Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza na mimi nianze kabisa kwa dhati ya moyo wangu kumpongeza Waziri wa Fedha, Ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, pamoja na Waziri wa Mipango, Ndugu yangu Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, kwa kweli nimesikiliza mawasilisho yao yote vizuri sana yanatia matumaini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipekee niweze kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuweza kuwateua ndugu zangu hawa wawili, mmoja aweze kuendesha Wizara ya Fedha na mwingine akae kwenye Mipango, hakika mapacha wale mnavyowaona pale walivyopendeza kazi yao ni nzuri, wanaifanya vizuri na kwa kupitia mawasilisho waliyowasilisha hapo tunaona matumaini na mambo mengi yanakwenda kufanyika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa lolote linalohitaji kuendelea kwa haraka na kwa kasi halina budi ya kuwekeza kwenye miundombinu ya ardhini, miundombinu ya usafirishaji kwenye anga na kwenye maji. Kwa kuwa Taifa letu linahitaji kuendelea kwa haraka hatuna budi nasi kama Tanzania kuweza kuwekeza kwenye miundombinu ya aina hiyo, mathalani kwa upande wa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakubaliana nami pamoja na Wabunge wote, kwamba Tanzania ni lazima tuendelee kuwekeza kwenye ujenzi wa reli ya kisasa SGR, lazima tuendelee kuwekeza kwenye kupanua viwanja vya ndege lakini na kuweka meli za kisasa ili ziweze kusaidia Watanzania kusafirisha mizigo yao na wao wenyewe kusafiri kutoka eneo moja kwenda eneo jingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalani kwa upande wa Jimbo langu la Ngara, pale Ngara kuna barabara ya kimkakati ambayo kama haitajengwa ndoto ya Tanzania ya kuvuna nickel, ambayo ni madini ya kimkakati yanayosubiriwa duniani ili yaende yakatengeneze betri hiyo ndoto haitatimia. Mheshimiwa Kitila Mkumbo, nataka nikupe taarifa hapa kwamba barabara ya kutoka Mlugarama kwenda Rulenge, kutoka Mlugarama – Rulenge – Kumbuga kilometa 75 na barabara ya kutoka Nyakahura – Kumbuga – Mlugarama – Mrusambaga – Gaumo kilometa 34 na barabara ya kutoka Rulenge – Tembo Nickel kilometa 32, jumla ni kilometa 141 kama hazitajengwa Mheshimiwa Kitila Mkumbo ile nickel ya Ngara haitovunwa kwa miaka 47.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kwa utaratibu wa Serikali uliopo sasa hivi wa kutoa shilingi bilioni tatu ile barabara ijengwe kilometa tatu kila mwaka na hapa tuna kilometa 141 itatuchukua miaka 47 kwa ile barabara kujengwa na ikakamilika. Kupanga ni kuchagua, tumepanga kuilisha dunia kuiuzia nickel iliyopo Tanzania na nickel hii siyo Tanzania pekee, hii nickel iko Tanzania lakini ndiyo nickel ya kipekee Afrika na pengine duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari kama Taifa tumeshaingia mikataba na wawekezaji. Wawekezaji wako pale kwenye ground lakini hawawezi kusafirisha makontena na mizigo mikubwa kutoka Dar es Salaam kuipeleka kule ili waanze kujenga ule mgodi kwa sababu ile barabara haipitiki na hakuna namna yoyote hata madaraja yale kuna mizigo ikipita pale madaraja yatadondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kupanga ni kuchagua tumeshaingia, tumeshaasaini mikataba na wawekezaji muda muafaka wa kujenga ile barabara kwa kiwango cha lami ni sasa ili zile nickel ziweze kutuletea tija kwa Taifa eneo la kwanza. Kwa hiyo Mheshimiwa Kitila Mkumbo, kwa kweli sitopitisha mpango huo kama tutapiga kura au hata bajeti ya mwakani kama hii barabara haijaingizwa kwa sababu nitashika shilingi mpaka hii barabara iingizwe ili zile nickel ziweze kuchimbwa na wananchi wangu waendelee kufanya kazi kwenye mgodi ule waendelee kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwa kweli kwa unyenyekevu mkubwa sina nia ya kushika shilingi maana najua utaweka Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo, kama utajisahau tunaweza tukafikia huko lakini kwa unyenyekevu mkubwa nikuombe kabisa kwenye mipango yetu hii ya maendeleo ya Taifa hasa huu wa 2024/2025 ujitahidi hii barabara iingie kwenye mpango ili uweze kupewa fedha na iweze kutekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni reli ya kisasa ya SGR kutoka Isaka ambayo ipo Kahama mpaka Rusumo. Kupanga ni kuchagua kutoka pale Rusumo mpakani na Rwanda, ni kilometa 200 mpaka Kigali kutoka Kigali kwenda mpaka Goma ni kilometa 150, kujenga kipande cha SGR cha kisasa kutoka Isaka mpaka pale Rusumo ni kilometa 338, kupanga ni kuchagua tukizubaa Watanzania soko la la Congo, Goma yote litachukuliwa na mataifa mengine ambayo yataendeleza SGR kutokea Kenya kuingia Uganda mpaka Rwanda na huko Goma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania Mwenyezi Mungu ametuwezesha kwamba sasa SGR inafika pale inakwenda mpaka kwenye kiwanda cha uchenjuaji cha Tembo Nickel pale Buzwagi, sasa Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, naomba tusaidie hili Taifa liweze kwenda kunufaika na masoko ya Congo na Rwanda, sisi tutajenga reli yetu mpaka pale mpakani lakini wenzetu hawatashindwa kujenga hizo kilometa 150. Ninaomba eneo hili liweze kufanyiwa kazi na liingizwe kwenye mpango wa maendeleo ya Taifa ili kama Taifa tuweze kunufaika na rasilimali ya sisi kuwa katikati ya mataifa mengine yanayotuzunguka.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la kilimo. Ninapendekeza Wizara ya Kilimo ipewe fedha za kutosha ili iweze kuwekeza kwenye kilimo kwa sababu mpaka dakika hii kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Tanzania na Watanzania wanasubiria kilimo ili waweze kuishi. Taasisi za kilimo kama vile TARI na Bodi ya Kahawa bila kuweka kwenye Mpango wa Maendeleo ya Taifa na kuhakikisha wanapata fedha ili waweze kuzalisha miche ya kutosha, nataka nikuambie tutakuwa hatuwasaidii Watanzania, namna pekee ya kuwasaidia Watanzania ni kuwawezesha kupata mbegu na pembejeo za kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameweka mazingira mazuri kwa Watanzania kuweza kupata mbolea za ruzuku. Ninampongeza Mheshimiwa Waziri Bashe, ameweka utaratibu mzuri sasa Watanzania wanapata mbolea za ruzuku, lakini sasa twende mbele tuwasaidie Watanzania kupata miche. Kwa mfano, upande wa Wilaya ya Ngara, mahitaji yetu ya miche ya kahawa 2024/2025 ni miche milioni tatu ya kahawa. Kwa mfano ukitupatia miche ya Robusta, tutaweza kupanda hekta 3,000, kwenye hekta hizo tutaweza kuvuna kilo za kahawa ambayo ni safi 3,300,000 ukizidisha mara mbili kwa maana ya kahawa yenye maganda tutapata kahawa yenye maganda zaidi ya 6,600,000 tukiuza kwa bei ya juzi ya shilingi 3,040 Wanangara tutaweza kutengeneza fedha zaidi ya bilioni 18 kwa kila mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaposimama hapa kuchangia Mpango wa Maendeleo ya Taifa, hii ndiyo vision, huu ndiyo muonekano na mkifanya hivi nchi nzima kwa maeneo mengi, Watanzania wanakwenda kutoka kwenye dimbwi la umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetumwa kama Mwakilishi wa Wananchi wa Ngara, nimetumwa nije hapa niwe kisemeo, nije niwatetee na kwa kuwa sasa tunakwenda kutengeneza Mpango wa Maendelea ya Taifa na kwa kuwa hakuna mradi utakaotekelezwa bila kuingia kwenye mpango wa maendeleo ya Taifa, ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa Wizara ya Kilimo tuende tuiwezeshe, iweze kuzalisha miche ya kutosha ili wananchi na Watanzania wanaohitaji kuwekeza kwenye kilimo waweze kupata miche hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwa upande wa Ngara, naomba Mpango wetu uainishe miche 3,000,000 ya kahawa na miche 2,000,000 ya parachichi tumechoka kuendelea kuishi kwenye umaskini. Tunataka ifike mahali sasa na sisi tuwe matajiri tujivunie kutumia ardhi ambayo Mwenyezi Mungu, alitupatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine. Kuna miradi mingi sana kwenye kilimo hasa ya masoko ya kimkakati ilishajengwa muda mrefu na kutelekezwa. Katika eneo hili naomba nisimung’unye maneno kuna watu walipiga hela lakini kwa bahati nzuri hazikupigwa katika kipindi hiki, zilipigwa kipindi mimi sijawa Mbunge, wamekwenda pale Kabanga wametengeneza soko la kimkakati la Kimataifa lakini limejengwa likaishia katikati na mradi ulikuwa unasimamiwa na Wizara ya Kilimo, moja kwa moja kutoka huku Dodoma. Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa, hawakuwa na nafasi ya kuweza kusimamia ule mradi, watu wamepiga hela document zinaonekana mradi umekamilika, majengo yamebaki yametelekezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tunapotengeneza Mpango wa Maendeleo ya Taifa, tuhakikishe miradi hii iliyosimama muda mrefu tunaijenga inakamilika, tumechoka kuona watu wanatoka Bunjumbura wanapitiliza kwenda kununua dagaa Bukoba na wanakwenda kununua vitu Dar es Salaam, soko likiwepo pale la kimkakati watu watatoka nje ya nchi watakuja Ngara kununua vitu mpakani, sasa miradi yote nchi nzima iliyotelekezwa muda mrefu, Mpango wetu wa Maendeleo ya Taifa ulenge kwenda kuhakikisha miradi hiyo inakamilika, kwanza inatuchefua, pili inatunyima kura, tatu inaonekana hatuko serious, ninaomba Wabunge wote wenye miradi ambayo haijakamilika huu ndiyo muda muafaka wa kuhakikisha miradi hii inaingizwa kwenye Mpango wa Maendeleo ya Taifa na tunahakikisha tunasaidia Tanzania.

MWENYEKITI: Ahsante, kengele yako ya pili hiyo malizia sekunde mbili.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia na eneo la mwisho la kuwasaidia Watanzania kupata vitambulisho vya Taifa. Kuna Watanzania sasa hivi hawawezi kumiliki laini ya simu kwa sababu hana NIDA, kuna Watanzania wa Ngara hawawezi kwenda Vyuo Vikuu kwa sababu hawana kitambulisho, hawezi kupata admission ya Chuo Kikuu.

MWENYEKITI: Ahsante. Mwandikie Waziri.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa unyenyekevu mkubwa naunga mkono hoja lakini naomba mpango usaidie Watanzania kupata vitambulisho vyao vya utaifa ili waweze kufurahia huduma ndani ya Taifa lao na wananchi wa Ngara wapewe kipaumbele, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)