Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa na mimi nichangie hoja ya mpango iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wezangu kuendelea kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri sana anayoifanya yakutuletea maendeleo watanzania. Kuna ule usemi wa Kiswahili unaosema kwamba, mwenye macho haambiwi tazama, kwa sababu tunaona maendeleo ambayo anatuletea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitazungumzia vipaumbele viwili ambavyo ni kukuza uwekezaji na biashara, lakini sambamaba na hilo nitazungumzia kuchochea maendeleo ya watu. Sina shaka kabisa kwamba Serikali yetu inafanya kazi kubwa sana katika kuleta maendeleo ya wananchi, sambamba na hilo Serikali yetu ina nia ya dhati kabisa kuwawekea mazingira wezeshi wafanyabiashara ndogo ndogo wakiwemo wamachinga, wakiwemo boda boda, waendesha bajaji, kina mama ntilie na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kundi hili ni kundi kubwa sana ambalo kama litatumika zile kodi zake vizuri, zikakusanywa vizuri, mwisho wa siku Serikali itapata tija kubwa sana kutokana na kundi hili na mwisho wa siku tuweze kuongeza Pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba hebu utafutwe mfumo mzuri wa kuona namna bora ya kuweza kufanya makusanyo katika kundi hili ili kuepuka ile mianya kwa baadhi ya Watendaji wachache ambao wamekuwa wakitumia fursa vibaya kwa kuyapindisha haya makusanyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilikuwa nataka kuzungumzia ni hili ambalo lipo kwenye shabaha ya mpango ambayo shabaha hiyo ni kuzalisha ajira kwa wingi ambayo ni pamoja na upatikanaji wa mikopo ya riba nafuu na mikopo isiyokuwa na riba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuipongeza sana Serikali kwa kuwa na mazingira ya kuhakikisha kwamba kundi hili la vijana wanapata mikopo iwe yenye riba nafuu au mikopo ambayo haina riba. Tukiangalia katika zile asilimia 10 ni kwamba hakuna riba yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nikumbushe kwamba kuna ile mikopo ya maendeleo ya vijana ambayo inatolewa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu. Mikopo hii kwa kweli ikiwekwa kwa umuhimu mkubwa sana na vijana wengi sana wakapata mikopo hii, naamini kabisa hili suala la kusema kwamba tunahitaji kukuza ajira, kweli linaweza likafanikiwa, kwa sababu vijana wengi sana wakipata mikopo mwisho wa siku wataweza kufanya kazi na wataweza kujitegemea. Wakiweza kujitegemea, maana yake ni kwamba hata suala la tabia zisizokuwa na maana zitapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kumekuwa na matukio, watu wamekuwa na stress hasa vijana, wengine kufanya mambo yasiyofaa, wengine kujiua na kuchukua maamuzi mengine ambayo hayafanani. Kwa hiyo, naamini kabisa kuwa iwapo kundi hili likipata mikopo ya kutosha, basi suala la ajira litawezekana na hatimaye tutaleta maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni kuhusiana na suala la kuchochea maendeleo ya watu. Nafahamu kabisa kwamba suala la kuchochea maendeleo ya watu ni pamoja na suala la elimu, suala la afya, suala la maji, sambamba na hilo suala la ustawi na maendeleo ya jamii. Suala hili ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niishauri Serikali katika mpango huu, kwamba suala la malezi na makuzi nalo linabidi liwekewe mipango ya uhakika na bajeti ya kutosha ili kuweza kunusuru hiki kizazi kilichopo. Nasema hivyo kwa sababu gani? Natamani Serikali izingatie ule mpango wa kuwezesha malezi na makuzi ambao uliandaliwa na Serikali mwaka 2021/2022 ambao unaendelea hadi 2025/2026. Iwapo mpango huu utahusishwa vizuri na ukaweza kujenga vituo vya huduma mbalimbali vya malezi na makuzi, itawawezesha wanawake wengi kuwapeleka watoto wao katika maeneo yale na mwisho wa siku wanawake hawa wataweza kufanya shughuli zao za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukiona akina mama mbalimbali wamekuwa wakitembea na watoto migongoni, wamebeba mabeseni vichwani, wanafanya kazi, wanatembea na wale watoto juani. Kwa hiyo, inawezekana kabisa afya za watoto hawa zinaweza zikapata madhara. Kwa hiyo, nilikuwa naomba niishauri Serikali kwamba kwenye suala zima la malezi na makuzi na kujenga hizi nyumba salama ni jambo jema ili kuwanusuru watoto wa kizazi hiki na mwisho wa siku akina mama waweze kufanya kazi zao bila kuwa na mashaka yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilikuwa natamani kulizungumzia ni suala zima la mmomonyoko wa maadili. Hili ni tatizo kubwa, tumekuwa tukipata matukio mbalimbali kila kunapokucha. Hili suala na mmomonyoko wa maadili, iwapo kutaimarishwa huduma ya ustawi wa jamii; kwa taarifa zilizopo ni kwamba wanataaluma wa ustawi wa jamii walioajiriwa ni wachache sana, ni kama 4%. Kwa hiyo, nilikuwa natamani katika mpango huu Serikali ingeweza kuona umuhimu wa kuweza kuweka mpango wa muda mrefu kuhakikisha kwamba Maafisa Ustawi wa Jamii wanaajiriwa kwa wingi ili kusudi kuweza kuiponya mioyo pamoja na akili za Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa kuna matukio mengi sana ambayo yamekuwa yakitokea, watu kujiua, watu kufanya ukatili, kufanya mambo ambayo hayaeleweki, lakini yote hii inawezekana kabisa inatokana na ukosefu wa kupata ile huduma ya ustawi wa jamii. Kwa hiyo, nilikuwa naomba katika mpango huu pia, jambo hili wangeweza wakalitilia maanani ili kusudi tuweze kuwaponya hawa vijana wetu na jamii kwa ujumla, kwa sababu Maafisa Ustawi wa Jamii wanahitajika sana katika nchi hii kwa ajili ya kuleta faraja kwa ajili ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilitamani nizungumze ni kwamba naungana sana na ushauri wa Kamati, pale ambapo Kamati ilibainisha kwamba Wizara, Idara, Mamlaka na Taasisi za Umma kutoshirikiana wakati wa kutekeleza baadhi ya miradi, hivyo kufanya ufanisi uwe hafifu au kuwa chini ya kiwango. Nataka nitoe mfano. Katika ujenzi wa zile Ofisi za Machinga ambazo zinatakiwa zijengwe kila mkoa, zilizopo chini TAMISEMI, pesa zimeshapelekwa kule, malekezo yote yameshapelekwa kule, Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Watoto wao ndio wanaoratibu shughuli ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tatizo linakuja kwamba pesa zipo kule lakini baadhi ya mikoa hawajajenga zile Ofisi. Sasa kama kukiwa kuna utaratibu mzuri kwamba Wizara hiyo hiyo inapewa fursa ya kusimamia hilo jambo, pesa zikakaenda kule na usimamizi ukaenda kule, naamini kabisa ufanisi unaweza ukapatikana. Kwa sababu, kama Wizara tatu au nne zikiwa zinashughulikia jambo hilo kwa kweli ufanisi wake unakuwa ni hafifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba kama itawezekana katika mpango huu basi hebu Serikali ione kwamba Wizara moja iweze kusimamia na kuleta ufanisi wa jambo fulani badala ya Wizara zaidi ya moja au tatu au nne, hiyo inaweza ikasababisha ufanisi usiweze kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nitumie fursa hii kushukuru sana. Yangu yalikuwa ni hayo. Baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)