Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu sana katika uendeshaji wa uchumi wetu kwa sekta zote ambazo ziko chini ya Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo napenda niweze kupata mikakati ya Serikali,ni suala la mahusiano kati ya madini tunayozalisha, thamani tunayopata ya uzalishaji ya hayo madini na mapato ya Serikali kutoka kwenye makampuni husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangaliwa hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukitazama ukurasa wa 86 na 87 ametoa takwimu za sekta ya madini. Utaona mwaka 2015 dhahabu peke yake ilituingizia dola za Kimarekani bilioni 1.6 takiribani trilioni 3.5 kwa maana ya thamani ya mauzo ya dhahabu nje. Lakini ukienda kuangalia mrabaha na mapato ya kodi kwa maana ya kodi zote ambazo zinakusanywa; kwa maana ya corporate tax, value added tax, pay as you earn, skills development levy na withholding tax, utakuta kwenye kodi tumekusanya shilingi bilioni 351 na kwenye mrabaha tumekusanya dola za Kimarekani 63.2.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua mapato haya, yaani revenue hii ya Serikali na fedha za kigeni ambazo makampuni ya madini yanapata kuuza dhahabu tu peke yake ni asilimia 15 tu ya dhahabu inayouzwa nje. Kwa hiyo, hii ni changamoto kubwa, najua tumetoka mbali tulikuwa tunapata chini ya hapo, tunahitaji kuongeza nguvu zaidi ili tuweze kufikia hatua kubwa zaidi ya mapato ambayo tunayapata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa ambalo tunalo sasa hivi, ni tatizo la makampuni makubwa ya madini kutumia njia za kihasibu kuhamisha faida kutoka nchini kwetu kupeleka kule ambako wamesajiliwa, inaitwa base erosion and profit shifting. Hili ni jambo ambalo ni lazima tulishughulikie vizuri, na tukiweza kulishughulikia hatutakuwa na haya matatizo ambayo tunayo sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuweza kupata maelezo ya Serikali, leo hapa tunapozungumza ndani ya siku tano zijazo, hakuna ndege ambayo inaweza ikatua nchini kwetu kwa sababu hatuna mafuta ya ndege (Jet A one) na hii inatokana na zabuni ambayo ilitolewa kutoka kwa kampuni moja ya kigeni, kampuni ile ikaleta mafuta, mafuta yale yote yameonekana yako contaminated hayawezi kuingia kwenye soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa Serikali haijachukua hatua yoyote ile, mafuta ambayo yalikuwa yaende Puma Energy peke yake,yana thamani ya dola za Kimarekani milioni 13 mpaka hapa tunapozungumza, hifadhi yetu ya mafuta ya ndege imebakia ya siku tano tu, baada ya siku tano kama hakuna hatua ambayo Serikali imechukua, nchi yetu hakuna ndege ambayo itakayotua kwa sababu hawawezi kutumia mafuta ambayo yako nchini hivi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba nipate maelezo ya Serikali,ni hatua gani ambayo wanachukua haraka kuweza kuhakikisha kwanza tunashughulikia jambo hili, tuweze kupata mafuta ya ndege ili ndege ziweze kutua. Tusipate aibu duniani, tusikose watalii ambao wanakuja nchini, lakini pili nihatua gani ambazo zitachukuliwa dhidi ya watu ambao walitoa zabuni kwenye mafuta ambayo yameonekana hayafai kutumika katika nchi yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nilikuwa naomba nipate maelezo hayo ya Serikali, na nina barua za Bulk Procurement Petroleum Agency, ambazo zinahusiana na jambo hili, kama Waziri akizihitaji kwa ajili ya ufuatiliaji naweza nikampatia ili aweze kulifuatilia jambo hili, na kuweza kuleta suluhisho.
Jambo la tatu ni suala la uzalishaji wa umeme. Nimeona miradi ambayo imeorodheshwa, ni miradi mingi na miradi ambayo inapaswa kuungwa mkono. Kwa sababu juhudi zozote zile za kwenda kwenye viwanda, kama haziendani na uzalishaji wa umeme wa kutosha zinakuwa hazina maana yoyote. Ndio maana leo hii sisi kule Kigoma tunahangaika kutafuta wawekezaji, Waziri wa Viwanda anahangaika kutafuta wawekezaji, lakini swali la kwanza ambalo mwekezaji atauliza kuna umeme? Hakuna umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana tunapigana sana kuhakikisha kwamba mradi wa Maragalasi unafanikiwa na ninapenda niwapongeze kwa kuhakikisha kwamba mradi wa Maragalasi umeingia kwenye mpango na hili ni kilio cha watu wa Kigoma cha muda mrefu na napenda niwashukuru sana kwa niaba ya wananchi wa Kigoma na kwa niaba ya wabunge wengine wa Kigoma kuhakikisha kwamba mradi huu unakuja jinsi ambavyo unavyotakiwa. Hata hivyo umeme sekta ya uzalishaji (generation part) ya umeme is liberalized,ni eneo ambalo Sheria ya Umeme ya mwaka 2008 imeruhusu private sector kushiriki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kama tukitumia vizuri hiyo mix ya public na private, tutaweza kuhakikisha ya kwamba tunazalisha umeme wa kutosha. Kwa hiyo, nilikuwa namsihi Mheshimiwa Waziri kwamba mikataba ambayo tayari tumesaini, inaweza kuwa inahitaji review ni sawa, kwa sababu ni lazima tufanye review kuangalia maslahi ya nchi namna gani ambavo inakuwa. Lakini tusifanye makosa tuliyoyafanya nyuma kujikuta tunapelekwa mahakamani tunalipa gharama kubwa, nyote hapa mnafahamu kwamba ilibidi tuwalipe DOWANS kisiri siri zaidi ya bilioni 200, kwa sababu ya kesi ambayo tulipeleka mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiingie kwenye mtego wa kupelekwa mahakamani tena, Rais alitoa tamko pale siku anaweka jiwe na msingi la Kinyerezi kuhusiana na kuzalisha wenyewe, ni tamko sahihi kabisa, ni tamko la kizalendo kabisa, lakini halina maana ya kwamba tuingie kwenye migogoro na watu ambao tayari tuna mikataba nao, halafu tuanze tena ku-negotiate mahakamani, itakuwa ni distraction mtapoteza muda na Mheshimiwa Waziri itakuondolea muda wa ku-concentrate kuhakikisha ya kwamba tunapata umeme wa kutosha, vijijini na miradi ambayo tunayo hivi sasa. Kwa hiyo, nilikuwa nashauri kwamba Serikali ijaribu kuangalia jambo hili na kuweza kuhakikisha kwamba tunakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni suala la TMAA na Dkt. Kafumu amelizungumza. Mimi nadhani tunaweza tukaangalia vizuri, ni namna gani ambavyo tunae-reform TMAA ipanuke zaidi, isiwe ni suala la kuangalia migodi peke yake, iangalie pia suala zima la mikataba yetu ya gesi, kwa sababu hatuna chombo ambacho chenyewe kiko dedicated kwa ajili ya kuangalia cost accounting na makampuni haya yanaingiza gharama nyingi sana kwetu, ili kuweza kupata sehemu kubwa ya mapato baada ya revenue sharing.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tuangalie namna gani ambavyo TMAA haitaangalia migodi peke yake, tuipanue iende ikiangalia mpaka kwenye mikataba yetu ya gesi badala ya kuivunja kama jinsi ambavyo Mheshimiwa Dkt. Kafumu anapendekeza. Muhimu ni kufanya reform ili kuweza kuifanya kazi yake iwe more relevant kuliko kwenda kuiondoa kwa sababu tunajua kazi kubwa ambayo wameifanya, ukaguzi mkubwa ambao wamefanya na mapato makubwa ya Serikali ambayo yameokolewa kulingana na jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa ni suala la mafuta na gesi Zanzibar. Mpaka sasa tunapozungumza bado Katiba inatambua kwamba suala la mafuta na gesi ni suala Muungano. Mpaka sasa tunapozungumza bado TPDC ambayo siyo taasisi ya Muungano inashughulika na mafuta na gesi Zanzibar, kuna haja kubwa, kwa sababu consensus tayari ipo, ni vizuri hata kama bado hatujafikia nafasi ya kwenda kwenye referendum ya Katiba au kuanza upya mchakato wa Katiba angalau tufanye amendment ya kisheria sasa hivi ili suala la mafuta na gesi liweze kutendeka Zanzibar bila kukiuka Katiba, bila kukiuka sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kuna consensus,lakini leo hii kampuni yoyote itakayoingia makubaliano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ina madhara ya kupelekwa mahakamani kwa sababu Katiba bado inatambua jambo hili la Muungano na nadhani kwamba halina ubishi. Hakuna mtu ndani ya Bunge hili ambaye atapinga jambo la kuhakikisha kwamba Zanzibar inaweza ika-manage mafuta na gesi yenyewe.
Kwa hiyo, naomba na napendekeza kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali tufanye amendment hiyo ili tuweze kuondoa tatizo hili la kisheria tuweze kuruhusu ndugu zetu wa Zanzibar waweze ku-manage resource hii kwa ajili ya faida yao na kwa ajili ya kuendeleza blocks ambazo tayari ziko Zanzibar na tayari zimeshaingizwa kwenye soko tuweze kuhakikisha kwamba na wenyewe hawarudi nyuma katika jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo nakushukuru sana.