Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ili nami nisije nikamaliza kama Mheshimiwa Mwambe bila kuunga mkono, naomba nianze kwa kuunga mkono hoja. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nguvu, afya na uwezo wa kusimama jioni ya leo, niungane na Watanzania wenzangu na Wabunge wenzangu ili kuishauri Serikali katika kuhakikisha kwamba kasi ya maendeleo na hasa umeme inaenda kutendeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kushauri kwa kuisaidia Serikali na hasa nimesikia hotuba nzuri ya Mheshimiwa Waziri, akiwa anaelezea jinsi ambavyo bajeti imeongezeka kwa kiasi cha asilimia 50. Naomba nimkumbushe, hiyo asilimia 50 atakuwa amesahau shilingi bilioni 79, kwa hiyo, inapaswa iongezeke kwa kiasi cha zaidi ya asilimia 50. Hiyo shilingi bilioni 79 iko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma katika Sheria ya Bajeti na hasa katika uanzishaji wa Mfuko wa REA, fungu lile ni ring fenced. Maana yake ni nini? Pesa hiyo haiwezi kwenda kutumika kwa shughuli nyingine yoyote. Kwa mujibu wa sheria inatakiwa iende upande wa REA. Sasa nini kilichotokea? Serikali inawezekana walijikopesha kiasi cha shilingi bilioni 79 ambacho wana wajibu wa kuhakikisha kwamba kinarudi na kinaenda REA, kwa sababu lengo lake ni kupeleka umeme vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika kile ambacho ametaja kwamba ni ongezeko la asilimia 50, ukichukua na hii bakaa unayovuka nayo, naomba urekebishe vitabu vyako visome kwamba kuna shilingi bilioni 79 ambayo inapaswa iongezeke katika bajeti yako. Najua Serikali wamejikopesha na muungwana akikopa ana kawaida ya kulipa na Serikali hii inayoongozwa na CCM italipa ili dhana ya kuhakikisha kwamba umeme unafika kila vijiji Tanzania inaenda kufikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine ambayo napenda kuchangia ni kuhusiana na suala zima la uzalishaji wa umeme. Ukimsikiliza Mheshimiwa Waziri, tunajipongeza tumezalisha umeme wa kutosha, lakini ukitazama projection tuliyokuwa nayo na nini ambacho tulitarajia kuzalisha, bado kasi yetu haitoshi. Tulisema kwamba tungezalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe pale Kiwira, ilikuwa tuzalishe umeme pale Mchuchuma, lakini haya yote hatujaweza kufanya. Ni vizuri Mheshimiwa Waziri anapokuja kumalizia hotuba yake, atuambie baada ya miradi hii kutofanya kazi, tunajielekeza wapi kwenye vyanzo vingine vya uhakika ili kasi ya kupata umeme wa kutosha kwa ajili ya kutosheleza Watanzania na kuuza kwa nchi jirani tunakwenda kuifikia? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nimwongezee vyanzo vingine vya umeme, ukienda Mkoa wa Rukwa pale, kuna makaa ya mawe maeneo ya Namwere pale. Wachunguzi wanasema kwamba makaa yale yanafaa kwa kuzalisha umeme. Namwomba Mheshimiwa Waziri aelekeze nguvu kule. Kama haitoshi, maporomoko ya Kalambo, maporomoko ya pili Afrika baada ya Victoria Falls ambayo hayajatumika vizuri na Wizara ya Maliasili na Utalii, hebu tutumie chanzo hiki kwa ajili ya kuzalisha umeme na kazi ni ndogo tu. Kama imewezekana kuwa na mahusiano mazuri tukaanza kuzalisha umeme kule Rusumo, ni rahisi kabisa kwenda kwa majirani zetu Zambia kwa sababu yale maanguko yako mpakani mwa Tanzania na Zambia. Hebu tufanye utafiti, maanguko yale tutumie kwa ajili ya kuzalisha umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze upande wa REA. Tumeambiwa tunaenda REA Awamu ya Tatu, ni jambo jema. Hata hivyo, ni lazima tujitathmini; katika hii Awamu ya Pili tumenufaika sawa? Haiwezekani maeneo kama Wilaya ya Kalambo ilikuwa na umeme sifuri, halafu unaposema tunaenda Awamu ya Tatu bila kutazama huyu ambaye alikuwa na sifuri amepata nini? Naomba kuwe na exception katika mtazamo kabla hatujakwenda REA Awamu ya Tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri na maeneo mengine ambayo umeme ulikuwa haujafika, barua nimepeleka ofisini kwake, kwa uchache tu nimtajie vijiji ambavyo vimetajwa kwenye barua niliyopeleka kwake, ni pamoja na Kijiji cha Mwazye ambako anazaliwa Muadhama Polycarp Pengo, hakuna umeme pale. Pia Kijiji cha Kazila, Kijiji cha Kamawe, Tatanda, Sopa, Ninga, Kanyezi, Musoma na vyote hivyo viko kwenye barua. Alikuja Makamu wa Rais Mstaafu, akawaahidi wananchi; amekuja Mheshimiwa Rais, akatoa ahadi, naomba aende kutekeleza kabla hatujaenda hiyo awamu ya tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala la TPDC. Ukitaka kushiriki vizuri, lazima uwekeze ili katika mnyororo wa uzalishaji na utafutaji wa mafuta na gesi, Shirika letu la TPDC ambalo ni kwa ajili ya Watanzania wote liwe na nguvu, linatakiwa liwekeze kwa maana ya mtaji. Ukisoma ile sheria, imeeleza kabisa kwamba ili uweze kushiriki, lazima uwekeze kiasi cha pesa ambacho kinatakiwa. Naomba Mheshimiwa Waziri kwa kupitia Wizara yake tutazame kwa jicho la huruma, jicho la maslahi mapana kwa ajili ya Watanzania wote tuhakikishe kwamba tunawekeza vya kutosha TPDC. Hii itaondoa hii dhana ambayo watu wengine wamekuwa wakisema eti wagawane wao lakini Watanzania kwa ujumla wetu tusiwe na shirika letu ambalo ndiyo kwa ajili yetu sisi sote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, itasaidia sana, itaondoa kelele ambayo imekuwa ikijengeka kwamba eti mzawa ni kumjali mmoja mmoja. Hebu tujaliwe kwa ujumla wetu tuwekeze katika kampuni yetu kama ambavyo Mataifa mengine wamefanya. Statoil, lile ni shirika la Kiserikali, Petrol Brass ni shirika ambalo part ni Serikali na watu binafsi. Kwa hiyo, ni vizuri tuhakikishe nguvu hii tunapelekea huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini haya machache ambayo nimeyaongea yamechukuliwa kwa uzito na yatafanyiwa kazi. Nakushukuru.