Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Prof. Adolf Faustine Mkenda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rombo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa fursa hii kwanza naomba nisimame kumshukuru sana Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo Mheshimiwa Husna Sekiboko na Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima na wajumbe wote wa Kamati kwa taarifa nzuri na kwa usimamizi mzuri wa Sekta yetu ya Elimu kwa kutuongoza na kutusimamia vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa sababu kazi kubwa iliyo mbele yetu sasa hivi ni mageuzi makubwa ya elimu. Wamesimama kidete na sisi na wamekuwa wakiuliza maswali mapendekezo kutufuatilia mpaka hapa tulipofika. Kwenye hili la mageuzi ya elimu niseme mambo machache kwanza. Moja, hii ilikuwa ni ahadi ya Rais wetu Mheshimwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliiotoa hapa Bungeni kwa Watanzania kwamba Serikali yake italeta mageuzi makubwa ya elimu kukidhi matakwa ambayo yapo hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hiyo imefanyika na imeanza na Mheshimiwa Profesa Ndalichako na tumeendelea nayo hadi sasa hivi. Tunayo sera sasa hivi inayotuongozo na tuna mitaala mipya. Nataka tu kuotoa taarifa kwamba tumeendesha mafunzo kwa zaidi ya walimu 10,000 kwa ajili ya mitaala mipya na tumepeleka mafunzo kwenye kata zote hapa nchini kwa ajili ya mitaala mipya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati ambao tunaufanya ni utekelezaji kwa awamu kwa sababu tulijua na haya mapendekezo ya wajumbe wengine na Wabunge kwamba tukifanya kila kitu kwa mkupuo tunaweza tukajikuta hatutekelezi kwa ufanisi mkubwa. kwa maana hiyo tuliamua kwamba mitaala mipya inaanza kwa elimu ya awali, darasa la kwanza, darasa la tatu, kidato cha kwanza kwa mafunzo ya amali ambapo mpaka sasa hivi ni shule 96 zinatekeleza mafunzo ya amali na baadae tutakuwa na kidato cha tano na mafunzo ya uwalimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo si kwamba madarasa yote yanatekeleza mitaala mipya tutakwenda taratibu tukifika Mwaka 2027 tutakuwa tumefika turning point ya utekelezaji huo lakini mafunzo yanaendelea vizuri yanakwenda kwa walimu wote na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme vile vile kwamba kupitia Bunge lako Tukufu na hasa kwa Kamati yetu Serikali imewekeza sana katika miundombinu ambayo ni muhimu sana katika mageuzi. Sitaweza kusema yote, natoa mfano tu; kupiti mradi wetu wa Higher Education for Economic Transformation, HEET, sasa hivi mikoa ifuatayo kwa mara ya kwanza kabisa itapata kampus ya vyuo vikuu. Naanza na Kagera ambapo Mheshimiwa Mwijage amesema tumepeleka elimu ambapo inastahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mikoa hiyo ni pamoja na Kagera, Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Lindi, Manyara, Ruvuma, Njombe, narudia tena Njombe, Singida, Kigoma, Katavi, Rukwa, Tabora, Tanga na Mtwara. Vilevile tunakaribia kutoa tangazo kwa maalum kwa Mtwara. Hayo yote ni maelekezo ya Rais wetu na usimamizi wa Bunge lako tukufu kwamba tutekeleze yale yote ambayo Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliahidi akaagiza tuyatekeleze. Yajayo yanafurahisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kadhalika, na kama ilivyosemwa hapa sasa hivi tunaendelea na juhudi za kujenga vyuo vya VETA kwa wilaya zote 64 ambazo sasa hivi hazina vyuo vya VETA. Ujenzi huo unaendelea, na kupitia Wizara yetu ya Fedha najua tutakuwa tunapata fedha kwa speed inayotakiwa ili tuweze kukamilisha ujenzi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kumalizia ujenzi wa VETA ya Mkoa wa Songwe ambao ndiyo mkoa pekee ambao tulikuwa hatujaanza ujenzi wa VETA kwa ajili ya mkoa huo tutakuwa tumekamilisha kila kitu katika shule zote. Kazi kubwa itakuwa ni hiyo ambayo mapendekezo ya Kamati na Waheshimiwa Wabunge kwamba tuhakikishe tuna wakufunzi na vifaa vya kufanyia kazi katika vyuo vyote. Serikali imejipanga vizuri tutahakikisha kwamba tunatekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa sasa hivi napenda kutaja tu baadhi ya taasisi ambazo zinasaidia kwa mfano, NBC Bank na KCB Bank. Wao wameamua kumuunga mkono Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kwamba si tu wanatoa ufadhili kwa wanafunzi kusoma kwenye vyuo vya VETA klakini wanawaandaa kwa ajili ya kuwa wajasiriamali. Kwa hiyo kila mmoja ambaye anapata ufadhili wa NBC Bank au KCB Bank anaenda anasoma VETA akitoka pale anasaidiwa yeye mwenyewe kuanzisha shughuli zake kwa kupewa, kama alivyosema Mheshimiwa mmoja hapa, mtaji mbegu na usimamizi ili elimu aliyoipata iweze kumsaidia siyo tu kujiajiri lakini vilevile kuongeza ajira kwa wengine hapa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imezungumzia suala la kuongeza bajeti ya elimu ya juu na kwa Wizara kwa ujumla wake. Ni vizuri wakati tunazungumzia hilo ambalo ni muhimu sana vilevile tuone muelekeo wa kibajeti ambao umekuwepo kwa sababu ni vizuri tukatoa maua panapostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2019/2020 bajeti ya mikopo ya elimu ya juu ilikuwa ni shilingi bilioni 450, 2019/2020 bajeti hiyo ikaongezeka kidogo kufikia shilingi bilioni 464. Alivyoingia Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na mmesikia hapa Bungeni, aliagiza kwamba haridhiki na ongezeko hili. Akaagiza tuongeze kwa kiasi kikubwa sana mpaka kufikia shilingi bilioni 570, hiyo ilikuwa 2021/2022 na hivyo sasa hivi bajeti kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu ni shilingi bilioni 738.7.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vyovyote vile hakuna mtu anayesema bajeti inatosha lakini cha muhimu ni kwamba kwanza kwa maelekezo ya Rais wetu kwa kweli tumekuwa tukiongeza bajeti vizuri sana. Kazi iliyopo kwetu sisi ni kuhakikisha kwamba tunapambana kuhakikisha wale ambao wamepata mikopo warejeshe. Hatua mbalimbali zinafanyika ikiwa ni pamoja na kushirikiana na mifumo mbalimbali kama NIDA kuhakikisha kwamba tunamtambua nani amepata mkopo na vilevile kutangaza ambao wanadaiwa ili kama ameajiriwa kwenye sekta isiyo rasmi watu wajue by naming and shaming kwamba rudisha fedha watoto wa Tanzania wengine wasome.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi limesemwa hapa na ni vizuri Watanzania wajue. Kupitia mapendekezo ya Kamati yetu na kwa kibali na maelekezo ya Rais wetu sasa hivi tumeanza kutoa mikopo kwa vyuo vya kati. Tumeanza na shilingi milioni 48 na tumechagua maeneo yale ambayo kwa kweli Serikali ikitangaza ajira tunakosa wataalam. Kwa hiyo tuna uhakika hawa tunaowapa mkopo sasa hivi wakimaliza watapata ajira na watarudisha fedha hizo kwa ajili ya kuweza kuwapa watu wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la Samia Scholarship. Ndiyo, kama ilivyopendekezwa tuongeze bajeti lakini vilevile tupeleke maua panapostahili. Tulianza na shilingi bilioni tatu na sasa hivi tuna shilingi bilioni 6.7.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhana ya Samia Scholarship ilitokana na maelekezo ya Rais wetu kwamba hebu wale vijana wanaosoma sayansi ambao wamefaulu vizuri sana, ambao ni vizuri tuhakikishe kwamba wakienda vyuo vikuu wanasoma mambo ya TEHAMA, hisabati, sayansi, uhandisi na elimu tiba hebu tuwape ufadhili wa asilimia 100 ili kuwashawishi waende huko, ili kile ambacho Profesa Muhongo alikuwa anasema kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaandaa wataalam wa big data, machine learning, block chain, artificial intelligence tuweze kufikia kwa kasi tuweke fedha hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tulipewa maelekezo, Wizara tukakaa tukasema kwa sababu ni maelekezo ya Rais wetu tutaita Samia Scholarship. Fedha zinaongezeka lakini tunazipeleka kwa wale ambao wamefaulu vizuri sana katika masomo ya sayansi kwa masharti kwamba watakwenda vyuo vikuu kuendelea kusoma sayansi, hisabati, TEHAMA, uhandisi au elimu tiba. Kwa hiyo, hata kama tunaona kwamba kiasi hiki ni kidogo tukipiganie kiongezeke lakini basis yake ndiyo hiyo, sababu ni kuendeleza masomo ya sayansi; kati ya hatua kadhaa; tunaona muda ni mfupi; ambapo tunachukua…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda umeisha malizia.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda umeisha nakushukuru sana. Naomba kusema moja tu, la mwisho ambalo linaleta taharuki kidogo kuhusu maji katika Chuo Kikuu cha Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aweso yuko hapa, tuliwasilana naye mara ya kwanza akapeleka wataalam kule, tulivyoona mambo hayaendi kwa kasi tukawasiliana naye, amekwenda mwenyewe pale, amebadilisha mfumo na ametuhakikishia kwamba tutapambana kuhakikisha kwamba UDOM inapata maji ya kutosha. Naomba tumpe Mheshimiwa Aweso maua yake. Nashukuru sana. (Makofi)