Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Nicholaus George Ngassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa 2024/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2000 wakati tunaweka Dira ya Maendeleo ya Taifa kwa maana ya 2000/2025 kama Taifa tuliweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha tunapambana na umaskini na kukuza uchumi. Tulianza na Mkakati wa Kupunguza Umaskini (Poverty Reduction Strategy Paper) tukaja MKUKUTA I, MKUKUTA II na sasa tumeingia katika ungwe ya Mpango ya Maendeleo ambayo kwa sasa tupo Mpango wa Tatu wa 2021 mpaka 2026. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipo hapa na niliposikia na kuchangia Mpango wa 2021 nilijipa kazi ya kufanya utafiti kidogo na kujua vitu gani vinatushika miguu kama Taifa katika kuhakikisha mipango yetu inafanikiwa. Jambo la kwanza, nilipitia Dira ya Maendeleo ya Taifa na kuona malengo makuu matano ambayo yameenda na Dira ya Maendeleo ya Taifa. Lengo la kwanza ilikuwa ni kuboresha hali ya maisjha ya Watanzania; lengo la pili kuwepo mazingira ya amani, usalama na umoja; lengo la tatu kujenga utawala bora; na lengo la nne ilikuwa kuwepo kwa jamii iliyoelimika vema na kujifunza na lengo la tano ilikuwa ni kujenga uchumi imara unaoweza kukabiliana na ushindani kutokana na nchi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupitia hayo malengo nilikuja kubaini kuna baadhi ya mambo, nilibaini mambo mengi lakini leo nitachangia mambo kama manne ambayo yamekuwa yakituvuta miguu katika kuhakikisha Taifa letu linakimbia katika kufikia malengo ya Mpango wa Maendeleo Taifa lakini pia katika mipango hii ambayo tumekuwa tukijiwekea na leo tuko Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo nimekuja kuligundua katika utafiti wangu mdogo ambalo linatushika miguu kwa kiwango kikubwa ni urasimu katika sekta ya umma. Serikalini bado kuna urasimu mkubwa sana jambo ambalo limekuwa likitukwamisha sana katika kukimbia. Unaenda kwenye ofisi za Umma jambo linalohitaji kufanyiwa maamuzi ndani ya siku mbili au siku tatu linakaa zaidi ya wiki mbili mezani na inatakiwa watendaji wetu wachukue mfano wa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Wabunge tutakapopitisha sheria itakapofika kwenye meza ya Mheshimiwa Rais huwa haichukui zaidi ya masaa 24 Mheshimiwa Rais ameshasaini zile sheria. Ninyi kama viongozi wetu mnatupatia taarifa Bungeni lakini bado kwenye utumishi wetu wa umma urasimu umekuwa ni mkubwa vitu vinakaa muda mrefu mezani, hata kwenye suala la uwekezaji, tunawakatisha tamaa wawekezaji kwa sababu ya urasimu ambao unaendelea. Waheshimiwa Mawaziri ambao mmewasilisha leo taarifa zenu tunaomba hili jambo mshirikiane na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma lakini na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambapo kuna asilimia 80 ya watendaji wote, urasimu upungue ili tuweze kusonga mbele na tuweze kukimbizana kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nilishawahi kutoa pendekezo moja, hakikisheni kwenye kila taasisi na Idara za Serikali wana Client Service Charter, kwa maana ya mkataba wa huduma kwa mteja. Wapeni muda, file likifika mezani ndani ya masaa 48 liwe limetoka ila tukiendelea, mtu anatoka ofisini hakaimishi ofisi anaenda kwenye kazi field anafunga ofisi anatumia siku tatu, nne ofisi imefungwa file limelala. Mwisho wa siku hata wananchi wetu tutaendelea kuwakatisha tamaa. Kwa hiyo, jambo la urasimu tuliangalie sana, linatukwamisha katika maendeleo yetu na kutekeleza Mipango ya Maendeleo ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ni jambo la muhimu sana ni miundombinu ya kiuchumi. Katika suala la miundombinu ya kiuchumi tunasema hii ndio ile mishipa ya damu katika uchumi wa Taifa letu na hapa naongelea suala la umeme, barabara, reli, mawasiliano na huduma za kifedha. Kwenye suala la umeme, tunaomba kabisa Serikali kwenye huu mpango muende mkalisimamie Bwawa la Mwalimu Nyerere likamilike tuanze kuzalisha umeme wa uhakika. Uzalishaji wa sasa kwa kutumia mafuta umekuwa na hasara kubwa sana kwa wawekezaji wa nchi hii, lakini pia katika ukuzaji wa uchumi ni jambo ambalo limekuwa likilitia hasara lakini pia na gharama ya uzalishaji imeongezeka matokeo yake tunawatia hasara wawekezaji wetu, wazalishaji na pia tunaathiri uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye suala la barabara kumekuwa na mkazo sana, tumejikuta tumeweka nguvu kubwa sana, tumetengeneza hizi barabara kubwa kwa maana ya trunk roads highways. Tunaomba sasa Serikali muweke mkazo kwenye barabara za ndani feeder roads ambazo ndizo zinalisha maeneo mengi zinatoa uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, pale kwetu Igunga tuna barabara moja ya Igulubi – Mutu – Igunga – Mwanzugi – Itumba, haya ni maeneo makubwa sana ya uzalishaji, tumekamilisha kufanya usanifu kupitia TARURA na tuliambiwa tutapewa shilingi bilioni 3 na milioni 500 kwa ajili ya kukamilisha hili. Naomba Waziri wa Fedha katika bajeti ijayo jambo hili ututilie mkazo, tupatiwe fedha. Sisi tunalima pamba kwa wingi, asilimia 90 ya pamba inayotoka Mkoa wa Tabora inatoka kwenye Wilaya ya Igunga na ukanda wote wa Igulubi ndio wakulima wakubwa wa pamba. Tunaomba tupatiwe fedha tuweze kurekebisha barabara hii ambayo ni muhimu sana katika uchumi wa Wilaya yetu, Mkoa wetu na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nimekuja kugundua linatushika kamba ni suala la ushiriki wa sekta binafsi. Tumekuwa tukisema kwamba tutashirikisha sekta binafsi katika ujenzi wa uchumi. Hii dhana ya sekta binafsi inaeleweka sana kwa ngazi yenu huku juu ngazi ya Mheshimiwa Rais na ninyi Mawaziri lakini kule chini bado watendaji wenu wa Serikali hawatoi ushirikiano mzuri kwa sekta binafsi. Bado kuna harassment kubwa sana kwa wafanyabiashara wadogo wadogo na wafanyabiashara wa kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo ambalo tunahubiri lakini katika utekelezaji linakwenda tofauti, tunaomba Waheshimiwa Mawaziri hili jambo mkalisimamie vizuri ili angalau sekta binafsi kinachohubiriwa na Mheshimiwa Rais na ndiyo maana mnaona Mheshimiwa Rais anapofanya ziara ukiacha wale watu anaoambatana nao kwa sababu za kiitifaki anaenda na wafanyabiashara, lengo ni kuhakikisha sekta binafsi inakuwa ni engine katika kusaidia Serikali kuendesha uchumi lakini kwa juu limekaa vizuri ukienda huko ngazi za chini kwenye Wilaya zetu, kwenye Mikoa yetu bado hali si nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia la nne katika mambo ambayo yanakwamisha sana mafanikio kwenye Mpango wa Maendeleo ya Taifa ni suala la Utumishi wa Umma. Kwenye utumishi wa umma bado kuna changamoto kubwa, jambo mojawapo ambalo ningependa kabisa kama Serikali mlitilie mkazo ni nidhamu ya kazi, bado nidhamu ya kazi siyo nzuri huko kwenu chini katika maeneo mengi ambayo sisi tunaendelea kuyaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta kuna mabishano, Mkuu wa Mkoa anabiashana na Watendaji. Mkuu wa Mkoa anatoa maelekezo anaandikia barua Watendaji kwa mfano TRA au Taasisi nyingine zozote wanambishia maelekezo hawayafanyii kazi. Sasa hii ni discipline ya aina gani katika utumishi wa umma? Tunaomba hili mlifanyie kazi ili angalau mipango yetu inapokwenda kule na kuweza ku-harmonize situation ili tuweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulisema katika upande wa utumishi wa umma ni motisha, kuhakikisha watumishi tunaendelea kuwapa motisha na motisha siyo lazima iwe fedha kwa upande wa utumishi wa umma, hata mahusiano. Wale Watendaji Wakuu wa Taasisi mhakikishe wanaishi katika mahusiano ambayo ni mazuri na watumishi wao wanaowaongoza ili waweze kuwapa ushirikiano na tuweze kujenga Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, nashukuru sana kwa kunipa nafas. Ahsante sana. (Makofi)