Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi ya kunzungumza ndani ya Bunge lako Tukufu. Kwanza kabisa napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kusimama ndani ya Bunge lako jioni hii ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kuunga mkono, lakini nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mwigulu kwa namna anavyofanya kazi. nimekuja kugundua kumbe walioimba wimbo kwamba tunaimani na wewe Mwigulu hawakukosea, na sisi Mheshimiwa Mwigulu tuna imani na wewe. Ninampongeza pia Naibu wako, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa namna mnavyofanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza mama Mheshimiwa Rais mama yetu mpendwa Mama Samia Suluhu kwa jinsi anavyofanya kazi ya kuwatumikia Watanzania ili kuweza kuwaletea maendeleo na kuwafanya waweze kuishi maisha ya furaha na amani.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi leo naomba niongelee kuhusu wafanyabiashara wa vitenge ambao wako pale Kariako, wengine wapo Kigoma na maeneo mbalimbali ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengi ukienda madukani utakuwa akina mama wanauza vitenge, utakuta akina mama wengine wanimachinga wanatembeza vitenge. Kwa wastani biashara ya vitenge ndani ya Taifa letu akina mama inawasaidia sana. kwa hiyo mimi nilikuwa ninaomba, ieleweke kwamba viwanda vya ndani sisi hatuvichukii, tunavipenda hakuna mtu anayekataa kitu cha kwake, lakini jinsi tunavyoagiza sukari kutoka nje, tunavyoagiza mafuta kutoka nje, namna hiyo hiyo ndivyo tunavyoagiza vitenge kutoka nje. Hii ni kwa sababu sukari na mafuta havitoshelezi ndani ya nchi yetu, lakini vitenge pia havitoshelezi ndani ya nchi yetu ndiyo maana vitenge vinaagizwa nje ili kuja kuongeza vitenge kwa vile ambavyo vipo ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hyo nilikuwa ninaomba kodi ipunguzwe kwa waagizwa vitenge vinavyotoka nje. Jana Mheshimiwa Kilumbe alizungumza vizuri sana vitenge vinapita kwenye bandari yetu, lakini kwa bahati mbaya vitenge vinavyopitishwa kwenye bandari yetu vikienda nchi za nje kodi ipo chini lakini vitenge ndani ya nchi yetu kodi ipo juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo nilikuwa namuomba Mheshimiwa Mwigulu ahangalie jinsi gani ya kuweza kupunguza kodi ili wafanyabiashara hawa wanawake waweze kufanyabiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, itakuwa ni ajabu wewe unapika chakula halafu hautaki watoto wako washibe lakini unataka Kwenda kuwashibisha watu wa nje. Kwa hiyo tunaomba kodi iwe rafiki kwa wafanyabiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano makontena yanayoingia nchini, makontena ya on transit ni mengi sana kwa sasa hivi. Mwanzo kontena za transit zilizokuwa zinaingia, kila mwezi, zilikuwa ni tatu, zimeenda zikawa mpaka kumi, lakini kwa sasa ni kontena 300 na kuendelea, unaweza kuona tofauti iliyopo. Kama mwanzoni ni kontena tatu mpaka kumi. Sasa hivi kontena hizo hizo za on transit ni kontena 300 hadi mia 500 zinazoingizwa kwenda nje, ni namna gani Serikali inapoteza mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, kontena hizo zinazopita nchini mwetu hizo za on transit kontena moja linalipiwa dola 400, angalia tofauti iliyopo. Yaani dola 400 kwa kontena moja halafu mtu anapitisha mzigo anapeleka mizigo inakwenda nje halafu mtu anapitisha mzigo anapeleka mizigo inaenda nje halafu mizigo hiyo hiyo inarudi kwa mlango wa nje kuja kuuza nchini mwetu. Tunaomba Serikali isikilize kilio cha wafanyabiashara wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi akina mama, tunavyomuona Mheshimiwa Rais anavyofanya kazi vizuri kwa kuwaongoza Watanzania, lakini pia Bunge letu linaongozwa na mwanamke ambaye ni Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunatamani kuona wafanyabiashara wanawake wa Tanzania wakipunguziwa kodi ili waendelee kufanya biashara zao vizuri. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri, chondechonde, mwaka jana nilikuja hapa nikazungumza kuomba kodi ipunguzwe iwe rafiki kwa akina mama wanaofanyabiashara ya kutoka nje. Kwa mara nyingine tena, na kwa heshima na unyenyekevu Mheshimiwa Waziri ninaomba ufikirie ili upunguze kodi ili wanawake waweze kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kodi kutokuwa rafiki Serikali inapoteza mapato mengi sana kwa sababu, kwanza tumepoteza walaji waliokuwa wakija kununua biashara nchini mwetu. Soko la vitenge Tanzania tumelihamishia nje. Tunaomba kodi ipunguzwe ili wale waliokuwa wamehamia nje warudi kwetu Tanzania ili tuweze kuendelea kufanyabiashara vizuri na kodi iweze kuongeza. Kuliko ilivyo hivi sasa tunapoteza mapato, na TRA wanajua ni jinsi gani walivyokuwa wakiingiza mapato wakati wafanayabiashara wa vitenge walipokuwa wakiingiza mizigo nchini mwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuzungumza maneno hayo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante kwa mchango mzuri.

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: … ninarudia tena kwa mara nyingine Mheshimiwa Mwigulu tunaomba ufanye kodi iwe rafiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)