Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kabla sijaingia kwenye kuchangia, natamani niwakumbushe Wabunge wenzangu, maana nimeona wakitoa maoni kwamba Wapinzani tulitoka nje siku ya hotuba ya Rais. Waheshimiwa Wabunge, kuna njia nyingi za kufanya advocacy. Tunafahamu fika Bunge letu ni moja ya Mabunge ya Jumuiya ya Madola, tunapotoka nje, ni pale ambapo umeona hoja ulizokuwa nazo aidha zimesikilizwa au hazijasikilizwa. Hivyo kutoka nje siyo dhambi, ni dalili ya kuonesha hisia na mawazo ambayo tunayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza kuzungumzia hotuba ya Mheshimiwa Rais, amezungumza mambo mengi na hata wengine wamesema kwa sababu hatukuwepo hatuwezi kujua ni nini amezungumza. Sisi wote ni wasomi, tunasoma habari za Vasco da Gama lakini hatukuwepo na tunanakili kwenye mambo mbalimbali. Tumesoma mambo ya Hitler tunayatumia na hatukuwepo wakati wa uongozi wake. Vivyo hivyo habari hii itasomwa na sisi, itasomwa na watoto wetu wa sasa na vizazi vijavyo. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Rais ilikuwa ni nzuri kama walivyosema wengine tatizo naloliona ni utekelezaji. Nitajikita katika mambo ya uchumi aliyoyazungumzia hasa katika ukurasa ule wa 19. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika tunapozungumzia kukuza uchumi wa viwanda, nchi ambayo wasomi hatujawaandaa kuwa wabunifu, hatujawaandaa kuwaweka katika hali ya utendaji kazi, inakuwa shida.
Tunapozungumzia uchumi kilimo chetu ambacho watu wengi ni wakulima kwa asilimia kubwa, mazao wanayoyalima hatujajua ni jinsi gani ya kuwapelekea viwanda hivyo kwenye sehemu husika. Binafsi siamini kwa maana najua Magufuli ni mtu mmoja, mfumo wa Magufuli
ndiyo uliooza, atawezaje kufanya kazi peke yake? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, amezungumza mengi na amezungumzia habari ya Katiba. Katiba ndiyo mama na mimi nilifikiri siku 50 za kwanza za Urais wake angeanza na Katiba.
(Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ametamka na namnukuu, anasema, Katiba ni kiporo. Unapozungumzia kiporo kinaweza kikawa kizuri au kikakuharibu, kikawa kimechacha. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Mheshimiwa Rais, Katiba ndiyo msingi wa kila kitu. Hata viwanda hivyo na huu uchumi tunaouzungumzia pasipo Katiba hiyo hatutaweza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bado naendelea kujikitia kwenye uchumi, amezungumzia wajasiriamali wadogo, amezungumzia wanawake na vijana ambao ni kundi kubwa sana lililosahaulika. Tunawezaje kuwaunganisha wanawake hawa na viwanda endapo elimu yao ni
ndogo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, tunafahamu tuko katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mheshimiwa Rais sijaona akizungumzia ni jinsi gani tutajua masoko haya ya watu wachache ambao ni wajasiriamali, wakulima wadogo, wataingiaje katika masoko hayo na kuweza kufaidika na Jumuiya hii ya Afrika Mashariki?
Mheshimiwa Naibu Spika, sijaona akizungumzia muunganiko wa vijana kujiajiri katika uzalishaji mali. Tunapokwenda kwenye viwanda, kama ni kilimo wanawezaje kujiunganisha na viwanda hivyo anavyovisema? Ndiyo maana nasema nina wasiwasi na suala hili la viwanda
analolizungumzia Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba hii imeelezea mambo mengi yanayofurahisha kwa kuyasikia lakini nafikiria, wakulima na hivyo viwanda anavyovisema, nikizungumzia Jimbo la Rungwe Magharibi kuna wakulima wa chai. Wakulima wale wanapunjwa, wanauzia makampuni binafsi kwa bei ndogo ambayo wawekezaji hao wanafanya kwa manufaa yao na kibaya zaidi wanashirikiana na watu walio katika madaraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia viwanda, Kiwanda cha Chai cha Katumba ambacho kinaweza kutoa ajira kwa vijana wengi tumekisaidiaje kukipelekea ruzuku na kusaidia wananchi wa mji ule? Kuna viwanda vingi, Mbeya Mjini kulikuwa kuna ZZK, leo hii imekuwa ni
ghala la kuwekea pombe. Tunawezaje kusaidia vijana wetu kupata ajira? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ni vyema Mheshimiwa Rais akatazama ni jinsi gani tutafufua viwanda vilivyokuwepo. Watu waliovifilisi pia wapo, tunawezaje tukarudisha vile viwanda vilivyouzwa kwa bei rahisi kwa watu ambao wamefanya maghala? Nadhani Mheshimiwa Rais angeanzia majipu ya aina hiyo kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sheria nyingi kandamizi kwa mfano Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, watoto wadogo tunasema wanapata mimba lakini sheria haiko sawa. Kabla hatujaenda kwenye mtazamo wa maendeleo lazima tubadilishe sheria kandamizi na nyinginezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sheria za kodi ndogo ndogo zinazowatesa wananchi tunazibadilishaje? Tunawaunganishaje wananchi kuingia katika uchumi na tukasema uchumi wetu umekua, jana tulikuwa tunaambiwa uchumi wetu umekua, kivipi? Tunawianishaje kukua
kwa uchumi mnaozungumza Serikali na maisha ya mwananchi wa kawaida, tunayazungumziaje? Tuondoe siasa tuweze kufanya kazi. Magufuli anayo kazi kwa sababu watendaji wake ni walewale, pombe mpya kwenye chupa ya zamani. Namwonea huruma na sijaelewa atafanyaje kazi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunao vijana wengi ambao mpaka leo hii tumeanza kufanya marekebisho mbalimbali, kwa mfano gesi, je, Serikali imepeleka vijana hawa kusoma? Wako wachache tena wa wakubwa mnawapeleka Ulaya, kwa nini msichukue mtaalam kutoka Ulaya
akaja kufundisha watoto kwa wingi hapa Tanzania? Kwa hiyo, kuna vitu vingi tunahitaji kurekebisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia amezungumzia haki, ataangalia makundi ya wazee, walemavu, hakuna haki kama hakuna Katiba bora. Tunaposema haki tunamaanisha ni lazima anayestahili haki apewe. Ndugu zangu wengi wamezungumza mambo ya Zanzibar na
mengine lakini kuna haki ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), hatuoni ni jinsi gani wakisaidiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kusema haya, nafikiri kuna haja ya makusudi kabla hatujaendelea na safari hii tuanze na Katiba, tena siyo pale ilipochakachuliwa, tuanze na Katiba ya Warioba, tuanzie pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)