Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Joyce Bitta Sokombi

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi hii kuchangia Wizara ya Nishati na Madini. Nitajikita sana upande wa Nyamongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa Nyamongo ulianzishwa na wananchi wenyewe pale Nyamongo na Serikali ikaleta wawekezaji kwa makubaliano kwamba watawajengea wananchi wa eneo husika watawawekea hospitali, watawawekea maji, watawajengea barabara yenye lami na pia watawajengea kituo cha afya. Matokeo yake hayo makubaliano mpaka leo hayajafanyika, watu wa eneo lile kwa kweli wanatia huruma na inatia aibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haioneshi kwamba wale wananchi wako kwenye nchi yao, ukikaa ukiangalia eneo kwamba linachimbwa madini na kwamba yale makubaliano ya mwaka 2011 walivyoenda Mawaziri yakawa kwamba wao wanachimba ule udongo ili wale wachimbaji wadogo wadogo wawe wanaenda kuchambua ule udongo, matokeo yake wakienda kuuchambua wanapigwa risasi. Je, ni halali kwa mwekezaji kuja kumpiga raia wa Tanzania?
Mheshimiwa Waziri ninakuomba na nina kusihi, hakikisha unaweka mipango ambayo ni mizuri kuhakikisha wale wananchi wa Nyamongo hawapati shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia mkataba wa wale wawekezaji pale Nyamongo uwekwe wazi na mnatakiwa pia muwaulize kama mkataba ulikuwa ni kwamba kuwajengea wananchi kuwawekea lami katika barabara na kuwawekea vituo vya afya, kwa nini hayo makubaliano hayakufanyika?(Makofi)
Mheshimia Mwenyekiti, nitajikita pia upande wa Dangote, nimeenda Mtwara. Dangote amekuja kuwekeza hapa nchini eneo la Mtwara kwa lengo la kutumia gesi yetu ya Mtwara. Lakini matokeo yake Dangote hatumii gesi yetu ya Mtwara anatumia mafuta. Je, yale mafuta wanayoyaagiza, yanalipiwa kodi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee pia kuhusu REA. REA ni nzuri na imekuja kwa ajili ya kumkomboa mwananchi ambaye yuko kijijini, lakini mmewasahau wale wananchi ambao wako pembezoni kwenye vile vijiji. REA imepita mjini tu, wale wananchi walioko pembeni ni ile wanakaa tu wanaangalia umeme ule. Jamani tunaomba kama Serikali imeamua kumkwamua mwananchi aliyeko kijijini, tuhakikishe kwamba REA inaenda kwenye kila kijiji na vitongoji vyake kwenye kila eneo, siyo REA ipite upande wengine wapate umeme, wengine wasipate umeme. Ninamuomba Waziri wa Nishati na Madini, kwenye hili suala la REA aliwekee mkazo, kwa kweli inatia aibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwa mfano kule Kangetutya, Kabulabula umeme umepita tu, wale walioko ndani ndani hawana umeme, watafikiwa na umeme lini? Ninakuomba Mheshimiwa Waziri, jikite sana katika maeneo ya ndani msipitishe tu umeme eneo la barabarani, wale walioko vijijini kwa ndani nao wanahitaji umeme. Mwananchi amezaliwa miaka nenda rudi anatumia kibatari, basi angalau hata miaka hiyo iliyobaki jamani angalau na inabidi aende mjini, yeye awashe umeme ajue umeme huu unawakaje na una starehe gani. Siyo hata ku-charge simu inabidi aende mjini kwenye center zinaitwa, watafanya namna hiyo mpaka lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee tena Mgodi wa Nyamongo. Ninakusihi sana Mheshimiwa Waziri, ninakusihi mno, wale wananchi wa pale kwa kweli wanateseka, watateseka mpaka lini? Wewe ukiwa Waziri tena mwenyeji wa Mkoa wa Mara nina hakika kwamba utaenda kulifanyia kazi kuhakikisha Mkoa wetu wa Mara unainuka, wale wananchi wa eneo la Nyamongo hawatapata shida tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba sana Mheshimiwa Waziri ukiangalia hata kama wakichimba visima eneo hilo yale maji siyo salama kutokana na ile sumu inayomwagwa kwenye Mto Tigiti, maji inabidi wayafuate mbali sana. Ninamuomba Waziri wa Nishati na Madini atusaidie kwa hilo tujikwamue maana hayo mauaji yanayotokea Nyamongo kwa kweli ni aibu kwa Taifa letu. Wawekezaji wanakuja nchini wanakuwa wao ni bora kuliko Watanzania wenyewe tuliozaliwa katika nchi yetu. Tutaendelea kudharauliwa namna hii mpaka lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengi, nashukuru.