Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na kwa ujumla wake, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI, kwa hiyo kwa kiwango kikubwa kazi unayoiona iliyoletwa mbele yako inaakisi yale ambayo na mimi kama Mjumbe nimeshiriki. Kwa hiyo, mchango wangu utajikita katika maeneo machache. Nitakwenda kwenye motisha, nitakwenda kwenye michezo na muda ukiruhusu nitakwenda kwenye TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maelezo ya jumla, kabla sijaja Bungeni nilikuwa nikiangalia kipindi cha National Geographic. Kipindi kile niliona wenzetu na adha wanayoipata kutokana na matatizo kama barafu, baridi kali na vitu vingine vya namna hiyo. Nikawa najiuliza sisi kwa bahati nzuri hapa tulipo, msaada wa Mwenyezi Mungu eneo zuri la kijiografia tulipo na tunalalamika; tukipata mvua tunalalamika, tukikosa mvua tunalalamika, vipi kama tungepata na baridi kali na mabarafu kama yale? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu huko duniani kwa kupitia mipango wanajua kuna kipindi cha baridi kali, kuna kipindi cha barafu, kuna kipindi cha mvua kwa hiyo mvua kwao si tatizo ni suala tu la kujua kwa mipango yetu tutakabiliana vipi na mvua na mambo mengine ya namna hiyo. Kwa hiyo nilichokuwa naomba kwanza tumshukuru Mungu kwa kuwa hapa tulipo kijiografia lakini huyu Mwenyezi Mungu tusimpelekee kila aina ya lawama, baadhi ya kazi ni za kufanya sisi wenyewe. Nilikuwa naomba nianze na hilo. Kwa hiyo jitihada zilizobaki ni zetu sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwa watu wa mipango wanatusaidiaje? Ni kweli mimi pia nashiriki katika suala la Chama cha Kibunge cha Idadi ya Watu. Kwa ujumla wake sisi kule kwenye Chama cha Kibunge cha Idadi ya Watu tunasema hivi, kuwa na idadi kubwa ya watu ikitumika vizuri ni fursa lakini kuwa na idadi kubwa ya watu kama hutotumia vizuri ni changamoto. Kwa hiyo kwa sura yangu tafsiri yangu ni nini? Kila mwaka tunapozungumzia habari ya ujenzi wa vyoo, utengenezaji wa madawati, kila mwaka hicho pia ni kipimo cha umaskini. Tunatakiwa kwa kupitia watu wetu wa mipango watusaidie tutoke huko, kwa sababu suala la kujua una idadi gani ya watu, utafanya vipi, maoteo yakoje ni suala la kimipango. Kwa hiyo eneo hilo kwanza nilikuwa naomba sana tujaribu kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitoka hapo, mmezungumzia suala la motisha, mimi eneo la motisha nishukuru kamati kwa maana ya ukurasa wa 21 imezungumzia wale waliofanya vizuri na katika hili nishukuru Mkoa wangu wa Katavi umefanya vizuri kwa ujenzi wa maboma; zaidi ya maboma 500 wanakusudia kuyajenga. Sasa nasemaje kwa maana ya motisha? Wale wanaofanya vizuri tuonyeshe kuwapongeza, kuwatia moyo na ikiwezekana kama kuna namna nyingine ya kuwaruzuku ili watu hawa waendelee kufanya kazi vizuri. Nikilisema hilo ukiacha hilo la kazi nzuri iliyofanywa na eneo hilo, tulipita Mbeya tukakuta kuna shule moja inaitwa Nsalanga, hii Nsalanga pale Mbeya jiji kuna mwalimu amefanya kazi nzuri kwa kwenye Mradi wa SEQUIP. Kazi nzuri kabisa, na kwa kiwango kile kile cha fedha ametengeneza kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilikuwa naomba motisha ya watu wanaofanya kazi; na huyu mwalimu kwa ajina anaitwa Mwalimu Pascal Lucas wa Nsalanga naona Mheshimiwa Spika amefurahi ni kweli kazi nzuri, shule nzuri wale watu wamejiongeza wamekuwa ni watundu wabunifu. Mahali pa shule wameweka mpaka badala ya tiles wameweka ile kitu wanaita tarazo wamejiongeza walikuwa watundu, wabunifu. Sasa watu kama hawa tuwatie moyo kuwapongeza katika maeneo mbalimbali ili na wengine waige. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hilo hilo la motisha mimi naomba, wenyeviti wa mitaa, wenyeviti wa vijiji, Madiwani wanafanya kazi nzuri tuwape motisha tuwatie moyo hilo ni eneo la motisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo nije eneo la michezo. Tumesema kwa kupitia Kamati yetu. Ujenzi wa viwanja katika maeneo mbalimbali leo tusiwe watu wa kulalamika kwa nini wenzetu wa West Africa wanafanya vizuri ni uwekezaji. Leo ukikuta kila huyu mchezaji mzuri duniani anatoka huko haijaja kwa bahati mbaya, ni kutokana na uwekezaji. Kwa hiyo na mimi naomba eneo la ujenzi wa viwanja tusiache katika maeneo yetu mbalimbali. Niwapongeze Arusha tulipita pale tukakuta wenzetu wa TARURA ile chenji iliyobaki wamekwenda kujenga viwanja vizuri vya michezo. Nitoe shime kwa wadau mbalimbali wa michezo waturahisishie kazi hiyo nikiamini tukifanya vizuri eneo hilo la michezo huo ni uwekezaji kama uwekezaji mwingine. Tumeona wachezaji waliofanya vizuri huko duniani wanarudi katika nchi zao wanawekeza; iwe katika shule au katika hospitali. Kwa hiyo kwanza umeanza kwa kuwekeza kwenye michezo baadaye utaiona tija baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi katika eneo la TARURA kwa maana ya kumalizia. Sauti ya wengi ni sauti ya Mungu, ukikuta watu wengi kwa nini wote tunazungumzia TARURA, TARURA, TARURA, niombe sana watu hawa kuwaongeza fedha mimi kwa suala la barabara na tatizo lilivyo naichukulia kama ilivyotokezea janga wenzetu hawa wa huku Hanang. Sura ile ilivyotokea na Serikali nzuri ikafanya kazi kwa uharaka ndivyo ilivyo. Kila sehemu ukienda ni tatizo, kila sehemu ukienda ni tatizo. Kwa hiyo hakuna namna zaidi ya kuwaongeza watu hawa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashindwa kwenda kwenye maeneo mengine ya kuboresha, kwa maana ya miradi mingine hiyo ya AGRI-CONNECT, TACTIC na RISE kwa maana tu huko kote tutafanya kazi ikiwa kwanza hii dharura iliyojitokeza tumei-address. Tulichukulie kama janga na watu hawa wapelekewe fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa muda naunga mkono hoja. (Makofi)