Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Alex Raphael Gashaza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia afya na uzima kuwepo ndani ya jengo hili.
Pili, nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi, kwa sababu tangu Mkutano wa Tatu umeanza nilikuwa sijapata nafasi ya kuchangia, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee, nachukua nafasi hii kumpongeza Waziri wa Nishati na Madini na Naibu wake na timu nzima kwa hotuba nzuri ambayo wameilata mbele yetu, hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mmoja anatambua umuhimu wa nishati hii ya umeme kwamba ni nyenzo muhimu katika maendeleo na mageuzi ya kiuchumi katika nchi yoyote ile. Kila Idara, kila sekta na kila Wizara inaguswa na Wizara hii, kwa maana hiyo ni cross-cutting Ministry. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na nishati ya umeme, katika Wilaya yangu ya Ngara Jimbo langu la Ngara, nina kila sababu ya kuipongeza Wizara hii na kumpongeza Mheshimiwa Profesa Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini na Naibu wake kwa kazi kubwa ambayo wameifanya katika Jimbo langu la Ngara. Amenitembelea Mheshimiwa Waziri Profesa Muhongo ametembelea Naibu Waziri, ametembelea Waziri Mkuu katika kuzindua Mradi wa Orion Holland ambao utazalisha megawatt 2.5 kitu ambacho nina amini kwamba kinafungua fursa kwa wananchi wa Jimbo la Ngara na kwa Taifa kwa ujumla kuleta maendeleo na hasa katika sekta ya uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima niendelee kukupongeza kwa jitihada zinazoendelea sasa kwamba kufikia mwezi wa nane mwaka huu Wilaya yetu ya Ngara itakuwa imeunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, kwa hiyo, kuendelea kutupa fursa ya kuwa na umeme wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haitoshi, Wilaya ya Ngara ni Wilaya ambayo mradi mkubwa ambao ninaweza kusema ni mradi ambao upo kwenye zile miradi ya flagship project ya umeme wa maporomoko ya Rusumo ambapo umeme huo utazalisha takriban megawatt 80, kati ya hizo megawatt 27 zitakuwa upande wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo kwamba wananchi wa Jimbo la Ngara wanafurahi na wanakupongeza kwa jitihada hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kwamba sasa tutakuwa na umeme wa kutosha ndani ya Jimbo la Ngara, kwa kuzingatia kwamba kwa sehemu kubwa tuna vijiji takribani 49 ambavyo mpaka sasa hivi havijafikiwa umeme, lakini kwa uhakika kwamba kufikia mwezi wa nane mwaka huu tutakuwa na umeme wa kutosha, wanataraji kwamba REA III sasa iweze kugusa vijiji vyote na vitongoji vyote takribani 240 ambavyo vimebaki ili kusudi umeme huu uweze kuleta tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye upande wa madini. Mheshimiwa Waziri anatambua kwamba Wilaya ya Ngara ni Wilaya ambayo ina madini mengi ambayo yanaweza yakaleta mabadiliko makubwa katika uchumi wa Tanzania. Wilaya ya Ngara ina madini ya nickel na ndiyo maana hata katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ile reli ya kati wameelekeza kwenda Keza. Keza iko Ngara ambapo kuna madini ya nickel. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, madini haya ni madini ambayo kwa Tanzania yanaifanya Tanzania i-rank nafasi ya tatu duniani kwa kuwa na deposit kubwa ikitanguliwa na Russia pamoja na Canada. Kumekuwepo na vikwazo ambavyo vimepelekea mgodi huu wa nickel usianze, mgodi ambao umeanza utafiti tangu miaka 1973. Nina uhakika wengi wetu humu walikuwa hawajazaliwa, lakini mpaka leo mgodi huo haujaanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu miaka 2002 kumekuwepo na ahadi kwamba mwaka kesho tutafungua, mwaka kesho tutafungua mgodi, lakini mpaka sasa hivi bado mgodi huo haujafunguliwa. Kwenye mpango wa maendeleo wa miaka mitano umeeleza vikwazo vitatu ambavyo vilikuwa vinaonesha kwamba mgodi huu ili uweze kufunguliwa ni lazima vikwazo hivyo viwe vimeondolewa. Ni pamoja na kikwazo cha umeme, kikwazo cha miundombinu ya usafiri na kikwazo cha bei kwenye Soko la Dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vikwazo hivyo viwili naweza kusema kwamba vimeondoka kwa sababu umeme sasa ambao tunategemea kuwa nao katika Wilaya hii ya Ngara ni umeme wa kutosha kuendesha mgodi huo na wananchi vijiji vyote wakapata umeme kwa matumizi ya majumbani na hata kwa matumizi ya viwanda vidogo vidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mawasiliano kulingana na bajeti kwamba reli ya kati sasa kwa standard gauge ndani ya miaka mitatu, minne ijayo kwa maana kufikia mwaka 2019 yawezekana tayari reli hii ikawepo.
Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri kwamba madini haya muhimu na ambayo yanaweza yakaleta mabadiliko ya uchumi katika nchi yetu, inaonekana kama vile inasahaulika sahaulika kwamba madini hayo yapo na mradi huu upo. Kwa sababu hata kwenye kitabu hiki cha bajeti haikuonesha kwamba mradi huo unafikiriwa. Ndiyo maana hata wawekezaji katika mgodi huo (Barrick) leo ukiangalia hakuna shughuli zozote zinazoendelea pale mgodini, pamoja na kuomba retention ya miaka mitano kwa maana ya mwaka 2015 kwenda 2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgodi haujengwi kwa siku moja, haujengwi kwa miaka miwili au miaka mitatu; tunahitaji kuona kwamba kunakuwepo na msukumo na kampuni hii ambayo inahusika pale iweze kuweka nguvu tuone jitihada. Sasa hivi wame-abandon site, hakuna kinachoendelea. Tunahitaji kuona jitihada zinazofanywa na Wizara hii kwa maana ya Serikali kuhakikisha kwamba wanapeleka miundombinu inayotakiwa, iende sambamba na jitihada zao katika kufanya maandalizi. Tunajua kufanya fidia siyo chini ya miaka miwili, wananchi hawajafidiwa.
Kwa hiyo, naomba Wizara iweze kusukuma kampuni hiyo ianze maandalizi ya ujenzi wa mgodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado pia katika Wilaya ya Ngara kuna madini ya manganese. Ipo kampuni ambayo sasa inafanya utafiti na uchimbaji pale. Nilikuwa najaribu kuteta na Naibu Waziri wa Nishati na Madini kwamba mazingira yalivyo ya shughuli inavyofanyika, inahitaji wakajiridhishe. Tuna mashaka kwamba pengine hawakufuata taratibu na sheria za utafiti na uchimbaji. Barua ambayo mwekezaji huyu ameandikiwa na Wizara ya Nishati na Madini kupitia Kanda Maalum, ni kwamba ni lazima awasiliane na Halmashauri na afuate taratibu na sheria za Halmashauri. Hakuripoti Halmashauri na mpaka sasa hivi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara imebidi kumwandikia barua kusitisha ili tuweze kupata ufafanuzi. Ninaamini kwamba hilo wataweza kulifuatilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye gesi. Baada ya kugundua gesi nchini Tanzania, imeonekana kwamba sasa ni tumaini la Watanzania wengi kwamba gesi hii itaweza kuleta mabadiliko ya kiuchumi na gesi hii maeneo mengi ndani ya nchi hii tunaitegemea ili iweze kusaidia kwa kuzalisha nishati ya umeme lakini pia hata kwa matumizi ya kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kuishauri Wizara hii ni kwamba tujaribu kuangalia ni namna gani ambavyo tunaweza ku-establish substations ambazo zitatumika kwa ajili ya kusambaza gesi hii katika maeneo mbalimbali ikiwezekana kutenga substations hizi kikanda ili kusudi wananchi wote waweze kunufaika na gesi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kwamba yapo makampuni kadha wa kadha ambayo yako tayari kuja kuwekeza kwa maana ya kutumia gesi hii na kufanya uzalishaji wa umeme. Kuna kampuni kutoka Uturuki, kuna kampuni kutoka maeneo mbalimbali ambao wanatamani waingie Tanzania kwa ajili ya kutumia gesi hii. Tunapoweza kukaribisha makampuni hayo, nina uhakika kwamba yataweza kutusaidia katika kuzalisha umeme wa kutosha kutokana na gesi na kusambaza kwa wepesi zaidi na kuweza kuleta mabadiliko mazuri ya kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye madini ambayo ni unique, madini ya Tanzanite. Kwa muda mrefu tumekuwa tukipiga kelele kwamba inakuwaje Tanzanite ambayo ni madini yanayozalishwa Tanzania peke yetu tunakuja kujikuta kwenye Soko la Dunia Tanzania tuko nyuma; eti nchi kama Kenya na South Africa ndio ambao wanaonekana kuuza na kuteka soko la Tanzanite! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inatutia aibu. Hebu niombe Wizara husika iweze kujikita na kuona ni namna gani ambavyo tunaweza tukawa na umiliki wa Tanzanite kama fahari ya Tanzania na madini ambayo yanaweza yakainua uchumi wa Tanzania na kuleta manufaa kwa watanzania walio wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba katika hili, hata kama ni kutafuta wataalam wa kufanya utafiti ili kuona ni namna gani ambavyo tunaweza tukarejesha heshima ya madini haya, kama nembo ya Taifa hata kwa jina lenyewe kwamba ni Tanzanite kwa maana ya kwamba ni madini yanayopatikana Tanzania tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina uhakika kwamba Wizara hii imejipanga na ndiyo maana hata katika bajeti yake imeonesha jinsi ambavyo matumizi kuelekea kwenye bajeti ya maendeleo imepewa kipaumbele kikubwa, asilimia 94. Zaidi ni pale ambapo nimefarijika kwamba katika fungu hili la maendeleo takribani asilimia 68 ni bajeti ya ndani ni fedha za ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaonesha kwamba ni rahisi na tutaweza kufanikiwa kutekeleza miradi hii ambayo tumeipanga kwa sababu ya own source kwa maana ya kwamba ni pesa za ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimtie moyo Mheshimiwa Profesa Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini; unajua wakati mwingine unapoenda kufanya kitu kizuri wengine hawakubali, ndiyo maana mtu mmoja akasema kwamba don’t focus on barriers or obstacles, always focus on your destiny.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kwamba Wizara hii chini ya Profesa Muhongo, mmeamua kuleta mabadiliko makubwa ndani ya nchi hii kwa sababu viwanda vitapatikana kutokana na nishati ya umeme, huduma bora za afya zitapatikana kutokana na nishati ya umeme kwa maana ya kutumia mitambo, Ultra Sound na CT-Scan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ubora wa huduma ya afya kwa Mtanzania inatokana na nishati ya umeme. Just keep on, usibabaike, songa mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru kwa kunipa nafasi na ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.