Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge kuhusu Wakala wa Kimataifa wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (International Renewable Energy Agency - IRENA) na Azimio la Bunge kuhusu mapendekezo ya kuridhia Mkataba wa Kuanzisha Taasisi ya Dawa ya Afrika wa Mwaka 2019 (Treaty for the Establishment of the African Medicine Agency - AMA)

Hon. Masache Njelu Kasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge kuhusu Wakala wa Kimataifa wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (International Renewable Energy Agency - IRENA) na Azimio la Bunge kuhusu mapendekezo ya kuridhia Mkataba wa Kuanzisha Taasisi ya Dawa ya Afrika wa Mwaka 2019 (Treaty for the Establishment of the African Medicine Agency - AMA)


MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kuwa mchangiaji wa kwanza siku ya leo kwenye kuazimia Azimio hili la Tanzania kuweza kujiunga na IRENA.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wakala huu wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu- IRENA ilianzishwa toka mwaka 2009 na sisi toka kipindi hicho 2009 tuliweza kusaini mkataba lakini hatukuweza kuridhia hili Azimio. Hatukuweza kuridhia hili Azimio kwa sababu tulitaka pia tuweze kujiridhisha tufanye utafiti wa kutosha, tuone kwamba manufaa ambayo tunaweza tukayapata kuridhia Azimio hili na changamoto ambazo pia tunaweza tukazipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ambavyo utafiti umeweza kufanyika kwa kipindi chote hiki toka 2009 tulivyosaini mkataba huu na tumeona baadhi ya nchi jirani ambazo zimeweza kuingia na kusaini mkataba huu wakiwepo nchi jirani za Afrika Mashariki, Kenya, Uganda, Rwanda na baadhi ya nchi za SADC. Mwaka 2011 waliweza kuridhia mkataba huu na wameweza kuendelea kufanya kazi kwenye utekelezaji wake na manufaa wameweza kuyapata.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo na sisi kupitia Serikali ya Awamu ya Sita baada ya kuwa muda mrefu kuweza kuhakikisha kwamba majadiliano yamefanyika na kujiridhisha vya kutosha. Sasa umefika muda muafaka wa kuona namna iliyokuwa nzuri Bunge letu tukufu kwa maana ya Tanzania turidhie mkataba huu na sisi tuweze kunufaika na Wakala wa Nishati Jadidifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya Watanzania huko nje wanaweza wakawa wanajiuliza hizi nishati jadidifu ni nini? Manake inaweza ikawa ni neno geni kwao lakini nishati jadidifu hizi ni pamoja na uwepo wa umeme wa jua, umeme wa upepo, umeme wa maporomoko, joto ardhi na mengineo. Kwa hiyo, mtu asije akaona nishati jadidifu akaona ni jina geni, hapana ni hizi nishati ambazo sisi tumekuwa tunazitumia lakini tumeendelea kuzitumia kuhakikisha kwamba umeme wetu umeweza kuwa wa uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkataba huu ambao sisi tulisaini lakini bado tulikuwa hatujauridhia, tukishauridhia hautufungi kwa namna yoyote ile ambayo tutaona kuweza kwenda kujitoa. Tukiona mambo hayapo sawasawa pia tuna nafasi ya kuweza kujitoa na baadaye kuweza kujipanga upya ili tuweze kurudi tena. Kwa hiyo, hakuna masharti yoyote ambayo yatatufunga kuhakikisha kwamba Mkataba huu au Azimio hili linaweza likaja likatufunga.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumza nishati jadidifu hizi sisi Tanzania tayari tulishakuwa wanufaika na tunatekeleza vya kutosha nishati ya umeme jadidifu. Tayari kwenye umeme wa upepo tunatekeleza Mradi wa Zuzu wa takribani megawatt 50, tunaanza hapa hapa Dodoma, hapa Zuzu. Pale Manyoni tunatekeleza Mradi wa megawatt 100 kwa maana ya pale Mkoa wa Singida. Same vilevile megawati 50 pia Kishapu kule megawati 150. Kwa hiyo, tayari kwenye utekelezaji huu tunakwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hivi vyanzo vya umeme jadidifu ambavyo sisi tunavyo vina uwezo wa kuzalisha takribani megawatt zaidi ya 5000 kutokana na joto ardhi na upepo tunaweza tukazalisha takribani megawatt 5000 baada ya utafiti ambao umeweza kuwa umefanyika. Kwa hiyo sisi wala tusiwe na shaka utekelezaji tumeshauanza, kwa hiyo turidhie kwa pamoja kuhakikisha kwamba Azimio hili liweze kupita ili tuweze kwenda kunufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo baadhi pia tuna manufaa ambayo tunaweza kunufaika ya moja kwa moja kupitia kuridhia Mkataba huu, ikiwemo kuliwezesha Taifa kuwa na vyanzo mchanganyiko vya uzalishaji wa umeme. Sasa hivi chanzo kikubwa tulichokuwa nacho ni cha uzalishaji wa maji, lakini sasa hivi kupitia Azimio hili na vyanzo tulivyokuwa navyo ambavyo tunakwenda kuvitekeleza kwa maana ya upepo, kwa maana ya joto ardhi, vinaweza kutusaidia sana kuweza kwenda mbele vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni kuweza kuimarisha utaalamu. Kupitia wanachama wenzetu wa IRENA wao kule kuna nchi ambazo tayari zimeshapiga hatua kwa kiasi kikubwa sana. Hivyo ushirikiano ambao tutakuwa nao sisi tutapata utaalamu pale wa kutosha kuhakikisha kwamba Tanzania tunapata wataalamu wa kutosha. Pia kupitia vyuo vyetu vya ndani tayari imeshasemwa hapa tunao DIT pamoja na Arusha Technical College. Sisi kama kamati pia tuliweza kuiambia Serikali, tuweze kuongoza na Chuo cha MUST pale Mbeya na wao pia waweze kuongeza kutoa hizi course ili tuweze kupata wataalam hawa wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu itatuwezesha pia kupata wawekezaji wa kutosha kupata mitaji pia kuweza kupata ushauri kutoka kwenye nchi ambazo zinakuwa zimeendelea. Kwa hiyo, kupitia Bunge hili niombe sana turidhie mkataba huu ili na sisi kama watanzania tuweze kunufaika kwenye umeme jadidifu kupitia IRENA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)