Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi hii nami kwa dakika chache niweze kuchangia Wizara ya Nishati na Madini. Kwanza kabisa, ningependa Mheshimiwa Waziri atupe status ya umeme nchini ikoje? Kumekuwa na tatizo la umeme kukatika mara kwa mara. Tuliambiwa hakuna mgao, je, mgao umerudi kinyemela? Hapa Dodoma peke yake umeme ulikuwa unakatika kila Jumapili kuanzia asubuhi unarudi saa 12.00. Siku hizi unarudi saa 9.00 kwa sababu Wabunge tupo Dodoma. Tunaomba hilo utuambie. Pia atujibu, kwenye fedha hizi za umeme, kiasi gani kinaenda katika kumalizia viporo? Kiasi gani kinaenda kwenye miradi mipya? Hilo pia tunaomba atufafanulie, siyo hivi tu kama ilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wale asilimia 30 tuliorudi humu ndani, mwaka 2015 nilipokuwa nikichangia Wizara ya Fedha, nilisema fedha zilizopaswa kwenda REA zimeenda kutumika kwenye matumizi mengine. Nilisema, Waziri kama huyo anaweza aka-survive kwenye nchi yetu. Kavunja Katiba, kavunja Sheria ya Bajeti, kavunja kanuni za nchi! Leo athari tunaiona hapa, miradi ya REA Awamu ya Pili haijatekelezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti anasema, shilingi bilioni 70 ilikopwa, Serikali yetu sijui nini! Imevunja taratibu, hapa hakuna kutafuna maneno, wamekwenda kutumia fedha zilizokuwa kwenye ring fence. Maana ya kuwa kwenye ring fence, hazipaswi kutumika kwenye matumizi mengine. Leo tutamnyooshea kidole Mheshimiwa Muhongo wakati hatukumpa hela, watu wamekwenda kunywea chai na maandazi huko ofisini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliyasema haya mwaka 2015 nikiwa Chama cha Mapinduzi. Leo Makamu Mwenyekiti wa Bajeti ameyasema. Tunapozungumzia haya jamani, kwenye mambo ya muhimu ya kuondoa Taifa letu kwenye giza, kweli tumeshindwa kuchukua maeneo mengine, tunaenda kuchukua fedha zilizowekewa uzio? Leo hapa kila mtu akisimama, vijiji vyangu vya Awamu ya Pili havijakamilika. Hakupewa hela. Pesa zimekwenda kutumika kwenye matumizi mengine. (Makofi)
Nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge ambao mmeingia sasa hivi, kama tusipoibana Serikali, huu utaratibu ukiendelea, Bunge lako Tukufu linapitisha fedha, Serikali inaenda kutumia kwenye matumizi mengine, hatuwatendei haki wananchi. Tukatae Bunge hili kuwa rubber stamp, tuseme mwisho, tuazimie pesa za REA, ile trilioni moja tunayoipitisha hapa iende, mwakani tuzungumzie mambo mengine tena, siyo umeme vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya hayana Chama! Wabunge wengi nyie tunatoka vijijini huko, tunajua hali halisi ikoje. Mimi Jimbo langu la Bunda Mjini, baba yangu alikata Kata saba vijijini alijua zitamsaidia na ndiyo nimemchapa. Kata saba ziko vijijini kule, nataka umeme uwake. Kaleta Kata saba Jimbo la mjini, nimemkunguta huko ndiyo nimemshinda vibaya hajaambulia hata Kata moja! Ndiyo nasema hizo zote ziwake umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Babu yangu, hapa hakuna cha viwanda kama hakuna umeme. Halafu tunazungumza mambo kama haya, Waziri wa Fedha hayupo! Hayupo! Lazima awepo! Mambo ya msingi kama haya, mwenzake alikula, hakupeleka fedha. Tunahitaji fedha hizi tunazotenga kwa mambo yanayogusa maisha ya Watanzania. Leo Vijiji vyangu kule vya Kangetutya, Kamkenga, Guta, Nyamatoke, Miale kote huko kuwe na umeme. Sasa leo shilingi bilioni 70 zile hazikwenda, halafu tunaongea lugha nyepesi eti Serikali umekopa hela iliyokuwa kwenye ring fence! This is the shame. Mpeni pesa Mheshimiwa Muhongo tumalize biashara ya kusambaza umeme vijijini. Sasa tunakula bila kunawa halafu tunakuja kufanya kazi tena ya kupitisha kumalizia viporo hapa! Bunge letu lazima liwe kali kwa maslahi ya Taifa. Hii tabia iwe mwisho! (Makofi)
Mheshimiwa Waziri kingine, Jimboni kwangu Kata ya Kabasa Kung‟ombe kuna mgodi pale. Naomba tutembelee ule mgodi, wanafanya kazi katika mazingira hatarishi. Kwanza hauwanufaishi wananchi wa Kata ya Kung‟ombe lakini mazingira yale siyo mazuri, hawafuati taratibu, kemikali zinawaumiza wananchi wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine pale kwenye Kata ya Mjini, umeme kwa wananchi ni shida, gharama kubwa, wananchi wa Bunda masikini…
NAIBU SPIKA: Tunaendelea.