Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Kunti Yusuph Majala

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia wasaa na mimi niweze kutoa mchango wangu kwenye bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanza naomba nianze na ukurasa wa 59 wa Hotuba ya Waziri Mkuu kwenye suala zima la upatikanaji wa maji na hapa naomba kwenda kwenye suala zima la ujenzi wa mabwawa ya kimkakati, mabwawa makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bwawa la Farkwa limekuwa ni wimbo wa Taifa ndani ya Bunge hili. Bwawa hili limekuwa likisemwa na kuandikwa kila mwaka wa bajeti, tangu Bunge lililopita lakini kabla hata mimi sijaingia humu ndani ya Bunge. Leo tena naona hapa kwamba watu wanaenda kwenye upembuzi, wanaenda sijui kwenye nini, hatuoni mwendelezo wa dhamira ya dhati ya kwenda kujenga bwawa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Waziri mwenye sekta pamoja na Waziri Mkuu ambaye ndiye Msimamizi wa Shughuli za Serikali watuambie Bwawa la Farkwa hatima yake ni nini? Ni lini bwawa hili linakwenda kujengwa na hizi stori za upembuzi, stori sijui za nini…(Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kunti kuna taarifa.

TAARIFA

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli bwawa hili limekuwepo muda mrefu sana kwenye vitabu, lakini kwa mara ya kwanza utekelezaji umeanza na tunavyozungumza mkandarasi yupo site. Kwa hiyo, ni habari ambayo ni halisi, ni habari ambayo siyo tena mradi wa kwenye makaratasi au mpango. Mradi unatekelezwa, tunavyozungumza tunauweka kwenye maendeleo kwa ajili ya kufanya tunaita conveyors kuchukua maji kutoka Farkwa kuleta Dodoma. Kwa hiyo mradi unaendelea. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Unaendelea na mchango, umemaliza? (Kicheko)

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema hivi, Bwawa la Kidunda mpaka sasa hivi, kwanza gharama yake imetajwa ni shilingi bilioni 329, limeshafikia asilimia 17. Bwawa la Farkwa tunaambiwa maandalizi ya ujenzi wa Bwawa la Farkwa wako wataalam washauri kufanyia mapitio. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hiki kitu ndicho ninachosema bado ni story. Angalau Kidunda tumeambiwa imefikia asilimia 17 na fedha zimetajwa… (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kunti aliyekujibu ni Waziri wa Mipango na hujui mambo yanakwenda vizuri.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, mambo kwenda vizuri ningemkuta mkandarasi yuko pale. Ma-bulldozer yako hapo na mokorokoro yote yako pale, ningejua mipango inaenda vizuri, lakini kwa mipango ya kwenye maandishi hatutaweza kufika huko tunapopategemea. Shida yangu huyo Waziri wa Mipango angeniambia ni wakandarasi wangapi mpaka sasa na shilingi ngapi wameshatoa kwa mkandarasi na nini kinachoendelea na si kuniambia kwamba wako kwenye michakato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hicho ndicho tunachokizungumzia. Hatuzungumzii suala la maandishi, kwenye karatasi. Tunataka kuona vitendo vikitendeka na watu wanapata maji na si vinginevyo. Kwa hiyo, nataka waje waniambie ni lini hii michakato yao inakwenda kuisha na wakandarasi wanaenda site na wanaanza kazi ya ujenzi wa Bwawa la Farkwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwenda eneo lingine ambalo nataka kuchangia. Suala zima la tawala za sheria, suala la ujenzi wa mahakama zetu, uwepo wa ukarabati pamoja na watumishi, kwa maana ya mahakimu na watumishi wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili ni muhimu sana. Watu wetu wengi wanakutana na kadhia mbalimbali na mahali pekee ambapo wanaweza kupata haki zao ni mahakamani. Mahakama zetu nyingi ni chakavu, lakini maeneo mengine hakuna mahakama kabisa lakini tatu watumishi hawajitoshelezi. Mahakimu leo hawapo wa kutosha, kwenye maeneo mengi mahakimu inabidi wafanye kazi na hatimaye unakuta wanafanya kazi na kuamua kesi kinyume kwa sababu kichwa kimejawa na msongo, kwa hiyo mwisho wa siku wanaamua kesi pasipokuwa na haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutolea mfano kwenye eneo hili la mahakama. Wilaya ya Chemba tuna mahakama kumi, katika hizi mahakama kumi zinazofanya kazi ni mahakama tatu tu. Mahakama ya Chemba, Mahakama ya Mrijo pamoja na ya Kwamtoro. Mahakama nne zilishakufa, majengo yalishaanguka, hakuna watumishi, hakuna chochote kinachoendelea. Kwa hiyo hawa watu wa ukanda wa Usandawe kule wanategemea mahakama moja, hakimu aliyepo ni hakimu mmoja na msaidizi mmoja. Hakimu huyo akiugua hakuna kesi zinazoendelea pale. Ndiyo maana tunaona hata wananchi wetu kwenda kuitafuta haki yao wanaona ni kheri tumalizane mtaani kuliko kuhangaika kutembea umbali mrefu, natumia gharama kubwa na akifika kesi zote zinaahirishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo bado tuna changamoto kubwa sana. Serikali waone ni namna gani sasa wanakwenda kuboresha mazingira rafiki kwa kuongeza mahakimu na kuboresha haya majengo ambayo yanatoa huduma hizi za haki ili kutoa fursa kwa Watanzania kupata haki zao za msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo natamani kulisemea ni suala zima la kilimo. Nasema humu ndani tangu Bunge lililopita na Bunge hili. Waheshimiwa Wabunge wote na Watanzania kwa ujumla tunafahamu kwamba Taifa letu linatumia gharama kubwa sana ya kuagiza mafuta ya kula kutoka nje. Tukaja na mkakati hapa wa kuhakikisha tunaondokana na changamoto hiyo kama si kuipunguza. Tukahamasisha wakulima wetu walime zao la alizeti, lakini sasa Serikali imekwenda kuondoa tozo kwenye mafuta ya kula ya kutoka nje. Hivi ni kweli tuna dhamira ya dhati ya kuondoa gharama kubwa zinazoingiwa na Serikali kwa kuleta mafuta kutoka nje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wamelima alizeti, bei imeporomoka, hakuna mfanyabiashara wala mwenye kiwanda anayeweza tena kununua zao la alizeti wamebaki kufukuzana wanapishana na vibali kwenye maofisi. Wanaagiza mafuta kutoka nje kwa sababu Serikali mmetoa kodi kwenye mafuta ya kula. Kwa hiyo, leo tumeamua kulizika tena zao la alizeti, hakuna tena mwananchi atakayeenda kuwa na morale ya kwenda kulima zao la alizeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo viwanda vya ndani ambavyo tunasema tuviimarishe, viweze kuhimili ili tujenge uchumi wetu bado yatakuja kuwa magofu tu kama magofu mengine ambayo yalikuwa miaka ya huko nyuma. Naiomba Serikali, mara hii Waziri wa Fedha akija tunaomba suala la kodi kwenye mafuta iongezwe na ikiwezekana iwe ni asilimia 50 isiwe tena ile 35 ambayo aliiweka mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la nishati mbadala. Serikali inafanya kazi kubwa sana ya kusambaza mitungi ya gesi. Hata sisi Waheshimiwa Wabunge tulipewa hiyo mitungi. Hata hivyo mimi nikawa najiuliza kwamba hii mitungi ya gesi tunayopewa 100 unaenda unaigawa kule, hivi huyu mwananchi nikishamgawia huu mtungi wa gesi akimaliza ile gesi iliyokuwemo mle huo mtungi anaenda kuujaza wapi tena? Kwa sababu mpaka sasa bado Serikali haijafika wilayani, kwenye kata na maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuweza kutengeneza mazingira rafiki, kwamba mwananchi huyu akishamaliza ule mtungi aweze kupata fursa ya mahali pa kujazia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sio hivyo tu, gesi hii bado gharama yake ni kubwa. Leo mafuta ya diesel, petrol, mafuta ya taa tuna bei elekezi, ni kwa nini suala la gesi hatuna bei elekezi? Leo gesi kilo sita ni shilingi 35,000, hivi mwananchi wa kijijini kwa uchumi uliopo wa leo ni mwananchi gani anaweza kumudu shilingi 35,000?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, suala hili pia Serikali nia yake ni njema…

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa mchangiaji kwamba tayari Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha wananchi wote wanapata gesi kwa bei rahisi. Tumeanza na ule mtungi wa kilo 52, tumeenda kwenye mtungi wa kilo tisa na sasa hivi tuna mitungi ya kilo tatu. Kwa hiyo, tunahakikisha mikakati yetu iko vizuri kuhakikisha kwamba wananchi wanaendelea kupata mitungi ya gesi kwa bei rahisi. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Haya, hiyo inaitwa jaza ujazwe. (Makofi/Kicheko)

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Sijauliza mipango na mikakati, nimeuliza gharama ambazo ziko kwenye gesi. Mtungi wa kilo sita ni shilingi 35,000, mtungi wa kilo tisa ni shilingi 58,000 hicho ndiyo tunachokiuliza, kwa nini gesi ni bei ya ghali? Tunachotaka Serikali waje hapa watuambie, kwamba gesi mtungi wa kilo sita kwa sasa kutoka shilingi 35,000 ni shilingi 10,000. Hicho ndicho tunachokitaka, ambayo ni bei rafiki na Watanzania wote wana uwezo wa kumudu kwa hiyo shilingi 10,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine wametangaza kwamba leo taasisi ambazo zinatumia kuni nyingi wanakwenda kupiga marufuku, wanataka waingie kwenye mfumo wa gesi. Bado hicho kitu hakitawezekana kutokana na gharama kubwa iliyopo kwenye upande wa gesi. Nataka kujua, Serikali imewawekea mkakati gani madhubuti na rafiki utakaosababisha taasisi hizi ziweze kumudu matumizi ya gesi kwa gharama nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuzungumzia suala zima la upande wa Polisi. Polisi wamekuwa wakikamata magari ambayo yana ving’ora na vile vimulimuli. Sasa nikawa najaribu kujiuliza, hivi ving’ora na vimulimuli Serikali imeruhusu viingie sokoni. Vinatoka huko vitokako vinaingia ndani ya nchi, vinalipa kodi, wanataka nani avitumie? (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa zilizidi sana, dakika moja tu.

NAIBU SPIKA: Ahsante.