Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Suma Ikenda Fyandomo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Kipekee nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kunitia nguvu ili niweze kuchangia kwenye Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kuchangia kwa namna ambavyo mwenendo wa halmashauri zetu. Halmashauri zetu zina Wakurugenzi ambao ni wachapakazi kwelikweli na vile vile zina Wakurugenzi ambao sio waaminifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ilianzisha utaratibu wa force account, kwa nia njema kabisa, lakini utaratibu huo kwa upande mwingine Wakurugenzi wanaosimamia hayo wanafanya vizuri sana, lakini kwa upande mwingine Halmashauri nyingine zinafanya vibaya sana. Hizi fedha ni za walipakodi masikini kabisa wa Taifa hili la Tanzania.

Mheshimiwa Spika, utakuta Mkurugenzi anakutwa na CAG kwenye ripoti zake, CAG anavyokwenda kukagua pale majengo ambayo yamejengwa kwa force account. Hayo majengo ni mapya, hayajaanza kutumika lakini wakati wa yalipokaguliwa yalikutwa na nyufa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, majengo hayo milango inadondoka yenyewe, hayajaanza kutumika, lakini Mkurugenzi alikuwepo kuangalia na kuhakikisha, maana yeye ndiye msimamizi mkuu wa hiyo halmashauri, lakini anakuwa yupo kama hayupo. Inatia uchungu sana na inasikitisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa majengo ya Serikali; yanatakiwa kujengewa vifaa ama hivi vifaa vya ujenzi ambavyo ni standard, ni imara kabisa. Kabla ya Force Account, mzabuni aki-supply ama mkandarasi ambaye anapewa jengo kulijenga, kama hajafanya vizuri, ukaguzi ukipita basi mzabuni ama mkandarasi huyo anawajibika kufanya ujenzi mwanzo mwisho ili kuhakikisha anakabidhi jengo hilo likiwa katika hali inayotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa, ujenzi huu wa Force Account jengo ni bovu, unakuta fedha shilingi milioni 800,000/= ama shilingi bilioni 1.2, jengo ni bovu, lina nyufa nyingi. Analaumiwa nani? Matokeo yake ni hasara.

Mheshimiwa Spika, Mtendaji Mkuu wa PPRA alipotutembelea kwenye Kamati yetu, nilivyokuwa nikichangia juu ya Force Account, namna ambavyo majengo mengi yanakuwa mabovu mapema kabisa kabla ya kuanza kutumika, nilivyokuwa namhoji kwamba moja ya halmashauri imepewa fedha zaidi ya shilingi bilioni 3.0, lakini jengo sio imara. Jengo wakati fulani limeshaanza kujengwa, fedha zimeisha jengo halijakamilika na fedha hazijulikani zimekimbilia wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inasikitisha sana. Mtendaji Mkuu yule wa PPRA akanijibu akasema, Mheshimiwa Mbunge, unachoongea kuhusu Force Account ni tatizo kubwa. Anasema mahali pengine wamepita wamepewa fedha shilingi bilioni 8.0, jengo halijakamilika. Shilingi bilioni 8.0 jengo halijakamilika, tunakwenda wapi? Watanzania tunatakiwa tufike mahali uzalendo ujae ndani ya mioyo yetu. Hizi fedha zinalipwa na mlipakodi. Kwenye halmashauri kuna matatizo makubwa sana. Kwa kweli matatizo ni makubwa, ni makubwa, ni makubwa, sijui ni namna gani tufanye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hizo fedha nyingi sana zinakwenda mabilioni kwenye Force Account. Sioni kama inatusaidia. Natamani sana kuishauri Serikali, fedha za Force Account angalau basi tuweke limit. Kama ni mambo ya Force Account, basi isizidi shilingi milioni 100, lakini kwa mabilioni eti Force Account, usimamizi unakuwa sifuri kabisa. Hilo linakuwa ni tatizo kubwa sana, mioyo inauma. Tunatakiwa tuwaonee huruma hawa walipakodi.

Mheshimiwa Spika, nakwenda kuchangia eneo la madeni ya wazabuni na wakandarasi…

MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika Taarifa.

TAARIFA

SPIKA: Mheshimiwa Suma Fyandomo, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Charles Kajege.

MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nataka nimuunge mkono msemaji. Force Account siyo kwamba tu miradi haikamiliki lakini hata ubora wake. Sehemu nyingi unakuta majengo yameshaharibika within mwaka mmoja. Kwa hiyo, nashauri kwamba ikiwezekana tuondoe kabisa mambo ya Force Account. (Makofi)

SPIKA: Sawa. Sasa, mwenye hoja yake alikuwa ameshatoa ushauri wake. Naona na wewe umeongeza wa kwako. Mheshimiwa Suma Fyandomo, endelea na mchango wako.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante.

NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Inatokea wapi taarifa.

NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, hapa.

SPIKA: Sasa, Mheshimiwa Waziri, ili nielewe taarifa unampa Mheshimiwa Kajege au Mheshimiwa Suma?

NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, wote wawili. (Kicheko/Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI, wote wawili! Haya.

NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kuwapa taarifa Waheshimiwa wachangiaji kwamba, kimsingi ukifanya tathmini ya utekelezaji wa miradi kwa kutumia Mfumo wa Force Account, kuna faida kubwa zaidi kuliko hasara. Kwa mfano, zahanati ambazo tunajenga kwa takribani shilingi milioni 100, ukichukua nguvu za wananchi na shilingi milioni 50 inaongezwa na Serikali, ukipeleka kwa mkandarasi zahanati ile siyo chini ya shilingi milioni 250 hadi shilingi milioni 300. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vituo vya afya ambavyo tunajenga kwa shilingi milioni 500, ukipeleka kwa mkandarasi si chini ya shilingi bilioni 2.0 hadi shilingi 2.1/=. Sasa, kuhusu udhaifu wa ubora wa miradi inategemea. Si kwa sababu ya Force Account, ni udhaifu wa usimamizi ambayo lingeweza kutokea pia, hata mkandarasi asiposimamiwa kuna miradi inakuwa na udhaifu wa aina hiyo. Kwa hiyo, naomba niwape taarifa Waheshimiwa Wazungumzaji kwamba, jambo la msingi ni usimamizi wa wataalam wanaokuwa katika maeneo yale badala ya mfumo kuwa Force Account au kuwa Contractor. Ahsante. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, tutatamani baada ya huo uzembe au udhaifu wa usimamizi, ni hatua gani zinachukuliwa ili wengine sasa wasiendelee na huo uzembe. Kwa sababu, haya yanayosemwa ya mabilioni hakuna mtu anayefurahi pesa iende halafu jengo lisikamilike. Pesa iende halafu jengo liwe halina viwango. Kwa hiyo, lazima tuone Serikali inachukua hatua gani kwa hao waliozembea ili huu mfumo uzuri wake uendelee na ule ubaya wake uondolewe kwa kuondoa hawa watu ambao wanaufanya mfumo mzima uonekane uko vibaya. (Makofi)
Mheshimiwa Suma Fyandomo, endelea na mchango wako.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, nilidhani kwamba unaniuliza kama napokea taarifa ama sipokei, ama maamuzi yameshatolewa. (Kichecho)

SPIKA: Nimeshindwa kukuuliza hilo swali, kwa sababu taarifa ya kwanza iliyotolewa ulikuwa umeshaingia kwenye hoja nyingine. Halafu Mheshimiwa Naibu Waziri amekuja baada ya ile taarifa nyingine na ushauri wa yule mwingine lakini naona kama wewe unakusudia kuipokea, basi nikuulize. Mheshimiwa Suma Fyandomo, unaipokea taarifa ya Mheshimiwa Naibu Waziri Kwa sababu, mchango ulikuwa wa kwako? Ahsante sana. (Kicheko)

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, naongea kwa uchungu mkubwa kwenye hili Taifa, nina uchungu moyoni. Siwezi kuipokea taarifa hii. Siwezi kuipokea kwa namna ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri, ni kaka yangu, namheshimu sana, ameongea anasema inatakiwa utafutwe utaratibu wa watu wa kwenda kusimamia fedha hizi. Utafutwe na nani na lini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunatakiwa tuwe makini sana na hizi fedha, tuwe na uchungu. Natamani sana na natamani wanaonipa taarifa, kwa maana wanaguswa na ninachokisema, wajiorodheshe na wenyewe waingie kwenye michango, ilikuwa njema sana. (Makofi/Kicheko)

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

TAARIFA

SPIKA: Mheshimiwa Fyandomo, kwa utaratibu wetu hii itakuwa ni taarifa ya mwisho. Mheshimiwa Mwanaisha, nimesikia kama sauti ya Mheshimiwa Mwanaisha Ulenge.

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nimpe taarifa dada yangu Mheshimiwa Suma Fyandomo kwamba, maneno anayoyasema ni sahihi na ni kwa mujibu wa tafiti. Aliyoyazungumza hapa Mheshimiwa Naibu Waziri, atuletee tafiti. Tafiti zimefanywa na PPRA ambaye ndiyo mwenye dhamana ya kusimamia manunuzi ya umma. Tafiti zimefanywa na Bodi ya Wahandisi. Tafiti zimefanywa na Baraza la Ujenzi Nchini kwamba, Force Account hazina tija kwa Taifa hili. Kwa nini tunaendelea kung’ang’ania? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiyo ndiyo taarifa ambayo nataka kumwongezea dada yangu Mheshimiwa Suma. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Haya. Mheshimiwa Waziri kaa kidogo. Mheshimiwa Suma Fyandomo, unaipokea taarifa hiyo ya Mheshimiwa Mwanaisha?

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ndiyo, naipokea kwa mikono miwili kabisa.

SPIKA: Ahsante sana. Sasa, kaa kidogo, nakulindia muda wako. Mheshimiwa Waziri wa Fedha naona umesimama, sijui umesimama kwa taarifa, utaratibu ama?

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, nilitaka kutoa taarifa na ufafanuzi. Pamoja na kuheshimu…

SPIKA: Sasa, ngoja tuliweke vizuri. Ufafanuzi utapata nafasi ya wewe kuchangia, ila kama unatoa taarifa, unaruhusiwa kuitoa sasa. (Makofi)

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, natoa taarifa.

TAARIFA

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, pamoja na maoni haya yanayotolewa na Waheshimiwa Wabunge, kuanzia mtoa hoja pamoja na Engineer ambayo yanalenga kusimamia rasilimali fedha za walipa kodi na value for money. Naomba tu kutoa taarifa kwamba, si kweli kwamba jambo hili halina tija yoyote. PPRA pamoja na Bodi ya Wahandisi waliishauri Serikali kuendelea kulifanyia maboresho na hicho ndicho tulichofanya, hata kwenye sheria tuliyoipitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge, utaratibu huu wa Force Account unatusaidia kujengea uwezo wananchi wetu kule majimboni. Utaratibu wa kutumia wakandarasi hata kwenye shughuli zinazotokea kwenye grassroot, unawafanya wananchi wetu wa kawaida wakose kazi. Utaona tulivyotumia Force Account kwenye fedha zile takribani shilingi trilioni moja, tuliweza kutengeneza mgawanyo wa fedha ziende kwenye kila wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kutumia wakandarasi, kuna baadhi ya maeneo huwa inaweza ikatokea mkoa mzima, wakandarasi wanaofanya shughuli hata za kujenga vyoo, hata za kujenga madarasa wanatoka mikoa mingine. Ni lini utajenga nguvu ya kazi na sasa hivi tumeshasomesha vijana karibu kila kata? Kwa hiyo, tutaendelea kuboresha na kusimamia mapungufu, lakini tutaendelea kuwatumia pia mafundi kujenga majengo yanayopatikana katika maeneo kule wanakoishi. (Makofi)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Tabasamu, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba alikuwa anatoa taarifa. Kwa hiyo, taarifa haiwezi kuwa juu ya taarifa nyingine. Muda wako Mheshimiwa Suma naulinda. Taarifa ya LAAC ukurasa wa 38 mpaka 39 unaonesha changamoto za matumizi ya Force Account na huku mbele umeeleza kuhusu maazimio, wanapendekeza nini kwa Bunge. Kwa hiyo, tunaweza kupitia hayo maeneo halafu tuone nini tunataka kufanya. Kwa sababu, ni kweli kwa upande mmoja kama alivyosema mchangiaji, inafanya vizuri. Kwa upande mwingine kuna changamoto. (Makofi)

Hizi changamoto siyo kwamba ni ndogo, ndiyo maana zinasemwa ili zifanyiwe kazi. Hakuna namna itaonekana huu mfumo uko vizuri kwa sababu tu maeneo yetu yale kuna watu wanaguswa, hapana. Tunataka tija kwenye matumizi ya huu mfumo. Nadhani ndicho ambacho Kamati inajaribu kusema kwenye hii taarifa yake. Kwa hiyo tupitie hayo maeneo ambayo taarifa ya Kamati imeyasema ili tuweze na sisi kujielekeza vizuri kwenye yale mapendekezo yetu kwa Serikali. (Makofi)

Kwa sababu, maeneo mengine inajengwa shule, Mwalimu Mkuu sijui Mkuu wa Shule ndiyo msimamizi. Sasa, yule siyo mtaalam. Kwa hiyo, mazingira kama hayo kidogo ni changamoto kubwa, kwa sababu, hata yeye ukisema unataka kumwajibisha unamwajibisha vipi? Yeye siyo mtaalam wa hilo jambo. Yeye kazi yake ni kufundisha lakini umempa kazi ya ziada. Kwa hiyo, kidogo inakuja hiyo changamoto kwa sura hiyo. (Makofi)

Kwa hiyo, katika yale maboresho itazamwe kwa sura hiyo pana anayochangia Mheshimiwa Mbunge. Mheshimiwa Suma Fyandomo, malizia mchango wako. Kwa maana ya kwamba muda wako ulikuwa umelindwa. Kwa hiyo, endelea kwenye hoja yako nyingine. Ahsante. (Makofi)

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Mheshimiwa Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba, ilitosha kabisa ile aliyoniambia kwamba wanafanya maboresho. Sasa, kwa sababu amejazia kitu kingine kaka yangu Mheshimiwa, basi naomba nimwambie. Unajua vifaa mfano vifaa vya bomba, inatakiwa kama ni koki ile ya bomba inunuliwe kifaa halisi. Sasa, hawa watu wakitumia Force Account kwenda kununua vifaa vya bomba, wananunua local kabisa, kiasi kwamba maji yanaanza kumwagika hovyo, mipira inapasuka na kila kitu. Ndiyo maana ya msisitizo kwamba, kwa sababu umesema maboresho boresheni kwa uhakika na kwa uhalisia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili suala lichukuliwe kwa uharaka sana na kwa umakini. Lichukuliwe kwa uharaka kwa sababu, kama ni maboresho watuambie ni lini ukomo wake wa maboresho kwamba, kufika kipindi fulani tutakuwa tumeshakamilisha maboresho, kila kitu kitakuwa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna upande wa madeni ambayo wazabuni wanadai. Inasikitisha sana na inatia uchungu sana. Kuna wazabuni ambao wali-supply vifaa vya ujenzi ama makandarasi kwa miaka mingi. Wengine miaka 10, miaka mitano na miaka 15, fedha zao mpaka sasa hawajalipwa. Ukimuuliza Mkurugenzi, kwa nini unadaiwa mpaka shilingi bilioni 4.0 na wazabuni pamoja na wakandarasi, tatizo ni nini? Kwa nini usilipe fedha zao na ni muda mrefu umepita? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, anakujibu kirahisi kabisa anasema mimi sikuwepo kipindi hicho. Sasa kama ulikuwa haupo kipindi hicho, wanavyokabidhiana ofisi wanakabidhianaje? Yaani kwamba hawakai wakakabidhiana haya madeni wanadai hawa, haya wanadai hawa, haya anadai huyu? Siyo tu madeni, kwa utaratibu mzima wa kila kitu kilichoko pale. Kukabidhiana kwao ni kama vile, akifika Mkurugenzi mwingine anamwambia hii ndiyo ofisi karibu, kwa heri naondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya madeni, hawa wazabuni wa Taifa letu la Tanzania wataendelea kuwa maskini, maskini, mpaka kwa sababu fedha zao hawalipwi. Halafu Mkurugenzi anakujibu swali lingine ukimuuliza. Kwa nini imefikia hapa shilingi bilioni tano au shilingi bilioni tatu? Anasema, unajua hapa Mheshimiwa Mbunge, mimi hapa upande wa hizi fedha shilingi bilioni tatu kama halmashauri, natakiwa nilipe shilingi bilioni mbili ama shilingi bilioni moja, shilingi bilioni mbili inatakiwa illipe Serikali ama Wizara husika. Huyu mkandarasi au mzabuni anajua wapi pa kuingilia Wizarani au huko kwenye ofisi anakosema kwamba, wafuate kwenye Serikali, anafuta wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba tuokoe maisha ya wazabuni na wakandarasi, kwa sababu fedha hizo wanakuwa wamekopa, fedha hizo mwisho wa siku wanauziwa nyumba zao, wanakuwa hawajui wataishi vipi, hela za kwenda kupanga hawana, wanabaki wanapigwa stroke, wanabaki wana presha, mwisho wake unakuwa ni kifo. Tuwanyanyue hawa wakandarasi wa Taifa hili la Tanzania lakini tuwanyanyue hawa wazabuni ma-supplier. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, lakini naomba haya wayatendee kazi. Ahsante. (Makofi)