Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nikushukuru kwa kunipatia hii nafasi; na tumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehrma, aliyetujalia na tuzidi kumuombea Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kumjaalia kuwa na afya njema na aweze kufanya kazi kwa ufanisi kwa kweli anakwenda kwenye ufanisi wa kidigitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru na niwapongeze Mawaziri wote wa hizi Wizara, Mheshimiwa Ndalichako, Mheshimiwa Adolf Mkenda, Naibu Waziri Mheshimiwa Katambi na Naibu Waziri Mheshimiwa Kipanga; na Makatibu Wakuu wote, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, ndugu yangu au mwanangu Luhemeja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Wanawake na Watoto, Mwenyezi Mungu, awabariki sana; na bila kumsahau pacha wangu Mama Dorothy Gwajima, kwa kweli wanafanya kazi ya ziada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lililopita nilikuwa nimelizungumzia suala la fedha kwa watu wenye ulemavu, lakini leo binadamu wanakwambia asiyekuwa na shukrani basi atakuwa kidogo siyo mpenzi wa Mwenyezi Mungu. Mimi ninamshukuru sana Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, ametekeleza kutoa fedha za mfuko kwa watu wenye ulemavu bilioni moja, kwa kweli na mimi nimefarijika. Kwa muda wa miaka kumi huu mfuko ulikuwa haujaingizwa hizo fedha na watu wenye ulemavu walikuwa wamekaa hawajui wanategemea nini; lakini kwa kweli jana nimepata simu kuambiwa watu wenye ulemavu fedha zimeingia katika mfuko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nina imani mambo yatakuwa super na hata timu yangu ya Tembo Warriors, ambayo inataka kuingia katika AFCON ifanya vizuri. Mwenyezi Mungu azidi kumbariki Mheshimiwa Mwingulu Nchemba, ambaye ni balozi wa watu wenye ulemavu. Katibu Mkuu wa Fedha pia naye alisimama kidedea, Mama Natu, Naibu Katibu Mkuu na yeye alikuwa anapambana nalo, kwa kweli nasema ahsante. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema tusameheane kwa yote, lakini hakika tumefikia mwafaka kuwa walemavu sasa hivi tuko kifua mbele. Tunaomba hizi fedha zisiwe mwaka huu ni kila mwaka iwe ni mtiririko hatutaki tena kuja kuzungumza humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia suala la ubunifu na usimamizi wa fedha ambazo zinabidi ziende katika Wizara hizi mbili. Mimi nazungumzia fedha za Machinga, Machinga kwa Tanzania ni watu ambao wanahitaji msaada wa kusukuma katika biashara zao, mikopo na kila kitu. Lakini kitu kinachosikitisha sana katika upande wa Machinga hakuna data base ambayo inaonyesha mpaka sasa hivi tuna Machinga wangapi, lakini katika data base hii tulikuwa tunatakiwa tuwe na vitambulisho vyao hawa Machinga. Chukua mfano wa Mbagala, palivyojaa watu wanaofanya biashara ndogondogo wale wote hawana vitambulisho, lakini wanakatwa kila siku wanalipwa shilingi 1000; ina maana kwa mwezi ni shilingi 30,000 kwa mwaka ni shilingi 360,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii haihitaji hata mazungumzo hii fedha 360,000 wanayotozwa Machinga ukiwa katika data base ya Machinga milioni tano, pigeni hesabu Waheshimiwa Wabunge, nalizungumza hili kila siku; tunafedha zaidi ya milioni 300 imekaa pembeni hivi. Zinakwenda wapi hizi fedha haijulikani. Hakuna hesabu ambayo inaonesha hizi fedha zinafanya nini, hakuna; shilingi 360,000 ukizidisha kwa watu wanaofanya biashara ndogondogo milioni tano, Tanzania tuna watu milioni 61, kwa kweli ni fedha nyingi ambazo Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, anauwezo fedha hizi akazifanyia Wizara mbili, bila kutegemea fedha zingine zozote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashangaa nazungumza zaidi ya mara tatu hakuna mtu anayekuja kuniuliza. Mimi niko tayari kushirikiana nao, kufanya nao kazi ili fedha hizi ziende kwa Machinga. Utasikia mwaka huu tumekwama hatuna mikopo kwa Machinga kwa vile hatuna fedha. Je, fedha zao hizi zinakwenda wapi, zinafanya kazi gani? Ninaomba tushirikiane kwa pamoja Wizara tatu; Wizara ya TAMISEMI, ambao wao ndio wanaokusanya ushuru, Wizara ya fedha, wanapokea ushuru lakini vilevile Wizara ya Wanawake na Watoto ili zile fedha zinazotoka kule pawepo na mgawanyiko maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunasema tunashindwa kufanya kazi, kutembelea taasisi mbalimbali na shughuli mbalimbali ikiwemo ya ukatili wa kijinsia ambao unaendelea sasa hivi lakini fedha walizotengewa Wizara, ni ndogo, kazi ni kubwa lakini bado kuna fedha zinachezewa chezewa chezewa tu. Mimi nasema kabisa tuzungumze na data. Data hizi zitatusaidia kuwa wabunifu na wasimamizi wa hizi fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini unakopa nje? Ni kwa sababu wenzetu walikuwa wabunifu na iwekwe akilini, kuwa kila siku tutakopa wakati tuna fedha yetu ya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifanya hesabu ndogo tu shilingi 360,000 ukizidisha kwa watu milioni tano tunapata takriban bilioni 1.8. Zinakwenda wapi hizi fedha? Ni fedha za ndani zinachezewa chezewa tu. Ukisema ile ambayo ililetwa shilingi 20,000. Shilingi 20,000 kwa watu milioni tatu ni bilioni 60 ni Bajeti ya Wizara moja. Lakini hizi fedha zinachezewa, hazifanyi kazi na zinaingia katika mifumo ambayo haiko sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Rais na timu zake sasa hivi kila Wizara imefungua mtandao wa kidigitali. Hii mitandao ya kidigitali inafanya nini? Ni kwa ajili ya kuingiza hizi data na kuwa na uhakika na tunachokifanya, kwamba zinaingia ndani ya data center ambayo itasaidia kujua. Kwamba, jamani katika fedha za Machinga milioni tano wana vitambulisho vyao. Na wala haina haja kuwawekea fedha nyingi. Ukiwapa kwa mwezi shilingi 5,000 ina maana kwa mwaka analipa shilingi 60,000. ukidisha 60 hapo mlipokaa kama mna calculator; zidisheni 60 mara watu 5,000,000 utaona fedha hizi mabilioni na mabilioni yanakwenda wapi. Mimi matumaini yangu tusimame kwa pamoja nchi ina uwezo wakuweza kutafuta resource findings za fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini watendaji wengi wavivu wanashindwa kusimamia hiki kitu kikawa kinaweza kusaidia kama revolving fund kwa kuwasaidia Machinga wakaweza kutoka. Ninazungumzia sasa hivi hizi Wizara, mimi baada ya kuingia kumbe ni Wizara ngumu kuliko Wizara zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nilikuwa Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini, nimeingia Maliasili, nimeingia Kamati ya Local Government (LAAC) wakati huyu alikuwa Dkt. Slaa. Kwa kweli kama kuna Wizara ngumu ni hizi mbili; Wizara ya Wanawake, Watoto na hii Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu ni Wizara ngumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanzia kwa wanawake. Tanzania tunaingia katika mazingira magumu sana ya ukatili wa kijinsia kila ukiamka watu wanauana, watu wanachinjana, watu wanatoa mpaka mtu ana mimba anaambiwa mke wako ana mimba ya watoto mapacha toa watoto hawa utakwenda kupata utajiri; yote ni ukatili. Lakini bila kuwa na fedha watafanyaje kazi hii Wizara? Kuna NGO’s. NGO’s Tanzania ziko 10,000 lakini hizi NGO’s mapato yake ni 2.4 trillion zinakwenda wapi hizi fedha? Zinaenezwa kwa ajili ya kuhakikisha Tanzania ushoga unawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hizi fedha zikaguliwe. Serikali isimame na hizi fedha ambazo zinaingizwa na NGO’s, na zote hizi zifanyiwe vetting. Hali ya ushoga Tanzania ni mbaya, mbaya, mbaya. Kwa nini nazungumza hivyo? Fedha nyingi zimepelekwa kwenye elimu, baadhi ya private schools wanapeleka prestation, wanapeleka misaada ya vitabu, wanapeleka misaada ya vyakula lakini sisi hatujui; na zinafanya kazi ambayo itakuja kuwafanya Watanzania tunaowategemea kizazi cha baadaye kuwa kimekufa kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna fedha zinakwenda kwa wasanii. Mimi kwanza niwapongeze watu wa Arumeru, wakimuona mtoto wao anasuka nywele wanamkata zile nywele, watu wa Arumeru inabidi wapongezwe. Leo kila unapomuona kijana amesuka nywele, amevaa pete, anavaa ndani koti la kike na blouse za kike, tunawaona. Tunazungumza nini? kimya, tumeona huyo mama ameonekana jana anagawa vitabu Tanzania, vile vitabu vyake anavyogawa vinaeneza ushoga. Naomba Serikali ituletee majibu amechukuliwa hatua gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemuona yuko baba anakaa Masaki ameoa watoto wa Kitanzania wawili mmoja anaitwa Kelvin, katika ile Kamati ya Mwakyembe, yule baba mpaka leo hatujui amefanyiwa kazi gani…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Riziki Lulida kwa mchango mzuri.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)