Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa jioni ya leo niweze kusema machache, hususani katika Wizara hii iliyopo mbele yetu. Naomba nichukue fursa hii kwanza, kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuiletea maendeleo nchi yetu. Watanzania ni mashahidi kwamba, Profesa Muhongo na Naibu wake wanafanya kazi iliyotukuka na sote hatuna budi kumpa pongezi na kum-support afanye kazi ya ziada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, itakuwa sio busara pia, kutokumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuhakikisha kwamba, Tanzania inapata bomba lile ambalo linatoka Uganda hadi Tanga. Bomba hili litatoa fursa ya ajira kwa vijana wetu, ndugu zetu, kabla na baada. Naomba niseme kwa niaba ya wachangiaji au Wabunge wa Mkoa wa Tanga, nikupe shukrani za dhati sana katika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo sasa naomba nichangie kuhusu REA, Umeme Vijijini; Waziri na Naibu Waziri ni mashahidi, mara nyingi nimekuwa nikizungumza nao na kupeleka ushahidi kwamba, Jimbo la Kilindi lina vijiji visivyopungua 102, lakini katika vijiji hivyo ni vijiji 20 tu, tena vilivyopo usoni mwa Makao Makuu ya Kata. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anaangalia suala la umeme wa REA vijijini, basi ajue Wilaya ya Kilindi wana changamoto kubwa sana. Naomba vijiji vilivyobaki, kama siyo vyote, tuweze kupata hata nusu ya vijiji hivyo kwa sababu, wananchi wa Jimbo la Kilindi wanahitaji umeme kwa ajili ya maendeleo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia sambamba na mambo ya umeme hapo hapo, ni kwamba umeme uliopo Kilindi uliletwa kwa ajili ya wakazi wachache sana. Jimbo lile sasa hivi lina wakazi takribani laki tatu, umeme ule unakatika mara kwa mara, wakati mwingine hata wiki umeme unakuwa haupatikani! Nashauri basi, kwamba Wizara iangalie namna gani inaweza ikaboresha ili wananchi wa Wilaya ya Kilindi waweze kupata umeme wa uhakika. Najua hilo kwamba, kuna utaratibu wa kuleta umeme kwa kiwango kikubwa, basi na Wilaya ya Kilindi kwa ujumla iweze kunufaika na mpango huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, napenda kuzungumzia suala la madini. Wilaya ya Kilindi imebahatika kuwa na madini ya dhahabu na ruby yanapatikana kwa kiwango kikubwa sana pale, lakini nimepitia kitabu hiki cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri, sijaona ni wapi! Sasa Serikali inatia msisitizo kuweka nguvu ili wananchi wa Kilindi waliobahatika kwa nguvu ya Mwenyezi Mungu kupata madini yale waweze kunufaika na madini yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwamba kuna utaratibu wa kupima, Mheshimiwa Waziri, Ukanda wa Ziwa unajulikana kwamba ni Ukanda wa Green Belt. Mzungumzaji aliyepita hapa amezungumza kwamba, migodi mingi kule inafungwa, Kilindi ina dhababu nyingi sana, kwa nini sasa tusiharakishe upimaji katika Jimbo la Kilindi ili wawekezaji wanaokuja kwa ajili ya dhahabu na ruby wakimbilie katika Wilaya ya Kilindi, hivyo wananchi wa Kilindi wanufaike na Taifa kwa ujumla. Naomba, Mheshimiwa Waziri aliangalie hili kwa jicho la tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ningependa kuzungumzia juu ya Sheria za Madini, Wilaya ya Kilindi kuna migogoro mingi; Mheshimiwa Waziri kwa sababu, utaratibu wa kutoa license mtu anaweza kupata license yupo Mwanza, yupo popote pale, lakini naamini na anafahamu hilo kwamba, wagunduzi wa madini mara nyingi ni wananchi au wakulima wa maeneo yale. Sasa inapokuwa mtu huyu kaja na license, amemkuta mwenyeji pale ambaye vizazi vyote kazaliwa pale, kazeekea pale, halafu anamwambia azungumze naye namna ya kumpisha ili aweze kuchukua madini pale ardhini! Mtu alikuwa analima mahindi, leo kaambiwa kwamba, pana dhahabu, hivi ni rahisi kuondoka eneo hilo? Siyo rahisi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri sheria hii iangaliwe kwa jicho lingine tena kwa sababu, wananchi wa maeneo haya wanadhani ndio wanapaswa kupata fursa ya kunufaika na madini yale. Hatukatai kwamba, wawekezaji wasije Tanzania, lakini utaratibu uwape fursa wananchi wa maeneo yale kwa sababu, migogoro ya mara kwa mara imetokea na Mheshimiwa Waziri ni shahidi. Nimeshakwenda ofisini kwake nikamwambia kwamba, tunahitaji Ofisi ya Madini katika Wilaya ya Kilindi ili iweze kusimamia taratibu za madini Wilaya ya Kilindi. Ni kwamba, ofisi ya madini ipo Handeni, lakini umbali kutoka Wilaya ya Handeni mpaka Wilaya ya Kilindi ni umbali mkubwa unahitaji gharama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri tu hakuna ulazima wa kujenga ofisi pale, tusogezee maafisa watakaoweza kuwahudumia wananchi kwa sababu, wananchi wa Kilindi na wenyewe wanayo fursa ya kupata huduma ya madini pale. Hii pia itapunguza migogoro ya ardhi ya mara kwa mara. Mheshimiwa Waziri naomba wakati ana-wind up aweze kunipa majibu katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kuchangia ni suala la REA. Inavyoonekana hapa wale wakandarasi, makampuni yale yanayosambaza umeme vijijini, inaonekana wamepewa maeneo mengi sana. Nilipokuwa nazungumza na Meneja wa Wilaya ya Kilindi aliniambia, mtu anayesambaza umeme vijijini amepewa Mkoa wa Morogoro na Mkoa wetu wa Tanga na Mkoa mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani wakati umefika wa kuwapunguzia wale work load ili waweze kufanya kazi hizi kwa ufanisi wa hali ya juu sana. Wakati mwingine tutakuwa tunawalaumu hawa watu, lakini hawafanyi kazi kwa ufanisi kwa sababu, kazi hizi wanazopewa vijiji vinakuwa vingi sana. Nashauri na naamini kabisa kwamba, kwa phase ya tatu, basi kazi zitakwenda kwa haraka ili wananchi waweze kufaidika na umeme huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia suala la kumsaidia Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla kwamba, tunatakiwa tuongeze wigo wa mapato. Wigo wa mapato upo katika maeneo haya ambayo nayazungumzia, hususani ya madini. Siku moja Mheshimiwa Waziri nimeshawahi kumwambia kwamba, watu wanagawana milioni 200, mia 300 Kituo cha Polisi, maana yake Serikali inapoteza mapato! Hebu, Wizara ya Madini ione namna ya kuweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba, mapato haya yanayopotea ya Serikali, basi yanadhibitiwa. Haiwezekani mtu anayechimba pale, mwekezaji mdogo apate milioni 300 wakagawane Kituo cha Polisi, usalama hapo uko wapi? Wizara ya Madini iko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani wakati umefika, Mheshimiwa Waziri aone na kunisikiliza kwa sababu maneno haya ninayozungumza siyo yakwangu mimi, ni ya Wapigakura wa Wilaya ya Kilindi. Naamini wananisikiliza na wanajua Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi itawasikiliza na itawaletea Ofisi Wilaya ya Kilindi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni juu ya hawa wachimbaji wadogo wadogo na wakubwa wa madini, wamekuwa wakifanya shughuli hizo wakati mwingine wakiathiri mazingira. Kwa mfano, katika Kata ya Tunguli, kuna mwekezaji pale ambaye anafanya shughuli za madini, lakini kwa taarifa nilizonazo ni kwamba, maji yanayomwagika…
MWENYEKITI: Ahsante, muda wetu ndio huo.