Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kunipa nafasi ya kuwa ndani ya Bunge hili Tukufu, nafahamu dhahiri kabisa kwamba siko hapa kwa sababu nina akili nyingi na uwezo mkubwa, bali niko hapa kwa sababu Mwenyezi Mungu aliamua niwe mahali hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mabadiliko anayoyafanya katika Taifa letu, ukitembelea Buchosa leo utashangazwa na uzuri wa barabara, utashangazwa na miradi mingi ya maji yenye thamani yenye karibu Shilingi Bilioni 15, utashangazwa na madarasa mazuri vijana wetu wakisoma katika hali nzuri kabisa, napenda nimpongeze sana Rais wetu na ninaipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, mimi huwapima watu na uwezo wao wa akili kwa matendo, nirudie tena uwapima watu uwezo wao wa akili kwa matendo yao. Mara ya mwisho niliongea hapa nikasema tuna best President, intelligent President and clever President, nilisema! Narudia tena leo maneno haya leo kuyasema na nitatoa sababu mtu yeyote ambaye ana mashaka na uwezo wa Rais wetu anisikilize kwa makini.

Mheshimiwa Spika, Rais wetu amefanya jambo moja kubwa sana kuonesha kwamba ana uwezo mkubwa, jambo hilo niuwekaji wa post code bajeti ya post code ilikuwa Bilioni 720 samahani, lakini alivyopelekewa mezani bajeti ile alikatakata mpaka Bilioni 28, ni mtu mwenye akili peke yake anaweza akafanya jambo la namna hiyo. Katika hali ya kawaida ukiletewa ripoti mezani huwa tuna tabia ya kupitisha tu, lakini Rais wetu alikata mpaka ikabaki Bilioni 28.

Mheshimiwa Spika, ninapozungumza na wewe leo tayari mradi wa kuweka post code nchi nzima umekamilika kwa asilimia 95. Narudia tena kusema kwa matendo haya nina kila sababu ya kusema we have the best President, intelligent President, clever President na smart President. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo ninampongeza Mheshimiwa Waziri kwa bajeti yake, nimeona ni bajeti ya kimapinduzi ameenda kuendelea kufanya mambo makubwa katika Taifa letu, nimuombe Mheshimiwa Waziri ajiepushe na kufanya vitu vinavyofanya awe popular badada ya kufanya vitu ambavyo vitamfanya vitu sahihi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, namuomba Mheshimiwa Waziri asiguse kabisa ile asilimia 10 aiache kama ilivyo hilo la kwanza, asiguse kabisa asilimia 10 aiache kama ilivyo na ikiwezekana aiongezee. Jambo lingine la muhimu sana ambalo nataka nilichangie katika bajeti hii ya leo ni kwamba tunakusanya fedha nyingi sana tunakopa fedha tunakusanya fedha kwenye kodi tunapeleka kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu, lakini kuna kitu kimoja muhimu sana ambacho mimi naona kama tunakisahau ni ufuatiliaji wa fedha zetu tunakozipeleka, monitoring and evaluation.

Mheshimiwa Spika, Dada yangu Mheshimiwa Eng. Ulenge aliwahi kuzungumza siku moja hapa ndani suala la monitoring and evaluation, ufuatiliaji na tathmini ni changamoto kwenye Taifa letu. Tunakusanya fedha nyingi tunapeleka huko kwenye Halmashauri zetu tunasahau kwamba kuna watu ambao hawaogopi fedha ya umma kabisa! Wanasubiri fedha ya umma ije waitafune. Niseme bila kupindisha maneno kwamba Halmashauri zetu ni mchwa wa fedha za umma narudia tena halmashauri zetu ni mchwa wa fedha za umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninawaomba kama Taifa ninawaomba Waheshimiwa Wabunge, tujue kabisa ya kwamba tunao wajibu wa kufuatilia fedha zetu ambazo tumezipeleka kwa wananchi, Rais wetu ana nia njema ya kuleta maendeleo lakini hatufuatilii fedha zetu. Mfano, mdogo wangu Mheshimiwa Aweso alienda Handeni, nikamsikia anasema nionyeshe bwawa akarudia nionyeshe bwawa hakuna bwawa akaoneshwa dimbwi Milioni 600 zimeliwa.

Mheshimiwa Spika, sijakaa sawa nikamuona Kaka yangu Mheshimiwa Prof. Mbarawa na yeye analalamika kwenye television ya kwamba nioneshe temporary office, temporary office imekuja kuonekana ya Milioni 100 ni kibanda cha mabati! Sijakaa sawa nikamuona ndugu yangu Mheshimiwa Musukuma Kaka yangu Kasheku analalamika kwamba kule kwake bati ya kununuliwa Shilingi 40,000 imenunuliwa Shilingi 72,000. Sijakaa sawa nikamuona Kaka yangu ambaye ninamheshimu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Kassim yuko MSD anasema vifaa vinavyotakiwa kununuliwa kama sijui ilikuwa Milioni 20 kimenunuliwa kwa Milioni 129.

Mheshimiwa Spika, hii ni mifano michache tu ambayo tumeiona kwenye television, iko mifano mingi sana ambayo hatuioni ya pesa za umma zinatafunwa na watu wenye nia mbaya na maendeleo ya nchi yetu! Monitoring na evaluation naungana na Dada yangu Mheshimiwa Ulenge leo hayupo kuiomba Serikali yangu iimarishe ufuatiliaji na tathmini ya pesa zinazoenda vijijini, tofauti na hapo tutakuwa tunapeleka fedha zinaishia mikononi mwa watu wachache, zinatafunwa, hakuna kinachofanyika. Hatuwezi kutimiza ndoto ya nchi yetu kama watu wachache wanatuvurugia movement yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilisoma ripoti moja na ilinisikitisha sana ripoti hiyo ya transparence international ambayo walisema dola bilioni 50 zinatoka Afrika kila siku kwenda mabenki ya Ulaya, nikasoma chini yake nikakuta wanatamka jambo la kusikitisha kabisa kwamba kiasi cha dola bilioni 4.5 zinapotea kama mapato katika Taifa la Tanzania, fedha ambazo zingethibitiwa zisipotee zingejenga Vituo vya Afya 1,730 kwa kituo kimoja milioni 600. Zingethibitiwa zisipotee zingeweza kujenga kilometa 5,300 za lami. Najenga hoja ya kwamba fedha zinazopotea zikidhibitiwa zisipotee maendeleo yetu yatakwenda kwa kasi kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tunafanya nini kama Taifa; Kwanza, nilizungumza tulipoitwa Ikulu na Mheshimiwa Rais kule Chamwino, nikasema Tanzania kama mataifa mengine ya Afrika yalivyo yanasumbuliwa na ugonjwa mmoja mbaya unaitwa Institutional failure. Taasisi zetu zime-fail, zime-fail tafsiri yake ni lazima ziimarishwe, kama taasisi zinafanya kazi zinavyotakiwa Mheshimiwa Aweso – Waziri wa Maji asingeweza kulalamika pale kuhusu bwawa, pale alipolalamika Mheshimiwa Aweso hakuna Mkurugenzi? Hakuna DC? Hakuna TAKUKURU?

SPIKA: Sasa ngoja Mheshimiwa nilikuwa nimekuacha ili uende na huo mtiririko lakini sasa wacha nikuongoze kidogo, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Aweso ni Mheshimiwa Aweso awe shemeji yako, kaka yako humu ndani ni Mheshimiwa, kwa sababu la sivyo tutafika mahali watu wanaanza kama mke wangu alivyosema. Sasa ngoja tuite kwa kadri Kanuni zinavyotuongoza humu ndani wote ni Waheshimiwa kwa sababu ukisema tu neno Aweso bila Mheshimiwa Baba yake anaitwa Aweso, sasa tunakuwa hatujui unamuongelea yupi unamuongelea huyu Waziri au yule mwingine. Ahsante sana.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, naomba nimuombe sana radhi mdogo wangu Mheshimiwa sana Jumaa Aweso kwa kumtaja tu kama Aweso na Mheshimiwa Spika nimeyapokea maelekezo yako vizuri kabisa.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba niseme what do we do? Nilizungumza alipotuita Mheshimiwa Rais Ikulu kwamba, tatizo kubwa la Tanzania na nchi za Afrika ni Institutional failure, taasisi zimeferi taasisi zingefanya kazi yake zisingemsubiri Mheshimiwa Aweso- Waziri wa Maji, zisingemsubiri Mheshimiwa Waziri Mkuu, palepale kuna DC, Mkurugenzi, kuna watu wa TAKUKURU wangefanya kazi yao sawasawa wasingemsubiri Mheshimiwa Waziri Mkuu au Mheshimiwa Waziri wa Maji aje.

Mheshimiwa Spika, naomba sana tuimarishe taasisi zetu zitimize wajibu wake kule chin,i tunafanyaje kwenye suala zima la mapato ya umma? Kwenye mapato ya umma tuimarishe TAKUKURU. Nilikaa wiki mbili zilizopita na Mkurugenzi wa PCCB ofisini kwake nikawa nazungumza naye nabadilishana naye mawazo, tunafanyaje tuweze ku-control tuweze kudhibiti rushwa katika Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, tulipoanzisha TAKUKURU ilianza mwaka 1974 lakini hata 1991 ilikuwa inaitwa (PCB) Prevention of Corruption Bureau, kazi yake ya kwanza TAKUKURU kabisa ya mwanzo kabisa ilikuwa ni kuzuia rushwa mwaka 2007 tukabili sheria tukaita Prevention and Combating of Corruption Bureau (PCCB). Tukaongeza suala la combating maana yake sasa ni kuzuia na kupambana na rushwa, TAKUKURU wamesahau suala zima la prevention wamejielekeza kwenye combating kwenye kupambana, wanazo kesi nyingi sana hivi sasa lakini bado kuna kesi nyingi zinatokea.

Mheshimiwa Spika, nataka TAKUKURU wawezeshwe, tuwawezeshe kufanya suala la prevention kuzuia rushwa wamelisahau hiyo task. Mheshimiwa Waziri amezungumza juzi hapa, akasema amewawezesha CAG kwa kuwapa fedha nyingi, namuomba Mheshimiwa Waziri hizo fedha badala ya kuzipeleka CAG awapelekee PCCB ili wawezeshwe kwa mafunzo, kwa idadi kubwa ya watu wa kufanya kazi maana yake labor force, mwisho wa siku tuweke sheria ya kwamba fedha inapokwenda kwenye Halmashauri yoyote iwe mandatory iwe ni lazima PCCB wapate kopi kwa ajili ya ufuatiliaji. Narudia tena iwe ni lazima PCCB kupata copy kwamba tumepeleka fedha Milioni 600 na isome ya Kituo cha Afya kwa hiyo TAKUKURU wapokee kwa ajili ya ufuatiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi sasa ninavyozungumza ni hiyari kuwapelekea TAKUKURU. Naomba niunge mkono hoja ahsante kunisikiliza. (Makofi)