Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Godfrey William Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Profesa Muhongo na Naibu wake kwa kazi nzuri sana ambayo wamekuwa wakiifanya katika kuhakikisha kwamba umeme unasogea na nishati ya umeme na madini zinaweza kusogea katika majimbo yetu na katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza tu napenda kugusia maeneo machache sana. Hotuba hii wengi wameshachangia na wameeleza kwa undani zaidi namna gani umeme ulivyokuwa na umuhimu katika majimbo yetu katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kujikita katika maeneo ya research na development. Nchi yetu ya Tanzania dakika hii kama tutafanya research ya kutosha, tutajikuta kwamba maeneo mengi ya nchi yetu yana madini, maeneo mengi ya nchi yetu yana kila aina ya utajiri ambao ungeweza kutusogeza mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu maeneo mengi ambayo tume-concentrate kama maeneo ya utafiti tumejikita katika eneo moja; eneo la madini tu. Madini hayo tumeangallya katika upande wa madini machache sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo katika nchi yetu ambayo yana madini ya kutosha na kuna watu ambao wameshaingia katika maeneo hayo na kuanza kupata faida na kuhakikisha kwamba wanachukua rasilimali zetu zote bila kujali nini wanakiacha katika nchi yetu ya Tanzania. Sababu moja, ni kukosa kufanya utafiti wa kutosha na kuhakikisha kwamba tunapata faida katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Kalenga kuna eneo ambalo tayari watafiti wamefika, wageni wamefika na wameanza kuchimba, lakini bado kama nchi hatujapeleka wataalam kule kuhakikisha kwamba maeneo haya kama Watanzania tunafaidika vipi? Hii inatugharimu sana kwa sababu tumekosa kufanya utafiti wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hilo hilo la utafiti, najikita hasa katika maeneo muhimu sana. Tanzanite kama nchi ya Tanzania tumeshindwa kuitumia na tumeshindwa kufaidika kupitia Tanzanite.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1967 Tanzanite ilipogunduliwa katika nchi yetu ya Tanzania mpaka leo hii tunaweza tukasema yote lakini bado hatujapata faida. Kama watu ambao tunaichimba na tunaitoa Tanzanite katika nchi yetu, bado tunasimama katika nafasi ya nne katika uuzaji, haya ni maajabu ya dunia. Nchi ya Kenya inatutangulia, Afrika Kusini inatutangulia, India inatutangulia, sisi ndio wenye Tanzanite.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna utafiti umefanywa na Waingereza, pesa ambayo tunaikosa katika nchi yetu kupitia Tanzanite ni kubwa. Kama tutaamua kwa hali na mali kujikita katika eneo hili na kama wachangiaji waliopita walivyoelezea, inasimamisha au inasimama kwa nembo ya nchi yetu, inasimama kwa jina la nchi yetu, tufanye nini zaidi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kusisitiza eneo hili ambalo lingetupa sisi pesa nyingi za kigeni, lingetusaidia sisi kuhakikisha kwamba miradi mbalimbali nayo inaendelea. Jambo moja ambalo naliona kama tatizo kubwa, ni namna gani tunaipeleka Tanzanite katika nchi za kigeni ili tuweze kwenda kuiuza? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa ni kwamba bado tuna miundombinu mibovu, usafirishaji wetu bado haujakaa vizuri. Kama tutapata ndege ambazo zitakuwa zinaweza kusafirisha Tanzanite hii kupeleka nchi za nje kwenda kuuza tuka-compete na nchi kama Kenya ambao wana ndege zaidi ya 45, South Africa wenye ndege zaidi ya 76 wanachukua Tanzanite hapa wanakwenda kuuza nchi za nje, wanatangaza nchi zao kwamba zinapatikana katika nchi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la muhimu sana kuhakikisha kwamba tunaamka na tunafanya jambo moja la muhimu kuhakikisha kwamba pesa zote ambazo tumekuwa tukizikosa tunazirudisha katika nchi yetu kupitia Tanzanite. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kujikita katika miradi ya REA. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Wizara yake yote kwa ujumla kwa kazi nzuri ambayo wameifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Kalenga, bado tunahitaji nishati ya umeme, lakini tunaipataje nishati ya meme? Leo hii bado ninafahamu kwamba tuko kwenye Phase Two ambapo miradi hii na nguzo zinapita kwenye barabara kuu. Ifike wakati sasa wananchi wetu tunajua kwamba wameshaanza kusogea ndani na vijiji vyetu vimeendelea kutanuka, mashamba yameendelea kulimwa na hivyo basi inawafanya wananchi waweze kusogea mbali kidogo na barabara.
Kwa hiyo, tunaomba sasa tutakapoingia kwenye Phase Three basi miradi hii ianze kuingia kule kwa wananchi, ifike kwenye vitongoji, ifike kule kwa mwananchi wa mwisho ili tuweze kuhakikisha kwamba watu wa vijijini wanapata faida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu hatuwezi tukasema tunakwenda kwenye industrialization kama hatujawafikia wananchi wa ndani. Wananchi wa ndani ambao nao wanafanya kilimo, ambao wanatakiwa wafikishe mjini, kuna viwanda ambavyo vinaanzishwa kule vijijini ndani. Ni jambo la msingi sana kuhakikisha kwamba tunapata umeme kwa wananchi wetu ambao wako ndani. Mimi nina imani kubwa sana na Mheshimiwa Muhongo na msaidizi wake kwa kazi nzuri ambazo wameendelea kuzifanya kwa kipindi kirefu, na ndiyo maana hata Mheshimiwa Rais aliona ni bora aweze kumrudisha Mheshimiwa Muhongo aweze kuchukua nafasi ile ile ambayo alikuwa nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikigusia masuala mengine, ninaangalia katika masuala ya bajeti kwamba asilimia 94 ya bajeti hii imeelekezwa kwenye maeneo ya maendeleo. Hili ni jambo la ajabu, kwa maana ya nzuri. Bado sijaona kwamba asilimia 94 katika nchi za Afrika kupeleka pesa za maendeleo kwenye nishati ya umeme na madini. Naomba tumpongeze sana Mheshimiwa Muhongo, tuipongeze Serikali yetu kwamba wamefanya jambo moja la maana sana. Na mimi naamini kwamba kwa utaratibu huu, miaka mitano ijayo tutafika mbali na nchi yetu itaendelea kusonga mbele kwa sababu tutapata viwanda vya kutosha kama tutaamua kuisimamia sera hii na tutaamua kuisimamia bajeti hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaelewa kwamba REA kuna pesa ambazo zinafungwa, lakini utaratibu kutoka Wizara ya Fedha kupeleka pesa kwenye mfuko huu au kupeleka pesa kwenye miradi ya umeme inachelewa. Hatuwezi tukasema tutafika asilimia 94 kama pesa hizi hazifiki kwa wakati. Hili ni tatizo kubwa, pesa ambazo zimefungwa zikae pale zisitumike vinginevyo ili tuweze kuhakikisha kwamba miradi hii inasonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini Waheshimiwa Wabunge wote bila kujali itikadi zetu tunahitaji umeme katika majimbo yetu. Tumuunge mkono Mheshimiwa Waziri na Serikali yetu tuweze kupata umeme na ninaamini ndoto yetu ya kuwa na viwanda, tutaweza kuwa na viwanda na tutasonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ningependa kuvitaja baadhi ya vijiji na kata ambazo napenda Mheshimiwa Waziri aweze kuviangalia. Nina kijiji kimoja kinaitwa Kipera, kipo katika Kata ya Nzii. Katika kata hii nina vijiji sita. Kijiji hiki ni kijiji pekee ambacho hakijapata umeme. Napenda sana Mheshimiwa Muhongo ajitahidi kwa kadri ya uwezo wake tuweze kupata umeme katika kijiji hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina Kata nyingine za Ulanda, Luhota, Lyamgungwe, Maboga, Wasa, Kihwele na Kata ya Mgama, bado tunahitaji umeme. Ninaamini kwa kupitia jembe letu, Mheshimiwa Muhongo tutapata umeme katika kata hizi na katika vijiji hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, napenda sana kuwashukuru wote ambao wamechangia, na ninaamini tutaisimamia Serikali vizuri kama tulivyotumwa na wananchi wetu tuweze kuisimamia Serikali yetu. Bila kujali itikadi, naomba tuunge mkono kwa asilimia mia moja bajeti yetu ya Wizara hii ya Nishati na Madini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana.