Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Mimi natokea Kamati ya PIC. Nitaongelea ufanisi…

MWENYEKITI: Waheshimiwa, naomba tupunguze sauti tuwasikilize wachangiaji wetu.

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea ufanisi wa mashirika yetu ya umma. Kamati imepitia mashirika ambayo Serikali yetu imewekeza zaidi ya trilioni 73.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuaji wa mitaji katika mashirika yetu, pamoja na uwekezaji mkubwa ambao Serikali imeweka lakini ukuaji wa mitaji unatia shaka na wasiwasi. Kwa kipindi cha miaka mitatu, ukuaji wa mitaji katika mashirika yetu ya umma ni asilimia nane tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama watangulizi waliochangia walivyosema, Serikali imewekeza fedha nyingi katika mashirika yetu ya umma lakini return katika uwekezaji ni mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Serikali kuwekeza trilioni 73 katika mashirika ya umma hayo mashirika ya umma yanayo matobo mengi sana. Asubuhi tumesikiliza ripoti tatu ambazo zimesomwa na Kamati tatu, kwa kweli inahitaji moyo mgumu kuzipokea na kuzikubali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uwekezaji katika mashirika yetu ya umma; mashrika yetu mengi yanasuasua. Serikali inawekeza fedha ya walipakodi lakini mapato yanayotokana na uwekezaji huo ni madogo. Tunayo kazi kubwa mbele yetu ya kufanya ili kuhakikisha kwamba uwekezaji unaendana sambamba na mapato tunayoyapata kutokana na uwekezaji huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya PAC imetoa taarifa yake asubuhi, kati ya mashirika 66 ambayo yalipaswa kutoa gawio ni mashirika 25 ambayo yametoa gawio, mashirika 41 hayajachangia chochote. Ni kana kwamba Serikali kwa kipindi cha miaka mitatu haijawahi kuwekeza fedha yoyote ya walipakodi; lakini tunajua Serikali imewekeza fedha nyingi lakini mashirika yanafanya vibaya na tumenyamaza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo mashirika 25 ambayo yamesema yamechangia mfuko mkuu wa Serikali ni mashirika matatu tu ambayo yamechangia zaidi ya asilimia 38, na hayo yametajwa hapa; ni BOT imechangia bilioni 200, Airtel imechangia bilioni ishirini na kitu na NMB; mashirika mengine yote yanasuasua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimenangalia hata kwenye mchango wa GDP mashirika yetu haya ambayo tumewekeza zaidi ya trilioni 73 kwa kipindi cha miaka mitatu mwaka 2019/2020 kwenye GDP yamechangia 0.6, yaani hata asilimia moja haifiki. Tumewekeza fedha nyingi lakini tunachokipata kama Taifa ni kidogo mno. 2020/2021 yamechangia 0.5, 2021/2022 ni 0.6 kwenye GDP, 2022/2023 0.6; kwenye bajeti yanachangia asilimia tatu kwa miaka mitatu mfululizo. Sasa tunajiuliza tunawekeza ili iweje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapowekeza kwenye kitu chochote; amesema mchangiaji wa mwisho kwenye TANOIL; tunapowekeza fedha ya walipa kodi tunatarajia baada ya mwaka mmoja au miwili tuweze kuvuna; na kama tunawekeza bila kuvuna haina maana yoyote ya kuwekeza kwenye haya Mashirika ya Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeangalia gawio, haya Mashirika ambayo hayakuleta gawio ni hatua gani zinachukuliwa na Serikali? Lakini kwa kipindi cha miaka mitatu hakuna hatua yoyote imechukuliwa dhidi ya mashirika ambayo hayakutoa gawio. Tunachokisikia ni Mkurugenzi anahamishwa anatolewa shirika moja anapelekwa shirika jingine na anapopelekwa kwenye shirika jingine ni business as usual.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo tunalijua, mwaka jana nilichangia hapa, kwamba tatizo la mashirika yetu ni sheria ambayo tunayo ambayo inaongoza mashirika haya. Mwaka jana nilisema na nikashauri, kwamba kama tunataka ufanisi kwenye mashirika ya umma lazima twende kubadilisha sheria ambayo ni kongwe sheria ambayo haimpi pia uwezo wa kuyasimamia mashirika haya ya mmma…

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Oscar kuna taarifa.

TAARIFA

WAZIRI WA MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri wa Mheshimiwa anayechangia nataka tu nimpe taarifa kwamba siyo sahihi kusema kwamba hakuna hatua yoyote inayochukuliwa kuhusu mashirika ya umma ambayo hayafanyi vizuri. Mnafahamu mwaka jana na mwaka huu Mheshimiwa Rais aliagiza mashirika ambayo yanasuasua yachukuliwe hatua na mnafahamu mwaka huu Msajili wa Hazina ametangaza hadharani kwamba yapo Mashirka ambayo yanakwenda kufutwa, yapo ambayo yanakwenda kuunganishwa. Lakini muhimu zaidi tumetangaza hadharani kwamba tunaanzisha sheria mpya ya kuyaangalia mashrika haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nakubaliana naye kwamba kuna Mashirika yana changamoto lakini siyo sahihi kusema kwamba hakuna hatua zozote ambazo zimechukuliwa. Kuna hatua zipo zinachukuliwa, ahsante sana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana nilitoa ushauri huo kama umechukuliwa na kama hatua zimechukuliwa tumshukuru Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ku-merge mashirika au kuunganisha mashirika bila kutibu ugonjwa unaotafuna mashirika yetu ni kazi bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria iiliyopo ya sasa ambayo wanasema wanakwenda kuifanyia marejeo kimsingi hatupaswi kufanya marejeo kwenye sheria iliyopo tunapaswa kutunga sheria mpya. Mwaka jana nilisema, kama Maandiko Matakatifu yasemavyo huchukui wine mpya ukaweka kwenye viriba vya zamani. Sheria iliyopo haifai, sheria iliyopo ni ya mwaka 1959, kipindi ambacho Taifa hili lilikuwa halijapata uhuru mpaka sasa bado tunatembea na sheria kongwe ya namna hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashuri na kupendekeza kwenye Sheria itakayotungwa ihakikishe inampatia uwezo TR kuyasimamia mashirika haya ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri au kupewa uwezo wa kuteua bodi kuzisimamia bodi na kuwasimamia watendaji wakuu wa hayo. Kama tunataka kufanya biashara tuondokane na tabia ya uteuzi wa Wakurugenzi kwenye mashirika yanayofanya biashara. Kama tunataka kwenda kufanya biashara kufanye biashara kama kampuni nyingine zinavyofanya; kwamba watendaji wakuu wapatikane kwa njia ya ushindani badala ya uteuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini haya mashirika yenyewe haya TR mpaka wakati huu tunapoongea hana mfuko wa kuyasaidia haya mashirika katika mizania ya uwekezaji. Tumeona mashirika mengi yanapotokea matatizo yanakosa uwezo wa kukabiliana na matatizo ya kibiashara; TR hana uwezo wa kifedha kuyasimamia wanabaki kusubiri Serikali iwapatie fedha na wakati mwingine fedha ya Serikali inaendana na bajeti ambayo Bunge lako limeipitisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kamati yetu tumebaini baadhi ya matatizo ambayo mashirika yetu yanakabiliana nayo; mojawapo ni kuchelewesha kumaliza miradi ya maendeleo. Tumeangalia kipande cha SGR kutoka Dar es salaam mpaka Morogoro kwa kipindi cha miaka mitatu tumeongelea hili tatizo tunasubiri nini? Tunaambiwa kipande kimekamilika asilimi 98.9 lakini kwa kipindi cha miaka mitatu tumekuwa tukisikiliza maneno yaleyale kutoka kwa watu walewale, hakuna kinachoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi mingine ya TANROADS; tuna Mradi wa Nyakanazi stopover tulikuwa na mradi wa kusuka magari pale Nyakanazi na mwingine upo pale Manyoni, hii miradi imesimama tangu mwaka 2016. Serikali imewekeza fedha yake pale ya walipakodi lakini hakuna kinachoendelea. Tunajiuliza, hivi wakati tunakwenda kuwekeza pale tulifanya upembuzi yakinifu au tulifanya due diligence au watu waliamua tu wakaamka wakaenda kufanya uwekezaji pale? Fedha ya walipa kodi imesimama, fedha ya walipa kodi imetumika na hakuna tija katika uwekezaji huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napenda nishauri Serikali, tunapoamua kutekeleza miradi ya maendeleo, tunapoamua kuwekeza katika sekta yoyote kwanza tumalizie miradi viporo ndio twende kwenye miradi mipya vinginevyo miradi ya zamani haikamiliki na tunayoendea mipya haikamiliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili la mwisho tumeongelea miradi ya maji; Serikali hususani Wizara ya Maji ilishatoa kiwango cha upotevu wa maji hapa nchini isizidi asilimia 25, wengi wamelisema hili, nitaomba nimalizie na hilo. Lakini ukiangalia mamlaka zetu za maji, mamlaka nyingi upotevu wa maji unakwenda zaidi ya asilimia 38 na tusipochukua hatua mapema, na muona Mheshimiwa Waziri wa Maji yupo, tusipochukua hatua mapema kwa uzembe ambao nauona watu mamlaka zinaanchaia mabomba hata leo nyumbani kwangu pale maji yanamwagika siku saba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: …tusipochukua hatua mapema maji tunayozalisha asilimia 50 yatapotea na tutakuwa tumewekeza fedha lakini wananchi hawapati maji kadri inavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.