskini, zinawasaidia watu matajiri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hayo kwa sababu leo hii Wabunge tuliopo hapa ndani ni asilimia 70 ambao wamekuja wapya na kuna asilimia 30 tu ya Wabunge waliokuwepo Bunge lililopita. Waheshimiwa Wabunge wengi walikuwa wanakaa kwenye nyumba za Shirika la Nyumba. Leo hii nyumba zile kuwapa Wabunge wapya waingie hawataki, wanakodisha kwa watu. Naomba mlishughulikie suala hili. Kama umeshakuwa Mbunge na umetoka, ukishatoka hapa huna mkataba wa kurudi Bungeni. Ni kwamba mkataba wako umekwisha na ulipewa nyumba na Shirika la Nyumba ili ukae kwa muda ule utakaokuwa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge leo anakaa Guest au hotelini wakati kuna majumba hapa yamekodishwa kwa watu, wanafanyia biashara ambazo hazina mbele wala nyuma! Naomba Mheshimiwa Waziri hebu fuatilia Shirika lako la Nyumba hasa kule walikotoka Wabunge wa zamani. Zile nyumba ambazo walikuwa wanakaa wenzetu, wapewe Wabunge wapya, wakae na wao waone faida ya hili Shirika. Tunalitetea Shirika hili, lakini halina msaada kwa Wabunge. Hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni kwamba, nyumba nyingi zilizoko Dar es Salaam zimechukuliwa na matajiri. Badala ya kuwasaidia maskini, wanawapangisha matajiri wenzao, wao wanakaa kwenye nyumba zao, zinakuwa ni nyumba tu ambazo zimekaa hazina faida yoyote kwa Watanzania. Sasa maana ya kusema tunajenga nyumba kwa ajili ya Watanzania, faida yake ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kuna maeneo ambayo wenzetu wa Shirika la Nyumba wamebomoa; maana ya kubomoa maeneo haya ni kwa ajili ya kujenga nyumba mpya. Nashangaa zinakwenda kujengwa nyumba nyingine leo hii Dar es Salaam, Magomeni, kumekuwa pori. Wezi wakiiba usiku, wanakwenda kujificha pale. Si muanze kujenga lile eneo pale ambalo mlibomoa kwa ajili ya kujenga nyumba nyingine!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo pale Tanga. Tanga wamekuja wamebomoa ambazo wazee wa kimaskini walikuwa wanakaa, wakaambiwa kunajengwa nyumba mpya. Leo mwaka wa nne karibuni, nyumba hazijajengwa. Sasa maana yake ni nini? Kama tunataka kujenga nyumba, basi anzeni kutakasa kwenye miji mikubwa ili ile miji mikubwa iwe mizuri halafu mnarudi huku katika maeneo ambayo mnafanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakuja katika suala la ardhi. Mheshimiwa Waziri, ni msikivu. Tumekuja hapa kuleta malalamiko kwa ajili ya ardhi, siyo kwamba kule kwetu Wakurugenzi wanashindwa kufanya kazi. Kwenye Jimbo langu nimebadilishiwa Wakurugenzi mara sita. Huyo Mkurugenzi atakayefanya kazi ya kuchunguza ardhi hii mpaka aorodheshe alete hapa, akitaka kuleta hapa anaambiwa ahame. Sababu za kuhamisha Wakurugenzi hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii katika Tanzania nzima, Jimbo ambalo linaongoza, ambalo lina mashamba makubwa ambayo hayaendelezwi ni Korogwe Vijijini. Nashangaa maeneo mengine yanagaiwa. Watu wanapewa maeneo, wanaambiwa hapa Serikali imechukua, Korogwe Vijijini kuna tatizo gani? Kwani haya maeneo kule ni ya nani ambayo Serikali inashindwa kuyatoa kwa wananchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati alikuja Waziri wa Kilimo wakati ule, alikuja akatoa hati kwamba wananchi wachukue Shamba la Chavda. Leo hii shamba la Chavda limekaa zaidi ya miaka 15 kuwapa watu wa Korogwe waendee hata kulima ni masharti. Leo hii kuna mashamba ya mkonge. Mashamba ya Mkonge ilikuwa ni kuendeleza mkonge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza, badala ya kuendeleza mkonge, watu wanafanya biashara zao. Wanaleta watu wengine wanakuja kufanya kazi, wanakuja kupanda mkonge; tena afadhali watengeneze wao. Wanachofanya wao ni kwamba wanangoja wakulima wadogo wadogo wamelima, wao wanakuja kupanda mkonge. Maana yake nini, kama siyo dharau? Serikali sikivu kama hii!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri, mara ya kwanza niliuliza swali hili na nikaomba kwamba nitoke na Mheshimiwa Waziri aende kule Korogwe akaangalie haki inavyotendeka. Leo hii watu wa Magoma hawana mahali pa kuzikana, shamba wamezungukiwa. Leo hii kuna mgogoro wa kijiji na kijiji, Kata ya Mkomazi; Kata ya Mnyuzi haina mahali, Kata ya Mswaha haina mahali; Makalamo na maeneo mengi. Mashamba 18 mtu mmoja kwenye shamba lao, halafu tunasema wakati huu ni wa Kilimo Kwanza. Watalima wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ni msikivu sana na namwamini sana. Tusifanye kazi kwa mazoea. Yeye hafanyi kazi kwa mazoea, ndiyo maana leo hapa kila Mbunge wa Upinzani, kila Mbunge wa CCM anamuunga mkono. Siyo tunakuunga mkono kwa sababu ya sura, bali kwa muda mfupi ambao smekaa katika Wizara hiyo, smeifanyia kazi nzuri kiasi ambacho hata sisi Wabunge tukimpinga ni kama tunajipinga wenyewe. Nimeona nimwambie suala hili hasa katika Mkoa wa Tanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tanga ulikuwa ni mkoa wa zao la mkonge, lakini baadaye mkonge hamna. Leo hii nenda Morogoro, kuna watu wamezuia mashamba makubwa, yasiyokuwa na faida, mtu anakwambia huyu alikuwa ni Waziri. Waziri wakati watu wanakosa ardhi? Kama Waziri alikuwa amechukua shamba, haliendelezi, watu wa Morogoro wanalalamika, wanagombana kila siku kwa sababu ya ardhi na mtu mmoja huyo huyo ana eneo zaidi ya hekta 1,000 na hajapanda hata mahindi; Serikali mna ugumu gani kuyachukua maeneo hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nenda Kilimanjaro, watu wanapata shida kama Ndugu yangu Mheshimiwa Selasini alivyosema hapa. Leo hii nimetoka Bukoba, watu wana ardhi nzuri, watu waende kule wakaendeleze ile ardhi kuwasaidia watu wa Bukoba wapande vitu, vionekane. Tusiangalie tu mji mkubwa wa Dar es Salaam, Arusha na Mbeya, angalieni na mikoa midogo midogo ambayo Watanzania wengi wako huko ambapo kuna ardhi ya kutosha lakini hawana mahali pa kusaidiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukijenga nyumba pale Bukoba Kijijini kwa rafiki yangu Rweikiza unaweza kupata wapangaji wengi tu, lakini watu wanang‟ang‟ania tu Dar es Salaam, Tanga na sehemu nyingine. Hizi sehemu nyingine kama Wilaya ya Korogwe, hizi Wilaya ndogo ndogo kwa ndugu yangu kule Mheshimiwa Nassari, kuna eneo kubwa kule ambapo nimemsikia hapa, naomba sana Serikali yangu sikivu, kama kweli mnataka kuwasaidia Watanzania, kwanza zichukueni zile nyumba za Wabunge wote ambao hawakurudi ili Wabunge hawa wapate.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tunaomba sana, ile ardhi ambayo imechukuliwa na watu ambapo wanakaa, watu hawana faida yoyote, hawaleti faida yoyote kwa Watanzania, Watanzania maskini wanalalamika kila wakati, hawapati msaada wa aina yoyote, tena ukienda ukiingia unapelekwa Mahakamani na ukifika kule unanyimwa dhamana. Sasa hii biashara ni kuoneana au ndiyo ubinadamu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.