Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Bahati Keneth Ndingo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mbarali

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kupata fursa, nami nianze kwa shukrani kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza tangu niingie hapa Bungeni nikiwa Mbunge wa Jimbo la Mbarali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukishukuru Chama changu, ninashukuru Halmashauri Kuu ya Chama changu na ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani kubwa waliyonayo na kurejesha jina langu ili nikawanie kiti hiki kwa kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi. Pia ninawashukuru sana wana CCM wenzangu wa Jimbo la Mbarali kwa imani yao kwangu na ninawashukuru sana wananchi wa Mbarali kwa kunipa heshima kubwa ya kuwa mwakilishi wao Bungeni. Niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa uwakilishi baadhi ya Wabunge walifika Mbarali kusaka ushindi wa Chama cha Mapinduzi, ninawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho siyo kwa umuhimu niishukuru familia yangu inayoongozwa na mume wangu kipenzi kwa mapenzi, umoja na mshikamano wao, kwa niaba yao ninawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze sasa mchango wangu, msingi wa maendeleo duniani ni watu, msingi wowote wa utawala duniani ni watu na maendeleo yoyote ambayo yanaweza yakafanyika yakaacha uchungu na maumivu kwa wanadamu au wananchi, hayo maendeleo si yenye tija. Ili maendeleo yawe yenye tija ni lazima yawe yanafurahiwa na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wowote ili utekelezeke, lazima uwe mpango shirikishi, ushirikishe wananchi. Vilevile ili mpango uweze kupangika na ukatekelezeka ni lazima mpango huo sekta zote zichukuliwe kwa uzito unaostahili. Nikianza kwa sisi Mbarali, mfano mwaka 2006 Mpango wa Serikali ulikuwa ni kutanua Hifadhi ya Ruaha. Utanuzi wa Hifadhi ile ulienda kuhamisha vijiji 10 na kata moja nzima ya kule kwetu Mbarali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango ule lengo lake, pamoja na kwamba mpango ulikuwa ni kuhakikisha mnaweka uhifadhi kwenye Bonde la Ihefu na mtiririko wa maji kwenda kwenye Mto Ruaha, mpango ule haukufanikiwa. Kwa sababu gani? Ni kwa sababu hamkushirikisha watu. Badala yake, mpaka sasa uharibifu kwenye Bonde la Ihefu umeongezeka kwa kasi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa suluhu ya wataalam wa Taifa hili, wanataka tena kuwahamisha wana-Mbarali kwenye maeneo yale. Hili jambo likanifanya niwe msomaji sana wa matatizo kama haya kwenye mataifa mengine. Ni lazima tukubaliane, sekta na mchango wa chakula kwenye Taifa hili na kwenye Bonde la Mbarali siyo jambo la kupuuzwa hata kidogo, pia sekta ya uhifadhi siyo jambo la kupuuzwa; sekta ya utiririshaji maji kwenye Mto Ruaha pia siyo jambo la kupuuzwa. Mambo haya yote matatu yana uzito sawa. Kwa hiyo, wataalam wa Taifa hili na ninyi mliopata fursa ya kumshauri Mheshimiwa Rais, ni lazima msiwe wavivu wa kufikiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasoma ripoti, mnamo mwezi wa Pili mwaka huu nchi sita zilienda kupeleka Umoja wa Mataifa mipango yao ya kurejesha maeneo oevu. Mheshimiwa Prof. Kitila hapo unapenda sana kusoma vitabu, sasa nami nakuomba ukasome ili mkashauriane vizuri kuhusiana na Mbarali. Nenda kasome mpango wa Zambia walivyofanya kurejesha maeneo oevu, kasome mpango wa Gabon, kasomeni mpango wa DRC Congo, kasomeni mpango wa Mexico, walifanya yafuatayo, na Mbarali inawezekana kufanyika ili wananchi waendelee kufanya shughuli zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, walivyofanya na nilivyosoma ripoti kwa udogo kabisa, na ni mambo ya kawaida, gharama ndogo kabisa kuliko gharama za kuhamisha watu kila baada ya muda fulani. Kwanza, walianza kujenga miundombinu ya umwagiliaji. Hiyo kazi Mheshimiwa Rais ameshaifanya Mbarali na anaendelea kuifanya. Leo Waziri wa Kilimo yuko pale, kaka yangu Mheshimiwa Bashe, tuna miradi sita ya umwagiliaji inaendelea, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameleta shilingi bilioni 78. Mnatuhamisha twende wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya hivyo, juzi nilikuwa namwuliza hapa kaka yangu Mheshimiwa Bashe, mna mpango gani wa kutujengea mabwawa? Akaniambia wanakuja Mbarali kujenga mabwawa ya umwagiliaji. Sasa mnawapeleka wapi hawa watu wakati Mheshimiwa Rais ameshaanza mipango?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, wenzenu walichofanya, tunajua sheria za kufanya kazi pembezoni ya mito ni mita 60. Twendeni tukapande miti pembeni ya hizo mita. Nasi wana-Mbarali tuko tayari kuongoza zoezi hilo, lakini siyo kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, wenzetu wanachofanya ili kurejesha maeneo hayo wanasema wanalima kwa msimu mmoja wa mvua. Wakulima wadogo wa Mbarali ndicho wanachofanya, wanalima msimu mmoja wakati wa mvua peke yake. (Makofi)

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa taarifa.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, anachokizungumza Mbunge wa Mbarali, nami ni Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, uvivu wa wataalam wetu Mheshimiwa Waziri Mchengerwa tulivyoenda kule, anawauliza kwa nini hapa mnawahamisha na hawa mnawaacha? Mtaalam anasema hawa hawana miundombinu mizuri ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, anachokizungumza Mheshimiwa Mbunge ni sahihi, wataalam wetu ni wavivu wa kufikiri. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa unaipokea taarifa hiyo.

MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipokea kwa mikono miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala la Mbarali kama mlivyotuhamisha mwaka 2008, uharibifu uliongezeka zaidi. Leo ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja ni zaidi ya 170,000. Upi mkakati wa ku-recover hizo ajira? Eti tunaenda kupoteza ajira 170,000 kwa ajili ya kuhamisha watu. Kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu nakuomba, ungesitisha hata zile fedha zile za tathmini, mgeendelea kutujengea miundombinu Mbarali ili tuendelee kuwa salama. Tathmini hizo za nini wakati utaalam unajulikana? Kasomeni ripoti, wenzenu wa nchi hizi wamefanya haya na yamewezekana. Leo wananchi wa Mbarali wamesimamishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Rais, alimtuma Makamu Mwenyekiti wa Chama hiki awaambie wananchi wa Mbarali walime, lakini yako maeneo ambayo walikatazwa kulima. Leo hii ugonjwa wa sukari na Mheshimiwa dada yangu Mheshimiwa Ummy ungepeleka vipimo kule. Katika Wilaya ambayo watu wanaumwa sukari na pressure, Mbarali inaweza ikaongoza. Kwa hiyo, naomba sana, jambo hili hebu wataalam wa Taifa hili msiwe wavivu kufikiri. Yanapokuja masuala magumu ya wananchi, twendeni tukahakikishe wananchi wanafurahia maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utiririshaji wa maji ni muhimu. Nimezunguka Mbarali wakati wa kampeni, hata kabla ya hapo tumezunguka maeneo mbalimbali. Tumewashauri watu wa mazingira, Mbarali inapokea maji kutoka maeneo tofauti tofauti, ina vijito; mito ile imeziba. Mnasema utiririshaji wa maji kwenda Ruaha ni mbaya, tumewaambia nendeni mkachimbue ile mito vizuri ili mtiririko wa maji uende vizuri. Leo hii tunakwenda kuwaadhibu masikini wenye heka mbili, tatu, nne. Ina maana kweli sisi hatuwajui watumiaji wa maji wakubwa Mbarali? Hapana, siyo sawa. Ni lazima ifikie wakati tumshauri Mheshimiwa Rais kwa kuangalia maslahi mapana ya wana-Mbarali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili inawezekana labda wenzetu, sijui, mnaogopa kuliwasilisha. Mimi binafsi nimemwandika barua Mheshimiwa Rais nikamwone kuhusiana na hili ili nikamweleze kama ninyi mnashindwa kutusaidia wataalam wa Taifa hili kupeleka maoni ya wana-Mbarali na utaalam halisi unaonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemeandikia nimwone. Naamini Mheshimiwa Rais atanipa fursa nimwone, nimwelezee nini wana-Mbarali wanataka? Naamini kwa usikivu wake, kwa upendo wake wana-Mbarali atatupa fursa tutaliangalia upya suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashukuru sana kwa kupata fursa hii. Nawaomba sana wataalam na mnaoweza kumshauri Mheshimiwa Rais, mkiwa mnakaa, suala la Mbarali siyo la kujadiliana kwenye karatasi kirahisi, siyo suala la kukaa na kujadiliana kwenye makaratasi. Chama cha Mapinduzi chenye Serikali hii, kiko na wananchi kwenye suala hili.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge waliokuja Mbarali wako na wananchi, lakini Wabunge waliofika Mbarali kwenye kampeni ni mashahidi. Wameona hali halisi ya wana-Mbarali. Vilevile CCM, mimi Mbunge wao tuko na wananchi na suala la kuhamisha siyo suala jema na wanaofikiria kumshauri Mheshimiwa Rais hivyo hawawatendei haki wana-Mbarali na hawamtendei haki Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, tushauri vitu ambavyo vitakwenda kujenga hata morally ya wananchi. Twendeni mkamshauri vitu vya msingi Mheshimiwa Rais. Fikirieni wataalam wa Taifa hili, nendeni mkaanzishe vituo vya kufuatilia uhifadhi. Niwaambie kabisa, katika mpango wenu Waheshimiwa sijaona mkakati madhubuti wa mambo ya uhifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnapenda kufanya vitu simple, yaani tunafanya tu uhifadhi kwa maneno. Uhifadhi unataka investment. Wekezeni kwenye uhifadhi. Kuhamisha watu siyo suluhu la uhifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashukuru sana kwa kupata fursa hii, naunga mkono hoja. (Makofi)