Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Agnesta Lambert Kaiza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia. Awali ya yote naomba kwa niunge mkono hoja taarifa zote za Kamati mbili kwa maana ya Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria pamoja na Kamati ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa leo nitajikita katika taarifa ya Kamati ya TAMISEMI. Tangia asubuhi wachangiaji wote ambao wamesimama hapa kuchangia taarifa hizi za Kamati majority walionesha ni namna gani ambavyo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweza kutoa fedha nyingi za maendeleo kushuka kule kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo ambalo halina ubishani. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa kwa wananchi wa huko chini, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametenga fedha nyingi za maendeleo kwenda kwenye Zahanati, kwenye shule kwenye kila namna ya maeneo yote ambayo maendeleo kwa wananchi yanahitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taarifa ya Kamati ya TAMISEMI pamoja na changamoto nyingi ambazo wameelezea wamesema moja kwa moja kwamba miradi ya maendeleo imekuwa haitimii kwa wakati, haikamiliki kwa wakati. Pia katika taarifa hiyo ya TAMISEMI wamesema kwamba, kutokana na miradi hii kutokamilika ni wazi kabisa kwamba kuna watumishi ambao wameshindwa kuwajibika kwa maana hawakutekeleza wajibu wao, hivyo Kamati ikaenda mbali ikashauri kwamba watu hawa wachukuliwe hatua za kinidhamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanzia hapo kwenda katika mchango wangu. Wote tumekuwa tukifuatilia ziara ya Ndugu Makonda ambaye ni Katibu Mwenezi wa CCM Taifa. Pasipo kificho ukiangalia kwa haraka na kwa karibu sana unaweza ukahisi kwamba uko chini haijawahi kuwepo Serikali kabisa. Unaweza ukadhani kwamba sasa Katibu Mwenezi wa CCM sasa ndiye ambaye anaenda aidha, kutengeneza Serikali au sasa ndiye mkombozi ambaye anashuka kwenda kutatua changamoto na kero za wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu wote kwamba wapo wateule wa Rais ambao Mheshimiwa Rais amewaamini kutoka katika idadi ya Watanzania zaidi ya milioni 60, akawapa madaraka kwamba waende huko chini kumsaidia. Nikisema wamepewa madaraka namaanisha akina nani? Ni Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na wataalamu mbalimbali kwenye maeneo hayo ambao wameajiriwa kwa taaluma zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni shahidi, Bunge lako ni shahidi, katika ziara ya Ndg. Makonda, badala ya kueleza namna gani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametekeleza Ilani ya Chama chake, amejikuta hafanyi hayo, mwisho wa siku anaanza kusikiliza na kutatua kero za wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua, na wote tunatambua kwamba Wakuu wa Mikoa ndio wasimamizi namba moja wa Shughuli za Serikali kule chini. Ndio wasimamizi namba moja wa fedha za Serikali za maendeleo zinazoshushwa katika maeneo. Vile vile wote tunatambua, kama jinsi ambavyo Mbunge ana Jimbo lake la utawala kwa maana ana Jimbo lake ambalo analisimamia, hivyo hivyo Mkuu wa Mkoa, Mkoa ule ndiyo Jimbo lake la uteuzi ambalo Mheshimiwa Rais amemwamini kwalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti na yale mema na mazuri aliyofanya Mheshimiwa Rais ambayo yalipaswa kusikika kule chini, Wakuu wa Mkoa hawa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi, wameshindwa kabisa kutekeleza wajibu wao, kabisa kwa asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mifano michache, nafahamu na wewe unafuatilia mambo haya. Katika mikoa yote ambayo Ndg. Makonda amekwenda, kuna maeneo alifika sehemu, mfano kule Rukwa, mpaka anamwambia Mkurugenzi kwamba, sikuruhusu uambatane na mimi katika msafara wangu huu, nakuacha hapa katika halmashauri yako utatue kwanza changamoto hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ziara ya Ndg. Makonda hakuna majungu, hakuna kusubiri, ni hapa na hapa; Mkuu wa Mkoa hapo, Mkuu wa Wilaya hapo, Mkurugenzi hapo, wananchi hapo. Jambo hili limefanyika? Mkuu wa Mkoa anasema ndiyo, Mkurugenzi ndiyo, Mkuu wa Wilaya ndiyo. Mmefanya nini? Wanabaki kupiga yowe yowe nyingi, hakuna jambo lolote ambalo wamelifanya kwa kumsaidia Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunafahamu kwamba Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi ikiwa atasimama vizuri kumsaidia Rais katika majukumu yake, huwezi kukutana na changamoto za miaka kumi au miaka mitano. Hii ni hujuma ya moja kwa moja kwa Mheshimiwa Rais kutoka kwa wateule hao. Siyo tu hujuma, lakini ni kutowatendea haki Watanzania ambao Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amejitoa kwa moyo mweupe kuwatumikia na kuhakikisha changamoto zao zinatatuliwa.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani mwacheni aongee.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Agnesta, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Benaya Kapinga.

TAARIFA

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kumpa taarifa mchangiaji, anachangia vizuri kwa kumpongeza Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi Paul Makonda kwamba anafanya kazi vizuri. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Agnesta, unaipokea taarifa? Malizia mchango wako pia muda umekwenda.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sipokei taarifa. Pia hiyo taarifa ni kwamba unakidhalilisha hata Chama chako, unadhalilisha Serikali yenyewe, hapo siyo suala la Makonda anafanya kazi vizuri, hapa ni suala kwamba majukumu ambayo amekwenda kuyafanya Ndg. Makonda ni majukumu ya Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi. Siyo Makonda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wapinzani tulivyoona ziara ya Makonda, tulianza kuogopa sana kwa sababu, Mama Samia Suluhu Hassan, ametekeleza Ilani ya Chama chake. Mama Samia Suluhu Hassan, amefanya mambo makubwa sana kwa wananchi. Kwa hiyo, tulitegemea anakwenda kuelezea namna gani Ilani ile imetekelezwa. Matokeo yake amekwenda kutatua kero za wananchi ambazo walipaswa kuzitatua.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dakika moja tu. Nusu dakika nakuomba.

MWENYEKITI: Malizia sekunde kumi Mheshimiwa.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, natambua tuko na Waziri wa TAMISEMI, naona hayupo lakini Manaibu wake wapo, nafahamu mtakuja mbele hapa ku-wind up kwa maana ya ninyi kuchangia, napenda kufahamu, kama Serikali kupitia TAMISEMI mmejifunza nini katika ziara hizi za Mheshimiwa Makonda na mnakwenda kufanya nini kuhakikisha Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanawajibishwa kikamilifu kwa sababu hii ni hujuma ya moja kwa moja?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)