Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja iliyoko mezani na nitajikita kwenye suala la michezo. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ya kuhamasisha michezo kwenye Taifa letu. Anafanya kazi kubwa sana ambayo kila mtanzania anaona, na kwa kweli anastahili pongezi nyingi sana kwa ku-support michezo nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mwenyekiti wa Kamati hii ambayo inasimamia mambo ya elimu na michezo kwa uchambuzi wao mzuri ambao umeweka wazi bayana yale yaliyoko na yale ambayo wameyaona kwenye utendaji wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitaomba nizungumzie suala la michezo; na michezo yote lakini nikijikita zaidi kwenye football. Sisi kama Taifa tumepata nafasi ya kuandaa michuano ya AFCON mwaka 2027 katika zile nchi tatu, kwa maana ya Kenya, Uganda pamoja na Tanzania, lakini niseme wazi hadi dakika hii ninavyozungumza na Watanzania wanaotusikiliza nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba Serikali au nchi yetu inafanya vizuri kwenye michezo hiyo hadi dakika hii hatujaiona dhahiri kama ambavyo Kamati imeyasema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilichangia hapa kuhusu ujenzi wa viwanja na nitumie nafasi hii kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jinsi ambavyo imejenga uwanja wao imeukarabati, uwanja ambao tumeenda kuushuhudia wakati wa Mapinduzi. Kila Mtanzania aliyeingia pale alitamani anakoenda awe na kiwanja angalau kile. Kiwanja ambacho hakichukui watu wengi lakini kina ubora na kina kidhi mahitaji ya matumizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii niiombe Serikali, kwamba tujisikie wivu, tujisikie wivu ninarudia tena. Kama Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alijenga viwanja nchi nzima kipindi ambacho teknolojia haipo, kipindi ambacho rasilimali ya watu iko chini, kipindi ambacho fedha hazikuwa nyingi, lakini akajenga viwanja vya Ali Hassan Mwinyi, CCM Kirumba, Sokoine na Mkwakwani; leo Taifa lenye watu milioni 61 tumekuwa tukipiga ajenda kila siku jinsi ya kujenga viwanja kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima Serikali ione dhamira ya dhati jinsi gani ya ku-support michezo hapa nchini. Mojawapo ni hili suala la asilimia tano. Tutamlaumu Ndumbaro, tutamlaumu Mheshimiwa Hamis Mwinjuma Mwana FA, tutalaumu Wizara ya Michezo; lakini Bunge hili lilipitisha five percent ya sport betting ambayo mimi nilichangia wakati ule, iende kwenye kusuport michezo kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii sport betting haipo kama michezo haipo, michezo yenyewe ndiyo inayozalisha fedha hii, kwa hiyo ni wajibu wa Serikali kuendelea kuipatia fedha Wizara; lakini ukisoma kwenye maoni ya Kamati wanasema toka tumepitisha asilimia tano hadi leo hakuna hata shilingi kumi iliyokwenda BMT kwa ajili ya ku-support michezo. Akina Ali Mayai watahangaika tu tutawapigia kelele lakini hawana fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi niiombe Serikali, asilimia tano ni fedhaa ndogo sana; tuombe angalau hata asilimia zaidi ya 60. Ukiwa ni mkakati wa miaka mitatu kuelekea AFCON Serikali iachie fedha za sport betting na zielekezwe kwenye kuwekeza maendeleo ya soka nchini ili Taifa letu tusije tukapata aibu mwaka 2027. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali iwe Sikivu; na bahati nzuri aliyeko kwenye Wizara ya Fedha kwenye kapu la fedhaa ni Mheshimiwa Mwigulu Nchemba ambaye ni mwanamichezo kwenye Taifa letu. Inasikitisha pale ambapo tunaona Waziri wa Fedha hajapeleka hata shilingi moja kwenye michezo. Sport betting wanaripoti kwamba ndani ya mwaka mmoja Bodi ya Michezo ya kubashiri wanatengeneza bilioni 170.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wanatengeneza bilioni 170, bajeti ya Wizara ya Michezo ni bilioni 35 zaidi ya mara sita ya fedha ambayo inazalishwa na sport betting. Kwa kweli Serikali ione haja ya kuwafanya akina Ndumbaro wapate fedha za kuendesha michezo kwenye nchi hii, na kumfanya Ali Mayayi mipango aliyonayo kichwani ya kuifanya TFF na Serikali iweze kufanya kitu kikubwa iweze kutekelezeka. Kwa hiyo niombe sana Serikali iachane na biashara hii ya kukalia hiyo asilimia tano ya sport betting na hivyo iweze kwenda kwa ajili ya ku-support michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kila sababu; ukifuatilia timu za taifa muda mwingine hadi kusafiri zinachangisha fedhaa ili ziweze kusafiri kwenda kwenye michuano. Tusiendelee kuleta mzaha huku kwenye michezo. Kuna sehemu nimezungumza wakati Brazil na Marekani au na Uingereza wanawaza kucheza fainali za Kombe la Dunia sisi Tanzania tunawaza nauli ya kuipeleka Timu ya Taifa kwenye michezo, jambo ambalo kwa kweli kwenye Taifa ni aibu. Ni vyema tukachukua hatua kuhakikisha kwamba hizi fedha zinaenda kwa ajili ya ku-support michezo kwenye Taifa letu ili mwaka 2025 kuwepo na tija kwenye hiki ambacho tunaenda kukifanya na Watanzania waone kwamba kweli Serikali ilikuwa serious na ujenzi wa hiki kinachofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la Uwanja wa Taifa ndani ya mwaka huu 2023/2024; kwa maana Oktoba mwaka jana hadi Juni mwaka huu; Uwanja wa Taifa ni zaidi ya mechi 25 za kimataifa zinachezwa, na the lowest amount ambayo inatolewa ni dola laki mbili tu; the highest amount zinaenda hadi milioni moja, timu kutoka Morocco, timu kutoka Rwanda, kutoka Burundi zinaomba kuchezea Uwanja wa Taifa. Mapato mengi yanakusanywa pale lakini Serikali inayachukua hairudishi tena ku-support Wizara ya Michezo ili iweze ku-run kwa maslahi makubwa ya Taifa letu. Niiombe Serikali uwanja huu uweze kujiendesha lakini pili Wizara ya Michezo iweze kuwezeshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ni kuhusu wachambuzi wa michezo kwenye Taifa letu. Nizungumze wazi; kwanza wachambuzi wasiokuwa na uzalendo, wachambuzi wasiokuwa na nia njema ndio wanweza kuilalamikia Wizara ya Michezo, kwamba wakianzisha Kozi ya Wachambuzi kwenye Taifa letu basi wao watakuwa wamekosa fursa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna-records, Taifa hili mwaka 2012 kuna mchezaji alikuwa anitwa John Bocco aliwahi kujiuzuru Timu ya Taifa kwa sababu ya wachambuzi na Watanzania wasiokuwa na uzalendo wa kuzomea wachezaji wetu. Sasa ni vema wanachoenda kukifanya Wizara ya Michezo lazima tuwe na certified and qualified hawa sport analyst ili watu wajue kwamba ile ni kazi mmalum kama kazi nyingine, kama ambavyo madaktari wako hospitalini wanafanya kazi ya specialist ndivyo ambavyo hii sport analyst iwe na watu ambao wana taaluma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, isingekuwa vyema kuwa na wachambuzi ambao wanaingia kuchambua kwa sababu mtu ana followers wengi Instagram, mtu anaweza kushawishi watu kwa mambo mengine akaenda kuchambua michezo na baadaye kusababisha wachezaji wetu au Taifa letu likaingia kwenye kuwakasirikia wachezaji na kukosa uzalendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hata kipindi hiki cha AFCON kuna wachambuzi wamechambua sana wachezaji wakati Taifa na Serikali inawekeza kuwaita Watanzania walioko nje kuja kulitumikia Taifa lao. Kuna wachambuzi kwenye vyombo vya Habari wamekuwa waki-discourage effort za Serikali wamekuwa wakishambulia wachezaji, ni wachezaji wadogo ambao wanahitaji kuwa moyo wa kulichezea Taifa lao. Sasa wakiona kwamba kuna wachambuzi ambao hawajitambui wanawashambulia kwa kweli inavunja moyo wa Serikali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Festo Sanga kwa mchango mzuri.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nakushukuru na niseme wazi kwamba Wizara inafanya vizuri; lakini Serikali kuelekea AFCON tujiandae vizuri ili tulifanye Taifa letu liwe na heshima kubwa kwa Watanzania, ahsante. (Makofi)